TATIZO la baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi katika Manispaa ya Moshi la kubaguliwa wakati wa chakula cha mchana kutokana na wazazi wao kutochangia fedha za chakula sasa limepatiwa ufumbuzi, FikraPevu inaripoti.
Tangu serikali ya awamu ya tano ilipofuta ada na michango mingine na kutangaza elimu bila malipo hadi Kidato cha Nne, baadhi ya wazazi wenye watoto katika shule za msingi, hasa za serikali, waligoma kuchangia fedha za chakula cha mchana.
FikraPevu imeelezwa kwamba, hatua hiyo ilitokana na serikali kufuta Waraka Namba 8 wa mwaka 2011 uliohusu michango mbalimbali wanayotakiwa kutoa wazazi ama walezi kulingana na makubaliano yao kupitia kamati za shule.
“Kufuatia Waraka Namba 5 wa mwaka 2015 na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 kuhusu utoaji wa elimumsingi bila malipo, serikali sasa imefuta nyaraka zote kuhusu malipo yaliyokuwa yakitozwa katika uendeshaji wa elimu msingi kutoka kwa wazazi na walezi.” Unasomeka Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016.
Kauli ya Mkurugenzi Manispaa ya Moshi
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, anasema kuanzia sasa ni marufuku wanafunzi kunyimwa chakula kutokana na wazazi wao kushindwa kuwalipia fedha kwa ajili ya chakula cha mchana.
Katika mahojiano na FikraPevu, Mkurugenzi huyo anasema kwa sasa suala la wazazi ama walezi kuchangia chakula cha mchana kwa wanafunzi si suala la hiari bali ni matakwa ya kisheria.
Anasema kumnyima mtoto chakula ni jambo ambalo kwa sasa halikubaliki na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo ni kumhukumu mtoto kwa kosa ambalo hajalitenda huku wanaostahili kuwajibishwa ambao ni wazazi, wakiachwa.
“Kwa kuanzia, tunawapeleka Baraza la Kata na huko wakitushinda tunawapeleka polisi, wanawajibishwa kwa kutumia Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 ambayo imeainisha haki ya mtoto na wajibu wa mzazi katika kumlea mtoto,” anasema.
Mkurugenzi huyo anasema, kitendo cha kumbagua mtoto wakati wa chakula cha mchana kutokana na mzazi ama mlezi wake kutomchangia fedha za chakula pia kinakwenda kinyume na sheria hiyo hiyo ya mtoto.
Kifungu cha 5 (2) kinaonya mtu yeyote kutombagua mtoto kwa misingi ya jinsia, tabaka, umri, dini, lugha, maoni ya kisiasa, ulemavu, hali ya kiafya, mila, kiuchumi, ukimbizi au kwa misingi mingine.
Akizungumzia hali ya chakula ilivyo kwa sasa shuleni, mkurugenzi huyo anasema kuwa kwa sasa kila mtoto anakula chakula na wanachokifanya kama serikali ni kuhangaika na wazazi wakorofi ambao hawataki kuchangia chakula.
“Unamnyima chakula mtoto ana kosa gani, unamwadhibu yeye badala ya kumwadhibu mzazi? Tatizo ninaloliona hapa watu wanaona kila kitu cha serikali ni bure wakati si kweli,” anasema mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, anasema wananchi wengi wamepokea kwa mtazamo hasi hatua ya serikali kuhusu elimu msingi bila malipo wakiamini kuwa kila kitu ni bure hata masuala yanayowahusu wazazi wanayapa kisogo.
Waraka Namba 3
Mkurugenzi huyo anasema Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 umeainisha majukumu ya kila mtu kuanzia serikali yenyewe, wazazi ama walezi, wakuu wa shule na kamati za shule na jamii kwa ujumla kuhusu utekelezaji wa elimu bure bila malipo.
Kwa mujibu wa waraka huo, kamati za shule zimepewa jukumu la kuhakikisha zinashirikiana na wazazi na walezi pamoja na jamii kuweka utaratibu wa chakula cha mchana.
Majukumu ya walimu ni pamoja na kuhakikisha wanawaongoza na kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora na kukua katika maadili mema ili waweze kuwa raia wema watakaoshiriki kikamilifu katika maendeleo yao, familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Kuhusu wanafunzi, waraka huo umeainisha majukumu manne ikiwamo kutoa mrejesho kwa wazazi ama walezi kuhusu jambo lolote linaloagizwa shuleni ili mzazi ama mlezi ashiriki kikamilifu katika maendeleo ya shule.
FikraPevu inatambua kwamba, kwa mujibu wa waraka huo, majukumu ya wazazi na walezi ni sita na mojawapo ni kushirikiana na uongozi wa shule kuweka utaratibu wa kutoa chakula cha mchana kwa shule za kutwa na bweni kulingana na mazingira yao.
Diwani wa Kata ya Kaloleni, Reward Shelukindo, anasema inasikitisha kuona mzazi ama mlezi anashindwa kumlipia mtoto wake Shs. 200 kwa siku lakini wakati huo huo anatumia Shs. 2,000 kwa siku kwa ajili ya kuvuta sigara kumi ambazo kila moja inauzwa Shs. 200.
Anasema, kwa kushirikiana na uongozi wa shule na ofisi ya mtendaji wa kata, wameweka vikao na wazazi na walezi na kukubaliana kuwa ni lazima kila mtoto apate chakula cha mchana shuleni.
“Lengo letu ni kuwafanya watoto kuwa kitu kimoja shuleni na kuwajengea usikivu mzuri darasani lakini pia itasaidia watoto hawa kuwaepusha na watu wenye tabia mbaya za ulawiti na ubakaji ambao kwenye kata yetu matukio ya aina hii yapo na tumeyaripoti polisi,” anasema.
Shelukindo anasema, wazazi ambao ni wakorofi na jeuri ambao hawataki kuchangia fedha kwa ajili ya chakula cha mchana licha ya kuwa na uwezo huo, watawajibishwa kwa kufikishwa Baraza la Kata kwa hatua zaidi za kisheria.
Wazazi na wanafunzi wanasemaje
Elizabeth Sayuni Seif mkazi wa Mtaa wa Reli mjini Moshi anaunga mkono msimamo wa serikali wa kuwawajibisha wazazi ambao hawachangii fedha za chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni.
Anasema, mtoto ambaye hajalipiwa chakula cha mchana shuleni na mzazi wake anaweza akatoroka shule na kwenda nje ambako huko anaweza akakutana na makundi ya watu wabaya yanayoweza kumharibu kwa kumshawishi wa pesa.
“Watoto wanaosoma shule zilizopo katikati ya mji hasa wasichana wapo katika hatari kubwa ya kuharibiwa na makundi ya vijana hasa hawa waliopo stendi kuu ya mabasi kutokana na kukosa chakula cha mchana,” anasema.
Mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Salma, anayesoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Uhuru iliyopo Kata ya Mawenzi katika Manispaa ya Moshi, anasema wanaotakiwa kubebeshwa lawama ni wazazi ambao hawachangii fedha za chakula cha mchana na si mwanafunzi.
Kwa upande wao, walimu wa Shule ya Msingi Mawenzi walioomba kutotajwa majina yao, wamedai kuwa waliokuwa wakishinika wanafunzi ambao hawajalipiwa fedha za chakula cha mchana ni wazazi wa wanafunzi waliolipia fedha za chakula.
Wanasema msimamo wa serikali wa kutowanyima chakula wanafunzi ambao hawajalipiwa fedha za chakula cha mchana na wazazi wao itakuwa suluhisho la watoto hao kubaguliwa wakati wa mlo.
Jamii inataka nini?
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Azimio, Doroth Mbuya, anashauri kuwepo na mjadala wa kitaifa utakaolenga kujadili kwa kina tatizo la chakula shuleni na wajibu wa wazazi katika kuchangia chakula cha mchana kwa watoto wao.