Wananchi wamshinikiza waziri Kituo cha Afya kifanye upasuaji

Jamii Africa

WAKAZI wa Kata ya Igoma jijini Mwanza, wamemshinikiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kuhakikisha Kituo cha Afya katani hapo kinafanya kazi ya upasuaji.

Hatua hiyo imekuja baada ya jengo la upasuaji katika kituo hicho kubadilishwa matumizi, huku vifaa ‘vikiozea’ ndani.

"Hili jengo la upasuaji walilijenga la nini hapa kwenye kituo cha afya, kama hawataki kutoa huduma?"

Mkazi wa Kata ya Igoma jijini Mwanza, Magreth Njile, alitoa kauli hiyo alipotakiwa  kueleza kule wagonjwa wanakopata huduma za upasuaji.

Mama huyo mwenye watoto sita, ameungana na wakazi wengine wa kata hiyo, kulalamikia ukosefu wa huduma ya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Igoma.

Baadhi ya madaktari wa kituo hicho wanasema kinahudumia kati ya wagonjwa 100 hadi 150 kwa siku, lakini hakina huduma ya upasuaji licha ya jengo na baadhi ya vifaa vya upasuaji kuwapo kituoni hapo.

Mwandishi wa makala haya amejionea baadhi ya vifaa vya upasuaji vikiwa vimefungiwa ndani kwenye chumba kimojawapo cha wagonjwa katika jengo la upasuaji lililokamilika mwaka 2015.

Bahati Maduhu, Samson Herson na Judith Malingo wakazi wa Kata ya Igoma na Kishiri jijini hapa, wanahoji sababu ya kutelekezwa kwa jengo hilo.

"Kama wameshindwa kazi waondoke. Haiwezekani tukakosa huduma wakati vifaa vipo. Hilo jengo la upasuaji walilijenga la nini?

"Tuliambiwa Shs. 65 milioni zilitumika kujenga jengo hili la upasuaji. Kwa sasa linachakaa tu. Hivi hizo fedha ziliwawasha? Sisi tunataka huduma ya upasuaji haraka hapa Igoma," anasema Elizabeth John.

 

Madaktari wapo, huduma hakuna!

Uchunguzi umebaini kituo hicho cha afya kuwa na madaktari wanne wenye taaluma ya masuala ya upasuaji.

Hata hivyo, hakuna daktari mwenye taaluma ya kumhudumia mgonjwa dawa ya usingizi, wakati wa maandalizi ya upasuaji.

Aliyekuwa Diwani wa Igoma hadi mwaka 2015, Adam Chagulani, alithibitisha kuwa, awali jengo hilo liliezekwa kwa kutumia mbao zisizokuwa na ubora.

"Kiongozi wa Mbio za Mwenge aliagiza paa la Kituo cha Afya Igoma libomolewe. Mbao zilizotumika ni zile za Kichina. Zilibunguliwa haraka," anasema Chagulani, huku akihoji kukosekana huduma ya upasuaji kituoni hapo hadi sasa.

Jengo hilo la upasuaji lilifunguliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Juma Khatibu Chum, wakati huo 2015.

Baadhi ya watumishi wa kituo hicho wanasema, kati ya wagonjwa 10 hadi 15 wanaofika kituoni hapo kutafuta huduma hiyo muhimu ya upasuaji, wanaikosa.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa wanasema, kwanza kituo hicho cha afya kimeelemewa na wagonjwa.

"Kama Mkurugenzi wa Jiji (Mwanza) ameshindwa kutusaidia kupata huduma ya upasuaji hapa Igoma aseme.

"Tunamuomba waziri anayehusika na afya (Ummy Mwalimu) atuambie ni lini huduma ya upasuaji Kituo cha Afya Igoma itaanza kupatikana?" alihoji mwanamke mmoja aliyekataa kutaja jina lake.

 

Viongozi watupiana mpira

Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo hicho cha Afya Kata ya Igoma, Dk. Gloria Bernard, amekiri kituo hicho kupokea wagonjwa wanaohitaji upasuaji, lakini wanakosa huduma hiyo.

"Kweli jengo la upasuaji lipo na wagonjwa wanakuja na kukosa huduma ya upasuaji. Yaani kila sehemu wagonjwa wanaohitaji upasuaji wapo.

"Zaidi ya yote nakuomba ukamuulize DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) atakueleza, au msubiri daktari wetu wa hapa aje umuulize hayo maswali. Kwa sasa anaumwa," anasema Dk. Gloria.

Ofisa Afya wa Jiji la Mwanza, Sofia Kiruvia, alipoombwa kuzungumzia kero hiyo na hatma yake, akasema siyo msemaji wa Jiji.

“Mimi niulize masuala ya vyoo na kipindupindu. Lakini hilo jambo muulize DMO atakupa ufafanuzi zaidi," anasema Sofia.

Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dk. John Andrew, amekiri Kituo hicho kutokuwa na huduma ya upasuaji.

Anasema: "Jengo hilo lina mapungufu. Tuna mikakati ya kuhakikisha huduma ya upasuaji katika Kituo cha Afya Igoma inapatikana haraka iwezekanavyo."

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, alipoulizwa sababu ya kukosekana huduma hiyo ya upasuaji licha ya jengo, vifaa na madaktari kuwapo kituoni hapo, akasema: "Hilo suala mpaka niwasiliane na kupata majibu kwa daktari. Sasa sina jibu nitakudanganya."

 

Waziri aapa kukishusha hadhi

Wakati uongozi wa Jiji la Mwanza ukieleza hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu, amesema atakishusha hadhi Kituo hicho cha Afya Igoma na vinginevyo nchini, iwapo hakitakuwa na huduma ya upasuaji ifikapo Juni 2017.

Waziri Ummy anasema, vituo vyote kikiwamo cha Igoma jijini hapa, atavishusha hadhi na kuwa zahanati, iwapo havitakuwa na huduma hiyo muhimu kabla ya Juni.

"Kila halmashauri itenge bajeti katika eneo hilo, badala ya kuelekeza fedha nyingi kujenga masoko na ofisi za watendaji, ambao wanaweza kufanya kazi zao hata chini ya mti.

"Ujenzi wa vyumba vya upasuaji siyo kusubiri wahisani, Serikali Kuu au wizara. Bali kupitia vyanzo vya mapato vya halmashauri husika vinapelekwa kwenye vipaumbele muhimu," anasema Waziri Ummy.

Waziri Ummy anasema: "Nitamwandikia barua Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, kukata au kupunguza fedha za bajeti zilizotengwa na halmashauri kujenga masoko na ofisi za watendaji, ili ziende kujenga huduma ya upasuaji katika vituo vya afya nchini."

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *