Viongozi wetu wanataka wakumbukwe kwa yepi?

Ramadhani Msoma

Kila mara niangaliapo jinsi mambo yanavyoendeshwa na walio kwenye madaraka ya umma na hasa katika serikali za hivi karibuni kuna jambo ninaloliona haliko sawa. Nafahamu ili uweze kufanya kazi yako vizuri iwe katika ofisi za umma au binafsi lazima uwe na ari na hamasa ya kuifanya hiyo kazi ili iwe na matokeo mazuri na mwisho wa siku tuwe na hayo maendeleo tunayoyataka.

Historia inatufundisha jinsi baadhi ya watu waliopata kuwa viongozi kwenye nchi nyingine  walivyoweza kufanya makubwa na kuacha majina yao mioyoni mwa watu waliokuwa wakiwaongoza “legacy”. Kwangu mimi, kiongozi lazima uhamasishwe na kuiacha hiyo legacy ili watu wakukumbuke hata baada ya kutoka uongozini na hata baada ya kutangulia mbele za haki (kufa).

Kwa bahati mbaya wengi wa watu wetu katika uongozi suala hilo haliwapi motisha. Watu hawa wanapenda vyeo “ubwana mkubwa”, na vitu vingine viendanavyo na ubwana mkubwa mathalani magari mazuri. Pia nyakati zingine kupata fursa za kusukuma masuala yao ya kujinufaisha binafsi (biashara; halali na zisizo halali) kwa kutumia hizo nafasi kupata hili au lile kinyume na utaratibu. Ukisoma historia za nchi za wenzetu na hata ya kwetu kwa wakati fulani kulikuwa na watu wenye hamasa hiyo mfano; Mwalimu Nyerere, kina Bibi Titi au Edward Sokoine ambao bado wanaishi kwenye mioyo ya watanzania.

Kwa nchi za wenzetu zinazopiga hatua kubwa za kimaendeleo, viongozi wao walikuwa na ari ya kufanya makubwa kwenye nchi na kuacha majina mazuri kwenye utendaji wao kwa mataifa na serikali wanazoziongoza. Watu kama Mahathir Mohamed (waziri mkuu wa zamani wa Malaysia), Lee Kuan Yew (ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Singapore) bado wanaishi kwenye mioyo ya watu waliokuwa wakiwaongoza kwa michango yao katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi. Watawala wetu wanajua haya lakini ni kama hawana hamu hiyo ya kukumbukwa na kuingia kwenye historia ya nchi hii! Na kama huna hamasa hiyo bali tu ya kujitajirisha wewe na familia yako, kwa kweli huna haja ya kuumiza akili yako kutafuta uongozi wa umma. Wananchi wanapaswa kuwaogopa viongozi wa namna hii. Wanapaswa kuwakataa na kutokuwapa ridhaa!

Tatizo kubwa linalosababisha ukosefu wa hamasa ya ikiwemo ya mambo ya msingi kama kupiga vita umaskini au kupambana na rushwa ambayo ni matatizo yanayoikwamisha nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo ni kutokuwa na mipango na fikra za kutizama masuala kwa muda mrefu. Wengi wa watawala wetu kutokana na matendo yao yanasanifu zaidi fikra zao kuwa katika vipindi vifupi vifupi kwa uwepo wao madarakani (kadiri ya vipindi vya kiuchaguzi). Hawataki kufikiria na kutizama taifa katika muda mrefu  hata baada ya wao kuondoka madarakani muda mrefu baadaye kwa hiyo hawana haja na kuacha majina yao yatajike kwa sababu nzuri.

Kuondoa umaskini na kupiga vita rushwa kwa vitendo badala ya maneno matupu ya kwenye majukwaa ya kisiasa tu ndiyo ingekuwa msukumo hasa unaowapa hamasa watawala wetu kutaka nafasi serikalini. Kwa kweli Tanzania isingewasahau kwa mchango huo lakini hakuna juhudi zinazotia matumaini yaani juhudi hazilingani na ukubwa wa matatizo. Bado kuna upungufu hasa wa kiutendaji kama tukipima kwa matokeo.

Nchini Brazili rais wao wa zamani, Lula da Silva atakumbukwa sana katika kujenga uchumi wa kisasa nchini mwake na hasa kupunguza umaskini wa kutupwa kwa kuwaondoka wabrazili milioni 30 kutoka kwenye umaskini wa kutupwa. Je, viongozi hujiuliza wanataka kuwaondoa watanzania wangapi kwenye umaskini wa kutupwa labda ndani ya miaka mitano?

Brazili ni mbali lakini tuangalie waethiopia watamkumbukaje waziri mkuu wao Meles Zenawi  aliyefariki mwaka jana (2012) ambaye alisimamia ukuaji wa uchumi wa Ethiopia kwa wastani wa asilimia 11 kwa miaka saba toka mwaka 2004 mpaka 2011 (kwa mujibu wa ripoti ya shirika la fedha la kimataifa (IMF)? Mwandishi na mchumi aliyebobea Joseph E. Stiglitz aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa “Globalization and Its Discontents”  juu ya waziri mkuu huyo wa zamani wa Ethiopia; “Meles showed that, with the right policies in place, even a poor African country could experience sustained economic growth, (Meles ameonyesha kwa kuwa na sera nzuri hata nchi masikini ya Afrika inaweza ikapata maendeleo chanya kwenye  maendeleo ya kiuchumi- tafsiri yangu).

Nawapongeza baadhi ya watendaji na mawaziri katika awamu hii hasa baada ya mabadiliko yaliyofanyika kwa kujitahidi kubadilisha hali ya wizara wanazoziongoza na taasisi zake. Tunapaswa kutambua bado kuna kazi kubwa mbeleni. Nilipata fursa kumsikiliza waziri wa uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe wakati wa uzinduzi wa safari za treni katika mji wa Dar es Salaam; kutoka Ubungo kwenda Stesheni akasema kuhusu hatua hiyo kuwa ni “kiburi tu cha mtu masikini”. Naamini tunahitaji kiburi hicho cha kujaribu pia kwenye maeneo mengine ya kupunguza kero hapana nchini.

Kwa ujumla, uongozi ni dhamana na sio kazi tu kama kazi nyingine kwamba mwisho wa siku alimradi mkono uende kinywani. Kiongozi inabidi awe mtu anayeweza kujinasibisha na watu maskini ambao ni wengi katika nchi hii. Mara nyingi naona kama wapiga kura nyakati nyingine hatufahamu ni nini viongozi wetu tunatakata watufanyie na namna gani wasipoenenda tuwawajibishe, ndiyo maana tunavumilia tu utendaji mbovu.

Ili mtu awe kiongozi lazima awe na hamasa ya kuleta mabadiliko na awe na hamasa ya kuacha jina zuri nyuma yake. Lazima awe mtu mwenye maono ya mbali, uelewa wa kutosha wa jamii hii ya watanzania anayefahamu matatizo ya watanzania na kama aliwahi kuwa kwenye uongozi basi angalau tujue aliwahi kufanya nini kwenye uongozi wake kabla labda hatujamchagua kuwa mbunge au rais.

Kinachosikitisha haionekani hamasa ninayoijadili katika nyuso na juhudi za wengi wanaoutaka urais wa mwaka 2015; naona uroho wa madaraka! Wataka uongozi wengi  hawatuonyeshi uongozi sasa! Watuonyeshe uongozi sasa kabla ya kuanza hizo mbio zao. Haiwezekani watu watumie muda mwingi kutafuta uongozi kana kwamba hiyo ni shughuli ya kudumu na pamoja na kuwa wako kwenye uongozi wa aina fulani, tayari badala ya kutumia muda huo kuonyesha uongozi washaanza kuwazia madaraka zaidi! Tumeshashuhudia baadhi ya viongozi walioenda na njia ya kutumia nguvu na mikakati mingi kupata madaraka na namna walivyoshindwa kuibadilisha nchi. Hivyo hatupaswi kuingia katika mtego ule ule.

16 Comments
  • kaka  msoma  nimesoma  kwa  makini  sana  makala  yako, ni  makala  nzuri  na  ya  kuumiza  sana  kwa  sababu  walengwa  hasa  wa  makala  yako  ni  viongozi.viongozi  wa  nchi  yetu  hawana  sifa  za  kiuongozi  kwani  mara  zote  wamwteuliwa  kirafiki  na  kindugu  ama  kichama  na  wala  si  kwa  vigezo  vya  uchapakazi.ukiwaangalia  kwa  machoo  kama  ya  kwangu  ya  miwani  utaona  kuwa  wala  hawana  haja  ya  kukumbukwa  kwani  tayari  matumbo  yao  yatawakumbuka, nyumaba  ndogo  zao  zitawakumbuka  ma  mabaa  makubwa  makubwa  ya  sinza  yatawakumbuka!!!!

    • Yah kweli Enock kuna shida ya uongozi nimependa hiyo observation yako kwamba watakumbukwa na matumbo yao.Tusiache kuwakumbusha lakini

  • That’s true, most of tanzanian leaders wapo for their own benefit,hvyo hawana jambo la mcng litakalopelekea wao kukumbukwa,,,jaman viongoz kumbuken mpo madarakan ili muwatumikie wananch na co kujinufaisha urself…

    Wekeni UZALENDO mbele ndio utakaosaidia kuiondoa nchi yetu kwenye umaskin pia HOFU YA MUNGU inahitajka ndani yenu.

    MUNGU IBARIKI TANZANIA.

    • Asante Joel kwa kusoma asante pia kwa kuwakumbusha viongozi watu majukumu yao tutafika tu, Kama sio sisi basi watoto na wajukuu zetu

  • Watanzania hatuna budi kuamka, tumebarikiwa kuwa na nchi yenye kila kitu ila uovu na kutowajibika kwa wachache kwa viapo walivyoweka kwenye hizo nafasi ndio kinachoirudisha nyuma nchi yetu. Tanzania inanuka, jamani watanzania tuamkeni.

    MUNGU IBARIKI TANZANIA

  • Ebana nimesoma article yako hongera sana kwa mchango mzuri kwa jamii yetu ambayo imejaa wapiga kura wa kipindi cha uchaguzi tu,wakipewa pesa ya pombe na kanga zenye picha ya mgombea…lakini ujumbe huu tunapata wa mjini tu ambao tuna uelewa mkubwa zaidi ya kijijini ambapo viongozi wetu wanapata kula nyingi sana kwa kuwalagai wananchi uko..!article km hizi zisomwe na watu vijijini pia wapate uelewa..

    • Yah Ben unayosema ni kweli inabidi elimu hii pia iende pembezoni ambako ni vijijini tujitahidi tutafiki tu huko tunakotaka kwenda.Asante kwa kusoma

  • ni changamoto nzuri viongozi wanaipata toka kwa Rama. lakini viongozi wanapatikanaje? walikua na vision na mission zipi kabla ya kupata madaraka? je wanapokua madarakani ni kwa vipi madaraka yanawaadhibu au kuwatunuku? mkataba gani tumewekeana saini kuufuata kati ya wananchi na watawala? 

  • Chriss viongozi wetu ni wa kawaida sana.Benchmark aliyoweka nyerere ni ya juu sana hawaifikii.Kama wananchi tusiwaache wakatuburuza tuangalie ni vipi tunawapata na tuwasaili vizuri kabla ya kuwaamini na hizo nafasi

  • JAMANI WANATAKIWA KUKUMBUKWA KWA HAYA:

    1:KUDANGANYA WANANCHI WAWAPO MADARAKANI

    2:KUJIPATIA MIANYA YA KUWA WAFANYA BIASHARA WAWAPO MADARAKANI.

    3:WACHEZA DILI MAARURU.

    4:WAPUUZIAJI WA VITU MUHUMU VYA MAENDELE NA USTAWI WA JAMII YA KITANZANIA.

    5:MATAJIRI KUTOKA SERIKALINI VIZIWI,VIPOFU NA WASIIOONA SHIDA ZA WATANZANIA KWA VIZAZI VIJAVYO.

    6:WANAOIPENDA NCHI KATIKA MAJUKWAA NAKUSEMA TUMIENI BIDHAA ZA KITANZANIA LAKINI WAO NI WAKWANZA KUNYA HEINEKEN KAMA BIA BORA,NYAMA ZA KUSINDIKWA KUTOKA MAGHARIBI N.K

    7:WANAO WAANDAA WARITHI WA VYEO NA NAFASI ZAO ILI SIRI ZAO ZISIFICHUKE.

    8:WAPENDA UBWANYENYE NA UHESHIMIWA WAKATI WAO TUMEWATUMA NA KUWALIPA VIZURI WATUTUMIKIE NA WANASAHAU WAJIBU WAO.

    9:WENYE KUTOA MAAMUZI KAMA WAO HAWATA STAAFU AU KUACHA KAZI

    10:WASIO MUOGOPA MUNGU KWA KUKAA MBELE YA MAJUMBA YA IBADA,KUTOA SADAKA NYINGI ILI WATUKUZWE

    (MUNGU WABARIKI WATANZANIA WENYE FIKRA SAHIHI KWA AJILI YA WATANZANIA WENZAO).

    • Robin,

      Nimependa kwa hayo mambo 10 unayodhani viongozi wetu ndo wanataka wakumbukwe nayo.Ulivyosema ni kweli kwa hivyo kama jamii yabidi tuamke na tuhakikishe wanatutendea haki kwenye uongozi wao tuwabane inavyowezekana ni jukumu letu sote.

      Asante sana kwa kusoma!!

  • Rama nimependa article yako,mi huwa najiuliza hii nchi mshauri ni nani?ambaye anatupeleka huku,viongozi wamekuwa hawana uzalendo as if wao wana inchi yao.lakini nashukuru watu tunauelewa siku hizi.lakini solution ni kumpata kiongozi ambae atakua dictator kwenye maamuzi nadhani tutanyooka.wanasema “roma haikujengwa kwa siku”,a day will come na kunawatu tutashuhudia wanaelekea “The hague”.

  • Yah Jose tunaangushwa na viongozi nguvu wanazozitumia kwenye kutafuta uongozi wangezitumia kwenye kuleta maendeleo tungekuwa mbali.Kuna tatizo la kiuongozi  Tanzania na labda duniani kwa ujumla.Tanzania tatizo hili ni kubwa zaidi na watu tubadilike ili tuwabane watawala watutumikie sio wajitumikie wao na familia zao.

    Asante kwa Kusoma JOSE

  • Yah Jose kuna tatizo kubwa sana la kiungozi hapa Tanzania wengi wanapenda uongozi lakini viwango vidogo.Watu wengi smart wanaona siasa uzushi.Viongozi wetu wangekuwa na viwango hii sio nchi ya kuwa maskini na kama unavyojua amani yetu pia imeanza kuwa hatarini ni wakati wao wa kutuonyesha uongozi sasa!!

    • Tatizo la wengi sasa hivi ni kutokuwa na utu wa kitanzania, kila mtu antaka kuwa kiongozi kwa manufaa yake na anatumia nguvu nyingi sana aingie kwenye madaraka matokeo akipata hiyo furksa fikra zake zinakuwa hazilengi kwenye mafanikio ya nchi bali mafanikio yake binafsi ambyo huzaa hasara kubwa kwa taifa hasa kwenye swala la mikataba mbalimbali ya sekta muhimu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *