Utafiti wa Twaweza: Kati ya Watanzania 10, saba wanamkubali Rais Magufuli

Jamii Africa

WATANZANIA saba kati ya 10 wanaukubali utendaji kazi wa Rais John Pombe Magufuli pamoja na serikali yake ya awamu ya tano.

Hayo yameelezwa katika utafiti wa Sauti za Wananchi uliofanywa na taasisi ya Twaweza kati ya Machi 31 hadi Aprili 17, 2017 ukiwahusisha wananchi 1,805 wa Tanzania Bara.

Utafiti huo ambao umewasilishwa leo Alhamisi, Juni 15, 2017 na Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, umesema kwamba, idadi hiyo ni sawa na asilimia 71 ya wananchi wanaoukubali utendaji wa Rais Magufuli, ikiwa imeporomoka kutoka asilimia 96 ya waliokubali utendaji wake mwaka 2016.

“Kati ya mwaka 2012 na 2015, viwango vya kukubalika kwa Rais Jakaya Kikwete vilikuwa kati ya asilimia 81 na asilimia 87,” umeeleza utafiti huo.

Hata hivyo, Rais Magufuli bado anaendelea kuongoza kwa kukubalika kwa wananchi wake ikilinganishwa na marais wengine wa Afrika, kwani kwa mujibu wa viwango vya kukubalika kwa marais barani humo vilivyorekodiwa katika tafiti 128 za utafiti wa Afrobarometer tangu mwaka 1999 ni asilimia 63.

“Ni kawaida kwa viwango vya kukubalika kwa marais kushuka baada ya kipindi cha mwanzo cha kuingia madarakani. Utafiti wa Pew kwa mfano, unaonesha viwango vya kukubalika kwa marais tisa kati ya 11 wa mwisho nchini Marekani vikishuka,” umeeleza utafiti huo wa Sauti za Wananchi.

Kushuka kwa asilimia 25 ya kukubalika kwa utendaji wa Rais kunaamsha maswali mengi miongoni mwa wananchi ambapo utafiti huo unahoji kama kushuka huko kuna uwiano wowote na matatizo ya upungufu wa chakula na hali ngumu ya uchumi.

“Je, ukosoaji unaofanywa na vyama vya siasa na watu wengine kuwa Rais hatoi uzito wa kutosha katika masuala ya kidemokrasia na haki za binadamu umechangia?” ni swali jingine linalohojiwa kwenye utafiti huo.

Muhtasari wa utafiti huo unaonesha dalili za wananchi kubadilisha matarajio yao ukiwa ni ujumbe kwamba wananchi wanajihisi wameangushwa na utendaji wa serikali katika kushughulikia shida zao za msingi, hususan uhakika wa kipato na kula.

“Hii ni ishara ya kupungua kwa matumaini waliokuwa nayo mwanzoni. Hata hivyo, hawajavuti wa na chama kingine chochote. Wanasiasa wote wanaambiwa kwamba siasa itumike kuwanufaisha wananchi moja kwa moja kwa kuelewa shida zao na kuzitatua kikamilifu,” umeeleza utafiti huo.

Utafiti huo umebainisha kwamba, pengo kubwa la kukubalika kwa Rais Magufuli linaonekana katika makundi ya rika mbalimbali ambapo anakubalika zaidi miongoni mwa vikundi vya wazee na wenye elimu isiyozidi ya msingi.

Inaelezwa kwamba, asilimia 68 wenye umri chini ya miaka 30 wanamkubali Rais ikilinganishwa na asilimia 82 wenye umri zaidi ya miaka 50.

Elimu nayo imetajwa kuchangia, ambapo asilimia 75 ya wananchi wasiokuwa na elimu au wenye elimu ya msingi tu wanamkubali Rais wakati asilimia 63 ya wale wenye elimu ya sekondari au elimu ya juu ndio wanaomkubali Rais. Pia kuna kiwango cha kukubalika ni kikubwa miongoni mwa wananchi masikini (asilimia 75) kuliko matajiri (asilimia 66).

“Hakuna tofauti kubwa katika viwango vya kukubalika kwa Rais kati ya wanawake (asilimia 73) na wanaume (asilimia 70), au kati ya wakazi wa vijijini (asilimia 72) na mjini (asilimia 70),” umeeleza utafiti huo.

Kwa upande mwingine, viwango vya kukubalika kwa wenyeviti wa vijiji/mitaa, kata, madiwani na wabunge vimeshuka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kwa mujibu wa utafiti huo, mwaka 2012, asilimia 88 waliukubali utendaji wa mwenyekiti wao wa kijiji au mtaa, lakini kwa sasa ni asilimia 66 tu walio na maoni kama hayo.

Vilevile, kati ya mwaka 2012 na 2017, idadi ya wananchi waliokubali utendaji wa madiwani wao imeshuka kutoka asilimia 85 mpaka asilimia 59, na idadi ya waliokubali utendaji wa wabunge wao imeshuka kutoka asilimia 79 hadi asilimia 58.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *