Wakazi Ileje wasubiri barabara ya Shs. 107.6bil. kuwaunganisha na Malawi

Daniel Mbega

WAKAZI wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe wamesema hawataamini ahadi ya serikali ya kujenga barabara ya Mpemba-Isongole mpaka watakapoona imekamilika, kwani wamemchoka na ahadi nyingi zisizotimia.

Akizungumza na FikraPevu kwa simu kutoka Isongole katika mpaka wa Tanzania na Malawi, James Mwandemane alisema kwamba, ahadi iliyotolewa hivi karibuni kwamba Serikali imetenga Shs. 107.56 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 50.3 kwa kiwango cha lami haiwezi kuwashawishi kuamini mpaka waone utekelezaji wake.

“Hizi ahadi zimetushosha, kumekuwepo na ahadi nyingi kuhusu barabara hii na nyingine zilitolewa na Rais (Dkt. John) Magufuli wakati ule akiwa Waziri wa Ujenzi, lakini hazikuwahi kutekelezwa, matokeo yake wananchi tunalazimika kwenda nchi jirani ya Malawi kupata huduma za afya,” alisema Mwandemane.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, licha ya makao makuu ya Mkoa wa Songwe kuwa katika Mji wa Vwawa wilayani Mbozi badala ya Mkwajuni huko Chunya kama ilivyokuwa awali, lakini bado miundombinu mibovu ya barabara imewafanya wakazi wengi hasa wa Kata za pembezoni mwa wilaya hiyo kuwa na wakati mgumu wa kufika huko kupata huduma mbalimbali.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, jumla ya wakazi 52,539, wakiwemo wanaume 24,677 na wanawake 27,864 kutoka Kata za Bubipu, Chitete, Ibada, Isongole, Itumba, Ngulilo na Ngulugulu, ambao ni karibu nusu ya wakazi wote wa wilaya hiyo, wanashindwa kufika katika makao makuu ya mkoa kutokana na ubovu wa barabara.

Wilaya ya Ileje ina jumla ya Kata 18, Vijiji 71 na Vitongoji 317 – vyote vikiwa ndani ya eneo la kilomita za mraba 1,880.35 na kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, wilaya hiyo ina wakazi 124,451, kati yao wanaume 58,453 na wanawake 65,988 huku kukiwa na wastani wa wakazi wanne katika kila kaya.

Katika ziara yake hivi karibuni, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani, alisema ujenzi huo ulipangwa kuanza mwezi Juni 2017 na kwamba utakamilika Juni 2019 kwa kuwa tayari wamekwishapata mkandarasi.

"Tayari mkandarasi amepatikana na sasa ameanza kufanya maandalizi ya kuleta vifaa vitakavyotumika katika ujenzi huu, Serikali ya imedhamiria kukamilisha ahadi hii kwa miezi ishirini na nne toka pale ujenzi utakapoanza," alisema Eng. Ngonyani.

Barabara hiyo inatarajiwa kujengwa na kampuni ya M/s China Engineering Corporation.

Aidha, akasema kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ni katika hatua za kutekeleza ahadi iliyotolewa na Serikali kwa wanachi wa mkoa huo katika vipindi tofauti tofauti vya uongozi.

"Wananchi wa hapa wana shauku kubwa na barabara hivyo kukamilika kwake kutasaidia kuufungua mkoa huu kwa upande wa Malawi ambao tunapakana nao na hivyo kukuza shughuli za kibiaahara baini ya nchi hizi mbili na kupelekea kukuza uchumi kwa wakazi hawa," alisisitiza.

Ahadi nyingi

FikraPevu imeelezwa kwamba, kukosekana kwa barabara hiyo kwa muda mrefu kumeifanya Wilaya ya Ileje iwe kama ‘kisiwa’ hasa nyakati za masika ambapo wananchi wanashindwa kwenda kwenye Hospitali ya Rufaa Mbeya kupatiwa matibabu ambako ni umbali wa kilometa takriban 200 kutoka Isongole, mji mdogo ambao uko mpakani.

“Kumekuwapo na ahadi nyingi za viongozi wa kisiasa na wasio wa kisiasa kuhusu kujengwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami lakini zote hazijawahi kutekelezwa na badala yake imekuwa ikitumika kama kigezo cha kuombea kura wakati wa uchaguzi,” alisema Salome Mwanahapa, mkazi wa wilaya hiyo.

Akaongeza: “Mwaka 2014 Rais Magufuli alipokuwa Waziri wa Ujenzi alisema barabara itajengwa kwa kiwango cha lami kama barabara zingine lakini hadi sasa haijajengwa, na mwaka 2015 wakati akigombea urais aliahidi kuwa barabara hiyo itaanza mapema kujengwa kwa kiwango cha lami.”

FikraPevu inakumbuka kuwa, mwaka 2014 wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, Dkt. Magufuli alisema serikali ingejenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mpemba-Itumba 58km ili kufungua fursa za uchumi wilayani Ileje na kuhakikisha barabara hiyo inaungana na nchi ya Malawi kwa kiwango cha lami.

“Barabara ya lami ni muhimu kujengwa katika Wilaya ya Ileje ili kukuza uchumi wa wananchi ambao wana mazao mengi yanayohitaji usafiri wa uhakika kufikia masoko,” alifafanua Dkt. Magufuli.

Dkt. Magufuli alizungumzia umuhimu wa kuiunganisha Wilaya ya Ileje na mtandao wa barabara unaoanzia Bukoba –Biharamulo- Uvinza-Mpanda-Sumbawanga-Tunduma-Mpemba-Isongole hadi Chitipa nchini Malawi ambapo ikikamilika kwa lami itafungua ukanda muhimu wa biashara na kukuza uchumi wa nchi.

Subira Cheyo, mkazi wa Kata ya Ngulugulu, alisema kwamba akinamama wengi wa wilaya hiyo wanalazimika kupata huduma za afya na uzazi katika Mji wa Chitipa nchini Malawi siyo kwa sababu tu ya huduma za bure zinazotolewa, lakini pia ni kutokana na eneo hilo kuwa karibu na kufikika kwa urahisi.

“Kutoka huku kwenda Wilaya ya Chitipa nchini Malawi ni rahisi sana kuliko kwenda Vwawa au Mbeya, halafu wenzetu tayari wamekwishajenga barabara ya lami hadi mpakani Isongole,” alisema Subira.

Asilimia kubwa ya barabara ya Mpemba-Isongole ni tambarare na haina milima itakayoigharimu serikali kwa ajili ya kupasua miamba au milima.

Inatengewa fedha kila wakati

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Rosemary Senyamule, alipata kukaririwa akisema kwamba barabara hiyo imekuwa na ahadi tangu awamu ya nne ya uongozi wa nchi lakini hazijatekelezwa licha ya kupangiwa bajeti.

Alisema katika bajeti ya mwaka 2015/16 zilitengwa Shs. 1.9 bilioni lakini hadi mwaka wa fedha ulipokwisha zilikuwa hazijatolewa.

“Kiasi hiki cha fedha kilitengwa lengo likiwa ni kukarabati barabara ili kupitisha magari makubwa lakini ahadi hiyo haikukamilika… katika bajeti ya mwaka 2016/17, barabara hiyo ilikuwa imetengewa Shs. 16 bilioni.

“Barabara hii imekuwa na ahadi nyingi sana wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 tuliahidiwa kuwa itajengwa kwa kiwango cha lami na hata Waziri Mkuu mstafu, Mizengo Pinda, wakati wa ziara yake aliahidi kuwa itajengwa,” alisema Senyamule.

Lakini hivi karibuni, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Eng. Yona Kasaini, alimhakikishia Naibu Waziri Ngonyani kuwa wakala utasimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati na viwango vinavyokubalika.

"Barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami ya daraja la kwanza ili kuiwezesha kudumu kwa muda mrefu, tutahakikisha kazi hii inakamilika kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo kwenye mkataba wetu,” alisema Eng. Kasaini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *