Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe amesema hatotumia laini ya kampuni ya simu ya Vodacom kama adhabu kwa uamuzi wa kampuni kufanya shindano la urembo wa Miss Tanzania wakati nchi ikiomboleza.
Zitto aliyasema hayo katika taarifa aliyoituma kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii jana mchana ikiwa ni siku moja baada ya watu zaidi ya160 kufariki dunia baada ya meli ya abiria LCT Spice Islander kupinduka na kuzama wakati ikisafiri kutoka Unguja kwenye Pemba.
Zitto alisema katika taarifa hiyo kuwa alisikitishwa sana na hatua ya kampuni hiyo kuendelea na mipango yake ya kufanya shindano la Vodacom Miss Tanzania 2011 hata baada ya ajali ya meli hiyo kutokea.
“Jumatatu, tarehe 12 Septemba 2011 ni siku ya hitma ya kuwaombea marehemu wetu. Nimeamua kutotumia simu yangu ya Voda kwa siku nzima, sina njia ya kuiadhibu kampuni hii isipokuwa kugoma kutumia simu yao japo kwa siku moja kuonyesha kutoridhishwa kwangu na uamuzi wao wa kutojali msiba huu kwa Taifa,” alisema Zitto katika ujumbe huo.
Katika taarifa hiyo Zitto amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliamua kukatiza ziara yake ya nchini Canada iliyokuwa imeandaliwa kwa muda mrefu na kwa gharama kubwa ili kuweza kushiriki kwa karibu katika janga hili kubwa la taifa. Hata hivyo, waandaji wa shindano la urembo la Miss Vodacom Tanzania 2011 waliona kuwa ilikuwa ni hasara kubwa kuahirisha shidano la urembo usiku huo.
“Hata wafadhili wao Kampuni ya simu za mkononi ya vodacom ambao miongoni mwa waliofariki wamo wateja wa vodacom, waliendelea na shindano hili,” sehemu ya tamko hilo ilisema.
Jumamosi asubuhi baada ya kupata taarifa za ajali hiyo, mbunge huyo kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alisema kupitia mtandao wa Twitter kuwa alikuwa ameahirisha safari yake kuelekea kwenye jimbo la Igunga ili kujiandaa na maandalizi ya kampeni za kiti cha ubunge.
Mpaka jana jioni, kampuni ya Vodacom ilikuwa haijatoa tamko lolote kuhusiana na tukio hilo lakini Ofisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Vodacom Tanzania, Bi. Mwamvita Makamba alisema kwenye mtandao wa Twitter kuwa alifurahishwa na maongezi na Waziri wa Afya wa Zanzibar Juma Duni Haji na kuongeza kuwa bidhaa muhimu zilizohitajika zingefika visiwani humo Jumatatu asubuhi kutoka kampuni ya Vodacom.
Alitoa shukrani kwa timu ya Vodacom huko Zanzibar kwa kazi yao nzuri na kusema akaunti ya kuwachangia wahanga wa tukio hilo kupita M-pesa itaanza kufanya kazi leo saa 12 asubuhi kupitia Vodacom Red Alert.
Watumiaji mbalimbali wa mitandao ya JamiiForums, Twitter na Facebook walisema haikuwa sawa kuilaumu kampuni ya Vodacom wakati waandaji wa shindano la Miss Tanzania ni Lino International na wadhamini wa shindao hilo ni kampuni zaidi ya moja.
Hata hivyo, Zitto aliungana pia na watu wengine kukilaumu kituo cha Televisheni cha Taifa (TBC1) kuwa kilikuwa kinaonesha muziki wa Taarab na baadaye vipindi vingine vya kawaida bila kutoa habari kwa umma kuhusu msiba huo.
“Watanzania waliokoa wakiwasiliana kupitia twitter na facebook walikuwa na hasira sana na kituo cha TBC1 kutoonyesha au kupasha habari juu ya ajali hii. Mpaka saa moja jioni kituo hiki cha Televisheni ya Taifa kilikuwa kinaonyesha watu wakicheza muziki wa Kongo, wanawake wakikatika viuno na hata ngoma za asili,” sehemu ya taarifa hiyo ilisema.
“Boti hiyo ilikuwa ya mizigo na siyo ya abiria”, alisema Zitto na kuongeza kuwa wakuu wa mamlaka zinazohusika watawajibishwa baada ya kumaliza kwa maombolezo ya siku tatu.
“Mkuu wa Bandari ya Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe na Waziri wa Miundombinu Hamad Masoud wanapaswa kufukuzwa kazi mara moja kama hawatawajibika wenyewe kwa kujiuzulu.
Kufukuzwa kwao kazi hakutarudisha ndugu zetu duniani bali itakuwa ni somo kuwa hatutarudia tena kufanya makosa yaliyoleteleza ajali kama hii,” alisema Zitto.
Hongera zito una akili kushinda viongozi wako
mi namshangaa zito, ameona mashindano ya urembo tu? mbona waliendelea na kampeni zao kule Igunga na kuna msiba wa taifa, mbona mechi za mipira ziliendelea na vitu vingine vingi tu, cha msingi ni sisi wenyewe kama tungejua kuwa kuna msiba wa watanzania wenzetu tungekaa majumbani na tusingeenda kuangalia hayo mashindano, tufikirie kabla hatujaongea jamani. ni mtazamo wangu tu