Uharamia kikwazo cha Maendeleo kwa wavuvi

Editha Karlo

UHARAMIA unaofanywa ndani ya Ziwa Tanganyika umekuwa ni kikwazo cha maendeleo kwa wavuvi na wamiliki wa mali za uvuvi katika Ziwa Tanganyika na kusababisha wavuvi watumie zana duni za uvuvi ambapo zinachangia kushuka kwa kiwango cha mapato yao.

Wakiongea nami, wadau wavuvi katika mialo ya Kibirizi na Katonga pembeni mwa  Ziwa Tanganyika walilalamikia vitendo hivo vya uharamia  wanavofanyiwa mara kwa mara wanapokuwa ziwani ikiwemo kuporwa zana zao za kisasa za uvuvi na hata baadhi ya wavuvi kuuwawa.

Mikidadi Habona ni mmiliki wa boti za uvuvi katika mwalo wa kibirizi alisema kuwa mara nyingi wavuvi wanapokuwa ziwani katika shughuli zao za kuvua wamekuwa wakiporwa zana zao za uvuvi za kisasa ambazo ni kama mashine za boti (mitumbwi), nyavu, kamba, mipira ya kuendeshea mashine na maelfu ya lita za mafuta.

”Kwa hali hiyo ndugu mwandishi hivi sasa wavuvi wengi wameshaanza kukata tamaa ya kununua zana za kisasa za uvuvi kwani ukinunua leo kesho ukienda Ziwani unaporwa, sasa tutaendelea kuwanufaisha hawa maharamia hadi lini? Sababu kila tukinunua wao wanatuvamia na kuchukua vifaa vyetu kama vyakwao vile” alisema  Habona.

Kwa upande wake wake Mwenyekiti wa wavuvi katika mwalo wa Kibirizi Issa Kanyongo alisema kuwa uharamia unaondelea kufanywa ndani ya ziwa Tanganyika ni kikwazo cha maendeleo kwa wavuvi na wakazi wa mkoa wa Kigoma kwani hali hii inachangia sana wavuvi kuendeea kutumia zana duni za uvuvi hivo husababisha kuendelea kuwa maskini.

”Matukio ya mara kwa mara yanayotokea ndani ya ziwa Tanganyika yanachangia sana kutusababishia sisi wavuvi kuendelea kuwa maskini kwani hata tukinunua zana za kisasa ili tuweze kujikomboa na hali ya umasikini baada ya muda mfupi tu tunavamiwa na maharamia ziwani nakutupora zana hizo” alisema Kanyongo

Mwenyekiti huyo alisema wananchi wanaoishi vijiji vya jirani na Ziwa Tanganyika Kalemei na Uvira  ambavyo zipo katika nchi ya Congo DRC ndiyo wamekuwa wakifanya uharamia ndani ya Ziwa Tanganyika kwa kuwapora  mali zao za uvuvi mara kwa mara.

Aliiomba serikali ya Mkoa wa Kigoma iweke ulinzi madhubuti ndani ya Ziwa Tanganyika ili kusaidia kukomesha vitendo hivo viovu visiendeelee kutokea tena ndani ya Ziwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *