Ukatili kwa watoto unavyosonga Songea

UKATILI kwa watoto ni kitendo ambacho kinachoendelea kupigwa vita wakati wote na dunia. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokamia kutokomeza ukatili huo kwa jitihada za wazi na hata zile za kiintelijensia.

Kuhusika kwa njia za kiintelijensia, kunatokana na kuwepo kwa njia nyingi za uficho na usiri ambao umekuwa ukitawala wahusika karibu wote wa vitendo hivyo viovu vinavyowakumba watoto.

Katika makala haya yaliyoandikwa na Judith Lugoye, yanaangaza zaidi hali ilivyo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ambapo kumekuwa na changamoto ya ongezeko la vitendo hivyo.

Uchunguzi umebaini kwamba katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2014, katika manispaa hiyo kumekuwa na matukio zaidi ya 400 yaliyoripotiwa juu ya vitendo kwenye vyombo vya usalama na hata serikalini.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka hadi mwaka, kumekuwa na ongezeko  la vitendo vya ubakaji, kuuawa kwa watoto, utoaji mimba, kutelekeza watoto (au familia), watoto wachanga kutupwa mara baada ya mama kujifungua, huku pia watoto wakipewa adhabu kali  kwa kupigwa na kusababishiwa majeraha na hata vifo.

Wananchi 23; wanawake wakiwa 14 na wanaume tisa, waliohojiwa kwa nyakati tofauti wanataja sababu ya kuwepo kwa ongezeko hilo la ukatili kwa kijinsia kuwa ni hali ngumu ya maisha, huku wengine wakidai kushamiri kwa roho mbaya na kutowajibika kwa wazazi au hata familia.

Wanawake sita kati ya 14 waliohojiwa walidai kuwa umasikini wa kipato umekuwa ukiwasukuma kuanza biashara za kuuza miili yao, au kuanzisha uhusiano wa mapenzi na watu wenye uwezo, lakini wanapopata mimba hukimbiwa na wenzi wao, hivyo kuona njia rahisi ya kuachana na kadhia ya ujauzito ni kutoa mimba, au  wengine kujiua.

Idadi hiyo ya wanaume wao wana maoni kuwa watoto wengi wamekuwa wakionewa, kutelekezwa au hata kuuawa kutokana na dunia kutokuwa na hofu ya Mungu.

Katika Manispaa ya Songea, habari za kuokotwa kwa watoto wachanga mara baada ya kuzaliwa zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara, hivyo kuonesha ongezeko la vitendo hivyo. Kati ya wawanaookotwa – baadhi hukutwa wamekufa na wengine wakiwa hai.

Vyanzo mbalimbali vimethibitisha kuwa kwa nyakati tofauti watoto saba wametupwa jalalani katika kipindi cha mwaka 2012 na 2013 kwenye maeneo tofauti ya Manispaa ya Songea. Huko eneo la Matogoro aliokotwa mtoto mchanga wa kike wa siku sita, Mateka – mtoto wa siku moja, Majengo – watoto wawili wa kiume ambapo mmoja wa miezi tisa alikutwa akiwa amekufa baada ya kunyongwa, inakadiriwa kuwa alikuwa na umri wa siku tano.

Katika eneo la Mfaranyaki, kichanga kinachokadiriwa kuwa na siku tatu kiliokotwa huku sehemu kubwa ya mwili wake ikiwa imeliwa na mbwa. Mtoto mwingine wa miezi mitatu aliokotwa eneo la Bombambili akiwa na umri wa miezi 10 ambaye aliuwawa kwa kunyongwa shingo na mama yake mzazi.

 Pamoja na ukatili huo, hasa kutoka kwa wanawake, wanume nao wamebainika kufanya ukatili kutokana na ugumu wa maisha, wengi wakiwa ni wale waliokata tamaa baada ya kupima afya zao na kujikuta wameambukizwa ugonjwa huo, hivyo, kujiingiza katika ubakaji. Hawa huanza ubakaji, hasa kwa kuwavizia  wasichana maeneo yenye vichaka na kutenda uovu.

Ukatili zaidi kwa watoto

Watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa ukatili wa kijinsia, mbali na kutupwa mara wanapozaliwa, pia wamekuwa wakikumbana na majanga mengine katika makuzi yao, ikiwamo kuteswa kwa kupigwa, kunyimwa chakula au hata kutelekezwa.

Wengine hutendewa ukatili kwa kupigwa fimbo au kuchomwa moto sehemu mbalimbali za miili yao endapo tu atakuwa amekosea. Vitendo hivi huwasababishia majeraha makubwa na zaidi sana kuwaathiri kisaikolojia.

kupigwa bakora kwenye makalio

Mtoto wa kike wa darasa la 3 alivyopiwa na baba yake mlezi kutokana na kupoteza sh. 1,000/=

Hivi karibuni mtoto wa miaka mitano (Jina tunalo) ambaye anaishi Mtaa wa Madizini, Songea alipigwa na mzee mmoja aliyejulikana kwa jina (jina tunalo) baada ya kumkuta mtoto huyo akiwa shambani kwake anachuma matunda, ambapo alimwadhibu vibaya kwa kumpiga na kitu kizito kichwani hadi kupoteza fahamu na kumtupa kwenye jumba bovu. Aliokolewa na wasamaria wema waliokuwa wakipita jirani na kumpeleka hospitali na kuyanusuru maisha yake.

Mwingine ni mtoto wa darasa la tatu, mkazi wa Ruhuwiko ambaye alichomwa moto mikono yote miwili na baba yake mzazi (jina tunalo) na kumsababishia majeraha, huku wengine wawili waishio Bombambili walivunjwa mikono yao na baba zao (majina tunayo) baada ya kubaini wamemwibia hela shilingi 1000. 

 Pia mtoto mwenye umri wa miaka 11 mkazi wa Mtaa wa Manzese alichomwa moto  kwa kumwagiwa mafuta ya taa mikono na kuwasha kiberiti.

 Unyanyasaji wa aina hiyo pia ulimkuta mtoto mmoja wa kike (jina tunalo), mlemavu wa viungo, mkazi wa Mabatini, alipigwa na jirani yake huku akiwa amemfunga kamba mikononi na miguu kwa madai kuwa alikuwa akimhimiza aende shule. Zaidi sana mtoto mwingine wa kike, alimchanja kwa nyembe sehemu zake za siri kwa madai kuwa amekuwa na tabia ya udokozi (wizi).

Ofisa Ustawi wa Jamii  Manispaa ya Songea, Victory Nyanza amethibisha kuwepo kwa matukio hayo na ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili wa kijinsia unaoendelea kufanywa kila kukicha na kutanabaisha kuwa wanaoongoza kutenda vitendo hivyo ni wanawake.

Anasema vitendo hivyo vimekua kwa kiasi kikubwa na kwamba ofisi yake imekuwa ikipokea kesi nyingi za ukatili wa kijinsia na kwamba baadhi huzimaliza kwa kufikia suluhu, huku zingine zikipelekwa mahakamani.

Kadhalika kwa watoto wanaotupwa na kuokotwa na wasamaria wema, anasema huchukuliwa na kupelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi, na baadaye hutunzwa katika vituo vya kulelea watoto yatima. 

 Anasema katika kipindi cha mwaka 2011/2012 kesi nne zimeripotiwa juu ya  wazazi kunyanyasa watoto wao kwa kuwapa adhabu kali na watuhumiwa walifikishwa mahakamani kwa uchunguzi zaidi wa kisheria.

"Mwaka 2012/2013 walipokea kesi tisa kati ya hizo tatu zimetoka Songea Vijijini na sita katika manispaa hiyo, huku kipindi cha mwaka jana na mwaka huu kesi tatu zimeripotiwa Polisi na mbili zipo Mahakamani, ikiwemo moja ya mtoto wa siku moja aliyeokotwa Desemba, 2012 katika makutano ya barabara za kwenda Mateka na Mahenge ambapo mtoto huyo hivi sasa bado analelewa na kituo cha kulelea watoto yatima Chipole kilichopo Songea vijijini," anaongeza.

 Ofisa huyo anafafanua kuwa aina nyingine ya ukatili ambao unakua kwa kasi ni juu ya utumikishwaji wa watoto kufanya biashara ndogondogo kama vile kuuza karanga, mahindi ya kukaanga ambao umri wao walitakiwa kwenda shule.

Dawati la Jinsia katika Jeshi la Polisi Ruvuma, makao makuu yakiwa Songea, limethibitisha kuwepo kwa ongezeko la vitendo hivyo vya ukatili.

Katibu wa dawati hilo, Fadhila Marwa Chacha anasema wamekuwa wakipokea kesi nyingi zinazotokana na vitendo vya ukatili hasa ubakaji, kupiga na kuchoma moto watoto, na wale wanaotupwa jalalani.

MKONO ULIO UNGUZWA

PICHA: Mtoto wa kiume wa darasa la tatu alichomwa moto mikono na jirani yake

Anazitaja sababu zinazosababisha ukatili huo kuwa ni ubakaji, matumizi ya pombe kupita kiasi na dawa za kulevya.

Katibu huyo amezitaja sababu zingine kuwa ni imani za kishirikina na tamaa ya kupata mali, huku akitaja wanaume kuwa wengi katika kundi hili ambapo huaminishwa kwamba wakitaka kutajirika lazima amuingilie kingono mama yake, mtoto ama ndugu yeyote wa karibu.

unyumba mama na mtoto

Kijana huyu na mama yake mzazi wanaishi kama mke na mume kwa zaidi ya mika 10 sasa

Anaeleza athari za ubakaji kuwa ni pamoja na kuwaathiri watoto kisaikolojia, maambukizi ya Ukimwi na mimba zisizotarajiwa.

Akizungumzia kuhusu wanawake wanaotupa watoto, Fadhila anasema hali hii mara nyingi inawakuta wanafunzi ambao hupata mimba bila kutarajia na kuona watashindwa kulea, na hivyo kufikia uamuzi wa kutupa vichanga baada ya kujifungua.

 Katibu huyo wa dawati hilo anasema dawati lake  katika jitihada zake za kudhibiti vitendo hivyo limefanikiwa kuwafikisha wahukusika mahakamani na wapo waliohukumiwa baada ya kukutwa na hatia, huku wengine wakiwekwa kwenye uangalizi maalumu wa dawati lake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusdedith Nsimeki amethibitisha kuwepo ongezeko la vitendo hivyo vya unyanyasaji na kueleza kuwa wahusika wa vitendo hivyo wamekuwa wakikamatwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi.

Anasema kipindi cha mwaka jana, kesi tano zimepelekwa mahakamani na kesi zaidi ya 20 zimefunguliwa majalada ya uchunguzi  ikiwemo ya mama mmoja mkazi wa eneo la Matarawe kutelekeza watoto sita. 

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk. Benedict Ngaiza anathibitisha kupokea kesi nyingi zinazohusiana na vitendo vya ukatili ikiwemo wanawake wawili ambao wamefariki dunia baada ya kujaribu kutoa mimba.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *