Tuimarishe maadili ya umma katika vita dhidi ya rushwa

Jacob Mulikuza

Tanzania iliadhimisha siku ya maadili na haki za binadamu tarehe 10 Desemba katika sehemu mbalimbali za nchi ambapo kilele chake kilifanyika Mnazi mmoja Dar es Salaam. Ikumbukwe kuwa tarehe 10 Desemba 1948 ni siku ambayo Umoja wa Mataifa walikaa huko Paris na kutengeneza tamko la duania juu ya haki za binadamu lenye vifungu thelathini.

Siku hii ya maadili na haki za binadamu iliazimishwa wilayani Tarime kwa mdahalo ulioandaliwa na TAKUKURU wakishirikiana na serikali ya wilaya. Mdahalo huo uliongozwa na kauli mbiu isemayo “Tujenge na kukuza maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa”.

Katika mdahalo huo nilialikwa kama mtoa mada juu ya haki za binadamu na uhusiano uliopo kati ya maadili na rushwa.

Kwanza nianze kwa kupongeza jitihada hii ya kuandaa mdahalo kwa serikali ya wilaya ya Tarime pamoja na TAKUKURU. Jitihada hii, ni moja ya mambo ambayo nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara yawe msingi wa maendeleo katika taifa letu. Ni ukweli ulio wazi ya kuwa, maendeleo endelevu ya taifa lolote yanahitaji mijadala ya kina ili kuweza kupata fikra mbadala katika kupata maendeleo tunayostahili.

Kwa maoni yangu midahalo ya namna hii ni vyema ikawepo katika sekta zingine za maendeleo kama kilimo, usafirishaji, madini, mafuta na gesi, elimu, afya na sekta zingine. Midahalo hii sio lazima ikasubiri mpaka siku za maadhimisho ya kitaifa ila inaweza kuwa inaandaliwa kwa ratiba maalum ambayo itaruhusu watu kupata fursa ya kuchakata bongo na kuleta mapendekezo mbadala na kuwasaidia wataalamu kuja na sera na sheria bora zitakazoweza kulikomboa taifa letu kutoka kwenye dimbwi la umasikini.

Tukirejea katika mdahalo huo wa siku ya maadili na haki za binadamu, katika wasilisho langu nilisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu kama sehemu moja ya maadili yanayoweza kuendana na tamaduni mbalimbali za makabila yetu Tanzania. Na kwa upande mwingine nilisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu kama njia moja wapo ya mapambano dhidi ya rushwa.

Katika mdahalo huo, niligundua ya kwamba haki za binadamu bado ni jambo geni kwa wengi ili hali Tanzania imetia sahihi matamko mbalimbali ya Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu. Ugeni wa haki hizi za binadamu unadhihirisha ya kuwa watu wengi hutendewa kinyume bila ya kutambua haki zao za msingi ni zipi na kushindwa kujua wapi na namna ya kuzidai.

Ni muhimu sasa haki za binadamu ili ziweze kufahamika kwa urahisi na watanzania wote zifundishwe kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na chuo. Natambua ya kuwa katika vyuo vikuu vingi hufundisha haki hizi japo sio katika kila taaluma kwani kuna baadhi ya taaluma huzibagua. Ila ni muhimu kusisitiza ya kuwa haki za binadamu ni vyema zikajulikana kwa watanzania mapema ili endapo zitavunjwa waweze kuzidai na kujua namna bora ya kuzidai pia.

Katika mdahalo huo nilisisitza uhusiano uliopo kati ya haki za binadamu, maadili na rushwa. Kwa kuanza hebu tuangazie uhusiano wa haki za binadamu na maadili. Ili kuweza kuhakikisha ya kuwa haki za binadamu zinaheshimiwa kwa hali ya juu kabisa ni kwa kufuata maadili ya kazi na yale yanayokubalika na jamii. Endapo jamii itakiuka maadili ya kazi, taaluma ama jamii ni dhahiri kutakuwa na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu.

Hebu tafakari matendo tunayoyasikia na kuyashuhudia juu ya mauaji ya Albino ambapo watu huyafanya kwa nia ya kupata vyeo kazini, kupata nafasi za siasa na wengine kutaka utajiri wa haraka katika migodi na uvuvi. Matendo haya ya uvunjifu wa haki za binadamu yanatokana na kukosa maadili kwani watu hawataki kutenda kutokana na taaluma zao ili wapate vyeo, kushindana kwa hoja ili wapate nafasi za kisiasa ama kutumia utaalamu katika uvuvi na uchimbaji madili ila wanategemea nguvu za giza ili kufanikiwa. Mpaka pale tutakapoamua kuchukua nafasi kila mmoja wetu na kutenda kwa maadili ndio tutakapoweza kugundua thamani ya haki za binadamu.

Tukitazama uhusiano kati ya haki za binadamu na rushwa ni kitu kilicho dhahiri kabisa. Endapo kutakuwa na matendo ya rushwa ni kweli haki za binadamu zitakiukwa kwa kiwango kikubwa sana. Mwalimu Nyerere mara nyingi alilisitiza ya kuwa ‘Rushwa ni adui wa haki’.

Katika kutafakari juu ya rushwa mara nyingi huwa najiuliza kwanini rushwa inakuwepo? Je ni kwa sababu mishahara ni midogo, je ni hulka ya mtu, je ukiritimba kazini ama nini chanzo cha rushwa hasa? Jibu moja ambalo mara zote huja ni kwamba maadili mabovu huleta rushwa katika jamii yetu. Endapo tutatenda kutokana na maadili ni dhahiri kabisa vitendo vya rushwa vitakoma kama sio kuisha.

Kwa kudhihirisha hili watu wengi wanaojihusisha na rushwa ni watu wasomi tena wa viwango vya juu kabisa, sisemi ya kuwa watu wasio na elimu hawajihusishi na rushwa la hasha. Ila ni ukweli kwamba wasomi wengi hufanya makusudi kabisa kukiuka maadili yao ya kazi ilimradi waweze kukidhi haja ya mioyo yao kwa kupokea rushwa. Wataalamu wengi kwa nafasi zao huamua kwa makusudi kabisa kukiuka maadili ya kazi ili tu kumshawishi mtu anayetaka huduma kuweza kumpatia rushwa.

Kwa kuhitimisha, katika matatizo makuu manne ambayo nchi za magharibi hunyooshea vidole nchi za Afrika ni pamoja na vita, njaa, umasikini na ruswha. Je hii inamaanisha ya kuwa nchi za magharibi hazina rushwa? La hasha, ila ukweli ni kwamba wamehakikisha wanaweka mifumo imara ambayo itamlazimisha mtu kuwa na maadili katika kutenda kazi ili kuzuia mianya yote ya rushwa.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *