Anthony Diallo kidedea Uenyekiti wa CCM Mwanza

Sitta Tumma

WAZIRI wa zamani wa Maliasili na Utalii, na mbunge wa zamani wa Jimbo la Ilemela jijini Mwanza, Anthony Mwandu Diallo, ameibuka mshindi kwa kura 611 katika wa nafasi ya uenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, kisha kumgalagaza aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Clement Gregory Mabina.

Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa CCM Kirumba jijini hapa, ulionekana kuwashangaza baadhi ya wajumbe kutokana na kitendo cha baadhi ya wanafunzi wa kike kutoka katika shule ya Sekondari ya Bwiru ya Wasichana, kuachishwa masomo yao kisha kupewa jukumu la kuhesabu kura za wagombea.

Anthony Mwandu Diallo; Mwenyekiti mpya wa CCM mkoa wa Mwanza

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wana CCM na wananchi wa kawaida waliohudhuria uchaguzi huo, walisikika wakilalamikia kitendo cha wanafunzi hao waliokuwa wamevalia sare za shule hiyo, kuachishwa masomo yao shuleni kisha kupewa kazi hiyo ya kisiasa ya kuhesabu kura.

Mbali na hilo, ilidaiwa kuwepo kwa mchezo mchafu ambapo mmoja wa wagombea alidaiwa kutoa rushwa ya sh. 50,000 kwa kila mjumbe, kati ya wajumbe wanaokadiriwa kufikia 988, na kwamba inadaiwa kigogo huyo alitumia zaidi ya sh. Milioni 56 kwa lengo la kutafuta ushindi wa nafasi mojawapo zilizokuwa zikiwaniwa.

Mbali na Diallo, wagombea wengine wa nafasi ya uenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, waliotangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na Bunge, William Lukuvi ni pamoja na Zebedayo Athumani (4), Hussein Mashimba (15), Joseph Langula Yared (30), na Mabina ambaye alipata kura 328 kati ya kura zote 988 halali zilizopigwa.

Awali, wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi walijikuta wakilipuka kumshangilia kwa nguvu kubwa aliyekuwa Waziri wa Naishati na Madini na mbunge wa jimbo la Sengerema, William Ngeleja, baada ya jina lake kutajwa kuwa mwenyekiti wa muda wa uchaguzi huo.

Uchaguzi huo ulifanikiwa pia kuwachagua wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mwanza, ambapo waliochaguliwa na wilaya wanazotoka kwenye mabano kuwa ni Mwamba Makune na Christine Mwalu Jilala (Misungwi), Joseph Langula Yared na Marco Mabihya (Sengerema), Stella Aya, Raban Mageje (Magu).

Wengine ni Angelina Mabula, Dede Swila (Ilemela), Sikitu Sanziyote na Charles Marwa Nyamasiriri (Nyamagana), George Nyamaha na Benadethar (Ukerewe), huku wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mwanza wilaya Kwimba waliochaguliwa ni Bujiku Philip Sakila na Dominic Kadaraja.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *