Wanawake wa kikundi cha Tabu na Raha katika kijiji cha Idukilo wanachangishana hela na kukopeshana ili wajikwamue na mahitaji yao ya kila siku.
Mwenyekiti wa kikundi hicho bi Yunisi Daudi alisema waliamua kujiunga wanawake 20, wakijumuisha wanaolima na wafanya biashara baada ya kuwa na changamoto nyingi za kimaisha kama kununua mahitaji ya nyumbani.
Alisema huwa wanachangishana fedha sh.1000, kila wiki na kupata sh. 20,000, huigawanya kwa watu wawili katika kikundi kila wiki na watatakiwa kurudisha sh.11,000 kila mmoja baada ya mwezi.
“Kila wiki tunakutana nyumbani kwa mwenyekiti ama katibu na kukusanya marejesho ya waliokopa hela,na kuchangisha hela zingine na kukopesha wengine wawili.”alisema bi Daudi.
Akizungumzia changamoto za kikundi chao,bi Martha Lazaro mjumbe wa kikundi hicho amesema kwa mwaka huu mvua ni chache hata ulimaji hauna uhakika na kwa uzowefu wa hali hii marejesho miongoni mwa wanachama unakuwa na utata.
Aidha mwenyekiti wa kikundi hicho tena bi Daudi aliongeza kwamba ikitokea mwenzao hajarudisha mkopo kwa wakati,watamsubiri mpaka arejeshe ndio wengine wakopeshwe kwani hali zao za kipato wanajuana.
Hata hivyo amesema wanaiyomba serikali kwanza kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kuwakopesha mikopo ili waweze kufanya shughuli za ufugaji wa ng’ombe,kuku na hata kilimo chenye tija kuliko hivi sasa wanavyopata hela ndogo na kuishia kununua mahitaji ya nyumbani.
Kwa mujibu wa mweyekiti huyo kikundi cha Tabu na Raha, kilianzishwa mwaka 2002 kikiwa na wanachama 20, mmoja alihama eneo hilo na kubaki 19 hata hivyo wameongeza mwingine mmoja kutoka kijijini hapo mwaka jana na namba kuwa kama ya awali.