Upungufu wa vitabu mashuleni ni kero!

Albano Midelo

SHULE ya msingi Ihovyo iliyopo mwambao mwa ziwa Rukwa  katika kata ya Totowe wilayani Chunya mkoani Mbeya inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vitabu hali inayosababisha walimu kushindwa kufundisha baadhi ya mada.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo yenye wanafunzi 348 Beston Mwambene alibainisha kuwa katika somo la Kiswahili stadi ya kusoma kimya haifundishwi kutokana na ukweli kuwa stadi hiyo inahitaji kila mwanafunzi asome mwenyewe kimya.

“Shule yetu ina upungufu mkubwa wa vitabu, kutokana na hali hiyo stadi ya kusoma kimya katika masomo ya Kiswahili na Kiingereza tumeziua kwa kuwa haiwezekani kufanyika  kama shule haina vitabu vya kutosha’’,alisema Mwalimu Mwambene.

Hata hivyo alisema katika masomo ya Lugha ,walimu wanafanya stadi za kusoma kwa sauti kwa kuwa mwanafunzi anaweza kusoma  mmoja mmoja kwa sauti  hata kama shule ina kitabu kimoja na kusisitiza kuwa stadi ya kusoma kimya haiwezekani kwa kitabu kimoja.

Kulingana na Mwambene upungufu wa vitabu katika shule hiyo unasababisha walimu kuandika mazoezi  yaliyopo katika kitabu cha wanafunzi ubaoni badala ya wanafunzi kusoma wao wenyewe kufanya mazoezi kwa kusoma katika vitabu vyao pale wanapokuwa na vitabu vya kutosha.

Alibainisha kuwa upungufu wa vitabu unatokana na fedha ndogo  inayotolewa kwa kila mwanafunzi kwa mwaka ambapo mwaka jana serikali ilitoa kwa kila mwafunzi kiasi cha shilingi 2400  na kwamba mwaka huu hakuna fedha iliyotolewa  hali ambayo imesababisha kushindwa kununua vitabu.

Wanafunzi wa shule  ya msingi Namambo wilayani Chunya mkoani Mbeya ambao wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada.

“  Awali fedha za  ruzuku ya vitabu kwa kila mwafunzi zilikuwa zinatolewa shilingi 10,000,mwaka jana ilitolewa shilingi 2400 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi, mwaka huu hadi sasa hakuna fedha ya ruzuku ya vitabu,

“Wakati mwingine unapewa shilingi 20,000 kwa mwaka kwa ajili ya kununua vitabu,sasa utanunua vitabu vingapi kwa kuwa hivi sasa vitabu vinauzwa kwa gharama kubwa, bei ya kitabu kimoja inafikia hadi shilingi 6000 vitabu ni shida kubwa’’,anasema

Serikali ilipoanzisha  elimu ya msingi bila malipo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM)  mwaka 2002 ilikuja na ubunifu mmoja muhimu kwa kutoa ruzuku kwa kila mwanafunzi.

Kwa upande wake mwalimu wa shule ya msingi Namambo iliyopo katika kata ya Totowe wilayani Chunya Agustino Mlekano anazitaja changamoto zinazoikabili shule yake yenye wanafunzi 450 kuwa  uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia,upungufu wa nyumba za walimu na tatizo la shule kujaa maji kila mwaka msimu wa masika hali ambayo inasababisha vyumba vya  madarasa katika shule hiyo kuanguka na wakati mwingine kufunga shule kwa dharura.

Hata hivyo anasema  ruzuku  kwa kila mwanafunzi iliyokuwa inatolewa awali iliweza kuziba pengo la mapato lililotokana na kuondolewa kwa ada katika shule za msingi na kwamba ruzuku hiyo pia ililenga kuinua ubora wa elimu kwa kuhakikisha kuwa rasilimali muhimu zinapatikana shuleni.

Anabainisha kuwa ruzuku iligharamia ununuzi wa vitabu vya kiada na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunza pamoja na kugharamia ukarabati,gharama za utawala na mitihani.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mlugo ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Songwe Chunya,katika kuhakikisha kuwa jimbo lake linapunguza tatizo la vitabu,hivi karibuni ametoa vitabu 6000 vya kiada na ziada kwa ajili ya shule za sekondari jimboni mwake.

Utafiti ambao umefanywa na  asasi  ya UWAZI iliyopo chini ya Hivos Tanzania mwaka 2010 imebaini kuwa Sera iliyopitishwa awali ya ugawaji wa ruzuku kwa wanafunzi ya dola 10 za kimarekani kwa kila mwafunzi haikuwahi kufuatwa  na kiwango kilichowekwa kwa kila mwanafunzi  ni  kidogo na hakikidhi gharama za vifaa vya kujifunzia.

Kulingana na UWAZI  ruzuku kwa wanafunzi haitoshi kununulia idadi inayokidhi ya vitabu vya kiada,ukitazama orodha ya bei ya vitabu za kampuni moja ya BEN AND COMPANY LIMITED  kati ya mwaka2008/ 2009,pesa iliyotolewa iliruhusu shule kununua si zaidi ya kitabu kimoja tu kwa kila mwanafunzi.

“Iwapo mtoto anasoma masomo sita,vinahitajika si chini ya vitabu sita ambavyo vitapatikana kwa gharama ya shilingi 38,900,chukulia kuwa vitabu vinadumu kwa miaka mitatu hata kama kiasi cha ruzuku kwa mwanafunzi kingekuwa ni shilingi 10,000 kwa mwezi kwa kila  mwanafunzi  kingekuwa pia hakitoshi kununulia idadi inayohitajika ya vitabu vya kiada’’,

Hata hivyo Kuanzishwa kwa ruzuku hii,kumewawezesha watoto wengi toka familia zenye uwezo unaotofautiana kiuchumi kwenda shule,hii imepunguza tofauti ya upatikanaji wa elimu kwa wasio na uwezo kwa kuwa hata watoto kutoka katika familia masikini wameweza  kwenda shule.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *