Utalii wa Fukwe washika kasi Ziwa Nyasa

Jamii Africa

SERIKALI mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, imefanikiwa kuhimiza kasi ya utalii wa fukwe katika Mwambao wa Ziwa Nyasa ambapo tayari watalii wengi wameanza kumiminika.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, fukwe nyingi katika mwambao huo zina mandhari mazuri pamoja na kuwepo kwa vivutio vingine vya utalii vikiwemo visiwa vilivyoko ndani ya ziwa hilo.

Jiwe la Pomonda lenye historia ndefu ndani ya Ziwa Nyasa kwa kuwahifadhi watu waliokimbia Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia.

Taarifa kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa zinaeleza kwamba, tayari watalii wengi wameanza kumiminika katika fukwe mbalimbali kwenye mwambao huo, hali ambayo inaongeza mapato ya taifa.

Mapema mwaka huu 2017, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alifanya ziara ya siku nne ya kutembelea Mkoa wa Ruvuma, ambapo pamoja na mambo mengine, alitembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa huo.

Profesa Maghembe alishangazwa na vivutio adhimu na vya kipekee vya utalii vilivyopo katika wilaya za Nyasa, Mbinga na Songea vinavyoweza kufungua milango ya utalii katika Ukanda wa Kusini huku akisisitiza kwamba utalii wa fukwe unaweza kuwa kivutio kikuu cha utalii kwa Kanda ya Kusini.

Vivutio vingi

FikraPevu inafahamu kwamba, akiwa katika Wilaya ya Nyasa, Waziri Maghembe alivutiwa na vivutio vya Ziwa Nyasa wakiwemo aina zaidi ya 500 za samaki wa mapambo ambao hawapatikani katika maziwa, mito na bahari sehemu nyingine yoyote katika Sayari ya Dunia.

“Tafiti zinaonyesha kuwa katika Sayari inayoitwa Dunia, hakuna ziwa lenye samaki wa mapambo wa aina zaidi ya 400. Ni ziwa Nyasa pekee, ambalo pia linaongoza duniani kwa kuwa na viumbe wengi kati ya maziwa yenye maji baridi. Tuna utajiri mkubwa, ziwa hili litakuwa kitovu cha utalii Ukanda wa Kusini,’’ alisisitiza Waziri Maghembe.

Aliahidi kwamba, wizara yake itaendelea na juhudi za kusimamia uhifadhi wa maeneo yaliyohifadhiwa na kuendeleza vivutio vya utalii katika Ukanda wa Kusini ikiwa ni pamoja na kuvitangaza ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wa pili wa Ziwa Nyasa hasa katika Wilaya ya Kyela, utalii wa fukwe umeshika kasi muda mrefu kutokana na kuwepo kwa Ufukwe maarufu wa Matema.

Ufukwe wa Matema wilayani Kyela

FikraPevu inafahamu kwamba, Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo imejaliwa kuwa na maeneo ya hifadhi na vivutio vizuri vya utalii kama vile Makumbusho ya Taifa ya Majimaji, Mapango ya Chandamali, majengo ya kihistoria Peramiho, samaki wa mapambo, fukwe na visiwa katika Ziwa Nyasa.

Vivutio vingine ni pamoja na maeneo ya wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika, mapori ya wanyamapori ya Liparamba, Selous, Litumbandyosi, misitu ya asili kama Matogoro, Gumburo na Chaburuma na uwepo wa mpaka wa nchi jirani za Malawi na Msumbiji.

Ili kuhakikisha maeneo yote ya vivutio yanapata watalii wengi na kuongeza pato kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa jumla, Waziri Maghembe alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na madaraja ili kuvutia watalii wengi waweze kufika kwa urahisi na kwa muda mfupi.

“Iwapo uboreshaji wa miundombinu utakwenda sambamba na ongezeko la ujenzi na uboreshaji wa hoteli zenye hadhi na sifa za kitalii zitasababisha watalii kukaa muda mrefu katika Mkoa wa Ruvuma, hivyo kuacha fedha nyingi,’’ alisisitiza Profesa Maghembe.

Visiwa kadhaa vilivyoko ndani ya Ziwa Nyasa vina mazingira mazuri ya utalii, mojawapo ni Kisiwa cha Pomonda kilichoko umbali wa kilometa 20 kutoka nchi kavu katika eneo la Liuli na ni mwendo wa dakika 30 kwa kutumia boti au mtumbwi.

Kisiwa hicho kimejaa historia ambapo jiwe kubwa la Pomonda lenye pango liliweza kuhifadhi watu zaidi ya 200 waliokimbia kujificha wakati wa Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia.

FikraPevu imeelezwa kwamba, ufukwe wa Bayi katika Kijiji cha Ndengere, Kata ya Mbamba Bay tayari umekwishapata mwekezaji na umekuwa kivutio kikubwa kwa watalii.

Ufukwe wa Bayi

Desemba 30, 2016, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alizindua tamasha la kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Wilaya ya Nyasa akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo Isabela Chilumba na Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Injinia Stella Manyanya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

FikraPevu imeelezwa kwamba, mbali ya kuzindua tamasha hilo, alihimiza wadau kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya mkoa kuwekeza wilayani humo kwenye shughuli za uvuvi, ujenzi wa hoteli za kisasa pamoja na viwanda vidogo vidogo.

Ujenzi wa viwanda hivyo utasaidia kuifanya wilaya hiyo ipige haraka hatua kimaendeleo katika kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa, kukuza uchumi na kuleta ajira kwa vijana.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *