Wagonjwa zahanati ya Bujonde walala sakafuni, Waziri awalaumu viongozi kutowajibika

Jamii Africa

Zahanati ya Bujonde ni miongoni mwa zahanati 29 zilizomo katika Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya lakini siku za hivi karibuni imeibua mjadala kutokana na uchakavu wa miundombinu ambapo imewalazimu wagonjwa kulala chini.

Zahanati hiyo iko katika kata ya Bujonde yenye  wakazi zaidi  ya 7,165 lakini haikidhi mahitaji  ya wananchi hao ikizingatiwa kuwa miundombinu yake imechakaa na kutishia afya za wagonjwa ambao wanatibiwa katika zahanati hiyo. Sehemu kubwa ya jengo lake imeharibika huku kuta zikiwa na nyufa kwasababu halijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.  

Kulingana na Sera ya Afya (2007) inaeleza kuwa, “Upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya. Aidha, upatikanaji wake ni moja ya vivutio kwa wananchi kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya”.

Licha ya sera ya Afya kusisitiza uwepo wa mazingira mazuri ya utoaji huduma katika zahanati, wakazi wa Bojonde hawafaidiki na kodi zao ikizingatiwa kuwa miundombinu ya Zahanati iliyopo katika kata yao imechakaa na maboresho ya haraka yasipofanyika afya za wakazi hao zitaendelea kuwa mashakani.

Ukifika katika jengo la zahanati hiyo utashangaa kuona kama kweli ni zahanati kutokana na mazingira yake ambayo sio salama kwa wagonjwa kulazwa hapo. Kubwa zaidi ni kukosekana kwa vitanda na wagonjwa kulazwa chini kwenye sakafu yenye vumbi ambapo hutandika nguo ili kujisitiri huku usiri ukikosekana kwasababu vyumba vingine havina madirisha na vifaa muhimu kama meza na viti vya kukalia.

 

Mgonjwa akiwa amelala chini katika Zahanati ya Bujonde iliyopo Wilaya ya Kyela

Pia zahanati hiyo haina uzio kuwahakikishia usalama wagonjwa wanaopelekwa kutibiwa na kuwaweka katika hatari ya kuvamiwa wakati wowote. Jengo hilo halina huduma muhimu za usambazaji wa maji na umeme kama muungozo wa sera unavyoelekeza ili kuhakikisha zahanati inakuwa ni sehemu salama ambayo mgonjwa akifika anapata matibabu sahihi.

Kwa wakazi wa Bujonde upatikanaji wa huduma bora za afya imekuwa ni changamoto ya muda mrefu na kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo katika hospitali zenye mazingira mazuri ya matibabu. Lakini kutokana na umasikini wa baadhi ya wakazi wa kata hiyo hutaabika na kupoteza maisha.

Zahanati ya Bujonde ni kielelezo cha hali halisi ya changamoto za miundombinu zinazoikumba sekta ya afya katika maeneo mbalimbali nchini ambapo zahanati nyingi hazina hadhi ya kuwa sehemu ya kutolea huduma kutokana na uchakavu wa miundombinu na uhaba wa watumishi wa afya.

Jengo la Zahanati ya Bujonde iliyopo Wilaya ya Kyela

 

Uendeshaji zahanati hutegemea mapato ya Halmshauri na michango ya wananchi katika maeneo husika. Lakini ufinyu wa bajeti na kukosekana kwa utashi wa kisiasa huwa kikwazo katika uboreshaji wa afya za wananchi. Na tatizo kubwa liko katika maeneo ya vijijini ambako mazingira sio rafiki kwa watumishi kwenda kufanya kazi.

Waziri aitupia lawama Halmashauri

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema amepata taarifa za zahanati hiyo, wizara inazifanyia kazi. Hata hivyo ameitupia lawama Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kwa kushindwa kusimamia utendaji wa zahanati ya Bujonde ikizingatiwa kuwa jukumu hilo liko mikononi mwao.

“Lakini hapa mimi naona ni uzembe wa halmashauri husika,wameshindwa kufanya ukarabati wa zahanati hii au kujenga nyingine”, amesema Waziri Ummy huku akieleza kuwa serikali imetoa vitanda 25 kwa kila Halmashauri ili kukabiliana na upungufu wa vitanda katika vituo vya afya.

Usimamizi wa Zahanati uko chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambayo ina jukumu la kusimamia na kuboresha miundombinu ya zahanati na vituo vya afya. Kutokana na ufinyu wa bajeti inayoelekezwa katika sekta ya afya haikidhi mahitaji yote ikiwemo ukarabati wa majengo na ununuzi wa vifaa tiba.

 Hata hivyo, juhudi za kumpata Mkurugenzi wa Manispaa ya Kyela kuelezea hali halisi ya zahanati hiyo hazikufanikiwa kwasababu simu yake ilikuwa haipatikani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *