Umoja wa Ulaya (EU) umesema ili kuimarisha utendaji na ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, serikali ya Tanzania inatakiwa kutengeneza mazingira mazuri ya biashara yatakayovutia sekta binafsi kuwekeza nchini.
Wito huo unakuja wakati kumekuwa na malalamiko kutoka sekta binafsi juu ya mazingira yasiyo rafiki ya kufanya biashara ambayo yanakwamishwa na ongezeko la kodi katika sekta ya usafiri na ughavi.
Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa EU, Neven Mimica amesema kutekeleza mkakati wa serikali wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri na ughavi katika Kanda ya Afrika Mashariki ni muhimu kuiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuwa yenye ushindani kwa kuboresha miundombinu na ufanisi.
“Mazingira wezeshi ya kufanya biashara ambayo yatavutia uwekezaji wa sekta binafsi ni muhimu katika kuimarisha ushindani wa bandari”, amesema Kamishna Mimica.
Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU), Neven Mimica akiwa na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Van de Geer wakati alipokutana na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam, hivi karibuni kuelezea ushirikiano uliopo katika ya Tanzania na EU.
Kamishna huyo ambaye ametembelea Bandari ya Dar es salaam na kupokelewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Lazaro Twange ambapo alikwenda kukagua mradi mkubwa wa upanuzi wa bandari hiyo unaojulikana kama ‘Dar es Salaam Marine Gateway Project (DMDP)’ ambao unalenga kuifanya bandari hiyo kuwa na hadhi ya kimataifa na kuwezesha kupokea meli kubwa na kuhifadhi mizigo mingi.
Mradi huo wa DMGP umefadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) ambayo ni mshirika wa karibu wa EU ambapo Tanzania imepokea Dola za Kimarekani milioni 345 kukamilisha mradi huo ambapo utaongeza uwezo wa kupokea mizigo kwa tani milioni 25 miaka saba ijayo. Pia utapunguza muda wa kusubiri kutoka saa 80 hadi 30.
Hata hivyo, Kamishna Mimica amesema mradi huo utaongeza wigo wa kufanya biashara za kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki, kuchochea uanzishwaji wa viwanda na kutengeneza ajira nyingi kwa kuwa wananchi wataanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao.
Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imedhamiria kukuza viwanda vya ndani na kuiwezesha nchi kuzalisha bidhaa mbalimbali zitakazoshindana na bishaa zingine katika soko la kimataifa. Ili viwanda vifanye kazi vinahitaji nishati ya uhakika ikiwemo umeme wa maji, upepo na gesi.
Ili kuinua viwanda, UE imetoa msaada wa bilioni 130 kwa ajili ya miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Kamishna huyo amesema nishati ya umeme ni muhimu hususani katika maeneo ya vijijini kwa kuwa inachangia uboreshaji wa huduma za jamii kama shule, vituo vya afya, hospitali, viwanda vidogo vidogo na kilimo.
Ujio wa wawakilishi wa EU unakuja kabla ya Mkutano wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya kufanyika siku ya 28 na 29 Novemba, 2017 ambapo utazikutanisha pande mbili kujadili maeneo muhimu ya ushirikiano ikiwemo nguvu kazi ya vijana kwa maendeleo endelevu.