KILIMO ndio uti wa mgongo wa Tanzania na takriban asilimia 80 ya Watanzania wanategemea sekta hiyo ikiwa ni shughuli yao kuu ya uchumi.
Kwa muktadha huo, kilimo ndiyo sekta kubwa ya ajira nchini na haishangazi kuona inachangia asilimia 29 ya Pato la Taifa na zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwa miaka yenye mvua za kutosha, hii ni kwa mujibu wa Bajeti ya mwaka 2016/17.
Tanzania ni miongoni mwa nchi nyingi duniani zinazofanya jitihadi za kuinua uchumi wake kufikia uchumi wa kati ikilenga kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2025 pamoja na Malengo Endelevu ya Milenia (SDG) yaliyoridhiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi Septemba 25, 2015.
Aidha, kilimo ni miongoni mwa sekta zinazowekewa mkazo na serikali katika kutokomeza umaskini na kuongeza uhakika wa akiba ya chakula ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi kupitia kilimo cha mazao ya biashara.
Katika awamu ya tano ambayo inasisitiza kauli mbiu ya ‘Tanzania ya Viwanda’, kilimo ndio muhimili mkubwa kwa sababu ndiyo chanzo cha malighafi ambazo zitahitajika kwenye viwanda hivyo.
Mazao kama chai, pamba, kahawa, mkonge, tumbaku, ufuta na korosho yanatiliwa mkazo na serikali ambapo kupitia viwanda hivyo yanaweza kuongezewa thamani na kusafirisha nje ya nchi ili kuingiza fedha za kigeni za kutosha badala ya kuuza yakiwa ghafi.
Korosho ni zao la biashara linalozalishwa kwa wingi kwenye mikoa iliyopo Kusini mwa Tanzania hususan Mtwara, Lindi, na Ruvuma japokuwa zao hilo linalimwa pia kwenye mikoa ya Tanga, Pwani na Morogoro.
Hata hivyo, pamoja na umuhimu mkubwa wa zao hilo kwenye uchumi wa taifa, bado uzalishaji wake ni wa kusuasua kutokana na kuzalishwa zaidi na wakulima wadogo wasio na uwezo kusimamia shamba lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 5.
Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, wakulima wengi huzalisha chini ya ekari 5, hali ambayo inasababishwa na uhaba wa pembejeo kama vile madawa (viuatilifu) na mitaji midogo ya kuwekeza.
Kila msimu, serikali inajitahidi kuwasaidia wakulima hao wadogo kwa kuwapa ruzuku ya pembejeo na viuatilifu, lakini ni wachache wanaopata misaada hiyo hasa ukizingatia inapitia kwenye vyama vikuu vya ushirika.
Mkulima hupata tija na hamasa zaidi ya kilimo cha korosho pale anapoona mazao yake yananunuliwa kwa bei yenye maslahi na kwa wakati, jukumu ambalo linapaswa kusimamiwa na Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi (Amcos).
Vile vile vyama hivi vina jukumu la kumsaidia mkulima wa chini kupata pembejeo bora zinazoweza kuleta ufanisi mkubwa katika kilimo hicho.
Vyama hivi ndivyo vinavyowaunganisha wakulima kwenye Bodi Kuu ya Korosho ambayo ndiyo mhimili mkuu wa usimamizi wa mwenendo wa vyama vya msingi na vya ushirika.
Hata hivyo, katika msimu wa 2016-2017 wakulima wengi wana wasiwasi juu ya ubora wa viuatilifu vilivyotolewa kwa ruzuku na serikali.
Ilidaiwa kwamba, dawa zilizotolewa zimepitwa na muda wake wa matumizi (expiry date), hali iliyosababisha baadhi ya maua machanga ya mikorosho kuungua baada ya kupuliziwa.
FikraPevu imeelezwa kwamba, mfumo wa ugawaji wa pembejeo hizo pia haukuzingatia mahitaji ya wakulima kwani wapo walioandikishwa kupatiwa idadi fulani ya dawa lakini idadi hiyo ilipunguzwa na wahusika kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.
Katika msimu wa 2016-2017 serikali imejizatiti kuwakomboa wakulima wa zao hilo kwani, tofauti na msimu uliopita, bei ya korosho imepanda na kufikia shilingi 1,300 kwa kilo moja ya korosho ya Daraja la I na shilingi 1,200 kwa Daraja la II kwa mauzo ya stakabadhi ghalani.
Maazimio hayo yalifikiwa kwenye kikao cha wadau kutoka kwenye mikoa izalishayo korosho waliokutana mjini Bagamoyo, Pwani Septemba Mosi, 2016.
Ni katika kipindi hicho ambapo serikali iliivunja Bodi ya Korosho na kuunda mpya ili kupambana na ubadhilifu na kuhimiza uwajibikaji.
Mbali na bei hiyo, korosho ziliuzwa kwa njia ya mnada ambapo kila kampuni ya ununuzi ilitakiwa kuchukua zabuni kutoka kwa wakulima kupitia vyama vikuu vya ushirika na vyama vya msingi.
Tangu Septemba Mosi, 2016 mpaka sasa, jumla ya minada 8 imefanyika kupitia kampuni hizo, lakini jambo la kushangaza wakulima wanalalamika kutopata malipo yao kwa wakati.
Sambamba na tamko hilo la Rais John Magufuli, serikali pia ilitangaza kufutwa kwa tozo tano kati ya tisa zilizokuwa zikitozwa kwa wakulima.
Tozo hizo ni pamoja na shilingi 50 ya usafirishaji, 1% ya uwezeshaji wa Sekretarieti ya Mkoa, shilingi 5 kuchangia Chama Kikuu cha Ushirika, tozo ya kulipia ghala na tozo ya unyaufu.
Licha ya hatua hicho kutangazwa na Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kasimu Majaliwa akiwa ziarani wilayani Ruangwa, bado wapo viongozi wa vyama vya ushirika na vile vya msingi na baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji na wahifadhi maghala wameendelea kuwabebesha mzigo wakulima kwa kuendeleza tozo ya usafirishaji, unyaufu na kulipia ghala kwa sababu tu ya maslahi binafsi.
FikraPevu inafahamu kwamba, bei ya korosho ilitofautiana kwa kila mnada ambapo kwa mnada wa 1 hadi wa 5 kilo moja ilifikia shilingi 3,710 kabla ya kuanza kuporomoka kuanzia mnada wa sita.
Katika hotuba yake aliyoitoa Septemba 31, 2016, Rais Magufuli aliwatoa hofu wakulima wa zao la Korosho kuwa bei ya korosho itafikia hadi shilingi 4,000 kwa kilimo moja ya korosho.
Lakini siku chache baada ya Bodi mpya ya Korosho kuundwa, Vyama Vikuu vya Ushirika kama vile CHAMALI (Masasi, Lindi), MAMCU (Masasi na Mtwara), TANECU (Tandahimba na Newala), na RUNALI (Ruangwa, Nachingwea na Liwale) vilipewa dhamana ya kusimamia mwenendo wa Vyama vya Msingi (Amcos).
Miongoni mwa majukumu waliyopewa ni kufuatilia mwenendo wa uuzaji na ununuzi wa korosho kwa kampuni zenye zabuni, wahifadhi maghala na serikali za vijiji katika kuhakikisha kuwa ununuzi wa zao hilo unafanyika pasipo na kero zozote kutoka kwa wakulima.
Zoezi hilo lilikwenda sambamba na kutekeleza matamko yote ya serikali yakiwemo ya ufutwaji wa tozo, lakini pia kuhakikisha kuwa kampuni zote zinazoshika zabuni ni halali na zinakidhi vigezo vilivyoainishwa na serikali.
Kwamba kila kampuni ilitakiwa kuhakikisha kuwa siku sita baada ya mnada, ikamilishe malipo kwa wakulima.
Ili kukamilisha hilo, kila kampuni ilitakiwa kuwa na akaunti ya dhamana (bond account) ambapo fedha za wakulima zitahifadhiwa ili inapotimia siku ya 6 malipo yafanyike bila usumbufu wala ucheleweshwaji.
Katika hali ya kushangaza, hilo halijafanyika licha ya uwepo wa viongozi wa vyama vya ushirika huku minada 8 ikiwa imefanyika.
Taarifa ambazo FikraPevu inazo ni kwamba, kucheleweshwa huko kumetokana na kuchanganywa kwa taarifa za stakabadhi ghalani (warehouse receipts) za wakulima waliouza korosho zao kwenye minada mbalimbali kama ilivyobainishwa na Mbunge wa Jimbo la Nachingwea kwenye barua yake kwenda kwa chama kimojawapo cha ushirika mkoani Lindi.
Inaonekana kwamba, tatizo hilo linaanzia kwenye chama cha msingi. Lakini swali la kijiuliza ni kwa vipi taarifa za wakulima zinachanganywa wakati kila mkulima anapata stakabadhi yake kutokana na taarifa zake?
Katika barua ya Januari 3, 2017 yenye kumbukumbu namba Nach/MP/GEN/016/01 kwenda Chama cha Ushirika cha Ruangwa, Nachingwe na Liwale (Runali), Mbunge wa Nachingwea, Elias Masala, aliweka wazi changamoto na kero wanazozipata wakulima wakiwa kwenye vyama vya msingi na ushirika, kubwa ikiwa ucheleweshwaji wa fedha za mauzo.
Pamoja na kupongeza mwenendo wa uuzaji na ununuzi wa korosho, mbunge huyo alisisitiza kupatiwa ufumbuzi wa haraka kwa suala la ucheleweshwaji wa malipo hayo ya wakulima kutoka kwenye kampuni zenye dhamana na zabuni za ununuzi.
Barua hiyo pia ililalamikia makato nje na mjengeo wa bei, ya kulipia zana za kuhifadhia korosho (magunia) na suala la kusahaulika kwa taarifa za stakabadhi (warehouse receipts).
Barua nyingine kutoka kwa mbunge huyo yenye kumbukumbu namba Nach/MP/017/01, ilitilia mkazo na kubainisha uwepo wa viongozi wasiojali maslahi ya wakulima waliouza kwenye vyama vya ushirika na vyama vya msingi.
Katika mkutano uliofanyika Bagamoyo, Bodi ya Korosho pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zilibaini upotevu na ubadhilifu mkubwa wa shilingi 5 bilioni ambazo zilikuwa mahsusi kwa malipo ya wakulima mkoani Lindi huku wilaya ya Nachingwea pekee ikiwa na upotevu wa shilingi 1.5 bilioni.
Swali la kutafakari ni kwamba, fedha hizo zimepoteaje ikiwa wasimamizi wakubwa ni vyama vya msingi, vyama vya ushirika na taasisi za fedha?
Licha ya upotevu wa fedha hizo hakuna hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa kwa washukiwa wa upotevu huu. Kwa muktadha huo mkulima anakombolewa ama anakomolewa?
Ni jitihada chache ambazo zimechukuliwa na serikali kuwavua madaraka na kuwashtaki baadhi ya viongozi wa chama cha msingi cha CHAMALI katika kile kinachodaiwa kuwa ni ubadhilifu wa fedha za wakulima.
Imefikaje hapa? Mazingira ya upotevu wa fedha hizo yanaonekana kuandaliwa na Bodi ya Korosho pamoja na vyama vya ushirika na vyama vya msingi kwanza kwa kuzipatia usajili na zabuni kampuni ambazo hazikukidhi vigezo vya ununuzi.
Kampuni nyingi zinadaiwa zilikwenda kama madalali (middlemen) pasipo kuwa na 'bond account' kwa ajili ya malipo ya wakulima, hali ambayo inaelezwa kwamba ndiyo sababu kubwa inayochelewesha malipo kwa wakulima hadi sasa.
Pili, ni hatua ya kuwachilia viongozi wa vyama vya ushirika wanaoendeleza tozo ambazo zimekwishaondolewa kwenye mfumo wa ununuzi na uuzaji wa korosho. Viongozi hawa ndio wanaosababisha upotevu wa fedha nyingi za wakulima.
Tatu, wapo viongozi wanaidhinisha kuwa mzigo umeuzwa na umeshalipiwa wakati bado haujalipiwa, suala ambalo linasababisha kuwa na tofauti ya bei za kwenye minada huku baadhi ya wakulima wakiangukia kwenye bei za chini wakati wameuza kwenye minada yenye bei za juu jambo ambalo linapunguza kiasi halisi cha fedha walichopaswa kulipwa.
Nne, uchangiaji wa tozo za magunia ya kuhifadhia korosho ambalo ni jukumu la vyama vya msingi umeendelea kuwabana wakulima na kuwapunja stahiki zao.
Tano, baadhi ya vyama vya ushirika na vyama vya msingi vimekuwa vikiongozwa na kamati za muda ambazo hazitambuliki kisheria, hali inayowafanya viongozi hao wajali maslahi binafsi na siyo ya wakulima wengi.
Wakati haya yakifanyika ni lazima serikali ikae na kuangalia maslahi ya mkulima wa chini kuona ni jinsi gani kilimo kinamkomboa na kumuinua kiuchumi bila kuwepo kwa changamoto zozote.
Ikumbukwe pia kuwa kila nyanja ya maisha ambayo mkulima wa korosho anapitia, basi anategemea maslahi na manufaa mazuri ayapatayo kwenye kilimo.