Vigogo watajwa mauaji wa albino Tanzania, lakini hakuna aliyekamatwa

Jamii Africa

CHAMA cha watu wenye ulemavu wa ngozi Mkoani Kagera (Albino) kimeieleza timu ya Tathimini ya Utawala Bora Barani Afrika (APRM) kuwa watuhumiwa wakubwa wa mauaji ya kundi hilo la walemavu ni wanasiasa na viongozi wanaosaka madaraka serikalini.

Picha-Mwenyekiti wa Chama Cha Watu wenye Ulemavu wa ngozi (Albino) Mkoa wa Kagera Burchard Mpaka

Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Mkoani Kagera, Burchard Mpaka, aliiambia timu hiyo iliyokutana na wadau wa utawala bora jana mjini Bukoba, ya kuwa mtandao wa wanasiasa na viongozi wanaotafuta viungo vya albino umesababisha baadhi yao kukimbia makazi yao.

Kwa mujibu wa Mpaka mbele ya Timu hiyo yenye wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali kutoka nchi za Afrika, alidai yameshatokea mauaji saba ya watu wenye ulemavu Mkoani Kagera.

“Watoto wenye ulemavu wa ngozi wamebaki kuwa wakimbizi watuhumiwa wakubwa ni wanasiasa, viongozi wanaotafuta madaraka serikalini na wafanyabiashara wa madini. Wanasiasa eti wakipata viungo vya albino wanashinda kura nyingi,”alidai Menyekiti huyo.

Hata hivyo maelezo ya Mpaka yalimfanya kiongozi wa timu ya APRM mkoani hapa Profesa Aderick Nade kutoka nchini Nigeria, ahoji ni wanasiasa wangapi wamefikishwa mahakama kutokana na tuhuma za kujihusisha na mauaji ya albino.

Washiriki wa mkutano huo walijibu kwa pamoja kuwa hakuna mwanasiasa aliyekamatwa,na kuwauliza tena kama ni hivyo ni nani wamefikishwa mahakamani na kujibiwa kuwa wanaoshitakiwa ni wakulima.

Profesa Aderick Nade kiongozi wa timu ya APRM liyofika Mkoani Kagera

Akizungumza na wadau hao Profesa Nade aliyeongoza timu ya wataalamu tisa waliofika Kagera wakiwa miongoni mwa 21 waliowasili hapa nchi mapema wiki hii, alisema lengo la Mpango wa Tathimini ya Utendaji kwa Nchi za Afrika (APRM) ni kuangalia mwelekeo mpya wa Bara hilo na kutafsiri misingi ya utawala bora.

Pia alisema tathimini hiyo inalenga kubaini mambo yaliyofanywa na serikali na kama yanafanyika kwa wakati, haki na uwiano sawa ukiwemo mgawanyo wa rasilimali za umma na ushirikishwaji wa wananchi katika maendeleo yao.

Awali akifungua mkutano huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Nassoro Mnambila, alisema Serikali inakabiliwa na changamoto kubwa katika suala la utekelezaji wa misingi ya Utawala Bora.

Alikiri kuwa miongoni mwa maeneo ambayo Serikali haijafanya kwa kiwango cha kuridhisha ni kuendelea kuwepo kwa maujai ya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe na baadhi ya makundi kutoshirikishwa kikamilifu katika masuala ya kisheria.

Hata hivyo Mnambila alisema suala la Utawala Bora linabeba tafsili pana katika matumizi bora ya rasilimali zinazotakiwa kuwa chanzo cha huduma bora, kujali haki za binadamu na Serikali kuwajibika ipasavyo kwa wananchi walioiweka madarakani.

Hoja zitakazobainishwa na timu ya wataalamu hao kutoka nchi mbalimbali zitawasilishwa katika kikao cha wakuu wa Nchi za Afirika kinachotarajiwa kufanyika Julai jijini Lilongwe ambazo zitatolewa majibu na wakuu wa nchi.

Habari imeandikwa na Phinias Bashaya mwandishi wa Fikra pevu-Kagera

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *