HALMASHAURI ya Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza, pamoja na Diwani wa Kata ya Bulyaheke wilayani humo, wameingia kwenye mgogoro mkubwa na wananchi wa Kijiji cha Lushamba kata hiyo, kutokana na wananchi hao kuanza kuhoji matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo katika Kijiji hicho.
Imeelezwa kwamba, uongozi wa halmashauri kwa kushirikiana na diwani wa Kata hiyo ya Bulyaheke, Bageti Ngele Nyuki (CCM), wamekuwa wakiingiza fedha za miradi ya maendeleo ya kijiji hicho cha Lushamba kwa kutumia akaunti ya kijiji kingine cha Itabagumba, anakokaa diwani huyo, jambo ambalo wanadai huenda kuna mpango wa kuliwa kwa fedha hizo.
Taarifa za kiuchunguzi wa FikraPevu, ambapo pia zimethibitishwa na uongozi wa Serikali ya Kijiji hicho, zimeeleza kwamba, mbali na fedha hizo kuwekwa kwenye akaunti ya kijiji kingine, pia diwani huyo amekuwa akisaini mikataba ya miradi bila kuishirikisha Serikali ya kijiji cha Lushamba na wananchi wake kwa ujumla, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Taarifa hizo zimedai kwamba, ndani ya mwaka huu halmashauri ya Sengerema iliingiza kwa ujumla sh. milioni 21 katika akaunti ya kijiji cha Itabagumba, ikiwa ni fedha za miradi ya maendeleo ya kijiji cha Lushamba, ambapo zilipaswa kuingizwa kwenye akaunti ya kijiji hicho cha Lushamba Na. 3162300639 ya benki ya NMB.
Inadaiwa kwamba, kati ya fedha hizo, sh. milioni 12 zimetolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba moja ya mwalimu wa Shule ya Sekondari Lushamba, huku sh. milioni tisa zikielekezwa kukamilisha ujenzi wa chumba kimoja cha darasa katika sekondari hiyo, ambapo wananchi walitumia nguvu zao kujenga hadi kwenye boma.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, wakiwemo baadhi ya wajumbe wa Serikali ya kijiji hicho waliliambia safu hii jana na leo walieleza wamba, hawaelewi sababu ya halmashauri na diwani wao huyo kuamua kuingiza fedha za kijiji chao kwenye akaunti ya kijiji kingine.
“Tunafikiria hapa kuna ufisadi unataka kufanywa. Haiwezekani, kijiji chetu kina akaunti hai lakini fedha za maendeleo zinaingizwa katika akaunti ya kijiji kingine.
“Tunapohoji sababu hasa tunapewa vitisho eti tukiendelea kuhoji sana halmashauri watawanyang’anya fedha hizo na kuzipeleka sehemu nyingine!. Tumechoshwa na hali hii, maana hadi wananchi wameanza kugoma kuchangia maendeleo”, alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho (jina tunalihifadhi).
Kwa mujibu wa wananchi hao, diwani wa kata hiyo ya Bulyaheke, Ngele Nyuki amekuwa akisaini mikataba peke yake na kandarasi bila kuushirikisha uongozi wa Serikali ya kijiji pamoja wananchi, na kwamba baada ya kusaini mikataba hiyo huwa anawaambia wanakijiji hao kwamba kuna kampuni ameipa kazi ya kujenga mradi.
“Kawaida Serikali ya kijiji ndiyo inayopaswa kuingia mkataba na mkandarasi, na siyo diwani peke yake. Sasa huyu diwani anajichukulia mamlaka ambayo si yake….hivyo tunataka akome na fedha za kijiji chetu ziingizwe katika akaunti ya kijiji”, alisema mkazi mwingine (jina tunalo).
Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Lushamba, Deus Gitulo Magumba pamoja na ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Ezekiel Galula (VEO), walipoulizwa leo kuhusiana na fedha hizo, walikiri fedha hizo za kijiji chao kuingizwa na halmashauri ya wilaya kupitia akaunti ya kijiji cha Itabagumba.
“Kwa kweli hata sisi kama viongozi wa kijiji tunashangaa kuona fedha za kijiji chetu zinaingizwa kwenye akaunti ya kijiji kingine. Akaunti yetu ipo na ina fedha sh. 900,000, kwa nini fedha hizi zipitishiwe akaunti nyingine?.
“Serikali ya kijiji ndiyo yenye mamlaka yote ya ujenzi wa miradi ya maendeleo. Ndiyo inayopaswa kuingia mkataba na mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo.
“Sasa inakuwaje tena diwani?. Tupo kwenye kikao tunajadili twende kuuliza halmashauri kuhusu utaratibu huu, maana halmashauri ndiyo mwajiri wetu na ndiyo mwenye fedha”, alisema mwenyekiti wa kijiji hicho cha Lushamba, Magumba, kisha kuungwa mkono kauli yake hiyo na mtendaji wa kijiji hicho, Galula.
Alipotafutwa leo na mwandishi wa habari hizi ili kuzungumzia malalamiko hayo, diwani wa Kata hiyo ya Bulyaheke, Ngele Nyuki alikata simu yake mara tu mwandishi alipojitambulisha na kuanza kumuuliza maswali kuhusiana na suala hilo. Na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS), akiombwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, hakujibu lolote badala yake alikaa kimya hadi tunakwenda mitamboni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Sengerema, Erika Musika alipotafutwa leo na mwandishi wa habari hizi ili kutoa maelezo juu ya suala hilo, hakupatikana kwani simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa, na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS), juu ya ufafanuzi wa jambo hilo, Mkurugenzi huyo naye alikaa kimya hadi tunakwenda mitamboni.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.
haka kanchi ketu mungu atusaidie tu ya ufisadi hadi kwa wenyeviti wa vijiji sijui tutafika kweli au ndio yale yale ukila wewe na sie tunakula.., poleni sana wanakijiji cha lushamba kama vipi mtieni ndani huyo m/kiti ili iwe fundisho..
Wa kwanza kufunguliwa mashtaka ni muhasibu aliyeingiza fedha kwa akaunti isiyohusika. diwani atakuwa amesuka mpango mzima.
Diwani kuna mchezo mchafu anafanya sasa mwisho wake umefika hawezi kujibu hiyo simu ukizingatia wimbi la CAG bado halijaisha. Wanachi au uongozi wa kijiji wafungue kesi juu ya diwani huyo. Huu ni wizi wa nje nje. Mkurugenzi anashiriki moja moja kwa moja hapo