Dodoma: Asilimia 95 ya wakulima wanatumia mbegu za kienyeji

Jamii Africa

TISHIO la Watanzania kufungwa jela hadi miaka 12 kwa kuuza mbegu bora zilizotafitiwa huenda lisiwakumbe wakulima wa Mkoa wa Dodoma, kwani asilimia 95 wanatumia mbegu za kienyeji.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, wakulima wengi mkoani humo siyo tu kwamba hawawezi kumudu gharama za ununuzi wa mbegu bora, bali wamekuwa na utamaduni wa kuchota mbegu kwenye vihenge na kupanda shambani kila msimu wa kilimo unapowadia, jambo linalodaiwa kusababisha kushuka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo.

FikraPevu imebaini kwamba, maeneo pekee mkoani Dodoma ambayo yamekuwa yakitumia mbegu bora zinazopatikana kutokana na ruzuku ya serikali kupitia vocha za pembejeo za kilimo ni katika wilaya ambazo baadhi ya wakulima wanaendesha ppia kilimo cha umwagiliaji kama Bahi na Mpwapwa.

Mwishoni mwa mwaka 2016 iliripotiwa kwamba, ili ipate misaada ya maendeleo, Tanzania ilikuwa imerekebisha sheria zake ili kuwapa fursa wawekezaji wa kibiashara kwenye sekta ya kilimo na hakimiliki za bidhaa zao (intellectual property rights).

Chini ya sheria hiyo mpya, wakulima wa Tanzania wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 12 jela ama faini ya Euro 205,300 (takriban Shs. 513.3 milioni), au vyote kwa pamoja, kama watauza mbegu ambazo hazitathibitishwa.

“Hicho ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho mkulima wa Tanzania hawezi hata kufikiria kukipata maishani. Wastani wa pato la Mtanzania ni chini ya Dola 2 kwa siku,” alisema Janet Maro, mkuu wa taasisi ya Sustainable Agriculture Tanzania (SAT).

Aidha, chini ya sheria hiyo mpya, kama mkulima atanunua mbegu kutoka kampuni za Syngenta (kampuni ya Uswisi) au Monsanto (kutoka Marekani), wahusika ndio watakaokuwa na hakimiliki na kwamba kama mkulima huyo atahifadhi mbegu hizo katika mavuno ya kwanza, anaweza kuzitumia mwenyewe tu na haruhusiwi kuziuza.

“Huruhusiwi kumpatia jirani yako au nduguyo wa kijiji kingine, na huwezi kuuza kabisa. Lakini huo ndio msingi mkuu kwa mfumo wa mbegu barani Afrika,” anasema Michael Farrelly.

Inaelezwa kwamba, Tanzania ilitunga sheria hiyo ya hakimiliki kuhusiana na mbegu kama moja ya masharti ya kupokea misaada ya maendeleo kupitia mpango wa New Alliance for Food Security and Nutrition (NAFSN).

Mpango huo wa NAFSN ulizinduliwa mwaka 2012 katika mkutano wa Wakuu wa Nchi Nane Duniani (G8) ukiwa na lengo la kuwasaidia watu milioni 50 waondokane na umaskini pamoja na baa la njaa katika nchi kumi za Afrika ambazo ni washirika. Mpango huo unafadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya, Marekani, Uingereza, Benki ya Dunia na taasisi ya Melinda Gates Foundation.

Lakini asilimia kubwa ya wakulima wa Dodoma wanaonekana hawawezi kumudu gharama za kununua mbegu hizo kila mwaka kama inavyotakiwa.

“Hatuna uwezo wa kununua mbegu hizo, kwa sababu kwanza ni ghali na mashamba tunayolima ni makubwa ambayo yatahitaji mbegu nyingi zaidi,” anasema Mashaka Lemunge, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Chigwingwili wilayani Kongwa.

Lemunge anasema kwamba, kwa kawaida wakulima wengi huhifadhi mbegu kutokana na mazao yao kwa ajili ya msimu unaofuata, utaratibu ambao wameutumia miaka mingi.

“Tunatumia mbegu ambazo zimekuwepo vizazi na vizazi, tukivuna mahindi tunachagua yaliyo bora na kuhifadhi kwa ajili ya mbegu, leo unaponilazimisha nikanunue hizo mbegu zilizotafitiwa kwa gharama kubwa, kwanza uwezo wenyewe sina kwa sababu shamba langu lina ekari 20 hivyo nitahitaji fedha nyingi kununua mbegu, halafu tunaweza kupoteza mbegu zetu za asili,” anaongeza Lemunge.

Licha ya kwamba ni asilimia tano tu ya wakulima mkoani Dodoma wanaopata pembejeo za kilimo, lakini wakulima walio wengi wanahofia kutumia mbegu hizo kutokana na taarifa zilizoenea kwamba, hazina mwendelezo kama mbegu za asili.

Jackson Malima, mkulima na mkazi wa Songambele wilayani Kongwa, anasema kwamba, hata kama wangeletewa mbegu hizo asingeweza kuzitumia kwa sababu anaamini mbegu nyingi zilizotafitiwa kwa teknolojia zinaweza kuwa na madhara na kwamba watalazimika kununua mbegu mpya kila mwaka kwa vile haziwezi kudumu kama zile za asili.

“Tumeambiwa kwamba mbegu za viwandani haziaminiki, huwezi kununua leo halafu ukatumia kwa miaka mitano ijayo kwa sababu hazitatoa mavuno bora, sasa za nini kwa sababu zitafanya mbegu zetu za asili zipotee, na je, kama usipokuwa na fedha inamaana hutaweza kulima tena,’ anasema Malima.

Mijadala mbalimbali kupitia mtandao wa kijamii wa JamiiForums inaonyesha pia watu wengi wanapinga hasa mbegu zilizotengenezwa kwa teknolojia ya uhandisi jeni (Genetically Modifies Seeds – GMO) ambazo zimebadilishwa vinasaba (genes) katika maabara ili kuboresha aina fulani ya tabia inayohitajika, kwa mfano kuongeza virutubisho, na kuongeza uwezo wa kujikinga na madawa.

Hata hivyo, wataalam wa kilimo wanasema, kuna mkanganyiko wa tafsiri ya mbegu bora kwa kudhani kwamba mbegu bora zote ni zile za GMO.

“Hakuna mbegu za GMO ambazo zimesambazwa nchini kwa matumizi ya binadamu, kwani bado zinaendelea kufanyiwa utafiti, kilichopo ni mbegu zilizorasimishwa (certified),” wanasema, ingawa hawaelezi mbegu hizo ni za aina gani ikiwa nazo zimezalishwa na kampuni maarufu za kutengeneza mbegu za GMO.

Serikali kwa upande wake imekuwa ikihimiza wakulima kutumia mbegu bora zilizotafitiwa ili kuongeza tija kwenye kilimo, lakini kwa wastani ni asilimia 20 tu ya Watanzania wanaotumia mbegu hizo.

Inaelezwa kwamba, asilimia 75 ya wakulima nchini kote bado wanaendelea kutumia mbegu za asili licha ya juhudi hizo za serikali za kuhamasisha matumizi ya mbegu bora.

“Ni asilimia 15-20 ya wakulima ndio wanatumia mbegu bora na mbegu hizo tunaagiza nje ya nchi,” aliyekuwa Naibu Waziri Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, alisema mwaka 2014 wakati wa makabidhiano rasmi ya shamba lililopo katika Kijiji cha Isuka, Kata ya Ng’uruhe wilayani Kilolo lenye hekta 1,058 kwa taasisi ya Clinton  Development Initiative ili kusaidia uzalishaji wa mbegu  bora nchini kwa kushirikiana na taasisi binafsi.

Baadhi ya mbegu zinazotumiwa, ambazo zimethibitishwa, mara nyingi huzalishwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) pamoja na baadhi ya taasisi za umma na binafsi, ambapo kwa ujumla, kuna takriban hekta 10,928 za mashamba ya kuzalisha mbegu kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mbegu bora.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, mahitaji ya mbegu ni makubwa nchini Tanzania, ambapo kwa mwaka 2009/2010 yalikuwa tani 30,000 lakini upatikanaji wake ulifikia tani 16,148.2 kwa mbegu za mazao ya nafaka, mikunde na mbegu za mafuta sawa na asilimia 53.7 ya mahitaji halisi.

Aidha, kwa mwaka 2015/2016, mahitaji halisi ya mbegu bora yalikuwa tani 60,000, lakini zilizopatikana ni tani 36,410.6 sawa na asilimia 60.7 tu ya mahitaji.

Kati ya mbegu hizo tani 21,407.29 zilizalishwa nchini ambapo asilimia 81.3 ni mbegu za mahindi na asilimia 6.7 ni mbegu za mpunga na tani 15,003.17 ziliagizwa kutoka nje ya nchi.

Wakati wa uzinduzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania mnamo Ijumaa, Agosti 7, 2015, Rais (mstaafu) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, alisema benki hiyo ndiyo mkombozi wa kweli wa mkulima na kwamba ingemaliza changamoto na kero ambazo kwa muda mrefu zimekwamisha maendeleo ya haraka katika sekta ya kilimo, ukiwemo upatikanaji wa mbegu bora.

“Wakuliwa wanatumia mbegu duni za asili. Matumizi ya mbolea ni kilo 13 tu kwa hekta wakati katika Uholanzi ni kilo 577 kwa hekta. Mazao mengi hupotea kwa mimea kuathiriwa na maradhi na wadudu na wakulima wetu wana maarifa na ujuzi mdogo wa kilimo na ufugaji wa kisasa,” alisema Dk. Kikwete.

Alisema, madhumuni ya uanzishwaji wa kuanzisha Benki ya Kilimo Tanzania unalenga kimsingi kumwezesha mkulima wa kawaida wa Tanzania kupata mikopo ya kuendeleza kilimo chake wakati wowote na mahali popote nchini.

Itakumbukwa kwamba, mwaka 2008, Dk. Kikwete aliagiza kuwa fedha zote zilizokuwa zimerudishwa Serikalini kutokana na sakata la Akaunti ya EPA katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT) zitumike kama raslimali ya kufungulia dirisha la mikopo ya kilimo katika TIB na huo ndio ulikuwa mwanzo wa Benki ya Kilimo.

Hata hivyo, suala la mikopo hiyo kwa wakulima linaonekana kusuasua kutokana na sababu mbalimbali, nyingi zikiwa kutokuwepo kwa taarifa sahihi na za wazi kwa Watanzania wengi kuhusu taratibu na masharti ya mikopo pamoja na woga unaowakumba wakulima wengi katika ukopaji.

Aidha, suala la taasisi za kibenki kutowapa kipaumbele wakulima kwa kisingizio cha kwamba ‘kilimo hakiaminiki’ linakwamisha upatikanaji wa mikopo ya kuendeleza kilimo, hali ambayo inawalazimu wakulima wengi kutumia pembejeo walizozizowea, ikiwemo matumizi ya mbegu za asili.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *