Uwazi na uwajibikaji katika jamii ni moja ya nguzo muhimu ya kuimarisha mfumo wa Demokrasia. Ili Demokrasia istawi na kuimarika ni lazima wananchi wapate nafasi ya kuzungumza kwa uwazi juu ya mustakabali wa maendeleo katika jamii yao.
Licha ya Tanzania kuwa na mfumo wa Serikali za Mitaa, inaelezwa kuwa mifumo hiyo haifanyi kazi kwa uwazi jambo linalozuia umiliki wa wananchi juu ya matumizi na uendelezaji wa rasilimali zao. Lakini hali hiyo inachangiwa na wananchi kuwa na uelewa mdogo juu ya haki zao na ushiriki wao katika ngazi za maamuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI) inayoratibu shughuli zake katika Kata ya Makumbusho jijini Dar es Salaam, Janeth Mawinza amesema uwazi na uwajibikaji unakosekana katika jamii kwasababu wananchi hawashiriki na kufuatilia mwenendo wa utendaji wa mamlaka zinazowaongoza katika jamii.
“Hakuna uwazi, hakuna uwajibikaji kwasababu wananchi hawana taarifa za utendaji wa mitaa yao, hawajui kwamba wao wana wajibu wa kutengeneza vipaumbele vyao”, amesema Janeth Mawinza na kuongeza kuwa hali hiyo husababishwa na wananchi kukosa elimu ya uraia na msukumo kisiasa wa kuwapa wananchi taarifa muhimu zinazohusu maendeleo.
“Hawana elimu, hawana nguvu ya dhati kwamba wananchi wanatakiwa wajue wana wajibu wa kutekeleza vipaumbele vyao. Huu ni mwezi wa 11 lakini katika mitaa kadhaa hakuna mkutano wa kijiji uliofanyika”, amesema Janeth Mawinza.
Kwa upande wake Lawrence Kilimwiko, Mkurugenzi Mtendaji wa Interstar Consults, taasisi inayotoa mafunzo ya Habari na Mawasiliano katika jamii, amesema uwajibikaji ni dhana pana ambayo inahitaji ushiriki wa kila mwananchi katika jamii, lakini mfumo wa uongozi na sheria ni kikwazo kikubwa kwa wananchi kuongea kwa uwazi na kuwawajibisha viongozi wao.
Anasema Serikali za Mitaa zinafanya kazi kwa maelekezo ya Serikali Kuu ambapo hutunga sheria na sera ambazo zinalenga kuwanufaisha wachache na wananchi kunyimwa sauti na hata wakipaza sauti zao hazisikilizwi.
“Kwasababu ya matakwa ya kisiasa watu hawa wanatunga taasisi ambazo zinakidhi matakwa ya kisiasa sio hali halisi iliyopo barabarani. Serikali za mitaa hazikuanzishwa na watu lakini kwasababu ya sheria ili kukidhi matakwa ya kisiasa. Serikali za Mitaa zinawajibika kwa ofisi ya Rais na sio kwa wananchi na hili ndilo tatizo linalojitokeza”, amesema Kilimwiko.
Wajibu wa Wananchi kuongeza Uwazi na Uwajibikaji
Kulingana na mazingira yaliyopo ya kuminywa kwa misingi ya demokrasia inayohimiza uwazi na uwajibikaji, wananchi bado wana nafasi kubwa ya kusimama na kudai mambo ya msingi yanayohusu maendeleo yao.
Imani Kija, mkazi wa Tandale, Wilaya ya Kinondoni anasema jamii inawajibika kwa maendeleo yake, “Wananchi tuamke na kufahamu tuna haki ya kupata taarifa na kutoa maoni yetu juu ya mwenendo wa viongozi wetu wanaotuongoza. Tukikaa kimya mambo yatazidi kuwa mabaya katika maisha yetu ya kawaida”.
Naye Mratibu wa Miradi, Mohammed Katundu kutoka Shirika la Tambani Rural Community Development Fund (TARUCODEFU) linalofanya shughuli zake Wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani anasema jukumu la maendeleo ni la wananchi ili kuhakikisha kunakuwa na uwazi na wanapaswa kufuatilia miradi na taarifa muhimu za mendeleo.
“Viongozi wanatakiwa wawe wawazi na wawajibike kwa wananchi wao na wanapopata taarifa wazitoe kwa wananchi, mfano fedha zinakuja kwa ajili ya miradi kwenye kata, mwananchi aliyepo kijijini lazima ajue mradi wa maji umeletewa fedha kiasi gani”.
Mchango wa AZAKI kuimarisha uwajibikaji na uwazi
Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIKI, Janeth Mawinza anaeleza kuwa kazi kubwa waliyonayo ni kutoa elimu na hamasa kwa wananchi ili watambue haki zao na kushirikiana na viongozi wa serikali kuimarisha mifumo ya uwazi itakayosaidia kukuwa kwa demokrasia nchini.
“Tunatoa elimu kupitia vituo vya taarifa na maarifa na tunajaribu kuwaweka karibu zaidi ili watimize majukumu yao”, anaeleza Janeth Mawinza na kuongeza kuwa changamoto inayowakabili ni kuhusisha shughuli za maendeleo ya wananchi na masuala ya kisiasa, jambo linaloleta mpasuko na malengo hayafikiwi kwa wakati.
Kwa mara nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Interstar Consults anashauri kuwa mabadiliko ya sera na sheria ni muhimu kwa sababu nguvu ya wananchi lazima itokane na sheria zinazokidhi matakwa ya walio wengi.
Umoja wa Ulaya kuwajengea Uwezo Wananchi
Umoja wa Ulaya (EU) kupitia mradi wake wa ‘Tuungane Kutetea Haki Zetu’ unakusudia kushirikiana na Asasi za Kiraia zilizopo nchini, Serikali za Mitaa kupanua wigo wa siasa, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ngazi ya Halmashauri ambapo wananchi watajengewa uwezo wa kushiriki kwenye michakato ya maendeleo kama vile kuibua, kupanga, kutekeleza, kusimamia, kufuatilia na kutathmini miradi ya maendeleo.
Mratibu wa Mradi huo, Maria Kayombo amesema, “tunatarajia kuifikia mikoa saba ya Tanzania na kuunganisha nguvu za wadau wa maendeleo wakiwemo Serikali za Mitaa, Wananchi, Vyombo Vya Habari na AZAKI ili washiriki pamoja kuongeza nguvu na sauti moja yenye lengo la kuhimiza uwazi na uwajibikaji kwenye rasilimali za umma”.
Umoja huo umetoa bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi huo ambao matokeo yake ni kuona Serikali za Mitaa kuonesha utashi na uwezo wa kutekeleza dhana ya uwazi na uwajibikaji. Na wananchi wawe na uwezo wa kufuatilia rasilimali za umaa na kujenga jamii inayoheshimu misingi ya demokrasia.