UBOVU wa barabara yenye urefu kilometa 82 kutoka wilayani Mbinga hadi katika kijiji cha Darpori kilichopo mpakani mwa nchi za Tanzania na Msumbiji kumesababisha abiria kulipa nauli kati ya shilingi 30,000 hadi 40,000.
Uchunguzi ambao umefanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa wananchi wanaoishi katika kijiji hicho na kilichopo katika kata ya Tingi wanakabiliwa na matatizo makubwa yanayotokana na tatizo sugu la ubovu wa barabara.
Mwenyekiti wa kijiji cha Darpori Andason Haule alisema kero ya barabara katika kijiji hicho inasababisha wananchi kulipa nauli ya shilingi 80,000 kwenda Mbinga na kurudi na kwamba gari zinazotumika ni landrover 110 ambapo wakati wa masika hutumia siku mbili hadi tatu kufika katika kijiji hicho.
- Huu ndiyo usafiri wa kutoka Mbinga hadi kijiji cha Darpori ambapo abiria wanakarishwa juu na mizigo ndani licha ya kulipa nauli ya shilingi 40,000 kwa umbali wa kilometa 82 tu
“Ndugu mwandishi pamoja na wananchi kulipa nauli kubwa kiasi hicho sio kwamba abiria wanakaa ndani ya gari, bali wanakarishwa juu ya bodi ya gari na wengine wananing’inia nyuma ya gari hadi mwisho wa safari,wenye magari wanaheshimu zaidi kubeba mizigo ndani kuliko kubeba abiria kwa kuwa mizigo ndiyo inayowalipa zaidi ’’,alisisitiza.
Hata hivyo mwenyekiti huyo alisema ingawa serikali imekuwa inaahidi kufanya matengenezo ya barabara hiyo kila mwaka,badala yake ahadi zimekuwa nyingi kuliko utekelezaji na kwamba kijiji hicho kinaiingizia serikali mapato makubwa kutokana wakazi wake kuchimba madini ingawa serikali inashindwa kuwatatulia kero ya barabara.
Godfred Nchimbi ni mwalimu katika shule ya msingi Darpori anasema mazingira ya kufanyia kazi katika kijiji hicho ni magumu kutokana na maisha kuwa magumu kutokana na wakazi wengi wa kijiji hicho kujihusisha na uchimbaji wa madini hali ambayo imesababisha bidhaa na vyakula kuuzwa kwa bei ya juu.
Maandalizi ya kupanga mizigo kwenye gari yakifanyika katika stendi ya kijiji cha Darpori ambapo hata bia zinasafirishwa chupa bila kreti ili kupata nafasi ya kutosha kwa mizigo mingi
Uchunguzi umebaini kuwa bei za vyakula na bidhaa ni mbaya katika kijiji hicho ambapo bei ya soda inafikia hadi shilingi 2000, chupa ndogo ya maji ya kunywa shilingi 1000,vocha ya simu ya shilingi 1,000 inauzwa hadi 1,500, bei ya mafuta ya petroli inauzwa kati ya shilingi 5,000 hadi 8,000 kwa lita.
“Wakati tunakwenda kuchukua mishahara mwisho wa mwezi hali ni mbaya kwa kuwa unapotaka kwenda kuchukua mshahara inabidi uchukue ruhusu ya wiki moja kwenda na kurudi, nauli ni shilingi 80,000 tena unakaa juu ya bodi la gari, ukipiga gharama za nauli, kulala na chakula karibu mshahara mzima tunamalizia barabarani, serikali ilituahidi kutupatia fedha za mazingira magumu lakini hadi sasa hakuna utekelezaji wowote”, alisisitiza mwalimu Nchimbi.
Anusiata Mbunda ambaye amefundisha katika shule ya msingi Darpori kwa miaka minne hivi sasa anasema ubovu wa barabara umesababisha mazingira ya kazi kuwa magumu na kutoridhisha,anatamani kuacha kazi ingawa amekiri kuwa kazi ya ualimu ni wito.
Aureus Masuja ni diwani wa kata ya Tingi yenye vijiji nane kikiwemo kijiji cha Darpori akizungumzia kero ya barabara alisema karibu vijiji vyote vya kata hiyo vinakabiliwa na ubovu wa barabara na kusisitiza kuwa hali ni mbaya zaidi kuanzia kijiji cha Mpepo hadi Darpori.
“Mimi mwenyewe kama diwani nimeshawahi kwenda kwa mwandisi wa ujenzi wa wilaya ya Mbinga kumuomba kutilia mkazo ujenzi wa barabara hii ambayo aliniambia kuna mkandarasi amepewa kazi na anatakiwa kukamilisha kazi Oktoba 30 mwaka huu”, alisema.
Kutokana na kukithiri kwa ubovu wa barabara kutoka kijiji cha Mpepo hadi Darpori baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi wameamua kutengeneza barabara katika sehemu korofi kwa kutumia majembe kisha kuwatoza madereva wa pikipiki na magari kiasi cha kati ya shilingi 1,000 hadi 3,000.
Mmoja wa watoto ambao wameweka vizuizi katika barabara ya Mpepo hadi Darpori wakitaka kulipwa hadi shilingi 3,000 na wenye vyombo vya usafiri baada ya kutengeneza sehemu korofi
Wanafunzi hao wanaweka vizuizi vya kamba, mawe au miti kwa lengo la kusimamisha magari na pikipiki na kisha wakishalipwa fedha wanafungua vizuizi hivyo na kuruhusu vyombo hivyo vya usafiri kupita na kuendelea na safari.
Huyo dogo haendi shule au ndo likizo?