UTAFITI: Wagonjwa watoa fedha, vitu  kwa daktari ili wapate upendeleo

Jamii Africa

Licha ya serikali kuboresha miundombinu ya sekta ya afya, bado vituo vingi vya afya vinatoa huduma hiyo kwa upendeleo na kuwabagua baadhi ya wagonjwa ambao hawana fedha.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa Shirika la Twaweza (2017) juu ‘Mitazamo na maoni ya watanzania juu ya rushwa’ unaonyesha kuwa kiwango cha rushwa katika sekta ya afya kimepungua ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita. Lakini changamoto iliyopo ni rushwa kujitokeza kwa sura tofauti ambapo huduma hutolewa kwa upendeleo kulingana mahusiano ya wagonjwa na madaktari wa vituo vya afya.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa rushwa katika huduma za afya imepungua hadi kufikia asilimia 26 mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 62 ya mwaka 2014 ambapo matukio makubwa ya ufisadi ikiwemo Escrow, Richmond, Rada yalisikika kwa viwango vya juu.

Wananchi waliohojiwa na utafiti huo wanasema wanalazimika kutoa fedha au vitu kwa madaktari ili kupata huduma,

“Vitendo vya wagonjwa kumpa daktari wa kituo cha afya cha umma fedha au vitu kwa ajili ya kupata huduma ni asilimia 51”, inaeleza ripoti hiyo ambapo huduma hizo huchukuliwa kama ni msaada na siyo haki ya msingi ambayo kila mwananchi anatakiwa aipate, “Asilimia 73 ya wananchi wanasema rushwa ni kitendo cha kutoa fedha kwa ajili ya kupata msaada”.

 

VIFUATAVYO VINATAJWA KUWA NI VITENDO VYA RUSHWA 

Utafiti huo unatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,705 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka 2017, zinaonyesha kuwa sababu kubwa inayowafanya wagonjwa kutoa rushwa ya fedha na vitu ni kupata upendeleo au kipaumbele wakati wa kuhudumiwa na daktari.

“Asilimia 73 ya wananchi wanataja watu kutaka upendeleo kama sababu moja kuu ya rushwa, na hii hufuatiwa na kukwepa adhabu (asilimia 30) kama sababu nyingine mojawapo, na kupata huduma sahihi (asilimia 24) kama sababu ya tatu”, inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

 

Wakati mwingine wananchi wanalazimika kutoa rushwa kwasababu ya ufahamu mdogo wa aina ya rushwa inayotolewa na mahali sahihi pa kuwasilisha malalamiko yao ili yafanyiwe kazi na wale wanaohusika kupokea wachukuliwe hatua za kisheria.

“Asilimia 56 ya wananchi wanafahamu mahali pa kuwasilisha taarifa za vitendo vya rushwa vilivyofanywa na watumishi wa umma. Hii inahusisha asilimia 42 waliotaja Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), asilimia 10 waliotaja polisi na asilimia 4 waliotaja mamlaka za kijiji na mtaa”, inaeleza sehemu hiyo ya ripoti ya Twaweza.

Mkurugenzi wa Utafiti na Udhibiti wa TAKUKURU, Sabina Seja amesema “Siwezi kusema moja kwa moja rushwa imepungua au imeongezeka ila niseme tu rushwa ipo kila mmoja anapaswa kutambua madhara yake. Tunawaomba waendelee kutupatia ushirikiano”,

Kwa upande wake,  Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zamani amesema  mamlaka zinazopambana na rushwa zinapaswa kuheshimu haki za binadamu. Kutumiwa kwa rushwa ni jambo moja na kubainika kuchukua au kutoa rushwa ni jambo nyingine.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze anasema wananchi wengi wanafurahishwa na jitihada za serikali kupambana na aina zote za rushwa hasa katika sekta ya afya lakini wanakwamishwa na kutokuwepo kwa uwazi na kuruhusu mijadala ya wananchi juu ya njia sahihi za kuboresha huduma za jamii.

“Serikali inafanya vitu vingine vinavyotishia kuathiri vibaya jitihada za kupambana na rushwa kama vile kuminya uhuru wa vyombo vya habari, mijadala ya umma pamoja na kuiondoa Tanzania kwenye Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP)”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *