Vijiji vya Masoko wilayani Rungwe vyakumbukwa miradi ya maji

Jamii Africa

Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inaelekeza kuwapatia wananchi waishio vijijini maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao. Lengo ni kufikia asilimia 85 ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2020.

Lakini matakwa hayo ya sera yamekuwa ni ndoto isiyotekelezeka kwa wananchi wengi wa vijijini ambao bado hawapati maji safi na salama na wakati mwingine hutembea umbali mrefu kuyafuata kwenye vyanzo vya uhakika.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Maji na Umwagiliaji zilizochapishwa kwenye tovuti ya wizara hiyo, hadi sasa, miundombinu ya maji iliyojengwa ina vituo vya kuchotea maji 123,888 ambavyo vina uwezo wa kuhudumia watu milioni 30.97 sawa na asilimia 85.2 ya wananchi milioni 36.34 waishio vijijini.

Hata hivyo, kati ya hivyo, vituo 85,286 tu ndivyo vinavyofanya kazi na kutoa huduma kwa watu milioni 21.32 sawa na asilimia 58.7 ya wananchi waishio vijijni.

Hali hiyo imechangiwa na changamoto ya mfumo uliopo wa usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji. Vijiji mbalimbali zimeendelea kukabiliwa na changamoto ya upotevu mkubwa wa maji kabla ya kuwafikia wananchi ikilinganishwa na kiwango kinachokubalika Kimataifa cha asilimia 20.

Pia ongezeko la shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo vya maji imekuwa ni changamoto inayosababisha uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Jumla ya vyanzo 298 vya maji vilibainishwa kuwa katika hatari ya kuharibika na kuathirika.

Kusimamia na kuendesha miradi ya maji ikiwa ni pamoja na kuviimarisha Vyombo vya Watumiaji Maji

 

Mikakati ya serikali

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Eng. Isack Aloyce Kamwelwe amesema ili kuwapunguzia wananchi gharama za uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza kubadilisha mitambo inayotumia nishati ya dizeli kusukuma maji na kufunga mitambo inayotumia nishati ya jua.

“Vilevile, Serikali inaandaa mifumo itakayofaa kusimamia na kuendesha miradi ya maji ikiwa ni pamoja na kuviimarisha Vyombo vya Watumiaji Maji”, amesema Eng. Kamwelwe.

Amebainisha kuwa wizara yake  inaendelea kutekeleza Mpango wa miaka mitano wa Utunzaji wa Rasilimali za Maji wa mwaka 2014 –2020 kwa lengo la kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji pamoja na kuzijengea uwezo taasisi 15 zinazosimamia  rasilimali za maji nchini ili wananchi waishio vijijini wapate maji kwa wakati.

“Wizara imeendelea kutafuta vyanzo vipya vya maji pamoja na kufanya tathmini na usanifu katika vyanzo vilivyobainishwa ili viweze kuendelezwa kwa matumizi mbalimbali,” amebainisha Eng. Kamwelwe.

Serikali inaendelea na ujenzi wa miradi ya maji vijijini pamoja na kutekeleza programu mbalimbali za kuimarisha uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji vijijini.

 

Mradi wa Maji Masoko

Mradi wa maji wa Masoko unaotekelezwa katika Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya na unahusisha ujenzi wa vituo 335 vya kuchotea maji, vidakio vya maji, matanki sita ya kuhifadhia maji na ulazaji wa mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 204.7.

Waziri Eng. Kamwelwe amesema  kukamilika kwa mradi wa maji wa Masoko kutaongeza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wapatao 19,624 wanaoishi katika vijiji vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa, Ikama, Itagata, 37 Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga.

Katika mwaka 2018/2019 Wizara imetenga Shilingi milioni 420 kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa mradi huo.

Hata hivyo, bajeti ya 2018/2019 iliyotengwa ya bilioni 727.3 itaweza kutatua tatizo la ukosefu wa maji vijijini?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *