Imeelezwa kuwa mipango mingi ya serikali inakwama kutokana na kutopatikana kwa takwimu sahihi za maendeleo zinazokusanywa na kuhifadhiwa na taasisi zilizopewa mamlaka kisheria kutoa takwimu za taifa.
Takwimu na taarifa sahihi zinahitajika katika mipango na matumizi ya rasilimali za serikali pamoja na mashirika ya kimataifa. Lakini malengo ya taasisi hizo hayafikiwi kutokana na takwimu za sekta husika zinazokusanywa hazikidhi vigezo vya kimataifa na wakati mwingine huchelewa kutolewa katika mamlaka husika.
Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Albina Chuwa wakati akizungumza katika Kongamano la Kimataifa la Takwimu za Malengo ya Maendeleo Endelevu (ICSDGS) nchini Ufilipino amesema hifadhi nyingi za takwimu hazina ubora ambapo ni kikwazo katika utekelezaji wa mipango ya utawala licha ya kuwepo kwa juhudi nyingi zinazofanyika ili kukusanya takwimu sahihi katika ngazi ya kitaifa.
“Kutokukamilika na kukosekana kwa usahihi wa hifadhi za takwimu ni kikwazo kikubwa katika uzalishaji wa data za utawala. Hali hiyo hupelekea kucheleweshwa kwa mchakato wa upatikanaji wa taarifa za mipango na kutishia ubora wa takwimu zinazotolewa kwenye vyanzo”, amesema Dkt. Chuwa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi wahisani ambazo zimesaini makubaliano ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s-2030), ili kuhakikisha malengo hayo yanatekelezeka zinahitajika takwimu na taarifa sahihi za watu na rasilimali zilizopo na kuziwezesha mamlaka husika kusimamia na kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Uwekezaji mdogo na kukosekana kwa utashi wa kisiasa katika taasisi za ukusanyaji wa takwimu katika nchi za Afrika unakwamisha upatikanaji wa takwimu kwa wakati na zenye ubora. Viongozi wengi wa Afrika hawataki kutoa taarifa sahihi za hali ya jamii zao.
“Uwezo wa wafanyakazi kujaza fomu, kupitia ubora na kuchambua takwimu katika wizara, idara na wakala hauridhishi. Ukosefu wa utashi wa kisiasa katika mipango umechangia kupunguza mchakato wa kuboresha takwimu katika nchi zinazoendelea”, amesema Dkt. Chuwa na kuongeza kuwa,
“Utashi wa kisiasa katika uzalishaji wa takwimu za utawala bado haujasisitizwa. Kutenga rasilimali, kujenga uwezo na maendeleo ya watu yanahitaji utashi wa kisiasa”.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Albina Chuwa
Inaelezwa kuwa mfumo mzuri wa ukusanyaji wa taarifa na takwimu katika nchi unapunguza gharama za kufanya tafiti za mara kwa mara na kutengeneza takwimu kwa wakati. Lakini matumizi sahihi ya teknolojia ya kisasa yatasaidia ukusanyaji na uhifadhi wa takwimu nyingi ili zitumike kwa muda muafaka.
Ofisi ya Takwimu kupitia mpango kazi wa maendeleo ya Takwimu imeamua kuachana na kusajili taarifa za watu kwa kutumia karatasi na sasa wanatumia Mfumo wa kielektoniki (Electronic Population Registry). Maboresho hayo yanatajwa kuwa ni hatua muhimu katika upatikanaji wa taarifa kwa wakati na zenye uhakika.
Kulingana na Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 inaipa nguvu Ofisi ya Taifa ya Takwimu kusimamia, ukusaji, uhifadhi na kuzitafsiri takwimu zinazopatikana nchini. Pia kuhakikisha takwimu zinazotolewa na taasisi au watu binafsi ni sahihi na zinakidhi matakwa ya kisheria ili kuepuka upotoshaji wa hali halisi ya wananchi.
Hivi karibuni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliingia matatani kwa kutoa takwimu za hali ya uchumi na ukusanyaji wa mapato zinazotofautiana na zile zilizotolewa na serikali. Zitto alisema hali ya uchumi sio nzuri kwasababu uchumi umesinyaa na biashara nyingi zimefungwa kutokana na kodi kubwa inayotozwa na serikali.
Siku chache baada ya tamko lake, Ofisi ya Takwimu ilijitokeza kukanusha madai ya Zitto. Lakini aliendelea kushikilia msimamo wake ndipo alipotiwa nguvuni na polisi kwa madai ya kupotosha takwimu za serikali.