ASILIMIA 84 ya wananchi wamesema watapiga kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 67 ambao walijitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Idadi hiyo imetokana na utafiti wa Sauti za Wananchi uliofanywa na taasisi ya Twaweza kwa kutumia takwimu zilizokusanywa kati ya Machi 31 na Aprili 17, 2017 ukiwahusisha wananchi 1,805.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo Alhamisi, Juni 15, 2017, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, amesema hata hivyo kwamba, asilimia 8 wamesema huenda hawatapiga kura, na idadi kama hiyo (asilimia 8) hawajaamua kama watapiga kura au la.
“Ieleweke kuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya wananchi wanaosema watapiga kura kutofanya hivyo ifikapo siku ya uchaguzi kwa sababu utafiti wa Sauti za Wananchi wa mwaka 2015 ulionesha kwamba, kati ya asilimia 99 waliosema watapiga kura mwaka huo, ni asilimia 67 tu waliojitokeza kufanya hivyo,” alisema Eyakuze.
Sauti za Wananchi ni utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi ambao kwa sasa una uwakilishi wa Tanzania Bara pekee ukitumia mbinu mbalimbali.
Kuhusu mtazamo na ushiriki katika vyama vya siasa, utafiti huo umeonesha kwamba, asilimia 63 ya wananchi wamesema wapo karibu zaidi na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuliko chama kingine chochote.
Aidha, asilimia 17 wapo karibu na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na idadi ndogo wapo karibu na Chama cha Wananchi (CUF) ambao ni asilimia 1, ACT- Wazalendo (asilimia 1) na NCCR Mageuzi (asilimia 1).
“Asilimia 17 ya wananchi wanasema hawana ukaribu na chama chochote cha siasa,” umebainisha utafiti huo.
Imeelezwa pia kwamba, kukubalika kwa Chadema kumeshuka hadi kufikia asilimia 17 tu ikilinganishwa na asilimia 32 ya wananchi waliosema wapo karibu na chama hicho mwaka 2013.
Wakati huo huo, uungwaji mkono wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa upande wa Tanzania Bara nao umeshuka kutoka asilimia 4 mwaka 2013 hadi asilimia 1 mwaka 2017.
“Hata hivyo, asilimia 17 wanasema hawana ukaribu na chama chochote, ikilinganishwa na chini ya asilimia 5 waliosema hivyo miaka iliyopita,” utafiti huo umeeleza.
Kwa upande mwingine, utafiti huo umesema CCM inakubalika zaidi miongoni mwa wazee, wenye kiwango cha chini cha elimu, maskini, wanawake na wakazi wa vijijini.
“CCM inakubalika zaidi miongoni mwa wazee (asilimia 80), ukilinganisha na asilimia 55 ya vijana. Wanawake (asilimia 68) wanaikubali CCM kuliko wanaume (asilimia 58), maeneo ya vijijini (asilimia 66) kuliko maeneo ya mijini (asilimia 57), na wananchi maskini (asilimia 69) kuliko matajiri (asilimia 53). Wananchi wenye elimu ya sekondari, elimu ya ufundi au elimu ya juu wanaikubali CCM kwa asilimia 46,” imeelezwa katika utafiti huo.
Imeelezwa kwamba, Chadema inakubalika zaidi miongoni mwa wanaume, vijana, matajiri na wenye kiwango kikubwa cha elimu, lakini pale CCM inapoungwa mkono kwa kiwango kidogo haimaanishi moja kwa moja kuwa Chadema inaungwa mkono kwa kiwango kikubwa, hasa katika maeneo ya mijini na miongoni mwa wasomi.
Hata hivyo, miongoni mwa makundi hayo, wananchi wasiofungamana na chama chochote ni wengi kuliko wale walio karibu na Chadema au upinzani kwa ujumla.