Uhaba na uchafu wa vyoo shuleni unahatarisha afya za wanafunzi jijini Dar es Salaam

Jamii Africa

MAZINGIRA bora ya kufundishia na kujifunzia katika shule ni kichocheo kwa wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao na kupata ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kutatua changamoto Za maisha.

Lakini shule nyingi za msingi na sekondari hazina mazingira rafiki kwa wanafunzi, ikiwemo mifumo mizuri ya maji safi na taka, vyoo na vifaa vya usafi, hali inayohatarisha afya zao na hata kuwa sababu ya magonjwa ya mara kwa mara.

Ni kutokana na kukumbwa na magonjwa, baadhi ya wanafunzi hukwama kuhudhuria masomo, hivyo kukwamisha ufaulu na ufahamu wa yale wanayofundishwa.

Takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zinaonesha kuwa asilimia 60 hadi 80 ya magonjwa yote ambayo watu hutibiwa hospitalini,  yanasababishwa na kutozingatia kanuni za usafi, ikiwemo matumizi ya maji yasiyo salama.

Matukio ya mara kwa mara ya magonjwa ya kuhara yanawafanya watoto kuwa katika hatari ya kukumbwa na magonjwa mengine.

Changamoto kubwa inayosababisha afya za wanafunzi kuzorota ni uhaba wa vyoo, maji safi na salama kwa ajili ya matumizi wawapo shuleni.

Juhudi mbalimbali za wadau zimefanyika kujenga madarasa, lakini eneo la kujenga vyoo vya kisasa halijazingatiwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari nchini.

FikraPevu ilitembelea Shule ya Msingi Victoria iliyopo kata ya Makumbusho, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kuona hali halisi ya vyoo katika shule hiyo.

Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 674 ambao hutumia matundu manane tu. Hii ina maana kuwa wanafunzi 84 hutumia tundu 1 la choo.

Kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2009 inaelekeza wasichana 20 watumie tundu moja la choo na wavulana 25 watumie tundu moja.

Shule ya Victoria ina wasichana 350 ambao hutumia matundu 4 na ili idadi hiyo ya wasichana ikidhi uwiano wa 1:20 inatakiwa wasichana hao wapate matundu 17 ambapo kwa sasa wana matundu 4.  

Kwa muktadha huo wasichana hao wanahitaji matundu 13 ya ziada ili kukidhi mahitaji yote ya vyoo.

Wavulana katika shule hiyo wako 323 ambao hutumia matundu 4, lakini kulingana na sera ya elimu walipaswa kuwa na matundu 13 na hivyo wanahitaji matundu mengine 9 ili kukidhi mahitaji yote ya wavulana.

Kwa ujumla shule hiyo ina upungufu wa matundu 22 ya vyoo kati ya matundu 30 yanayopaswa kuwepo shuleni hapo.

Upungufu wa vyoo katika shule hii unaweza kuakisi hali halisi iliyopo katika shule mbalimbali nchini ambapo shule nyingine hazina vyoo kabisa, ziko ambazo zina vyoo vichache ambavyo havikidhi mahitaji ya wanafunzi na maelekezo ya sera  na kuhatarisha afya za wanafunzi hasa wa kike ambao hupata hedhi kila mwezi.

Katika uchunguzi uliofanywa na mpango wa kuwepo vyoo na maji safi na salama shuleni, (Swash mapping survey -2015) katika shule za msingi na sekondari katika wilaya 16 za Tanzania, ulibaini kuwa hali ya maji, usafi na afya katika shule hizo hairidhishi kulingana na mahitaji.

Ni asilimia 11 tu ya shule zote zilizochunguzwa zilikidhi kiwango cha taifa cha wasichana 20 na wavulana 25 kutumia tundu moja la choo.

Asilimia 20 ya shule zote ambao ni wanafunzi zaidi ya 100, hutumia tundu moja la choo na asilimia sita ya shule hizo hazina vyoo kabisa.

Licha ya upungufu wa vyoo katika shule ya Victoria, walimu bado wanalazimika kuwafundisha wanafunzi namna ya kutumia kwa usahihi vyoo vilivyopo na kuhakikisha afya za wanafunzi zinapewa kipaumbele.

“Changamoto tuliyonayo hapa shuleni ni upungufu wa walimu na vyoo ambavyo ni vichache ukilinganisha na idadi ya wanafunzi tulionao,” anaeleza mwalimu mmoja katika shule hiyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Anasema, “hata vyoo vilivyopo havina milango na maji ya kutosha lakini tunaendelea na jitihada za kutafuta wafadhili wa kutujengea vyoo vya kisasa ili kuondokana na tatizo lililopo sasa.”

FikraPevu haikuishia hapo, ilifunga safari na kufika katika Shule ya Msingi Kijitonyama Kisiwani iliyopo katika Kata ya Kijitonyama, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo ilibainika kuwa suala la vyoo bado ni changamoto.

FikraPevu ilikutana na wanafunzi kadhaa ambao walieleza kukerwa na kuwepo kwa matundu machache ya vyoo.

Shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 950 ambao hutumia matundu nane tu ya vyoo. Shule hii pia haina uzio kuzunguka majengo ya shule.

Licha ya shule hiyo kuwa na upungufu wa vyoo, lakini upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya vyoo ni changamoto kwa sababu maji yako mbali na vyoo, hivyo huwalazimu wanafunzi kutumia “bidhaa zingine” ikiwamo karatasi chafu na ngumu, hasa za magazeti, kujisafisha baada ya kujisaidia.

“Tunatumia maji yaliyohifadhiwa katika matanki ambayo yako mbali kidogo na vyoo, na wakati mwingine wanafunzi huogopa kutumia maji hayo kwa sababu ni ya kisima na wakati wa kuyatumia huwa yanawasha” anaeleza mwanafunzi mmja wa darasa la saba.

FikraPevu ilibaini kuwepo kwa harufu kali na mbaya, inayozalishwa na vyoo vichafu visivyokuwa na maji ya kusafisha. Pia kulikutwa idadi kubwa ya nzi wanaozunguka na kutua ndani na nje ya matundu ya vyoo hivyo.

Katika shule hiyo, upo mtandao wa maji ya bomba, lakini umekaa kama mapambo, maana hakuna maji yanayoonekana kutiririka kwa muda mrefu.

“Hapa maji hakuna, mabomba unayoyaona hapa ni mapambo, yameshindwa kutoa maji kwa muda mrefu,” anasema mwanafunzi ambaye hatumtaji jina lake kwa sababu maalum.

Kama ilivyo kwa Shule ya Msingi Victoria, ambayo vyoo vyake havina milango ili kumsitiri mtumiaji, hali hiyo iko pia kwa Shule ya Kijitonyama Kisiwani.

Pia shule nyingi za Dar es Salaam, hazina sehemu maalumu ya wanafunzi kuosha mikono yao baada ya kumaliza kutumia vyoo.

Mbali na shida ya vyoo, shule nyingi za jiji hilo hazina vifaa vya kuhifadhi uchafu wala maeneo ya kuchomea taka.

Takwimu za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (2016) zinaonesha kuwa ni asilimia 38 pekee ya shule zina vyoo vya kutosha; asilimia 20 ya shule zote zina miundombinu ya kusambaza maji katika maeneo ya shule.

Pia chini ya asilimia 10 ya shule zote nchini zina vifaa vya kuoshea mikono na upatikanaji wa maji kuwawezesha wanafunzi kuwa na usafi binafsi na mazingira yanayowazunguka.

Taasisi ya HakiElimu katika tafiti zake inabainisha kwamba uhaba wa matundu ya vyoo ni changamoto inayozikabili shule nyingi za msingi hapa nchini hali inayosababisha wanafunzi, katika baadhi ya shule, kujisaidia kwa kupanga foleni na huku baadhi ya shule zikiwa hazina kabisa huduma ya choo na hivyo kulazimu wanafunzi kujisaidia vichakani.

Hata hivyo, Kamati za Shule zinaelezwa kuwa na wajibu wa kuhakikisha vyoo vinapatikana ili kuondoa changamoto ambazo zinawakabili wanafunzi katika suala zima la afya na mazingira.

Kwa muda mrefu sekta binafsi nayo imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa vyoo shuleni na shule nyingi zimenufaika na misaada hiyo.

Wasichana na wavulana wako katika hatari ya kuathirika kwa namna tofauti kwa sababu ya uhaba wa maji, hali mbaya ya usafi katika shule ambayo huchangia kukosekana kwa usawa wa kujifunza.

Kwa hali iliyopo sasa ambapo ni asilimia 38 ya shule zote nchini zina vyoo, je Tanzania tunaweza kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo 2030 (lengo la 4) na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu bora?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *