Mwalimu ni mtu muhimu katika kumsaidia mwanafunzi kupata maarifa yaliyokusudiwa akiwa darasani, japo mwanafunzi anatakiwa kusoma kwa bidii lakini mwalimu ana nafasi kubwa ya kufanikisha au kuzuia ndoto za mwanafunzi kupata elimu bora.
Licha ya serikali kuendelea na jitihada za kupunguza tatizo la uhaba wa walimu katika shule za msingi, bado walimu waliopo katika baadhi ya shule za msingi wanalazimika kufundisha masomo ambayo hawana taaluma nayo. Hali hiyo imetajwa kuathiri ufundishaji katika shule nyingi za msingi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambayo ni msimamizi wa mitaala na sera ya elimu inamtambua mwalimu ni mtu aliyepata mafunzo ya ualimu katika fani aliyoichagua kusomea akiwa chuoni.
Ni dhahiri kuwa kila mwalimu anatakiwa kufundisha masomo ambayo amesomea akiwa chuo lakini mgawanyo usio sawa wa walimu na masomo katika shule, hulazimika kufundisha masomo ambayo hawajasomea.
Hali hiyo huenda sambamba na ongezeko la vipindi wanavyotakiwa kufundisha ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma masomo yote kwa wakati uliopangwa. Fikra Pevu ilitembelea shule mbalimbali za Dar es salaam ili kujionea hali halisi ya walimu na wanafunzi.
“Hapa tunao walimu 28 na walimu watatu tu ndio wanaofundisha darasa la kwanza, lakini kusema kweli tunatakiwa tupatiwe walimu watano zaidi kwa darasa la kwanza kutokana na wingi wa vipindi,”
“Darasa la kwanza lina mikondo mitatu ambapo kwa wastani kila chumba kina wanafunzi 36 kwa mwaka huu ikilinganishwa na wanafunzi 56 mwaka 2016,” anaeleza mwalimu mmoja kutoka shule ya Msingi Makumbusho (jina tumelihifadhi) ambapo anasema kwamba kwa wastani mwalimu mmoja anafundisha vipindi 3 hadi 5 vya masomo tofauti kwa siku.
Walimu hao wanasema kuwa tatizo la upungufu wa walimu bado lipo lakini linajitokeza kwa sura tofauti ya upungufu wa walimu kwa baadhi ya masomo hasa hisabati, sayansi na kiingereza.
Ili kuwasaidia wanafunzi wanalazimika kutumia uzoefu ili kuweza kufundisha masomo ambayo hawana ujuzi nayo matokeo yake uelewa wa wanafunzi huwa mdogo ikilinganishwa na masomo ambayo mwalimu anayafahamu vizuri.
Mwalimu mwingine katika shule ya msingi Mapambano (jina tunalihifadhi) iliyopo Wilaya ya Kinondoni analalamikia wingi wa vipindi anavyofundisha kila siku na kusema “darasa la sita lina walimu wawili ambao wanafundisha masomo 10 na vipindi ni vingi kwa siku, inatulazimu kufundisha masomo ambayo hatujayasomea, wanasema hakuna upungufu wa walimu lakini tatizo ni vipindi vingi tunavyofundisha kila siku”.
Mwalimu akiwa darasani akifundisha wanafunzi
Kwa mtazamo wa kawaida shule nyingi za msingi katika maeneo ya mjini zina uwiano mzuri wa mwalimu kwa wanafunzi kama ilivyoainishwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2010 ambapo uwiano sahihi wa mwalimu kwa wanafunzi (PTR) katika shule za msingi kuwa ni mwalimu mmoja kwa watoto 40 (1:40).
Shule ya msingi Makumbusho ina walimu 28 na wanafunzi 1,133, kwa muktadha huo uwiano wa mwalimu na mwanafunzi ni 1:40 ambao ni kiwango sawa na maelekezo ya Sera ya Elimu na Mafunzo.
Lakini changamoto inayojitokeza ni walimu kufundisha masomo ambayo hawajasomea na wingi wa vipindi ambavyo wanatakiwa kufundisha kwa siku ili kuwafikia wanafunzi wote katika darasa husika
Ripoti ya utafiti ya ‘Ufanisi katika Ufundishaji’ ya Shirika la HakiElimu (2014) inaeleza kuwa katika shule nyingi za umma, walimu hufundisha masomo ambayo hawajasomea kutokana na upungufu wa walimu.
“Kwa hakika shule ya msingi Hurui iliyopo katika Wilaya ya Tanga vijijini haikuwa na mwalimu wa somo la Bailojia lakini mwalimu wa somo la Kiingereza alijitolea kufundisha somo hili. Vilevile, kulikuwa hakuna mwalimu wa Hisabati lakini kulikuwa na mhitimu wa Kidato cha Sita aliyekuwa akifundisha somo hili kwa kujitolea”, inaeleza ripoti hiyo ya HakiElimu.
Wingi wa vipindi hupunguza ufanisi wa mwalimu katika kufundisha na matokeo yake wanafunzi wanakosa uangalizi wa karibu kutoka kwa mwalimu kwasababu muda mwingi anatumia kuaandaa masomo na kupitia kazi za wanafunzi.
Hali hiyo huathiri uwezo wa wanafunzi kujifunza na kinachotokea wanafunzi hukaririshwa mambo mengi ili wafaulu mitihani na sio kupata ujuzi ambao wanaweza kuutumia katika maisha yao.
Ripoti ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s-2017) inathibitisha kuwa “licha ya wanafunzi wengi wanaenda shuleni lakini wengi wao hawapati maarifa ya msingi ya kujua kusoma na kuhesabu. Tathmini ya mafunzo ya hivi karibuni inaonyesha kuwa wanafunzi 9 kati ya 24 katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, waliomaliza shule ya msingi ambayo ni pungufu kidogo nusu ya wanafunzi hao hawakupata stadi muhimu katika somo la hisabati”.
Ikiwa imebaki miaka 9 kutekeleza Mpango wa Taifa wa Maendeleo (Development Vision-2025) ambao unalenga kuifanya jamii ya kitanzania kuwa ya watu walioelimika ambapo nchi itajikita katika ubunifu na ugunduzi. Kwa changamoto hizi za walimu, taifa tutaweza kuwa na elimu bora na kushindana na mataifa mengine katika Nyanja za sayansi na teknolojia ifikapo 2025?