Mauaji ya Mwandishi Iringa: Waandishi wataka Waziri, IGP wang’oke

Jamii Africa

WAKATI Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC) ikituma ujumbe mzito mkoani Iringa, Chama cha waandishi wa habari mkoani Mbeya, kimetoa tamko rasmi la kumtaka waziri wa mambo ya ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa kujiuzulu mara moja kufuatia matukio ya mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polsi ikiwemo la Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari mkoani Iringa, Daud Mwangosi.

Tukio la kuuwawa kwa Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi

Aidha MBPC  imetoa tamko la  kusitisha kuandika habari zozote zinazohusiana na Jeshi la Polisi nchini, kuunda tume  ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi ambaye pia ni mwandishi wa habari wa Channel Ten  itakayowahusisha  wanahabari na wadau wengine na siyo DCI Manumba na maofisa wengine wa jeshi la Polisi na kuvitaka vilabu vyote vya wanahabari nchini kuunga mkono kauli hiyo.

Akitoa tamko hilo lililojadiliwa na wanachama wa Mbeya Press Club,uhindini jijini Mbeya leo,Mwenyekiti wa MBPC,Christopher Nyenyembe amesema wamepokea taarifa ya kifo cha Mwangosi kwa masikitiko makubwa  na wanahabari wameathirika kisaikolojia na kiutendaji.

Nyenyembe ambaye pia ni Mwakilishi wa gazeti la Tanzania Daima mkoani Mbeya   alisema wanahabari mkoani Mbeya wamekubaliana kwa pamoja kutoandika habari za polisi hadi watakapowahakikishia usalama na mazingira mazuri ya kufanya kazi nao kwa kuweka mikataba ya kufanya nao kazi  ikiwemo na vyama vya siasa.

Alisema Viongozi wa juu wenye dhamana ya ulinzi na usalama wamekuwa wakifumbia macho matukio ya Polisi kuuwa raia na kutoa taarifa zisizo sahihi  kutokana na kuwashirikisha polisi hivyo wana kila sababu ya kuwajibika kuhusiana na tukio hilo na mengine yaliyoundiwa tume kwani yanahatarisha uvunjifu wa amani.

“Tunataka waziri wa mambo ya ndani ajiudhuru,IGP Said Mwema,RPC Kamhunda,walioshiriki Nyololo na wale waliohusika kufanya mauaji,lakini pia tunasitisha kuandika habari za Polisi na wanasiasa hadi pande zote  tubaliane kuandikishiana mkataba wa kufanya nao kazi,kwa sababu tunaokufa ni sisi wa chini mbona hata Viongozi wa siasa hawafi,”alisema

Mwenyekiti huyo alisema kuwa Jeshi la Polisi lina maofisa habari wao hivyo waendelee kuwatumia hadi pale watakapotekeleza tamko hilo,na kuhakikisha usalama wa wanahabari katika kazi.

Alisema Mwanahabari huyo amekufa kishujaa akiwa kazini huku akiendelea kutetea haki za mwanahabari mwenzake hadi tone la mwisho la damu  na kwamba ni ushindi mkubwa kwa wanahabari wote na kuendelea kupata ujasiri wa kufanyakazi.

“Tusivunjike moyo ingawa  hali hii inatudhihirisha jinsi tulivyo na mazingira magumu na mwangosi amekufa kutokana na mfumo mbaya wa serikali kutothamini media kama mhimili wa nne wa nchi…sote tumeona alivyouawa kinyama na kikatili haiwezi kuvumilika, tunatoa pole kwa familia, Iringa Press Club na wanahabari wote,”alisema.

Matukio ya kupigwa,kunyang’anywa vifaa vya utendaji wa kazi na kudhalilishwa kwa waandishi wa habari  yametokea mara kwa mara ambapo Mwanahabari wa chombo kimoja cha radio (jina tunalihifadhi) alipigwa bomu la machozi wakati akiripoti laivu katika chombo chake kuhusu tukio la vurugu za wamachinga jijini Mbeya.

Tukio jingine limewahi kutokea maeneo ya Airport  ambapo mwanahabari mmoja amewahi kunyang’anywa kamera  na polisi  akiwa anapiga picha mwili wa marehemu licha ya mwanahabari huyo kuwapa taarifa Polisi katika tukio hilo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Nyenyembe,alisema taarifa za kuwasiliana na Viongozi wa klabu ya Iringa ambapo taarifa za awali zinasema kuwa mwili wa marehemu Mwangosi unatarajiwa kuzikwa wilayani Rungwe ambako ndiko nyumbani kwa marehemu.

Tayari Umoja wa Vyama vya waandishi wa Habari umemtuma ujumbe mzito mkoani Iringa kufuatilia sakata hilo, kushiriki mazishi na kuangalia hatua zaidi za kuchukua. Marehemu Mwangosi alikua  mjumbe wa Umoja huo.

Imeandikwa na Thompson Mpanji, FikraPevu – Mbeya

20 Comments
  • Hata ninyi wahandishi wengi wenu ni vinyonga.

    Kama kweli hizi habari zimewauma kutoka rohoni basi msiandike habari za CCM na serikali yake. kuhusu vyama vingine andikeni ili ccm na serikali yake waumie.

    Mnajua wazi kuwa ccm wana vyombo vya habari, pia serikali nayo inavyo vyake, so hayo maamuzi ya kusitisha vyama vingine ni sawa na kuendelea kuipigia kampeni serikali ya CCM kwani itatumia mwanya huo kujisafisha kwa kutumia vyombo vyake pamoja na vle vya serikali.

    Tafakari na mchukue hatua, watanzania kwa sasa hutudanganyiki hata mkitumiwa tunajua la kufanya.

  • Sitashangaa mkigeuza ukweli kuwa uongo maana nanyi ni waoga kuliko dr. ulimboka.

    IGP anafanya vikao na viongozi wenu, wakisha Chukua Chao Mapema wanasahau waliyotendewa na mpaka sasa wanausalama wanafanya kila juhudi kuipoza familia ya marehemu na kigogo mmoja wa ccm anatumiwa kwa hili ili kutoa misaada na ahadi tele kwa familia kuipoza na kuwashauri wasiambatane na waandishi habari pamoja na wana CHADEMA. Mda si mrefu hatutasikia chombo chochote kikizungumzia habari hii.

    Tunajua chenu mtachukua lakini jamii isipotoshwe kwa hili.

  • kimsingi masikitiko hayaishi kwa kumpoteza mpiganaji.

    Kwa wanaomfahamu marehemu mwangosi bila shaka hawataacha kubaini umuhimu wake hasa wakati huu atakapokosekana.

    Bila shaka ipo haja sasa waandishi wa habari kuelewa hatari inayotukabili tunapokuwa kazini, hasa na wanasiasa kwani licha ya kuwa katika wajibu wetu wa kitaaluma na kijamii, wenzetu wamekuwa hawana nadhari kwetu na kutufanya kuwa ni wahanga wa matendo yao.

    Kama mwanachama wa Press Club napenda niungane na msimamo wa MBPC kwani ni hatari iliyo ndani yetu na ni vyema nasi tukalielewa hilo badala ya kushabikia mambo kwani wanasiasa wanatutumia na polisi wanatuua na kutunyanyasa badala ya kutulinda.

    • Sikuungi mkono kwa suala moja, vyama vya siasa vinachangia mwananchi kupata haki yake.

      Acha uccm ndg yangu, wanawatumia kwa maslai ya nani? miundombinu mibovu, mishahara haitoshi, katiba mbovu halafu unadai wanatumiwa!!

      Nakushangaa sana kwa sababu kwa haraka unadhani waandishi hawahathiriki na matatizo hayo y kijamii, inamaana unataka wananchi wakiandamana kupinga mfumko wa bei waandishi wawe wapi? walimu wakihitaji maslai bora ili vijana wetu wapate elimu stahili waandishi wawe wapi?

      Madaktari wakidai haki zao ili watoe huduma bora kwa wananchi waandishi wawe wapi? Suala unalolisema linamkono wa serikali kuwapoza kwa maneno mepesi na nyororo bila kuchukua hatua kama ilivyotokea Zanzibar kwenye uchomaji wa makanisa.

      FIKIRI KWA MAKINI NDUGU YANGU USIKUWA MMOJAWAPO UNAYETETEA SUMU huku ukijua watakao angamia na wewe umo.

  • ni ujinga kukubali kila amri tena isiyo halali. IGP anaformulate laws zake, anajipa kibali cha kuua, analeta undugu kwenye mambo ya kitaifa. polis wanaua wanaumiza na wengine wanageuzwa vilema yeye anachekelea 2 il-hali aendelee kusifiwa na rais na chama tawala. siwaelewi kabisa hasa ikulu sijui inatoa kauli gani kuhusu hili.

  • waandishi siwaelewi kama kweli mnafikili kwa makini, kaeni na mtafakari hili kwa makini maana tunaona kama mnacheza mchezo wa kuigiza huku maisha ya mwenzenu yamepotea bila hatia.

  • hivyo ndivyo jeshi la polisi lilivyo jipachika jina baya la uuwaji wa raia badala ya usalama wa raia. lakini je hii yote ni kwa faida ya nani ccm au serikali ya ccm ni mbaya sana vyombo mvya dola kugeuzwa vyuombo vya watu fulani kwa kuwa jeshi la polisi kwa sasa si usalama wa raia inabidi huyu mkuu wa jeshi hili ndg said mwema ajiwajibishe bila kusubiri kuwajibishwa maana kazi imemshinda.

    Na kama hataweza yeye binafsi kujiondoa madarakani inabidi tumpeleke mahakamani mara moja kujibu mashtaka ya mauaji wa raia wasio na hatia. binafsi nimesikitika sana kwa mauaji haya. nimtakie marehemu mwangosi mapumziko mema na wale woote walioo uwawa wakiwa chini ya jeshi la polisi.

    Shime watanzania tupinge kwa nguvu zetu zoote huu uovu unaofanywa na jeshi la polisi kwakutumia kodi zetu nwenyewe kwa kweli huuu ni upuuzi wa kupitiliza.

  • waandishi itisheni maandamano nchi nzima, mnajifanya kuhuzunika na kusikitishwa na jambo hili kumbe hakuna lolote, mnageuza kifo cha mwenzenu kuwa mtaji wenu na kujiingizia kipato mifukoni.

    Kwa sasa mnasubili mpewe chenu ili mtulie na mjadala huu ufungwe. Siwaungi mkono hata kidogo kwa sababu najua mtailaghai jamii, roho za watu ziwe juu juu, huku nyuma mpozwe na kutulia tuli zaidi ya maji ndani ya glass. Mfano halis ni huu: Gazeti la mwanahalis lilifungiwa, mlijifanya kuwa mbogo mkaishia kwenye tamko dhaifu la kutoandika habari za wizara husika.

    Huu ni udhaifu mkubwa ningekuwa mimi ningeshauri habari zote nzuri za serikali ya CCM na za Chama tawala zisitolewe kabisa. pili mabaya yote yanayofanywa na serikali na chama chake yapewe kipaumbele. Sasa ninyi mnataka chenu ili msusie habari zote za vyama vya siasa ili ccm na serikali wanufaike kwa sababu wanavyombo vyao. Acheni woga itisheni maandamano nchi nzima ili wananchi tuwaunge mkono kuishinikiza serikali kutenda haki mahali husika. videos zipo tume ya nini kufanya uchunguzi kama sio kwamba mnataka kupeana ulaji?

    Serikal inasema vikao havikuwa halali kwa sababu ya sensa, lakini mbona dr. bilal aliendelea mkutano wa hadhara kuitangaza ccm? msitufanye wajinga, waandishi wengi ni mamluki wa ccm ndiyo maana hamwezi kutoa maamzi stahiki. nawashauri kama hamtaweza kuchukua hatua stahili basi kuweni kimya kuliko kutulaghai sisi huku mkiwa na chenu mifukoni. Kumbukeni leo ni yule, kesho waweza kuwa wewe au mwanao, mzazi wako, rafiki au jirani.

    UNGANISHENI JAMII NA WATANZANIA WOTE TUANDAMANE KUPINGA UBABAISHAJI HUU

  • hivi ni kwann siku zote lawama zote ziende upande mmoja tu,watanzania tuangalie kwa makini mambo haya tujiulize nini chanzo ndipo tuanze kulaumu

  • Waziri wa mambo ya ndani ameunda tume, itafute majibu ya maswali, ambayo hata mtoto mdogo anayajua majibu hayo. Tume inatakiwa kumtaja aliye amuru polisi wakawapige raia wasio na hatia hata kusababisha vifo. Na hatimaye wote wafikishwe mahakamani.

    • itamaliza leo hiyo tume? mauaji ya arusha tume ilisemaje?, ya dr. ulimboka? mauaji ya songea? morogoro? tupo!

  • inauma sana kuona serikali yetu imetugeuka!
    Dah, nakumbuka usemi usemao…mafahali wawili wagombanapo nyasi hupata shida! Jamani tanzania ya leo si ile tena ya kisiwa cha amani, bali ni kisiwa cha mauwaji, uporaji wa mali za wanyonge, yaani ni nchi iliyo jaa uchafu wa kila aina wa manyanyaso
    Kiukweli katika tanzania ya leo maskini kama mimi hatuna haki kabisa, leo hii kauwawa mwandishi imesikika lakini ningeuwawa miye au maskini mwenzangu hata jirani yangu hasingejua..
    Inauma sana, serikali yetu kutugeuka, jesi la polisi halitufai kabisa lipo kwa ajili ya maslai binafsi na si kwaajili ya kutulinda watanzania!

    Jamani watanzania, narudia tena jeshi la polisi halitufai………….!

  • imefika wakati serikali igeuke nyuma na kuangalia wapi tulikuwa, mshikamano tulionao, na hali halisi ya sasa kwa kweli hali iliyopo hivi sasa ni mbaya na kinyume na maadili ya mtanzania kwa kweli tumefika katika red point.

  • Kuhusu kukamatwa askari aliyeuwa sio dawa, mbona waliobaki ni vibaraka na wamefundishwa kufanya alichofanya huyo mmoja. kazi bado, tena naona kama anaonewa tu maana kama kweli alisomea anatambua kabisa alichofanya kuwa ni kutii amri, atafutwe aliyemtuma na mwingine na yeye awe wa mwisho kuhukumiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *