Uhalifu Mara kuondoka kwa maamuzi ya wananchi

Mkoa wa mara ni mkoa ulio katika kanda ya ziwa unaoundwa na wilaya sita ambazo ni Serengeti, Butiama, Rorya, Tarime, Bunda na Musoma mjini. Mkoa huu umebarikiwa kuwa na rasilimali mbalimbali zinazouwezesha mkoa kujipatia kipato kama vile madini, hifadhi ya wanyama, uvuvi pamoja na uwepo wa mpaka unaoiunganisha Tanzania na nchi ya jirani ya Kenya pamoja na vyanzo vingine ambavyo havikutajwa hapa kama vile kilimo.

Pamoja na kuwepo kwa fursa za uchumi kama hizo mkoa huu bado unakabiliwa na changamoto ya uhalifu ambao hupelekea mkoa huu kupoteza sifa ya uzuri wake na kubeba sifa na sura mbaya miongoni mwa wana jamii na nje ya mkoa huu.

Uhalifu unaofanyika sana katika mkoa huu ni pamoja na mauaji ya kikatili hasa kwa akina mama, ukatili wa kijinsia, wizi na unyang’anyi wa kutumia silaha, makundi ya vijana wadogo kujeruhi na kukaba watu na mengine kadha wa kadha.

 Matukio haya yamesababisha wananchi kuishi kwa hofu na kuwaza usalama wao huku waathirika wakuu wakiwa ni akina mama ambao wamekuwa wakikumbwa na mauaji ya kikatili huku yakihusishwa na imani za kishirikina, wafanya biashara, waendesha pikipiki (bodaboda).

Katika makala hii tunaangalia hali ilivyo kwa sasa katika manispaa ya Musoma baada ya sintofahamu hii kwa jamii.

Hali ilivyokuwa kipindi cha nyuma

Mwaka 2012 kurudi nyuma hali ilikuwa tete kwa baadhi ya maeneo katika manispaa hii ya Musoma.Maeneo ambayo yalikithiri kwa uhalifu ni Nyakato, Kwangwa, Kigera na Kiara. Matukio ya kuvamia kupora na kuiba kisha kuua au kujeruhi yalikuwa na kasi sana.

“Hali ni mbaya sana yaani ukiacha vibaka wanaotusumbua usiku sasa ni hofu juu ya hao wauaji wanaoua wanawake, amani hakuna kabisa. Majuzijuzi hapa wameua binti wa shule ya sekondari” alisema Bi. Bukehere Changwe mkazi wa Kwangwa.

Matukio ya kuuawa wanawake yamekuwa yakitokea mara kwa mara na yamekuwa yakihusishwa na imani za kishirikina kwani baadhi ya viungo vya mwili hunyofolewa baada ya mauaji. Wauaji hawa wamepewa jina la makhirikiri.

Kundi jingine la watu wanaoathirika ni waendesha pikipiki . Hubeba abiria ambaow akati mwingine wanawageuka.

Malindi ambaye ni dereva wa bodaboda mjini musoma anasema kufanyakazi hiyo kwa sasa kunataka moyo kutokana na matukio ya mauaji na uporwaji wa pikipiki.

Mbali na matukio haya ya kuuawa kwa wanawake, uporaji, unyanganyi, wizi na uvamizi nyakati za usiku pia ni tatizo kubwa katika manispaa hii ya Musoma. Wezi au vibaka huvamia nyumba au sehemu ya biashara na kuchukua wanachotaka kisha kuua au kujeruhi.

“Mimi nina duka maeneo ya Nyakato kwa Saanane, tumewahi kuvamiwa mara mbili dukani na wakabeba kila kitu ila tulijikongoja tukaendelea na biashara, baadae kundi la watu lilivamia nyumbani kwangu na kumuua mume wangu akiwa anaingia nyumbani toka katika mizunguko yake na kisha kunijeruhi mimi” alisema Bi Martha Machunde ambae ni mfanya biashara wa duka.

Wananchi wamekuwa wakitupa lawama zao kwa jeshi la polisi kuwa halifanyi kazi ipasavyo kutokana na kutofika katika tukio kwa wakati na pia kutofanya doria katika maeneo ambayo ni hatari zaidi.

Katika mahojiano na Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Bwana Ferdinand Mtui, amesema kukithiri kw amatukio hayo kunatokana na jamii kutoshirikiana na polisi katika kuhakikisha usalama upo.

“Ni kweli tunapata malalamiko kama hayo lakini kumbuka idadi ya askari ni ndogo kuliko idadi ya watu wanaotakiwa kulindwa, kwa kawaida askari mmoja analinda wananchi 1,050 kwa hiyo bado hawatoshi, askari anaweza kuwa katika maeneo hayo na pakatokea uhalifu hivyo bila msaada wa wananchi wenyewe inakuwa ngumu”

Bi Perusi Masokomya, mwenyekiti wa mtaa wa Kiara anasema baada ya kuona dhiki iliyopo aliungana na viongozi wenzake kuitisha vikao ili kuhamasisha wananchi kuona faida ya ulinzi hivyo walichagua kamati 3 za kisheria ambazo ni kamati ya ulinzi na usalama, kamati ya huduma za jamii na shughulu za kujitegemea pamoja na kamati ya fedha uchumi na mipango.

“Baada ya kutokea maafa yaliyopewa jina la “Mugaranjabo” huko Buhare ambayo yaliua watu 17 na kujeruhi wengine yalishtua wananchi na viongozi hivyo mafunzo mbalimbali kwa viongozi yalitolewa katika kata ya Kigera yakihusisha Madiwani, Wenyeviti wa serikali za mtaa, Watendaji wa kata na mitaa, Wataalamu na wakuu wa idara, Viongozi wa vyama vya siasa na wengineo ambapo mafunzo hayo yaliongozwa na Afande Ntobi”

Hali ilivyo kwa sasa

Kwa matukio haya na mengineyo yalipelekea baadhi ya viongozi na jeshi la polisi kuumiza vichwa ni namna gani wataweza kupunguza kama si kutokomeza kabisa uhalifu katika manispaa hii ya Musoma vongozi hao walikuja na dhana ya ulinzi shirikishi njia ambayo ilionekana kuwa nzuri zaidi.

Mkuu wa wilaya ya musoma Bwana Jackson Msome alitoa agizo la kila mtaa/kata kuitisha mikutano mbalimbali ya kikanda na yeye kutoa ajenda ya ulinzi na usalama, kwa mfano mnamo tarehe 3/1/2013 aliitisha kata ya Buhare, Kigera na Nyamatare na kuagiza wenyeviti wa Mitaa kufanya mikutano ya ulinzi na usalama. Hakuishia hapo katika ufuatiliaji alikuwa akituma wajumbe wake kufuatilia kama zoezi hilo linafanyika tena kwa usahihi.

Kuwepo ama kuanzishwa kwa dhana ya ulinzi shirikishi kuna tajwa kuwa njia nzuri ambayo inasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza uhalifu mtaani kwani ulinzi huu unahusisha vijana ndani ya mtaa ambao hulinda usiku kucha.

Ushauri

Kwa hakika naweza sema kuwa jeshi la polisi linafanya kazi yake japo si kwa asilimia mia, ila mtetezi mkuu wa amani ni mwananchi mwenyewe.

 Kuna maeneo mengine jiografia yake si nzuri namaanisha maeneo ambayo ni skwata hata gari la polisi kupita ni tabu hivyo bila sisi wananchi kuwa mlinzi wa mwenzako tutaisha, nina imani wahalifu tunawajua ila tunaogopa kuwataja sasa ifike mahali tuuvue uoga na kupambana ili tuweze kupunguza matukio haya.

Lakini polisi pia waonyeshe mfano japo mzuri katika uwajibikaji wao japo kwa kuhukumu na kutoa adhabu kwa wavunjifu  wa amani (wahalifu) Naimani kama kila mmoja wetu akiwa mlinzi wa mwenzake na tukishiriki vizuri huu ulinzi shirikishi tutafanikiwa sana kupunguza kwani askari hawezi kulinda mtu mmoja mmoja.

Nakuu usemi usema “Local problem needs local solution” kwa maana hiyo hatima ya usalama wetu uko mikononi mwetu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *