Wafungwa wamuonya Rais Kikwete kuhusu posho za wabunge

Jamii Africa

WAFUNGWA wa Gereza Kuu la Musoma mkoani Mara, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete na Bunge la Jamhuri kutoidhinisha posho mpya ya sh. 200,000 za wabunge, badala yake fedha hizo ziongezwe kwenye mishahara ya wafanyakazi, wakiwemo Majaji na Mahakimu, ili kujenga taifa llisilo na mizizi ya rushwa kubwa kubwa.

Wamesema, nyongeza hiyo ni matumizi mabaya ya fedha za walipakodi wa Kitanzania, na kwamba licha ya wao kuwa wafungwa hawataki kabisa kusikia wala kuona Rais akiidhinisha malipo hayo waliyoyaita ni ‘malipo ya anasa’, na waliwataka wabunge wote wa CCM kuungana na wabunge wa Chadema kukataa posho hizo walizodai hazina manufaa kwa taifa, bali manufaa binafsi.

prisoner
Kauli hiyo ya wafungwa wa Gereza la Musoma, imetolewa leo na mbunge wa Jimbo la Musoma mjini, Vincent Nyerere (Chadema), baada ya kutumwa na wafungwa hao alipofanya ziara juzi ya kutembelea wafungwa hao kisha kuwapa zawadi ya vifaa mbali mbali za kijamii, ikiwa ni kusherehekea pamoja sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya kwa furaha.

Akizungumza na FikraPevu, mbunge huyo wa Musoma mjini, Nyerere alisema: “Wafungwa wameniambia hawataki kusikia Rais ama wabunge wanakubali kupewa posho ya sh. 200,000 badala ya sh. 70,000.

“Tena wametaka kuona wabunge wa CCM wanaunga mkono msimamo wa wabunge wa Chadema kukataa posho, badala yake fedha hizo waongezewe mishahara majaji, mahakimu na watumishi wengine!. Wanaamini hiyo itaondoa vitendo vya rushwa kubwa kubwa”, alisema Nyerere akinukuu maagizo aliyopewa na wafungwa hao wa Gereza la Musoma mkoani Mara.

Kwa mujibu wa mbunge Nyerere, kero nyingine iliyoelezwa na wafungwa hao ni kuhusu kucheleweshwa kusomwa kesi za watuhumiwa walio wengi, hivyo kusababisha mrundikano mkubwa wa watuhumiwa wakiwemo mahabusu gerezani humo pasipo sababu zozote za msingi.

Walisema, hivi sasa asilimia kubwa ya watuhumiwa waliomo gereza hilo la Musoma ni mahabusu ambao kesi zao zinaonekana bado zinapigwa danadana na vyombo vya dola, na kumtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani kuhakikisha mahakama zinaondoa ukiritimba wa kuchelewesha kusoma kesi.

“Ndugu zetu wanalalamika sana mrundikano wa mahabusu gerezani ambao kesi zao hazisomwi. Wameniomba nifikishe kilio chao hiki Serikalini ili hatua zichukuliwe kuondoa hali hiyo mbaya”, alisema Nyerere ambaye amekuwa na desturi ya kutembelea wafungwa na kuwapa zawadi mbali mbali.

Hata hivyo walisema, wanahitaji kuona kila mkoa Serikali inajenga ofisi za majaji, ili kuondoa ucheleweshwaji wa kesi na matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kuwagharimia majaji punde wanapokwenda kusikilia na kutoa hukumu katika kesi za watuhumiwa waliopo mikoani, na kwamba wabunge wanatakiwa waishinikize Serikali kutekeleza hilo haraka sana iwezekanavyo.

Kuhusu Katiba mpya, wafungwa wa gereza hilo la Musoma waliitaka Serikali kuhakikisha inawashirikisha katika mchakato mzima wa kuundwa kwa chombo hicho kwani na wao ni Watanzania na wanastahili kushirikishwa katika mambo muhimu kama hayo.

Walisema, ingawa wapo gerezani, lakini wamekuwa wakifuatilia kwa umakini mkubwa kupitia vyombo vya habari (televisheni, redio na magazeti), mwenendo mzima wa kuundwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wanataka Serikali isiwabague katika kutoa mawazo yao wanavyotaka katiba iwe vipi, na kazi hiyo ifanywe kwa kila gerezani hapa nchini.

“Tunataka Serikali ipite kila gereza kuchukuwa mawazo ya wafungwa kuhusu namna tunavyotaka katiba iwe. Hatutaki kuona tukibaguliwa katika hili la katiba mpya, maana na sisi ni Watanzania na tunahaki ya kuthaminiwa na si kubaguliwa”, walisema wafungwa hao wa Gereza la Musoma mkoani Mara, kupitia kwa mbunge wao, Nyerere.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Musoma

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *