Saa 5 asubuhi napita mtaa wa Golani, kata ya Kimara katika jiji la Dar es salaam, watu wanaendelea na shughuli zao kuhakikisha uchumi unakaa vizuri.
Ni mtaa ambao shughuli za mama lishe na bodaboda zimeshika kasi, huku magari ya maji yakipita kusambaza maji kwa wakazi wa mtaa huo.
Hiki ni kiashiria kuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa maji katika mtaa huo, ambao haujafikiwa na maji ya bomba, badala yake wananchi wananunua maji yanayoletwa na magari yakiwa katika matanki makubwa.
Hali hiyo imewafanya kutenga bajeti kubwa ya maji kuliko mahitaji mengine ya nyumbani.
Peter Kasyupa, mkazi wa mtaa wa Golani anasema “tatizo la ukosefu wa maji limedumu kwa muda mrefu na tunalazimika kununua maji yanayoletwa na magari ambayo tunanunua kwa gharama kubwa ili kukidhi mahitaji ya familia zetu”. Anaongeza na kusema kuwa bajeti ya maji ni kubwa ikilinganishwa na shughuli nyingine.
“Kila wiki tunanunua lita 2000 za maji na kulipia shilingi 96,000 kwa maji yasiyo na chumvi ili kukidhi mahitaji yote ya familia lakini wakati mwingine tunanunua ya rejareja ambayo ndoo ya lita 10 inauzwa sh. 200” anaongeza mkazi huyo wa Golani.
Kwa nyakati tofauti wananchi wa mtaa huo, wamekuwa wakipaza sauti zao kwa serikali ili iwaletee maji ya bomba na kuwachimbia visima ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa maji. Kelele hizo zilimfikia rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2013 na kuagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kuchimba kisima katika mtaa huo ili kupunguza kero ya maji.
Wananchi walishirikishwa katika hatua zote za maradi wa kisima na walikubaliana kuchangia shilingi 60,000 kila mmoja ili kununua matanki ya kuhifadhia maji, mabomba na gharama za kuunganisha maji katika nyumba zao. Baada ya mradi wa kisima kukamilika maji yalianza kutoka yakiwa na chumvi nyingi na kuzua minong’ono kutoka kwa wananchi kwa sababu yalikuwa hayafai kwa matumizi ya nyumbani.
Mkazi mwingine ambaye alijitambulisha kwa jina la Gwankipya Mwaikinda alisema kuwa serikali ya mtaa iliwachangisha fedha hizo na kuwaunganishia maji ambapo maji yalitoka kwa miezi michache na tangu mwezi februari 2014 maji hayajatoka tena mpaka leo Fikra Pevu inatembelea mtaa huo.
“Wakati mradi umekamilika maji yalitoka takribani miezi 3 na baada ya hapo maji hayakutoka tena na tulipofuatilia suala hili kwa uongozi wa mtaa hatukupewa majibu ya kuridhisha mpaka leo hii”, anasisitiza mkazi huyo na kuongeza kuwa “ Maji yalikuwa na chumvi nyingi na hayakufaa kwa matumizi ya nyumbani”.
Hata hivyo, Fikra Pevu haikuishia hapo ilimtembelea Mwenyekiti wa mtaa wa Golani katika ofisi yake ili kufahamu undani wa maradi huo na jitihada zinazofanyika kutatua kero ya maji katika mtaa huo.
Laurent Mtoi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Golani alikiri kuwepo kwa mradi huo wa maji ya kisima na kusema kuwa “ Niliingia madarakani mwaka 2014 na kukuta mradi wa kisima lakini ulikuwa hautoi maji kwa sababu pampu ya kuvuta maji kutoka kwenye kisima iliharibika na matengenezo hayakufanyika” anaongeza kuwa alianza jitihada za kulifuatilia suala hilo kwa mamlaka husika ili kuwaondolea wananchi hadha ya maji.
Anasema kwa muda wa miaka miwili amekuwa akiyumbishwa na wahusika hao ambao ni Halmashauri ya Kinondoni. Baada ya kelele za muda mrefu, mwaka huu wa 2017 Halmashauri hiyo imeanza ukarabati wa miundombinu ya kisima hicho ili kuwarejeshea wananchi huduma ya maji ambayo imesimama takribani miaka miwili sasa.
“Mafundi toka Halmashauri walifika hapa wiki iliyopita na wameanza kukarabati miundombinu ya kisima na kufikia mwezi wa pili maji yataanza kutoka hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi wote, suala hili tunalifanyia kazi” anasisitiza Mtoi, Mwenyekiti wa mtaa wa Golani.
Pamoja na jitihada hizo, pia alifanikiwa kuchimba kisima kingine katika mtaa wake kupitia Ubarozi wa Kuwait nchini Tanzania ambaye alichimba na kuzindua kisima hicho mwaka 2015.
“Kutokana na mradi wa kwanza kutofanya kazi, nilipata msaada kutoka Ubalozi wa Kuwait mwaka 2015 ambao walituchimbia kisima kingine na sasa kinatoa maji ambayo yanasambazwa kwa wananchi wote wa mtaa wa Golani” Alisema Mwenyekiti Mtoi na kuongeza kuwa kwa kiasi kikubwa amepunguza tatizo la maji katika mtaa wake.
Ili kuhakikisha wananchi wa mtaa huo wanapata maji safi na yenye uhakika, Mwenyekiti Mtoi anasema wanaendelea na mazungumzo na Mamlaka ya Maji Safi na Taka Dar es salaam (DAWASCO) kuwaletea maji ya bomba ili wananchi waepukane kero ya uhaba wa maji.
“Mpaka sasa DAWASCO wametandandaza mabomba ya maji katika kata ya Kimara na muda si mrefu wataanza kuwaunganishia wananchi katika nyumba zao” aliongeza mwenyekiti huyo wa mtaa.
Licha ya DAWASCO kutandaza mambo bado maji hayajaanza kutoka katika mtaa huo na wananchi kuendelea kutaabika. Kwa upande wao DAWASCO wameendelea uboreshaji wa miundombinu ili kupunguza tatizo la maji ambalo linajitokeza katika maeneo mengi ya mkoa wa Dar es salaam.
Maji ya DAWASCO hupatikana kwa mgawo kati ya masaa 16 hadi 24 kwa wiki kutoka eneo moja hadi lingine ambapo uzalishaji wa maji katika mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini katika mto Ruvu kuhudumia wakazi wa Dar es salaam na Pwani.
Tathmini ya Hali ya watu na Afya ya mwaka 2010 (Demographic and Health Survey 2010); ni asilimia 4.8 tu ya kaya zilizopo vijijini ndiyo zinazopata maji katika eneo lao la kaya (water on premises) wakati ni asilimia 19.4 tu ya kaya kwa mijini ndizo zenye maji katika kaya zao