Tanzania kama zilivyo nchi nyingine za Afrika hutegemea misaada na mikopo kutoka katika nchi zilizoendelea ili kujiendesha kiuchumi na kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.
Kutokana na kuwa na rasilimali mbalimbali wawekezaji toka nje huitumia fursa hiyo kutoa misaada na kujipatia malighafi kwa ajili ya viwanda vilivyopo katika mataifa yao. China ni miongoni mwa mataifa ambayo yamewekeza rasilimali nyingi Afrika ambapo hali hiyo inatishia kuligeuza bara hilo kuwa koloni la taifa hilo lenye nguvu kubwa ya kiuchumi na kijeshi.
Kulingana na ripoti ya Shirika la Misaada la China (ChinaAID-2016) linathibitisha kuwa mafungamano ya China na nchi za Afrika ni makubwa na kuifanya nchi hiyo kuwa na sauti katika maamuzi muhimu ya rasilimali za nchi husika.
Inaelezwa kuwa uwekezaji wa China kwa Afrika ambao unapitia kwa njia za misaada, mikopo na miradi mbalimbali unatazamwa na wananchi wengi kama ni wenye manufaa licha ya kuwepo kwa tahadhari zinazotolewa na nchi za Magharibi kuwa nia ya China ni kuzinyonya nchi za Afrika.
Jarida la Kimataifa la Brookings linaeleza kuwa China inatoa aina 8 za misaada ambayo ni miradi iliyokamilika, bidhaa na malighafi, msaada wa kiufundi, rasilimali watu, matibabu, huduma za dharura za kibinadamu, programu za kujitolea na msamaha wa madeni.
Misaada ya China kwa Afrika imejikita katika sekta za kilimo, elimu, usafiri, nishati, mawasiliano na afya. Kwa mujibu wa wasomi wa China tangu mwaka 1956, China imetoa miradi na misaada 900 kwa nchi za Afrika ikiwemo viwanda vya nguo, vituo vya uzalishaji umeme, viwanja vya mpira, hospitali na shule.
Pia Angola ndio nchi ya kwanza kupokea misaada mingi kutoka China na kuanzia 2000 imepokea zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 12, ikifuatiwa na Sudan, Ghana na Ethiopia ambazo zimepokea Dola bilioni 10 kila moja katika kipindi hicho.
Mwaka 2013 pekee China iliwekeza zaidi ya Dola bilioni 2.17 katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo sekta za uzalishaji, uchukuzi, nishati, madini, usafiri, mawasiliano na utalii.
Kutokana na China kupiga hatua kubwa katika sekta ya mawasiliano hasa matumizi ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii, imeifanya nchi hiyo kupata soko la uhakika katika nchi za Afrika ambazo zinakabiliwa na changamoto za teknolojia duni ya mawasiliano.
Lakini nchi hizo zimeonywa kuwa makini na uwekezaji wa China katika sekta ya mawasiliano ikizingatiwa kuwa sera zake zinalenga kudidimiza uhuru wa vyombo vya habari na haki ya faragha. China inajaribu kupenya katika maeneo ya vijijini kuhakikisha wananchi wanapata taarifa zinazohusu nchi yao na utamaduni wake na kuzuia jitihada zozote za watu kutoa maoni yaliyo kinyume na maslahi ya nchi hiyo.
Miundombinu ya Mawasialino ya China inawezesha Kudukua na kudhibiti taarifa
Hivi karibuni Kituo cha Kimataifa cha Usaidizi wa Vyombo vya Habari (CIMA) katika moja ya taarifa zake kimeeleza kuwa ukuaji wa uwekezaji wa mawasiliano wa China duniani unatishia faragha ya watumiaji. Kadiri mfumo wa mawasiliano unavyokuwa katika nchi za Afrika kupitia misaada ya China imekuwa ni rahisi kutambua hatari inayoweza kutokea katika vyombo vya habari vya bara hilo.
Taarifa za chombo kimoja cha habari cha Zambia kijulikanacho kama Zambian Watchdog zinaeleza kuwa Kampuni ya China ya Huawei imefunga vifaa maalumu vya udukuzi kwa watoaji wa huduma za intaneti (Internet Service Providers). Hatua hiyo ilifikiwa mwaka 2013 kutokana na agizo la rais wa zamani wa nchi hiyo, Michael Sata kuingilia mawasiliano ya simu na intaneti ya wananchi wake.
Inaelezwa kuwa serikali ya Zambia iliwasiliana na wataalamu kutoka China ambao walifunga vifaa hivyo vya udukuzi ili kusimamia, kudhibiti na kukusanya taarifa za mawasiliano ya kijiditali. Huawei ni miongoni mwa kampuni kubwa Afrika zinazotengeneza simu ambazo hutumia na watu wengi.
Hali hiyo pia imeanza kujitokeza Tanzania ambapo mikakati ya kuthibiti mawasiliano ya watu na vyombo vya habari inaendelea. Hivi karibuni serikali ya Tanzania ilifanya mkutano maalumu na wataalamu kutoka China jijini Dar es Salaam ili kuiwezesha serikali kuthibiti taarifa za watumiaji wa mitandao ili kuwaepusha na uharifu wa mtandao.
Lengo hasa ni kuwa na uwezo wa kuingilia mawasiliano ya wananchi ambao wanaonekana kuwa na maoni tofauti na viongozi waliopo madarakani. Na njia rahisi kuwathibiti ni kuingilia mawasiliano yanayofanyika kupitia simu na mitandao.
Hata hivyo serikali ilipitisha Sheria ya Makosa ya Mtandao (The CyberCrime 2015) ili kudhibiti uharifu wa mtandaoni. Lakini hivi karibuni imekuja na Kanuni mbili za kusimamia Maudhui ya Mitandao ya Kijamii na Utangazaji wa vituo vya redio na runinga (TV), ambapo sheria hizi zinatajwa kama mkakati wa kuminya uhuru wa watu kujieleza na kupata taarifa.
Kama hiyo haitoshi, kuna tetesi kuwa utungaji wa kanuni nyingine ya kulinda faragha na usalama wa watumiaji iko mbioni kupitishwa, lakini lengo lake ni kudhibiti na kusimamia mawasiliano ya watu ambayo yanadhaniwa kuhatarisha maslahi ya baadhi ya watu walio katika madaraka.
Mwaka 2016, kiongozi mmoja mwandamizi wa serikali alinukuliwa na vyombo vya habari akisema “Natamani malaika ashuke azime mitandao ya kijamii, irudi baada ya mwaka 1 ikute hatua kubwa za kimaendeleo tulizopiga”.
Baada ya kauli hiyo hatua mbalimbali zilianza kuchukuliwa ikiwemo kufungia magazeti yenye mawazo tofauti na watawala. Magazeti yaliyofungiwakatika uongozi wa awamu hii ya tano ni Tanzania Daima, Raia Mwema, Mawio, MwanaHalisi na Mseto. Radio na TV nazo ziko shakani kutokana na kuandaliwa kwa Kanuni mpya ya Utangazaji.
Udukuzi wa taarifa kwenye simu
Mabadiliko ya mfumo wa utangazaji kutoka Analojia – Dijitali
Uwekezaji wa maendeleo ambao China umewekeza Afrika ni kufadhili mabadiliko ya mfumo wa utangazaji wa runinga kuelekea mapinduzi ya dijitali. Wajenzi wa miundombinu ya mawasiliano kutoka China wamekuwa wakitoa huduma bora na zinazofikisha matangazo ya runinga hata katika miji midogo ambayo teknolojia ya dijitali ilikuwa haipatikani.
Inaelezwa kuwa Mfuko wa Maendeleo wa China na Benki ya Maendeleo ya China zilitoa fedha nyingi kufadhili uhamaji huo wa dijitali. Mfano China iliikopesha jimbo la Kaduna nchini Nigeria Dola milioni 30.6 kuwezesha mji huo kupata matangazo ya TV yenye ubora wa hali ya juu.
Kwa Tanzania, mchakato wa kuhamia katika mfumo wa dijitali ulianza 2005 na ilipofika 2010 serikali ilitoa leseni kwa kampuni 3 ikiwemo Startimes kutoka China kujenga miundombinu ya utangazaji wa dijitali na mpaka sasa tumefanikiwa kuingia katika mapinduzi ya dijitali.
Kupitia kampuni ya Startimes inatoa huduma ya ving’amuzi ambapo inaweka zaidi maudhui kutoka China ambayo yanapatikana kwa bei rahisi ikilinganishwa na yale ya nchi za Magharibi. Mfumo huo unatafsiriwa kama njia mojawapo ya China kuimarisha diplomasia katika nchi za Afrika na kuthibiti maudhui ya vyombo vya habari.
Licha ya sekta ya mawasiliano kupata uungwaji mkono wa China, nchi za Afrika zimeshauriwa kuwa makini na sera za mawasiliano za China ambazo zinakuja na misaada ambayo ina lengo la kuminya uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari.