SOKO la Kimataifa la Nafaka Kibaigwa mkoani Dodoma ni jeupe baada ya kukosekana kwa nafaka, hususan mahindi huku wimbi la njaa likizikabili familia nyingi.
Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, kwa zaidi ya mwezi sasa hakuna mahindi yanayoingia sokoni hapo na mara chache sana mahindi kidogo huletwa sokoni kutoka Mutukula nchini Uganda.
Hata hivyo, haijajulikana ni kwa namna gani mahindi hayo yanavuka mpaka wa Tanzania na Uganda na kusafirishwa hadi Kibaigwa kutokana na hali ya ukame na tishio la njaa lililoikabili mikoa mbalimbali katika eneo la Afrika Mashariki.
Kutokana na uhaba huo wa nafaka, hivi sasa kilo moja ya mahindi sokoni hapo inauzwa kwa Shs. 1,070 hivyo kufanya gunia moja lenye uzani wa kilogramu 130 kuuzwa kwa takriban Shs. 140,000, kiwango ambacho mwananchi wa kawaida anashindwa kumudu.
Februari Mosi, 2017 kilo moja ya mahindi ilikuwa ikiuzwa kwa Shs. 970, lakini wafanyabiashara wa soko hilo wanasema kwamba, mara nyingi bei iliyoandikwa kwenye ubao siyo halisi kwani inayotembea sokoni huwa iko juu zaidi.
“Kama unavyoona, ni wiki mbili sasa zimepita tangu tani 90 zilipoingia kutoka Mutukura, nchini Uganda lakini yale mahindi yaliyokuwa yakiletwa na wakulima wa mkoa wa Dodoma na Manyara hayapo, kwa kifupi hali ni mbaya,” anaeleza Godfrey Ndigomo, mmoja wa madalali wa soko hilo.
Ndigomo anasema, kudorora kwa biashara ya nafaka sokoni hapo kumechangiwa na sababu nyingi, lakini kubwa zaidi ni ukame pamoja na wakulima kushindwa wa mikoa ya Dodoma na Manyara kushindwa kuzalisha kiwango kinacholingana na mahitaji hasa baada ya kufukuzwa kwenye mbuga ya Emboley Murtangosi wilayani Kiteto.
Aidha, anasema kwamba, hali ya ukame nayo imechangia kwa kiasi kikubwa wakulima wengi wenye akiba kushindwa kupeleka mahindi hayo sokoni hapo kwa hofu ya wao wenyewe kukumbwa na njaa kwa kutojua lini mvua zitanyesha.
“Wakulima wengi wenye akiba ya mahindi wanahofia kuuza kwa sababu hawajui lini mvua zitanyesha, hapa bado pakavu kabisa. Hali hii imefanya familia nyingi ziwe katika hali ngumu kimaisha kutokana na njaa kwani wengi wanategemea soko hili kujipatia mahitaji ya chakula,” anaongeza.
Meneja wa soko hilo, Kusekwa Dalali, alikataa kuzungumza lolote kuhusiana na hali hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wa nafaka sokoni hapo wamebainisha kuwa hali ni mbaya kuliko miaka yote tangu soko hilo lilipofunguliwa.
“Biashara ndiyo kazi yetu inayotuingizia kipato, lakini kwa hali hii tunaona kabisa majaliwa yetu ni madogo, hakuna mahindi,” alisema Juma Mwalubanda, mmoja wa wafanyabiashara hao kutoka Dar es Salaam wakati akihojiana na FikraPevu.
Jesca Mazengo ni mfanyabiashara mdogo ambaye mtaji wake unamuwezesha kununua maguni 10 ya mahindi na kuyauza kwa rejareja, lakini anasema kwa zaidi ya mwezi hajaweza kupata mzigo wowote.
Anaongeza kwamba, hata kama yatapatikana kwa sasa, hataweza kumudu kununua kwa kuwa bei iliyopo ni kubwa na itamwingizia hasara.
“Nilikuwa nanunua maguni 10 kwa Shs. 65,000 kila moja, lakini kwa bei ya sasa sitaweza kumudu… mvua ingekuwa inanyesha pengine wakulima wangeleta mahindi sokoni kwa kuwa na uhakika kwamba wanaweza kuvuna tena shambani, lakini kwa ukame huu hata ningekuwa mimi nisingeweza kuuza chakula cha akiba,” Jesca, mama wa watoto wanne aliieleza FikraPevu.
Lakini James Mamboleo, mmoja wa wanunuzi wakubwa wa mahindi sokoni hapo, anasema soko limebaki jeupe na upatikanaji wa mahindi ni mgumu ambapo kwa sasa anapata kwa shida mzigo wa tani 30 hadi 50 kwa mwezi wakati awali alikuwa akinunua hadi tani 500 kwa mwezi.
FikraPevu imebaini kwamba, baadhi ya wakulima katika vijiji vya Ngomai, Manyata, Hembahemba, Njoge na Makawa mkoani Dodoma pamoja na vijiji vya Emalti, Engusero, Ndirigishi na Dongobeshi mkoani Manyara wanayo akiba ya mahindi, lakini hawako tayari kuuza nafaka zao.
Kabla ya kufukuzwa katika mbuga ya Emboley Murtangosi kufuatia mapigano baina ya wakulima na wafugaji yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 200 kati ya Desemba 2013 na Februari 2014, wakulina hao walikuwa wakizalisha zaidi ya tani 100,000 za mahindi kwa mwaka, lakini kwa sasa kiasi hicho kimeshuka hadi kufikia tani 27,000.
Januari 17, 2017 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi, alitembelea maghala ya kuhifadhia nafaka katika soko hilo na kujiridhisha na takwimu za uhifadhi wa chakula wilayani humo, lakini hali aliyoikuta mwezi mmoja uliopita ni tofauti na iliyopo sasa kwani hakuna kabisa nafaka za aina yoyote.
"Nimekuja kujua kama kweli kuna ujazo wa kutosha katika maghala yetu, nimeona kuna chakula cha kutosha na hakuna haja yakusikiliza maneno ya hao wanaotaka kutia hofu Watanzania ya kuwa eti Taifa lina njaa na litakumbwa na njaa kwa kiwango cha aina yoyote," alikaririwa akisema wakati wa ziara yake.
Takwimu katika soko hilo zinaonyesha kwamba uzalishaji wa mahindi umekuwa ukiyumba mwaka hadi mwaka tangu kufukuzwa kwa wakulima katika eneo la Emboley Murtangosi mwaka 2010 ambapo wakati huo uzalishaji ulikuwa tani 71,739, mwaka 2011 tani 116,095; 2012 tani 96,587; 2013 tani 65,867; 2014 tani 84,071 na mwaka 2015 uzalishaji ulifikia tani 27,756.
Mahindi ya soko la Kibaigwa yalikuwa yakisafirishwa kwenda kuuzwa nchi za Kenya, Malawi na Zambia ambapo yalikuwa yakitokea katika vijiji vya Ndirigishi, Nhati, Emarti, Magungu, Laitimi, Mberi, Mbumbuseseni na Kilimbogo wilayani Kiteto ambako mkulima wa kawaida aliweza kumiliki hadi ekari 200 wakati wakulima wakubwa walikuwa wakimiliki zaidi ya ekari 5,000.
Mwenyekiti wa Bodi ya Soko la Kibaigwa, Jeremia Mhina, anasema mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji katika eneo hilo ulianza mwaka 2006, lakini ulipamba moto mwaka 2010 baada ya serikali wilayani Kiteto kudai kuwa wakulima hao ni wavamizi wa maeneo ya hifadhi na kuwataka kuondoka.
Kwa sasa soko hilo limekuwa likitegemea mahindi kutoka Kibakwe na Pwaga wilayani Mpwapwa, wilaya za Kilindi mkoani Tanga, Mvomero, Gairo na Kilosa mkoani Morogoro, wakati kwa miaka zaidi ya 20 asilimia 90 ya nafaka ilikuwa ikitoka maeneo ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.
Soko hilo ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, ambapo taarifa zinasema, kati ya Julai na Septemba 2016 halmashauri hiyo ilikusanya kiasi cha Shs. 130 milioni kutoka sokoni hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, katika ziara yake ya Januari 2017 katika mji huo mdogo, alijionea mwenyewe jinsi soko hilo lilivyo jeupe, lakini akasema pamoja na sababu za kuondolewa kwa wakulima katika eneo la hifadhi huko Kiteto, bado kuna sababu nyingine zinazochangia uzalishaji mdogo wa nafaka.
“Kuna sababu nyingine ambazo tunazifuatilia kama mkoa na kuzifanyia utafiti kwamba baadhi ya maeneo ya wakulima yaligeuzwa kuwa sehemu ya hifadhi ambayo yamechangia kupunguza eneo la kilimo na kwamba yalitokana na migogoro ya mipaka,” alisema.
Akaongeza: “Wataalam wa hali ya hewa wamekuwa wakitahadharisha na kuwataka wakulima kulima mazao yanayoweza kustahimili ukame na yanayoweza kuvunwa katika muda mfupi, kwa sababu eneo kubwa la Mkoa wa Dodoma ni nusu jangwa.”
Soko la Kibaigwa ambalo linalenga wakulima wa aina zote lilijengwa kwa ushirikiano na Serikali ya Ufaransa pamoja na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) na kisha kukabidhiwa kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.