Wakulima wa tumbaku hatarini kukosa soko, mahitaji ya zao hilo yapungua duniani

Jamii Africa

Mafanikio ya mkulima ni kupata soko la mazao ambalo litakuwa na bei nzuri ambayo itampatia faida na kurudisha gharama zote uzalishaji alizotumia katika kipindi chote cha kulima kwake.

Bei ya mazao hutegemea zaidi mahitaji ya wanunuzi. Kulingana na kanuni za kiuchumi kadiri mahitaji yanapokuwa makubwa na bei ya bidhaa huongezeka. Vilevile kadiri mahitaji ya bidhaa yanapopungua na bei hushuka, hapo ndipo hasara hutokea kwasababu bidhaa huwa nyingi sokoni kuliko mahitaji halisi ya walaji.

Kanuni hiyo ya soko imewakumba wakulima wa zao la tumbaku hasa katika mkoa wa Tabora ambao ndio mzalishaji mkubwa wa zao hilo nchini Tanzania. Kinyume na matarajio ya wanunuzi wa zao hilo, wakulima wamezalisha tumbaku nyingi kuliko mahitaji ya wanunuzi ambao kila mwaka hukubaliana na wakulima hao kiwango kinachohitajika kwa muda husika.

Licha ya kuwepo kwa shehena kubwa ya tumbaku ghalani ambayo imekosa wanunuzi, wakulima hao wanakabiliwa na changamoto nyingine ambayo kupungua kwa mahitaji ya zao hilo duniani ambapo wanaharakati wanaendesha kampeni ya kuzuia zao hilo na kuwataka wakulima walime mazao mengine. 

Tumbaku inatajwa na wataalamu wa afya kusababisha magonjwa mbalimbali kikiwemo kifua kikuu na kansa ya mapafu. Pia ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira kutokana na kutumia nishati ya kuni inayotokana na ukataji wa miti.   

Ili kuwanusuru wakulima wa tumbaku na hasara wanayoweza kuipata ya kukosa soko, serikali imeanzisha majadiliano na nchi nne za India, Misri, China na Iran ambazo zimeonyesha nia ya kununua shehena hiyo ya tumbaku.

Akizungumza katika kikao cha tisa cha Bunge la Tanzania, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa amesema katika msimu 2016/2017 wakulima wamelima tumbaku nyingi kinyume na makubaliano na wanunuzi. Amewata wakulima kuwa wavumilivu wakati serikali inaendelea na jitihada za kuwatafutia wakulima hao soko la uhakika katika nchi mbalimbali duniani.  

 “Kwa kawaida wakulima huingia kwenye makubaliano na wanunuzi kulingana na kiwango cha tambuku kinachotakiwa kuuzwa lakini mwaka huu inaelekea kuna mavuno mengi matokeo yake bado shehena kubwa iko ghalani”, amesema Waziri Mkuu.

Kulingana na maelezo ya Waziri Mkuu, mpaka sasa nchi ya India imeonyesha muitikio mzuri na timu ya wataalamu wa Tanzania inafanya mazungumzo na wanunuzi juu ya bei. Serikali inataka wakulima wafaidike na bei nzuri ili kuboresha maisha yao na kuongeza Pato la Taifa.

Bei elekezi ya tambaku kwa msimu huu 2016/2017 ni kati ya shilingi 4,400 na 4,500 kwa kilo ambapo serikali imeziagiza kampuni za ndani kununua tambuku kwa shilingi ya Tanzania ili kuwawezesha wakulima kufaidika na zao hilo.

Wadau na wanaharakati wameitaka serikali kutafuta suluhisho la kudumu la tumbaku nchini. Njia mojawapo ni kukaa na wakulima hao ili kuwatafutia zao mbadala ili kuwaepusha na madhara ya tumbaku kwa afya zao na kuzuia uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wao, Chama Cha Wakulima wa Tumbaku Duniani (ITGA) kimeitaka serikali ya Tanzania kufungua milango ya majadiliano ili kuwawezesha wakulima kulima mazao mbadala ikizingatiwa kuwa tumbaku inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Rais wa wa chama hicho cha ITGA, Daniel Green amesema tumbaku ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kwasababu inazalisha ajira na kutengeneza kipato. Amezitaka serikali za nchi zinazolima zao hilo kuwatafutia wakulima zao mbadala kabla ya kuwazuia kuzalisha tumbaku.

 “Hatupingani na sera zinazolinda afya ya jamii, jambo moja ni kuwa tumekuwa tukiomba tuwe sehemu ya mchakato ambao utawasaidia wakulima wa tumbaku kuwa na mstakabali mzuri”, amesema Green.

Kulingana na taarifa ya Jukwaa la Tanzania Tobacco Control Forum (TTCF) inaeleza kuwa ikiwa uzalishaji wa tumbaku utaongezeka matokeo yake ni kuongezeka kwa matumizi ya tumbaku jambo ambalo linahatarisha afya za watu na uharibifu wa mazingira. 

Ripoti hiyo inabainisha kuwa nchi za Kenya na Uganda zimepunguza uzalishaji wa zao hilo, ambapo makampuni ya tumbaku katika nchi hizo yameamishia ofisi zao Tanzania ili kutafuta soko.

 

Tumbaku ikiwa imepangwa katika tayari kupelekwa kiwandani

 

Mchango wa Tumbaku kwa Uchumi wa Tanzania

Licha ya wakulima kutakiwa kuachana na kilimo cha tumbaku, bado zao hilo lina mchango mkubwa katika kuliingizia taifa mapato ya kigeni. Zao hilo linachangia asilimia 40 ya mauzo yote ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonyesha kuwa huliingizia taifa mapato ya Dola za kimarekani milioni 252 na kutengeneza ajira 70,000 kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.

Kila mwaka tani zaidi ya 120,000 huzalishwa Tanzania huku mkoa wa Tabora ukiwa mzalishaji mkubwa wa zao hilo. Na inakadiliwa kuwa kila mwaka watu 6800 hufariki kutokana na magonjwa yanayoambatana na matumizi ya tumbaku nchini.

Kulingana na Shirika la The Tobacco Atlas (2012) linaeleza kuwa zao hilo linalimwa katika nchi 124 duniani kote. Mwaka 2012 tani milioni 7.5 za tumbaku zililimwa katika ardhi yenye ukubwa hekta milioni 4.3, eneo ambalo ni kubwa zaidi ya nchi ya Switzerland.

China ni nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa tambaku ambapo tani milioni 3.2 zilizalishwa mwaka 2012. Kila mwaka watumiaji wa tumbaku zaidi ya milioni 7 hufariki na watu laki 7 ambao wako karibu na wavutaji wa tumbaku hufariki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *