RAIS Jakaya Kikwete, amekiri wazi kuwepo kwa vuguvugu la upinzani lenye nguvu kubwa hapa nchini, na kuonya kwamba, iwapo Chama cha Mapinduzi (CCM), hakitajirekebisha katika mienendo yake inayoonekana kuwaudhi wananchi, chama hicho kipo hatarini kupoteza hatamu ya kuliongoza Taifa na kusisitiza nia ya chama hicho kuwaondoa mafisadi.
Kadhalika, Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Taifa, ametetea uamuzi wa kujivua gamba ndani ya chama hicho, uliopewa baraka zote na Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC), dhidi ya viongozi mafisadi kuhakikisha wanajiondoa ndani ya chama kabla hawajaondolewa, na kusema uamuzi huo haukuwalenga watu fulani wanaotuhumiwa kwa ufisadi, bali viongozi wote wasio na maadili mema ndani ya CCM.
Mkuu huyo wa nchi, aliyathibitisha hayo leo Jijini Mwanza, wakati akihutubia maelfu ya wanachama wa CCM katika sherehe za maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM, iliyofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.
Katika sherehe hizo, CCM ililazimika kutumia mtindo wake wa kukodi mabasi na maroli, kwa ajili ya kusomba watu kutoka maeneo mbali mbali ndani na nje ya mkoa huo, kwa ajili ya kuhudhuria maadhimisho hayo, ambayo hata hivyo yalionekana kughubikwa na imani za kishirikina ndani ya uwanja huo wa CCM Kirumba.
Katika hotuba yake kwa wana CCM, Rais Kikwete alisema kwamba, kwa sasa nchi imekumbwa na mtikisiko mkubwa wa vuguvugu la upinzani, na kwamba viongozi wa CCM na Serikali kwa ujumla wasiwe watu walioganda.
“Wapo wanaobeza mafanikio tuliyofikia, nasema huo ni uroho mbaya. Sisi tuwapuuze. Lakini tutambueni kwamba kwa sasa vuguvugu la upinzani limezidi kuwa na nguv kubwa hapa nchini.
“Kushika ama kuendelea kushika madaraka inatokana na ridhaa ya wananchi wenyewe. Hivyo wana CCM tutambueni hilo kwamba wananchi ndiyo wenye uwezo wa kutupa ama kutukataa kuwaongoza. Tukishindwa hilo tutashindwa”, alisema Rais Kikwete ambaye wakati wa kuingia uwanjani CCM Kirumba wasaidizi wake kitengo cha usalama wa taifa waliona chupa mbili zilizokuwa zimejazwa vitu vilivyodaiwa dawa za kishirikina, kisha mmoja wa saidizi wake hao kuipiga teke chupa moja.
Chupa hizo mbili za kampuni moja ya kutengeneza maji (jina tunalihifadhi), zenye ujazo wa lita 1.5, zilionekana moja kuwekwa upande wa zuria na nyingine upande wa pili wa zuria lililotandikwa uwanjani hapo kwa ajili ya mgeni rasmi na wageni wengine wanapopita kwenda meza kuu (V.I.P), kwa ajili ya shughuli hiyo ya maadhimisho hayo.
Alisema, lazima viongozi wa CCM na Serikali wawajibike kikamilifu katika kusimamia maendeleo ya wananchi, ili kuendelea kuwajengea imani raia hao dhidi ya chama chao tawala na Serikali kwa ujumla, na kwamba chama hicho tawala kimeathiriwa sana na viongozi wake wasiokuwa waaminifu mbele ya jamii ya Kitanzania.
Kuhusu kujivua gamba.
Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alisema: “Hivi karibuni nikiwa na NEC hapo Dodoma, nilitumia neno nyoka kujivua gamba. Usemi huo ulienezwa tofauti kabisa. Kimsingi tulipitisha maazimio mengi, lakini wenzetu wameona azimio moja tu la kujivua gamba.
Alisema, hoja ya kujivua gamba iliyopitishwa na NEC mwaka jana si ya ovyo, hivyo kiongozi na mwanachaa yeyote ndani ya CCM anayeuona uamuzi huo ni wa ovyo, basi yeye ndiyo wa ovyo mbele ya jamii.
“Uamuzi wa kujivua gamba ndani ya CCM si wa ovyo. Ukiuona wa ovyo wewe ndiyo wa ovyo. Haiwezekani tukaendelea kuwa na watu wa ovyo. Lazima chama kijipange na kujiweka sawa ili kisipoteze sifa kwa jamii”, alisema mwenyekiti huyo wa CCM taifa ambaye alipokea wanachama wapya wapatao 1,847.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete ambaye alianza kuhutubia saa 8:45 mchana na kumaliza saa 9:37 alasiri, alikiri pia ajenda ya watu ndani ya chama hicho kujivua gamba imegonga mwamba, na amewatupia mzigo wanachama wake kuwawajibisha viongozi hao na wale wanaowaona hawaendani na maadili wala sera za chama hicho tawala.
Alisema, maamuzi ya kujivua gamba hayakulilenga kundi ama watu fulani ndani ya CCM, bali linawahusu wanachama wote wanaojitambua kwamba si waaminifu kujiondoa wenyewe ndani ya chama kwa kuachia nyadhifa za kiuongozi badala ya kusubiri kuondolewa na mamlaka za juu.
“Wito wa kujivua gamba haujapewa mwitikio mzuri. Tumetupa mpira huo kwa wanachama kuwawajibisha viongozi hao, maana tunawafahamu. Sasa kazi kwetu sote”, alisema Rais Kikwete pia alishuhudia uwanja huo wa CCM Kirumba kutokujaa watu kama ilivyokuwa mwaka 2005 wakati alipowasili kwa ajili ya kuomba kura ya kuwa mtawala wa nchi.
Uchaguzi wajumbe wa NEC.
Mwenyekiti huyo na Rais wa nchi alisisitiza kwamba, lazima wajumbe wa Halmashauri kuu ya chama (NEC), wachaguliwe kutoka kwenye wilaya zao, na si vinginevyo, na kusema hiyo itasaidia zaidi kukiimarisha chama chake hicho kinachonyemelewa na vuguvugu kali la upinzani nchini.
Hata hivyo, alikwenda mbali na kuwataka wanachama wasiokuwa wasafi, wenye upeo mfupi, wabakaji na mafisadi wasijidanganye kuomba uongozi huo wa NEC, maana wanachama hawatawachagua kutokana na matendo yao mabaya ndani ya jamii inayowazunguka.
Mwenyekiti huyo wa CCM aliiagiza Taasisi ya Kuzuia Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuanza kunyemelea nyendo za baadhi ya wanasiasa wanaotaka kugombea UNEC ndani ya chama hicho, kwani wapo baadhi yao wamepanga kutumia rushwa kuwahonga wanachama ili wawachague kushika nafasi hiyo ya juu.
Katiba mpya.
Rais Kikwete aliwapongeza wabunge wa CCM kwa uamuzi wao wa kuitetea Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mpya 2011, na kwamba muswaada huo umeshawasilishwa tena bungeni, hivyo ataunda tume ya kukusanya maoni kwa Watanzania, ambapo aliwaomba wana CCM kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao, maana mmbamba ngoma huvutia kwake.
“Hili la Katiba mpya tumechukuwa mapendekezo ya vyama vya upinzani, kikiwemo CCM ambacho nacho kimetoa mapendekezo manane. Nawashukuru sana wabunge wa CCM katika hili, lakini wana CCM jitokezeni kwa wingi kutoa maoni yenu maana mmbamba ngoma huvutia kwake”.
Hata hivyo, Rais Kikwete alikwepa waziwazi kuzungumzia tatizo la mgomo wa Madaktari linaloikumba nchi kwa sasa, na kuahidi kulitolea ufafanuzi na maelezo muda si mrefu.
Alikitaka pia kitengo cha propoganda ndani ya chama hicho kufanya kazi vizuri, maana chama hicho kinaonekana kuzidiwa nguvu na wapinzani ambao wao hutumia propoganda za aina mbali mbali, hivyo wananchi kuanza kuamini maneno ya wapinzani.
Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – Mwanza.
Hotuma kamili ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete:
HOTUBA YA MWENYEKITI WA CCM TAIFA, MHESHIMIWA
JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA SHEREHE ZA
KUTIMIZA MIAKA 35 YA CCM, KWENYE UWANJA WA
CCM KIRUMBA,TAREHE 05 FEBRUARI, 2012
Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa,
Mhemiwa Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,
Mheshimiwa Wilson Mukama, Katibu Mkuu wa CCM,
Waheshimiwa Wajumbe wa Sekretariat, Kamati Kuu na Halmashauri
Kuu ya Taifa;
Waheshimiwa Waasisi wa TANU, ASP na CCM;
Wanachama wenzangu wa CCM;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kidumu Chama cha Mapinduzi……..!
Naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kutupa afya na uzima na kutuwezesha kukutana tena katika
maadhimisho ya siku hii adhimu na ya kihistoria kwa Chama chetu na
nchi yetu.
Tumekusanyika hapa siku ya leo kusherehekea miaka 35 ya
kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Nawashukuru na kuwapongeza
sana viongozi, wana-CCM na wakazi wa Mkoa wa Mwanza kwa
mapokezi mazuri na kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizi. Hakika
sherehe zimefana sana. Hongereni wote mlioandaa sherehe hii kwa kazi
nzuri sana mlioifanya. Nawapongeza sana wanachama na wananchi,
kwa kujitokeza kwa wingi katika matembezi ya mshikamano leo
asubuhi na sasa katika kilele cha sherehe. Aidha, nawashukuru kwa
2
burudani mbalimbali na wimbo mzuri wa halaiki ambao umetugusa
sana na kukonga nyoyo zetu. Wahenga walisema “mwenye macho
haambiwi tazama”. Tunawashukuru sana. (Mwabeja sana).
Napenda pia kuwapongeza viongozi, wanachama, makada,
wapenzi na mashabiki wote wa CCM kote nchini kwa kuadhimisha
miaka 35 ya uhai wa Chama chetu. Kama nilivyosema kule Dodoma
mwaka wa jana kwamba tunastahili kujipongeza kwani tumefanikiwa
kwa mengi, na tunazidi kufanikiwa. Wapo wanaotubeza, sisi
tuwapuuze kwa kuendelea kutekeleza ahadi na mipango.
Tuwashangaze kwa kufanikiwa ili wachukie.
Ndugu Wananchi;
Sherehe hizi ni fursa ya kufanya tathmini ya kiasi gani
tumefanikiwa kujenga na kuimarisha Chama chetu na jinsi gani
tumefanikiwa katika kutimiza wajibu wetu kwa taifa na wananchi
ambao tuna dhamana ya kuwaongoza.
Kwa Chama chetu kufanikiwa kudumu na kuwa kimoja kwa
miaka 35, na zaidi ya nusu ya miaka hiyo ikiwa ni ndani ya ushindani
wa vyama vingi, ni mafanikio makubwa ambayo wote hatuna budi
kujivunia. Ni jambo la fahari kubwa kwa Chama cha Mapinduzi
kwamba nchi yetu imesherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara
wakati Chama chetu kikiwa kinaendelea kushika hatamu za uongozi wa
nchi yetu.
Tumefanikiwa kufanya hivyo kwa miaka yote hiyo kwa sababu
tumetambua na kutimiza wajibu wetu wa uongozi wa taifa kwa namna
na kiwango ambacho kimewaridhisha wananchi wa Tanzania. Ukweli
huo unadhihirishwa na jinsi Chama chetu kilivyoendelea kupata
ushindi katika chaguzi mbalimbali tangu tuanze mfumo wa vyama
vingi mwaka 1992 mpaka sasa. Tumeendelea kupata ushindi mzuri
3
hata katika kipindi hiki ambacho vuguvugu la upinzani nchini
limeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Ndugu zangu, Viongozi wenzangu na Wana-CCM wenzangu;
Kama nilivyokwishawahi kusema mara kadhaa kwa wana CCM
siku za nyuma kwamba wakati tunapojipongeza kwa mafanikio
tuliyoyapata, hatuna budi kutambua kuwa ili Chama chetu kiendelee
kupata ushindi na kuongoza taifa letu kwa miaka mingi zaidi, hatuna
budi kwenda na wakati. Lazima tuwe na sera nzuri zinazotambua
matakwa ya raia na matatizo yanayowakabili na kuyatafutia majawabu.
Tuchukue hatua thabiti za kutatua changamoto na matatizo ya
wananchi na kufanya mambo mapya ya kuleta maendeleo. Tukifanya
hayo wananchi wataendelea kuwa na mapenzi na imani na Chama
chetu na kutuwezesha kuendelea kuongoza kwa miaka mingi zaidi.
Bahati nzuri Chama chetu kina sifa ya kutekeleza sera zake na
ahadi zake kwa wananchi pamoja na changamoto mbalimbali
tunazokabiliana nazo. Tumethibitisha ukweli huo kwa jinsi gani
tumetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 – 2010 na tulivyoanza
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 katika mwaka wa kwanza
wa ngwe yetu ya pili. Ni ukweli kwa nchi nzima na ukweli kwa Mkoa
wa Mwanza kwamba tumetekeleza ahadi zetu kwa kiwango cha juu
sana. Tunasema tutakayotekeleza na tunatekeleza tuliyoahidi.
Viongozi wenzangu na Wanachama Wenzangu;
Chama chetu kinayo sifa nyingine nzuri nayo ni kufanya tathmini
ya shughuli zake mara kwa mara ili kubaini mafanikio tuliyoyapata na
pale ambapo hatukufanikiwa. Lakini huwa hatuishii hapo bali
hukubaliana juu ya hatua za kuchukua kuimarisha na kuendeleza
tuliyofanikiwa na kusahihisha tulipokosea. Hiyo ndiyo siri ya
mafanikio yetu.
4
Kukamilisha Mageuzi Ndani ya Chama
Ndugu Wana CCM;
Katika hotuba yangu ya mwaka jana pale Dodoma nilieleza haja
ya kufanya tathmini ya uchaguzi uliopita na kufanya mageuzi ndani ya
Chama chetu kwa lengo la kukiimarisha. Shabaha yetu kuu ni
kukihuisha Chama chetu na kukipa taswira mpya na mvuto zaidi mbele
ya jamii. Katika kusisitiza umuhimu wa kufanya hayo nilitoa mfano wa
tabia ya nyoka kujivua gamba. Nilieleza kwa kina faida ya kufanya
hivyo na athari za kutochukua hatua hizo mapema.
CCM ni chama cha siasa ambacho mtaji wetu uko katika kuungwa
mkono na watu. Hivyo basi, hatuna budi kuwa makini, sikivu na
kwenda na wakati. Ni ukweli ulio wazi kuwa uhai na uhalali wa
Chama chetu kushika hatamu za dola unategemea ridhaa ya wananchi.
Hisia zao na mtazamo wao juu ya Chama chetu ndizo zinazowafanya
waamue kutupatia au kutunyima ridhaa hiyo. Hivyo basi, lazima
wakati wote Chama chetu kijitahidi kuhakikisha kuwa kina taswira
nzuri katika mitazamo na hisia za wananchi. Lazima tuwe na sera nzuri
na tufanye mambo mema. Pia lazima Chama chetu kijenge uwezo wa
kupambana na propaganda chafu zinazojenga taswira mbaya ya Chama
kwa jamii. Lazima tujenge uwezo wa kujisemea kwa mema mengi
tunayofanya.
Chama hiki ndio zindiko la nchi hii na matumaini ya wananchi
walio wengi. Kamwe tusikubali sisi viongozi kuwa chanzo cha
kuipoteza tunu hii ya Watanzania kwa kushindwa kuchukua hatua
sahihi. Tukichelea kufanya hivyo, tutachekwa na kulaumiwa sana na
kamwe historia haitotusamehe.
Ndugu Wana-CCM;
Kwa kutambua ukweli huo na wajibu wa kihistoria kwetu wa
Chama chetu, Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama chetu katika kikao
5
cha mwezi Aprili, 2011 kiliazimia kuchukua hatua mbalimbali
zitakazokipa uhai mpya Chama chetu. Miongoni mwa hatua hizo ni
kuiunda upya Kamati Kuu na Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Aidha, kuutazama muundo wa Chama chetu na iliamuliwa kuwa
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wachaguliwe kutoka Wilayani
badala ya utaratibu wa sasa wa kuwachagua kutoka Mkoani na Taifa.
Lengo ni kuusogeza uongozi huu wa juu wa Chama chetu utoke karibu
na kule wanachama waliko. Tulikubaliana pia kwamba sote tuelekeze
nguvu zetu katika kuimarisha Matawi na Mashina walipo wanachama.
Hivi sasa nguvu nyingi imeelekezwa Wilayani, Mkoani na Taifa.
Halmashauri Kuu ya Taifa imejadili kwa kirefu nafasi ya viongozi
katika ujenzi wa Chama na sifa yake mbele ya watu na jamii. NEC
imekubaliana kwa kauli moja kwamba, kuwa na viongozi hodari na
wenye mwenendo mwema ni rasilimali yenye tunu kubwa. Kinyume
chake ni kubeba mzigo mkubwa wa lawama na kushusha heshima na
sura ya Chama katika jamii. Halmashauri Kuu ya Taifa ilikubaliana
kwamba sifa na sura ya Chama katika macho ya jamii imeathiriwa sana
na kuwa na viongozi wanaonyooshewa vidole na kutuhumiwa kwa
mwenendo mbaya hasa vitendo vya rushwa, wizi, utovu wa nidhamu
na ubadhirifu. NEC iliamua kuwa viongozi wa namna hiyo hawafai
kuwemo katika safu za uongozi wa Chama chetu. Ikaamuliwa wapime,
watafakari na kuamua kujiondoa katika uongozi na wasipofanya hivyo
waondolewe.
Baada ya kuridhika kuwa wito huo haukuitikiwa ipasavyo, NEC
imeagiza vikao vya Chama vya ngazi zote wawatambue viongozi wa
namna hiyo na kuwachukulia hatua kuwawajibisha. Hayo ndiyo
maelekezo, sasa kazi kwetu sote kwani watu hao wapo katika ngazi
zote, wapo kwenye Matawi, Kata, Wilaya, Mikoa na Taifa. Bahati
mbaya ilijengwa dhana kana kwamba wapo taifa tu.
6
Ndugu Wanachama;
Nafahamu kuwa baadhi ya viongozi na wanachama wenzetu
hawakupendezwa na hawapendezwi na uamuzi huo na mageuzi ya
Chama kwa jumla. Wanataka tubaki tulivyo. Hawa hawakitakii mema
Chama, tuendelee kuwaelimisha. Wako waliotafsiri kuwa mageuzi
haya yanawalenga watu Fulani tu, hayo siyo kweli ni upotoshaji. Kwa
kweli huku kutia fitina kwa jambo ambalo liko dhahiri. Sote tu
mashahidi wa kilio cha wanachama wetu, wapenzi na wananchi kwa
ujumla kuhusu haja ya kukibadili Chama chetu. Tunatambua kilio cha
wanachama na wananchi cha kutaka Chama chao wanachokipenda
kiwe na viongozi waadilifu wasiokuwa na tuhuma za rushwa au
ubadhirifu, wanaotenda maovu.
Kilio hicho ni cha kututakia mema na kinaonyesha kuwa watu
wengi bado wana imani kubwa na CCM na wangependa kuona
tukichukua hatua za kukisafisha na kukijenga upya. Maana wangekuwa
wametuchoka wangejikalia kimya na kusubiri kutunyima kura wakati
wa uchaguzi. Hatuwezi kuzipuuzia sauti hizi za wengi na hatuwezi
kujificha katika visingizio visivyo na msingi. Tusichelee kuudhi
wachache kwa manufaa ya Chama chetu. Mzee wetu Mhe. Benjamin
Mkapa alituusia, “Chama kwanza, mtu baadae”. Chama ni muhimu
zaidi kuliko mtu.
Wana-CCM Wenzangu;
Kazi hii tuliyoianza lazima tuifanye bila ya kuchoka mpaka
tuifikishe ukomo wake. Iwe ni ya kudumu, tusiifanye kuwa ya mara
moja au ya tukio. Iwe ni sehemu ya mila yetu na kila kunapotokea
kiongozi kupoteza sifa achukuliwe hatua. Tuimarishe Kamati za
Usalama na Maadili za ngazi zote ili ziweze kufanya kazi hii. Kusafisha
safu za viongozi na wanachama wetu ni jambo lenye maslahi kwa
Chama chetu.
7
Majukumu yetu kwa 2012
Uchaguzi wa Chama na Jumuiya zake
Ndugu Wana CCM,
Kama tujuavyo, huu ni Mwaka wa Uchaguzi ndani ya Chama
chetu na Jumuiya zake kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa. Tofauti na
chaguzi zilizopita, uchaguzi wa mwaka huu unahusisha Chama na
Jumuiya zake. Huu ni utekelezaji wa moja ya mambo 23
tuliyokubaliana tufanye katika mageuzi ya ndani ya Chama. Sababu
kubwa iliyotufanya tuamue hivyo ni kutaka tupunguze muda
tunaoutumia kwa shughuli za uchaguzi ili tupate muda wa kutosha wa
kushughulikia kazi za ujenzi wa Chama na utekelezaji wa majukumu
yake ya msingi.
Nawasihi viongozi wenzangu na wanachama wenzangu tuitumie
fursa hii vizuri kuchagua viongozi wazuri watakaokiongoza vyema
Chama chetu. Viongozi watakaokijenga na kukiimarisha Chama, siyo
wale watakaokigawa na kukidhoofisha. Tuchague viongozi ambao ni
wabunifu na wana uwezo wa kukisemea na kukitetea Chama chetu na
sera zake badala ya kuwa na viongozi ambao hawana wanalolijua, wana
upeo mfupi wa mawazo, hawana uwezo wa kukisemea na kukitetea
Chama chetu na wakati mwingine hata kupotosha ukweli. Tusichague
viongozi ambao wapo kwa ajili ya kunufaika wao binafsi na siyo Chama
kunufaika na uongozi wao. Tuchague viongozi wenye tabia na
mwenendo mwema na tuepuke kuchagua watu ambao jamii itaguna
kwa sababu ana tabia mbaya, mtenda maovu na asiyekuwa mwadilifu.
Tuchague viongozi wachapakazi hodari, wazalendo wa dhati, wenye
mapenzi mema na nchi yetu, Serikali na Chama chetu.
Ndugu wana CCM;
Nimezieleza sifa hizo kwa kirefu kwa sababu ya umuhimu wa
viongozi kwa uhai na maendeleo ya Chama chetu. Aidha, kwa sababu
8
kiongozi ndiye kioo ambacho huonesha jinsi Chama chetu
kinavyoonekana mbele za watu. Ni ukweli ulio wazi kuwa viongozi
wasiokuwa na sifa njema wamekuwa wanakiathiri Chama chetu katika
chaguzi za dola. Uchaguzi huu unatupa fursa nzuri ya kuachana na
viongozi wasiokuwa na sifa njema za uongozi ndani ya Chama chetu.
Katika kipindi hiki cha mageuzi, wana-CCM mmeona mengi na
mmesikia mengi. Viongozi wachochezi sasa mmewajua, viongozi watoa
na wala rushwa sasa mmewajua, viongozi wenye fitina pia mmewajua,
viongozi wanaokumbatia sera za kibaguzi za ukabila, udini na ukanda
nao mmewajua. Aidha, viongozi waadilifu, wazalendo na
wanaounganisha watu kwa kauli zao na matendo yao mmewajua.
Naomba tutimize wajibu wetu.
Wanachama mmepewa fursa ya kutekeleza mageuzi ya uongozi
katika Chama chetu kupitia Uchaguzi Mkuu wa Chama na Jumuiya
zake. Hii ndiyo maana ya kaulimbiu ya sherehe hii: “CCM imara
Inaanza na Mimi”. Hivyo, tusifanye ajizi katika uchaguzi huo. Ada ya
mja kunena, muungwana ni vitendo. Shime tukatende kwa kupiga
kura za mageuzi ya Chama. Kijua ndio hiki, tusipouanika mpunga
tutaula mbichi’.
Ndugu Wananchi na Viongozi wa CCM;
Ni imani yangu kwamba vikao vya Chama vitakavyoshughulika
na zoezi la kuchuja na kupitisha wagombea katika nafasi mbalimbali
watazingatia sifa za kikatiba nilizozitaja ambazo ni ufafanuzi sahihi wa
Katiba ya Chama. Wale watu wenye kukipunguzia Chama chetu hadhi
na sifa kwa kuwa na tuhuma mbalimbali za rushwa, ubadhirifu, wizi
n.k. wasipitishwe kugombea nafasi za uongozi. Aidha, wana-CCM
tusikubali kuchagua viongozi wetu kwa ushawishi wa fedha. Kufanya
hivyo ni haramu kwani kutakidhoofisha Chama chetu na historia
9
itatuhukumu. Jambo hili limeshusha sana haiba ya Chama chetu mbele
ya macho ya Watanzania, lazima tubadilike.
Vile vile tunapochagua wagombea, ni lazima sasa tuangalie
changamoto zilizo mbele yetu katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Tuchague viongozi ambao watakuwa mstari wa mbele kukisemea,
kukitetea na kukipigania Chama chetu katika uchaguzi wa Serikali za
Mitaa 2014 na katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Tusichague watu ambao
ni mzigo na kuwa chanzo cha kukipunguzia Chama chetu sifa na
kutusababishia tusifanye vizuri. Lazima tuwachague viongozi wa
Chama wenye mvuto kwenye makundi yote katika jamii, vijana na
wazee, wanawake na wanaume, maskini na matajiri, wasomi na
wasiokuwa wasomi.
Mwisho naomba wana-CCM wenzangu mjitokeze kwa wingi
kugombea nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali. Hususan
ningependa kuona vijana na wanawake wengi wakijitokeza na naomba
vikao vya kujucha wagombea viwape nafasi wagombee.
Dhima ya CCM katika Mchakato wa Katiba
Ndugu viongozi na wanachama wa CCM;
Mtakumbuka kuwa tarehe 31 Desemba, 2010 katika salamu zangu
za kuuaga mwaka 2010 na kukaribisha mwaka 2011, nilielezea uamuzi
wangu wa kuanzisha mchakato wa kufanya mabadiliko ya Katiba
ambayo hatimaye yatalipatia taifa letu Katiba mpya. Utekelezaji wake
umeshaanza kwa kutungwa Sheria ya mabadiliko ya Katiba. Hivi sasa
Serikali imewasilisha Bungeni mapendekezo ya marekebisho ya baadhi
ya vifungu vya Sheria hiyo kwa nia ya kuiboresha. Mapendekezo hayo
yametokana na sisi wenyewe katika Serikali pamoja na vyama vya siasa
na Baraza la Mashirika ya Kijamii. Kwa upande wa vyama vya siasa
hata Chama cha Mapinduzi kilileta mapendekezo yake tena manane.
10
Baada ya kikao hiki cha Bunge tutaiunda Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ili mchakato wa kukusanya maoni uanze. Napenda kutumia
nafasi hii ya kuadhimisha miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM kuwaomba
wana-CCM wote kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao. Viongozi wa
CCM wa ngazi zote wanalo jukumu la msingi la kuhakikisha kuwa
wanachama wetu wanaelimishwa vya kutosha kuhusu Katiba na
Mchakato mzima wa kutoa maoni. Andaeni mikutano ya kutoa elimu
na watafuteni watu wenye ufahamu wa masuala ya Katiba wasaidie
kuwaelimisha wanachama wetu. Katika kikao kilichopita cha Kamati
Kuu tulikubaliana kuwa Chama chetu nacho kitoe mwongozo wa
mafunzo hayo kwa wanachama. Kazi hiyo inaendelea na
itakapokamilika mtaarifiwa ipasavyo. Kwa muhtasari ninachosema ni
kuwa wana-CCM tujipange vizuri ili tuweze kushiriki kwa ukamilifu
katika mchakato wa kutengeneza Katiba mpya.
Ndugu Wanachama, Viongozi wa CCM na Wananchi Wote;
Kuna msemo wa Kiswahili usemao mcheza kwao hutunzwa.
Napenda kwa niaba yenu nitambue na kutoa shukrani maalum kwa
Wabunge wetu wa CCM kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya
kuelimisha wananchi kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Kulikuwepo na kutokueleweka au hata kupotoshwa kwa Sheria hiyo.
Lakini, kutokana na kazi nzuri waliyofanya sehemu kubwa ya
Watanzania wameelewa. Hata hivyo, kazi hii endeleeni nayo kwani
hatujafika mwisho wa mchakato wenyewe. Hivyo naomba waendelee
kuelimisha sambamba na viongozi wa Chama na watu wenye nia njema
na nchi yetu
Mwisho
Ndugu viongozi na wanachama wa CCM;
Narudia kuwapongeza kwa mara nyingine tena wale wote
waliohusika na maandalizi ya sherehe hizi. Kwa hakika zimefana sana.
11
Zinafanana na hadhi ya mkoa wa Mwanza. Nawapongeza viongozi,
wanachama, makada, wapenzi na mashabiki wa CCM kwa kutimiza
miaka 35 ya uhai wa CCM. Nawaomba tutoke hapa na ari mpya, nguvu
mpya na kasi mpya kwenda kukijenga Chama chetu kote nchini. Na
kwa hapa Mwanza kujiandaa kuyakomboa majimbo ya Ilemela,
Nyamagana na Ukerewe. Kuteleza si kuanguka. Yaliyopita si ndwele,
tugange yajayo.
Ndugu Viongozi, Wanachama na Wananchi;
Kabla ya kumaliza, napenda kusema mambo mawili: Kwanza,
kuhusu vijana Wamachinga. Nimefurahi sana na maneno yenu.
Naahidi kuwa nitawasaidia. Tukutane baadae na uongozi wenu. La
pili, ni kwamba sikuyasemea masuala ya Madaktari na mengineyo kwa
vile katika siku chache zijazo nitapata nafasi ya kufanya hivyo. Kwa ajili
hiyo leo nimeona nizungumzie masuala yahusuyo Chama cha
Mapinduzi.
Mwisho kabisa, napenda kusema kuwa Chama chetu bado imara
na kwamba hatuna budi kuhakikisha kuwa kinazidi kuimarika.
Inawezekana. Timiza Wajibu wako.
.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZIII!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!