Uhusiano wa Marekani na Urusi: Trump, Putin wanauficha nini ulimwengu?

Jamii Africa

UHUSIANO wa Rais wa Marekani, Donald Trump na mwenzie wa Urusi, Vladimir Putin, umegubikwa na siri nzito.

Katika mazungumzo yao ya Jumamosi – wiki iliyopita, kwa njia ya simu, Rais Trump, alivunja utaratibu uliozoeleka kwa viongozi wakuu wa Marekani, kusikiliza na kufuatilia kinachozungumzwa baina ya kiongozi wao na viongozi wengine wa nje.

Hali ilikuwa tofauti katika mazungumzo hayo, kwani Rais Trump, licha ya kushindwa kuwaalika washauri wake wakuu; hasa mwanasheria mkuu, waziri wa mambo ya nje na wakuu wa vyombo vya usalama, alizima kabisa njia yoyote, ya mtu mwingine kusikia kilichokuwa kikizungumzwa.

Taarifa zinaeleza kwa Rais Trump, aliamuru pia kutorekodiwa kwa mazungumzo yake na Rais Putin.

“Viongozi wakuu wa Marekani wamekuwa na utaratibu wa kujua na kufuatilia kinachozungumzwa na rais wao na viongozi wa nje, lakini Rais Trump, ameamua kuwaweka kando wote,” amelalamika Ian Berman, Makamu wa Rais wa Kamati ya Sera za Nje wa Marekani (AFPC).

Berman alisema usiri huo wa waliyozungumza Trump na Putin, huenda hauna nia nzuri na Marekani na watu wake. Taariza zaidi zinadai kuwa hata picha iliyopigwa ndani ya ofisi ya Rais Trump, kuwa na wasaidizi wake wa karibu, huenda ilichukuliwa kabla ya mazungumzo hayo kuanza.

Ikulu ya Marekani (White House) baada ya mazungumzo hayo ilitoa taarifa ya aya moja tu, ikieleza kwamba Rais Putin alimpigia simu Rais Trump kumpongeza kwa ushindi na kuapishwa kwake kuwa kiongozi wa taifa kubwa duniani.

Hata hivyo, Ikulu ya Urusi ilitoa taarifa ya kurasa 10 ikieleza namna viongozi hao wawili walivyozungumza juu ya kuimarisha uhusiano kwa faida ya nchi zao na watu wake. Haikueleza Zaidi na inaelezwa kuwa ilijaa maneno ya kujirudiarudia.

Mazungumzo hayo ya saa moja tayari yamezua mijadala katika vyombo vya habari, hasa mitandao ya kijamii. Wachangiaji wengi wamelaani usiri huo na kuuita – “hauna afya kwa Marekani.”

Kumekuwepo na taarifa kwamba Rais Putin alisaidia sana ushindi wa Trump katika uchaguzi mkuu wa Marekani, huku ikielezwa kuwa Urusi ilisadia udukuzi na hujuma zingine katika uchaguzi huo. Bado uchunguzi wa suala hili unaendelea. Katika uchaguzi huo, Trump kutoka chama cha Republican, alimshinda mshindani wake wa karibu, Hillary Clinton wa Democratic.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *