Wagonjwa wanyang’anywa chakula na nyani Bunda

Jamii Africa

NYANI  wanaoishi katika  milima wa Balili, Bunda mkoani Mara, sasa  wamefikia  hatua ya kusaka vyakula vya wagonjwa  wanaolazwa  kwenye wodi za  Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda.  Hayo  yalibainika wiki  iliyopita, wakati  Fikra Pevu  lilipoamua  kutembelea  hospitalini hapo baada ya kupata taarifa  kwamba  wanyama aina ya nyani  wameanza kuwa kero na wakati mwingine kusababisha  hasara pamoja na hofu  miongoni mwa wagonjwa  katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda..

 

“ Mimi  nilipigwa kofi na nyani; na kisha nikanyang’anywa mkate” alidai  mwanamke  aliyejitambulisha kwa jina la Rita Ikandalo ambaye alisema alikuwa hospitalini kwa siku kadhaa,  kwa ajili ya kumuhudumia  mgonjwa  mmoja (jina linahifadhiwa)ambaye ni  ndugu yake.

 

Ikandilo  alisema   kasheshe  hilo lilitokea  Desemba 16 mwaka huu, majira ya saa 3 asubuhi, baada ya  kundi la nyani  kuingia wodini.

 

“ … katika  tukio hilo nyani  alinipiga kofi  na kufanikiwa kuchukua chakula. Hata hivyo  alipasua chupa yangu ya  chai” alidai mwanamke mwingine  aliyejitambulisha kwa jina la Wegesa Chacha(miaka 53).

 

Wegesa alisema   wakati huo  yeye  alikuwa  nje ya wodi  akipumzika na kwamba  baadaye nyani hao walitokomea  mlimani.

 

Alisema  hiyo ni mara  ya kwamba kukumbwa na mkasa huo  na hali hiyo imezua  hofu miongoni mwa wagonjwa  waliolazwa  hospitalini hapo.

 

“ Tukio hilo lipo; lakini usinitaje kwa sababu mimi siyo msemaji wa hospitali” alisema mmoja  wa Wauguzi katika Hospitali hiyo.

 

Alisema mara kadhaa nyani huonekana  kuzagaa   ndani ya uzio wa hospitali ingawa hawajawahi  kusikia  kuwa  wamesababisha madhara  kwa wagonjwa.

 

Daktari Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Said Kalamba  hakupatikana ofisini kwake. Ilidaiwa kuwa alikuwa  nje ya ofisi kikazi.

 

Hata  hivyo, kwa nyakati tofauti tangu juzi simu ya  Kalamba ilikuwa ikiita  pasipo kupokelewa.

 

Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda iko pembezoni mwa mlima Balili; ndani ya eneo la Mamlaka ya Mjimdogo wa Bunda.

 

Mwisho.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *