Vifo vyashamiri kwa wanaotoa mimba Tanzania. Wazanzibari wafanya ngono wakijitambua

Jamii Africa

WANAWAKE 390,000, kati ya milioni moja, nchini Tanzania hutoa mimba kila mwaka kwa njia za kinenyeji.

FikraPevu imeelezwa kuwa idadi hiyo (milioni moja) inawahusu wanawake wanaopata mimba zisizotarajiwa kwa kufanya mapenzi yasiyozingatia njia za kujikinga na mimba. Idadi kubwa ya hawa wanaotoa mimba hufariki dunia, kwani hufanya kitendo hicho kwa kutumia njia za kienyeji na kuhusisha watu wasiokuwa na ujuzi.

Njia za kujikinga na mimba zisisotakiwa ni pamoja na kutumia kondomu, kuhesabu tarehe na kutoingia manii kwa mwanamke.

FikraPevu imeambiwa kuwa baadhi ya wanawake, hasa wenye umri kati ya miaka 16 hadi 23, wamekuwa wakitumia waganga wa kienyeji na mangariba kutoa mimba.

“Wapo wanawake, hasa mabinti, wanaposhika mimba wasizotarajia, huamua kuzitoa kwa njia za kienyeji,” anaeleza Elizabeth Mageni, maarufu – Mama Jully wa Tabata ambaye aliwahi kuwa muuguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Anasema wasichana wengi wakipata mimba wasizotarajia, huamua kuzitoa kwa kunywa maji ya majani ya mwarobaini yaliyochemwa, kutumia majani ya chai mengi na vidonge vya flagyl.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa pamoja na matumizi hayo, hivi sasa vijana wengi wa kike “wanachangamkia” Zaidi kutumia dawa za  Misoprostol  kutoa mimba.

Mama Jully, pamoja na kueleza kuwa hafahamu zaidi kuhusu Misoprostol, lakini anasema “kutoa mimba ni jambo baya linalohatarisha maisha.”

FikraPevu imetembelea maduka ya dawa, maeneo ya Gongolamboto, Mikocheni na Buguruni, yote ya Dar es Salaam na kubaini kwamba dawa hiyo ya Misporostol, imekuwa ikiuzwa sana, tena bila hata cheti cha daktari.

“Kwa kweli tumekuwa tukiuza sana kwa wasichana na wanakuja bila vyeti, sasa unafanyaje na sisi tunataka pesa,” anahoji muuza wa duka moja la dawa Buguruni ambaye ameomba kutotajwa jina lake wala duka.

Ripoti ya utafiti iliyotolewa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ikishirikiana na Taasisi ya Guttmacher na Chuo Kikuu cha Muhimbili mwaka 2015 inathibitisha kuwa “Tanzania ni kati ya nchi zenye uwiano wa juu wa vifo vya wajawazito duniani (vifo 410 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai) na utoaji mimba usio salama ni moja kati ya sababu zinazoongoza.”

“Utoaji mimba usio salama unachangia zaidi ya theluthi moja ya wanaolazwa hospitalini kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba na takribani robo moja ya vifo vya uzazi”.

Mnamo mwaka 2007, Tanzania ilisaini mkataba wa Afrika wa Haki za Wanawake kuwaruhusu kutoa mimba zinazosababishwa na kubakwa au ikiwa ujauzito unahatarisha maisha ya mwanamke.

Katika mkataba huo, wengine wanaoruhsiwa kutolewa mimba kitaalamu ni wanawake wenye magonjwa ya afya ya mwili na akili au maisha ya kiumbe kilichopo tumboni yanapokuwa hatarini.

Matatizo ya kiafya hudhihirika kwa wanawake wanaopelekwa hospitali kutibiwa baada ya kutekeleza vitendo hivyo ambapo wengine hupata ugumba, kupoteza damu nyingi, kifafa cha uzazi na maambukizi hatarishi katika mfuko wa uzazi au mirija ya uzazi na vifo.

Tatizo la utoaji mimba ni kubwa Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Jumuia ya Afrika Mashariki (Kenya, Uganda, Tanzania na Burundi) ambapo uwiano wa Tanzania uko juu ya nchi hizo.

Hatua stahiki zisipochukuliwa kutatua tatizo hili, matukio zaidi yatajitokeza na kuathiri maendeleo ya wasichana na wanawake nchini.

 “Inakadiriwa kuwa, mimba 405,000 zilitolewa ndani ya mwaka 2013 nchini Tanzania. Idadi hii ni kiwango cha utoaji wa mimba 36 kwa kila wanawake 1,000 wenye umri kati ya miaka 15-49 na uwiano wa utoaji mimba 21 kwa kila watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai,” inaeleza ripoti hiyo.

Inaelezwa kuwa kiwango cha utoaji mimba Tanzania ni kikubwa Zaidi ya kile cha wastani wa nchi zingine za Kusini Jangwa la Sahara, ambako kiwango chake ni wastani wa 31.

Matukio ya utoaji mimba yanatofautiana kutoka eneo moja hadi nyingine nchini. Kanda ya ziwa ambayo hujumuisha mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga, Simuyu, Mara na Geita, inaripotiwa kuwa na idadi kubwa ya utoaji mimba ikifuatiwa na Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Njombe na Iringa) huku Zanzibar ikiwa na matukio machache.

FikraPevu inaweza kueleza kwa uhakika kuwa Zanzibar ina matukio machache ya utoaji mimba ikilinganishwa na kanda nyingine kwa sababu wanawake  wa visiwa hivyo (Unguja na Pemba) huanza vitendo vya ngono katika umri mkubwa, hivyo mimba zisizotarajiwa ni chache.

Taarifa zinaeleza kuwa mwaka 2013 Zanzibar ilikuwa na matukio ya utoaji mimba 3,714, ikifuatiwa na kanda ya Mashariki yenye mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro ikiwa na matukio 54,655 na kanda ya Ziwa matukio 120,857.

Ni tofauti na Kanda ya Ziwa ambapo matumizi ya njia za uzazi wa mpango yako chini na  matukio ya mimba zisizotarajiwa ni mengi, hivyo huongeza uwezekano wa mimba nyingi kutolewa.

Kanda ya Mashariki ina matukio machache ya utoaji mimba kwa sababu inafikiwa kirahisi na huduma za afya na elimu ya uzazi.

Baadhi ya tafiti zinaeleza kwamba, kati ya asilimia 27 ya wanawake wanaotumia njia za uzazi wa mpango nchini Tanzania, asilimia 80 wako mijini. Elimu ya uzazi wa mpango ikitolewa kwa usahihi itasaidia kupunguza tatizo la utoaji mimba.

 Wakili wa Kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Anna Shimba  ameiambia FikraPevu kwamba takwimu zinaonesha ni asilimia moja tu ya mimba zisizotarajiwa hutolewa na wataalamu wa afya, hasa katika maeneo ya vijijini.

Anasema pamoja na kwamba kutoa mimba ni kosa kisheria, bado wanawake, hasa wasichana wanatoa mimba bila kujali.

“Ili kupunguza vifo vitokanavyo na utoaji mimba usio salama na madhara yake, serikali inapaswa kuingiza vipengele vinavyohusu haki ya afya ya uzazi vilivyopo kwenye mkataba wa Afrika wa Haki za Wanawake  kwenye sheria za hapa nchini,” anaongeza.

Mwanasayansi mtafiti wa NIMR, Godfather Kimaro, anaishauri serikali na wadau wa afya kuongeza wigo wa kupatikana elimu na huduma za afya kwa wanawake ili kujitambua na kuelewa madhara ya mimba zisizopangiliwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *