Ugomvi wa Kiir na Machar unavyoisambaratisha Sudan Kusini

Jamii Africa

Sudan Kusini ni nchi changa iliyojipatia uhuru wake miaka michache iliyopita na kuwa taifa huru lenye mamlaka kamili ya kisiasa na kiuchumi. Nchi hiyo  ilitangaza uhuru wake tarehe 9 Julai 2011 na kuwa nchi ya 54 Afrika na 193 duniani na kujitenga rasmi na nchi ya Sudan ambayo imekuwa na migogoro ya kisiasa muda mrefu.

Utengano huo ulitokana na ukweli kuwa Sudan ina wakazi wengi ambao ni Waislamu na wenye kufuata tamaduni za Kiarabu, wakati huohuo wakazi wengi wa Sudan Kusini ni Wakristo na wanaofuata mila za jadi. Mgongano huo wa kidini na kisiasa ulisababisha mizozo isiyoisha, kila upande ukitaka kutimiza matakwa yake na kudharau dini nyingine.

Lakini kiuchumi na kielimu nchi hiyo iko nyuma ikilinganishwa na Sudan ambapo mgawanyo wa rasilimali hasa mafuta haukuwa wa haki na usawa na kusababisha upande mmoja kutofaidika na utajiri uliopo katika eneo hilo la Afrika.

Kutokana na hali hiyo tete ya kisiasa ambayo iliharibu uhusiano wa nchi hizo mbili ambapo hapo awali Sudan Kusini ilikuwa ni  moja ya majimbo ndani ya Sudan, ikawalazimu wananchi wa Sudan Kusini kupiga kura ya kujitenga na Sudan mnamo Januari 2011. Na matokeo yake wananchi wengi wa Sudan Kusini walipendekeza kujitenga na miezi michache nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake.

Lakini ikumbukwe juhudi zote hizo ziliongozwa na raisi wa kwanza wa nchi hiyo Dkt. John Garang ambaye aliliongoza kundi la wanamgambo lijulikanalo kama Sudan People’s Liberation Army (SPLA) mwaka 1983 kupigania uhuru wa nchi hiyo baada ya Sudan kutangaza kuwa nchi ya kiislamu. Pamoja na harakati hizo, nchi hiyo iliingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Vita hivyo viliisha mwaka 2005 kwa mkataba wa amani uliocha Kusini kama sehemu ya kujitawala ndani ya Sudan hadi ilipopigwa kura ya kujitenga. Nchi imeathiriwa vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya SPLA ambavyo vilidumu kwa miaka 21.

Agosti 1 mwaka huohuo John Garang alifariki baada ya ndege ya rais wa Uganda aina ya helikopta Mi-172 aliyokuwa akisafiria kuanguka katika mojawapo ya milima iliyoko kusini mwa Sudan.

Baada ya kifo cha Garang majeshi ya Sudan Kusini na ‘South Sudan Defence Force’ (SSDF) yalisitisha uhasama wao na kuungana mnamo mwaka 2006 chini ya Azimio la Juba. SSDF ilianzishwa na Makamu wa Rais wa wakati huo wa Sudan Kusini, Dkt. Reik Machar  aliyefukuzwa na rais Salva Kiir baada ya kutoelewana katika masuala ya uongozi.

John Garang siku za uhai wake

Wakati huu tunashuhudia Sudan Kusini iliyoanza kustawi na kuimarika kiuchumi,  kutumbukia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya majeshi yanayomtii raisi Salva Kiir na Dkt. Reik Machar yaliyoanza  miaka minne iliyopita.

Vita hivyo vya ndani vimewaacha raia wa Sudan Kusini katika hali ya wasiwasi ikizingatiwa kuwa raia hao wamegharimika na kumwaga damu yao kuupata uhuru.  Lakini raia wengine wamekimbilia nchi za jirani, huku miundombinu ikiharibiwa vibaya na shughuli za kiuchumi kusitishwa.

Hatua hiyo ilifikiwa pale rais Kiir alipomvua wadhifa wa umakamu wa raisi Dkt. Machar Julai 2012, kwa madai kuwa makamu huyo alitangaza kugombea nafasi ya uraisi katika uchaguzi uliotarajiwa kufanyika mwaka 2015 ambapo angechuana vikali na raisi Kiir.

Duru za kisiasa zinasema kutokana na changamoto hiyo ya kiuongozi na malumbano yasiyoisha baina ya wawili hao, rais Kiir kulinda heshima yake alimfukuza kazi makamu wake ili ajipange vizuri kuendelea kukaa madarakani na washirika wake.

Hadi kufikia sasa, Dkt. Machar alikimbilia uamishoni Afrika Kusini lakini bado anaoongoza mapambano dhidi ya Kiir katika nchi yake. Kiir alimchagua James Wani Igga kuwa Makumu Rais na Taban Deng Gai kuwa Makamu Rais wa kwanza.

Licha ya mabadiliko hayo bado Sudan Kusini haijapata muafaka wa kisiasa. Kulingana na ripoti ya Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR-2017)inaeleza kuwa zaidi watu 2.7 wameikimbia nchi hiyo na kwenda mataifa ya jirani kutafuta hifadhi, huku wengine wakibaki kuwa wakimbizi wa ndani.

Shirika hilo linasema zinahitajika Dola za Kimarekani bilioni 1.4 ili kukagharimia mahitaji ya chakula, maradhi, maji na huduma za afya kwa wakimbizi waliopo nje ya Sudan Kusini ambao wanafikia million 1.8. Wakimbizi hao wanapatikana katika nchi za Uganda, Kongo DRC, Sudan, Kenya, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kwa upande wake mchambuzi wa siasa ya Afrika na Mashariki ya Kati, Ahmed Rajab katika safu yake iliyoitoa katika gazeti moja  hapa nchini anasema mapigano yalipozuka mjini Juba kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir  na Dkt. Reik Machar vyombo vya habari vikayaelezea mapigano hayo kuwa ni ya kikabila. Sababu yao kubwa ni kuwa Kiir ni Mdinka na Machar ni Mnuer.

Anasema ingawa mzozo huo ulichukuwa sura ya kikabila chanzo chake ni tofauti za kisiasa za mahasimu hao wawili ambapo Machar anaungwa mkono na mjane wa John Garang kiongozi muasisi wa vuguvugu la kupigania Sudan ya Kusini (SPLA). Rebecca ni Mdinka kama Kiir.

Anaongeza kuwa Wadinka na Wanuer wamekuwa mahasimu tangu jadi na jadi. Daima wamekuwa wakizozana kuhusu ardhi na wakiibiana ng’ombe. La ajabu ni kwamba makabila yao mawili yamekuwa na uhasama mkubwa  licha ya kwamba yana mila zinazofanana sana na tamaduni zao zinalingana.

“Wadinka wa Bor wanawaogopa watu wa kabila dogo la Murie ambao raha yao ni kuyavamia mazizi ya ng’ombe ya Wadinka karibu na mji wa Bor. Wadinka siku zote wanakashifu Wanuer kwa kusema kwamba ni wakali, wanakasirika mara moja na Wanuer kuwa ni vichaa” anasema Rajab.

Mchambuzi huyo anasema Wadinka wanadai kwamba hawasahau aliyoyafanya Machar mwaka 1991. Mwaka huo Machar aliparurana na Garang na Kiir akawaacha  mkono na kuunda vuguvugu lake ambalo liliungwa mkono na watu wa kabila lake.

Baadaye Machar akawa anashirikiana na serikali ya Khartum ili kuwadhohofisha akina Garang na Kiir na chama chao cha SPLM.

Lakini mwaka 2002 Machar akapatana na Garang na Kiir na kurudi katika chama cha SPLM  na kuteuliwa kuwa kamanda mkuu wa jeshi la Sudan Kusini. Alipofariki Garang Machar akawa makamu wa rais huku Kiir akiwa rais wa nchi hiyo.

Rais Salva Kiir (Kushoto) akiwa na Reak Machar kabla ya Makamu huyo wa rais kuondolewa

katika nafasi yake

Kwa uchambuzi huo wa Ahmed Rajab, utagundua wazi kwamba ukabila unahusishwa na siasa, na matokeo yake taifa hilo kutotengamaa na kustawi kiuchumi. Taifa lolote ambalo halitengenezi maridhiano ya kisiasa na watu wake wakaendelea kupigania haki za makundi yao ni vigumu kusimama na kujenga uchumi imara.

Pamoja na mzozo huo nchi wapatanishi za jumuiya ya Maendeleo ya Pembe ya Afrika (IGAD) yalianzisha mazungumzo ya kuzipatanisha pande zote mbili, ambapo mazungumzo yalifanyika Ethiopia makao makuu ya Umoja wa Afrika. Mazungumzo hayo yanaendelea lakini mwafaka bado haujapatikana.

Ni muhimu mahasimu hao wafahamu kuwa wanaoumia ni wananchi na sio viongozi, hivyo maridhiano yanahitajika haraka ili kujenga taifa hilo changa ambalo limekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe zaidi ya miaka 21. Mstakabali wa Sudan ya Kusini uko mikononi mwa wananchi wake.

Umoja na mshikamano ndio silaha pekee ya kufikia maendeleo endelevu,kwa sababu mataifa makubwa yanapigania kuungana ili kutumia rasilimali zilizopo katika nchi zao ili kutengeneza mstakabali mzuri wa raia.

Kuna haja ya viongozi wa Sudan Kusini kuliona hili ikizingatiwa kuwa nchi hiyo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ukabila na urasimu wa madaraka ukiwekwa kando utachagiza mwafaka baina ya pande mbili hasimu na kuliweka taifa hilo katika sura mpya mbele ya diplomasia ya kimataifa ambalo lina utajiri mkubwa wa mafuta.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *