Waliochangia maoni ya katiba wahojiwa!

Jamii Africa

BAADHI ya wanafunzi wa shule ya sekondari Ihungo Manispaa ya Bukoba waliotoa maoni ya mabadiliko ya katiba katika kongamano lililofanyika wiki moja iliyopita wamehojiwa na maofisa usalama.

Hali hiyo imekuja baada ya kutokea mgomo na vurugu katika sekondari za Kahororo na Nyakato na kulazimika kuzifunga zikiwa ni siku mbili baada ya baadhi ya wanafunzi wa shule hizo kuhudhuria kongamano.

Mmoja wa wachangiaji katika katika kongamano hilo

Kongamano hilo liliandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema(Bavicha)wilaya ya Bukoba na kuhudhuriwa na mamia ya vijana ambapo mbunge wa Kawe Halima Mdee ndiye alikuwa mgeni rasmi.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Fikrapevu kupitia vyanzo mbalimbali shuleni hapo baadhi ya wanafunzi wametiwa msukosuko na maofisa usalama pamoja na kuwa hakuna mgomo wala vurugu zozote zilizotokea.

Hata hivyo mmoja wa walimu aliyeomba jina lake lihifadhiwe alisema hatua ya maofisa usalama kuwahoji wanafunzi hao inatokana na hofu ya shule hiyo kukumbwa na vurugu kama zilizotokea katika sekondari za Kahororo na Nyakato.

Katika shule hizo zenye kidato cha tano na sita baadhi ya wanafunzi waliochangia umuhimu wa kuwa na katiba mpya walionyesha ufundi mkubwa wa kujenga hoja huku wakiichambua katiba na mapungufu yake.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Henry Salewi ambaye alituma maaskali wa kuzima ghasia zilizolipuka usiku katika shule hizo alisema hawezi kuthibitisha kama vurugu hizo zina uhusiano na kongamano la Bavicha.

“Wanadai uji hauna sukari wale ni wakorofi, vurugu hizo hazina uhusiano na kongamano lililofanywa na Chadema,siwezi kusema sina ushahidi kamili”alisema Salewi akifafanua vurugu za shule zote mbili.

Wakati wa kongamano hilo la 1,Desemba lililohudhuriwa pia na Mbunge wa viti maalmu Conchester Rwamlaza pia lilijadili miaka hamsini ya Uhuru na hatima ya vijana ambapo wengi walilalamikia ukosefu wa ajira.

Wanafunzi kutoka shule hizo wakati wa maoni yao walihoji madaraka makubwa ya rais katika uteuzi wa nafasi mbalimbali na kuwa serikali ilifanya usanii kufuta masomo ya kilimo shuleni wakati huo ikisisitiza kauli ya kilimo kwanza.

Pia wanafunzi hao walilalamikia serikali kushindwa kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na kujikuta wataalamu wengi wanakimbilia kwenye siasa huku wakimtaka Halima Mdee awape sababu za chama chake kususia mjadala wa mswada wa katiba mpya uliopitishwa hivi karibuni.

 

Habari hii imeandikwa na Phinias Bashaya – Bukoba

4 Comments
  • Maoni ya katiba mpya na mgomo wa wanafunzi wapi na wapi??? serikali ya CCm iache kutapatapa kwani wameshaaliza kuvuana magamba????????

  • Kama kweli Serikali ya Tanzania inaamini inatenda mema sana kwa wananchi wake. Kwanini inahofia vitu kama hivyo?
    Ama inaona wanafunzi wa sekondari hawana haki ya kuchangia katiba ya nchi yao?

  • Nikweli vijana wamezoea kuonewa ,pale hambapo wanatoa fikira zao.pamoja na kwamba halina ukweli zaidi.lakini hapa uwa atupewe aki stahiki kama ya vijana kutoa mawazo yao sas hwa mahafisa wanaenda kufanya nini?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *