Walaji wa samaki hatarini. Zebaki yaongezeka maji ya Ziwa Victoria

Jamii Africa

“MWANZA ohhh Mwanza, Mwanza mji mzuri ohhh, Mwanza nitarudi Mwanza, Mwanza nitakuja tena….”

Hiki ni kibwagizo cha wimbo maarufu wa Mwanza, uliotungwa na kuimbwa na gwiji la muziki wa dansi Tanzania, Dk. Remmy Ongala, wakati akisifia uzuri wa mazingira na mandhari ya Jiji la Mwanza.

Dk. Remmy ameimba mengi na hakika sifa hizo zimekuwa zikipazwa na idadi kubwa ya watu wanaotembelea Mwanza au kuishi. Hilo ni jiji linaloelezwa kukua kwa kasi na ubora miongoni mwa majiji ya Afrika Mashariki.

Mwanza ni jiji  la pili kwa ukubwa Tania, ikiwa na kiwango cha ongezeko la watu kwa wastani wa asilimia 3.0, huku idadi kubwa ya wakazi wake wakitegemea maji ya Ziwa Victoria kwa chanzo cha maji kwa ajili ya matumizi ya kila siku hata viwandani na kwenye migodi.

Kutokana na hali hiyo, Mwanza inashuhudia ongezeko la viwanda, kwa mujibu ya taarifa ya ilani ya Mkoa wa Mwanza, inaonesha mpaka kufikia 2013 viwanda vikubwa na vya kati  viliongezeka na kufikia 81 kutoka 58.

Kutokana na ongezeko hilo la watu na shughuli za binadamu, ikiwamo viwanda, majitaka yanayozalishwa kutoka viwandani na majumbani, hasa wilaya za Ilemela na Nyamagana, kwa asilimia kubwa yanaelekezwa Ziwa Victoria, hivyo kuongeza uchafu katika ziwa hilo.

Kiwango kikubwa cha majitaka ambayo hayatibiwi, kimesababisha sehemu kubwa ya maji ya ziwa hilo kutokuwa salama kwa matumizi.

Hayo yanathibitishwa na mtaalamu wa Usimamizi wa Bonde la Ziwa Victoria (LVEMP), Simon Msemwa alipowaasa wananchi kutotumia maji ambayo yana rangi ya kijani au maziwa kwani hizo ni ishara ya uwepo kemikali ambazo zinatokana na kemikali kutoka viwandani, migodini, usafiri, kuongezeka kwa taka ngumu na kilimo cha bustani kinachotumia asidi.

Lakini hayo yote yanasababishwa kutokana na kutokuwepo kwa mfumo madhubuti ambao ungetumika kukusanya majitaka kutoka majumbani, viwandani pamoja na migodini, hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa hatari innayoweza kusababishwa na uwepo wa kemikali kwenye maji ya ziwa hilo.

Kwa bahati mbaya sio watu wote ambao wameunganishwa na mifumo ya majisafi ya mamlaka ya majisafi na majitaka mwanza kwani ni asilimia 53 ya wakazi wa Mkoa wa Mwanza ndio wanaopata maji safi na salama.

Asilimia 47 ya wakazi wa Mwanza hutumia maji yasiyokuwa salama; yenye  mchanganyiko wa vinyesi na kemikali.

Kipindi cha mvua wakazi wa mwanza hasa waishio milimani, huachia vinyesi kuchanganyika na maji ya mvua na kwenda moja kwa moja kwenye mitaro inayopeleka majitaka ziwani, bila kupitia mfumo wowote ambao unasafisha maji hayo.

Ieleweke kuwa Mkoa wa Mwanza una visiwa ambavyo wakazi wake, kwa silimia 100 hutumia maji ya ziwa hilo, bila kuwekewa dawa ya kuua vimelea na kuondoa uchafu.

Visiwa vikubwa ni pamoja na Ukerewe na Ukara, vingine ni Saanane na Rubondo, ambako wakazi wake wengi wamejenga vyoo jirani na maeneo ya ziwa. Haliambayo ni hatari kwa afya ya maji.

Viwanda, migodi na vyombo vya usafiri (vyombo kama boti na mitumbw inayotumia injini) vinazalisha kemikali ambazo huchanganyika na maji, hivyo kuharibu ubora wake.

Migodi ndiyo inaongoza kwa kuzalisha kemikali hatari ya zebaki, ambayo ikiingia kwenye maji madhara yake ni makubwa kwa watumiaji na viumbe hai.

Madhara makubwa ya kutumia zebaki, hasa kupitia samaki ndani ya maji ya kemikali hiyo ni pamoja na saratani.

Dalili za wazi kwamba maji yana madhara ni pamoja na kubadilika rangi, hasa kuwa ya kijani au rangi ya maziwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika tafiti ambazo imewahi kufanya imeonesha miongoni mwa madhara yanayosababishwa na kemikali ya zebaki ni utindio wa ubongo kwa watoto, matatizo mfumo wa upumuaji, kuharibika kwa ubongo na matatizo kwenye mfumo wa mmeng`enyo wa chakula.

Ipo mifano hai ambayo imewahi kutokea  Japan na hii ni kutokana na maji yaliyozalishwa kiwandani hayakusafishwa. Hii ilikuwa kati ya mwaka 1932 na 1968 ambapo kiwanda cha kuzalisha dawa zenye asidi kiliachia majitaka yenye zebaki kwenye ghuba ya Minamat, kwa muda wakazi wa eneo hilo waliugua ugonjwa usiofahamika na kuathiri watu 50,000 kutokana na kula samaki wa maeneo hayo waliochanganyika na kemikali za zebaki.

Endapo kama kungekuwepo mfumo wa kusafishia maji kama ilivyo kwenye Jimbo la Ohio, nchini Marekani, ambao umepakana na ziwa kubwa kabisa duniani – Superior,  madhara hayo yasingetokea.

Hakika bila kuwa na njia sahihi za kutibu maji yanayoingia Ziwa Victoria, Watanzania, hasa wa vizazi vijavyo, wanaweza kupata madhara makubwa.

Ieleweke kuwa Watanzania wengi wanatamani kuona nchi ikisonga mbele na kuwa na uchumi mkubwa (au wa kati) wa viwanda, lakini viwanda vinavyotakiwa ni vile visivyohatarisha maisha ya binadamu na viumbe hai.

Ni vyema, kuanzia sasa, serikali ikachukua hatua kuepusha hatari ya maji ya Ziwa Victoria kuchafuliwa, kwa njia yoyote ile, ili basi liendelee kuwa salama na kuwanufaisha zaidi wananchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *