Wanawake wasioolewa hupata zaidi mimba zisizotarajiwa na huishia kuzitoa

Jamii Africa

Licha ya jitihada mbalimbali za serikali na wadau wa afya ya mama na mtoto kuhamasisha matumizi ya njia sahihi za uzazi wa mpango, bado idadi ya wanawake wanaotoa mimba ni kubwa nchini Tanzania. Wanawake 390,000, kati ya milioni moja, nchini Tanzania hutoa mimba kila mwaka kwa njia za kienyeji.

FikraPevu imeelezwa kuwa  idadi hiyo inawahusu wanawake wanaopata mimba zisizotarajiwa kwa kufanya mapenzi bila kuzingatia matumizi ya njia zinazozuia upataji wa mimba. Idadi kubwa ya wanawake wanaotoa mimba hufariki dunia, kwani hufanya kitendo hicho kwa kutumia njia za kienyeji na kuhusisha watu wasiokuwa na ujuzi.

Ripoti ya utafiti iliyotolewa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ikishirikiana na Taasisi ya Guttmacher na Chuo Kikuu cha Muhimbili mwaka 2015 inathibitisha kuwa “Tanzania ni kati ya nchi zenye viwango vya juu vya wanawake wanaotoa mimba kwa njia zisizo salama”.

 Utoaji mimba ni kosa kisheria kwa Tanzania kwa mujibu wa sura ya 16 kifungu cha 150, 152 cha kanuni za adhabu hupelekea wasichana wengi ambao hupata mimba zisizotarajiwa kutoa  kwa siri kwa hofu ya kukamatwa.


“Mwaka 2013 pekee asilimia 18 ya mimba zote zisizotarajiwa zilitolewa ikilinganishwa na asilimia 15 ya mimba zote zilizoharibika” – Ripoti ya utafiti NIMR (2015)


Inasemekana kuwa wanawake wasioolewa hupata zaidi mimba zisizotarajiwa kutokana na kushiriki vitendo vya ngono mara kwa mara. 

Wanawake wenye mimba zisizotarajiwa katika Nyanda za Juu Kusini, ambapo matumizi ya uzazi wa mpango ni ya juu ikilinganishwa na kanda ya Ziwa, wana uwezekano zaidi wa kutoa mimba kuliko wale wa maeneo mengine, na kusababisha  kiwango cha juu utoaji mimba.

“Nchini Tanzania, viwango vya utoaji mimba hutofautiana sana kwa ukanda, kutoka 11 kwa wanawake 1,000 kwa Zanzibar hadi 47 kwa Nyanda za Juu Kusini na 51 kwa Kanda ya Ziwa. Ukanda wa Ziwa na Nyanda za Juu Kusini huwa na viwango vya juu vya matibabu kwa matatizo yatokanayo na utoaji mimba pia”, inaeleza ripoti hiyo.

Licha ya wanawake hao kutumia njia mbalimbali za kuzuia mimba bado wanajikuta wakipata mimba. Mwaka 2013 pekee, wanawake 6 kati ya 10 wenye mimba zisizotarajiwa katika Nyanda za Juu Kusini waliishia kuzitoa kwa njia za kienyeji na baadhi waliripoti hospitali kupata matibabu baada ya kupata matatizo ya kiafya.

Njia za uzazi wa mpango hutumiwa na wanaume na wanawake kuzuia ujauzito kwa madhumuni ya kupanga uzazi ili kuwa na familia bora. Ni vigumu kusema kuwa kuna njia iliyo bora zaidi ya uzazi wa mpango kwa kuwa kila njia ina faida na hasara zake.

Matokeo ya utafiti  wa Afya ya Uzazi na Mtoto uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara na Wizara ya Afya-Zanzibari ya mwaka 2015-2016, yanaonyesha kuwa asilimia 54 ya wanawake wasiolewa  wenye miaka kati ya 15 hadi 49  wanatumia uzazi wa mpango.

Njia ya kisasa ambayo hutumiwa sana na wanawake wasioolewa ni kondomu ya kiume, vipandiki pamoja na vidonge.

Matumizi ya kondomu ya kiume yasiyo sahihi yanaweza kuwa sababu inayowafanya wanawake wasioolewa hasa Nyanda za Juu Kusini kupata mimba zisizotarajiwa.

Ripoti ya utafiti wa NIMR na Guttmacher  inaeleza kuwa takribani mwanamke 1 kati ya 5 wenye umri kati ya miaka 15 – 49 nchini Tanzania wanataka kuchelewesha au kusitisha kuwa na watoto lakini hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango. Kundi hili la wanawake huchukuliwa kama lenye mahitaji yasiyofikiwa ya uzazi wa mpango.

Utoaji mimba usiokuwa salama

Utoaji mimba usio salama ni ukiukaji wa haki ya binadamu ya kuishi lakini humsababishia mwanamke matatizo mbalimbali ya kifya ikiwemo kifo.

Dk. Bahati Maxwell wa Kituo cha Afya cha Buguruni – Anglican Ilala na Dkt na Pasiens Mapunda wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), kwa nyakati tofauti wanasema, utoaji mimba usio salama ni ukatishaji wa uhai wa mtoto aliye tumboni mwa mama unaofanyika kinyume cha sheria katika mazingira na njia zisizo rasmi na salama.

Sababu zitolewazo kuhusu utoaji mimba

Wanawake ambao wamekuwa wakijuhusisha na vitendo vya kutoa mimba wanasema wanafanya hivyo ili kukwepa aibu kwa mimba zitokanazo na ngono katika umri mdogo na kabla ya ndoa; hofu ya kukatisha masomo na na kushindwa kupanga uzazi wa kupishanisha watoto kiumri.

Sababu nyingine iliyotolewa ni hofu ya ugumu wa maisha, kubakwa na wapo wanawake ambao hutumia utoaji mimba kuwakomoa wenza wao.

Kaimu Mkurugenzi wa Programu, Uzazi na Malezi Tanzania (UMATI), Dk. Saili Mbukwa anasema hofu ya kushtakiwa kwa wanawake na watoa huduma za afya kuhusu utoaji wa mimba huchochea utoaji mimba wa siri na usio salama.

Dk. Bahati Maxwell anasema kuwa, “Kisheria utoaji mimba salama unaruhusiwa kwasababu maalum za kitabibu ambapo jopo la madaktari wasiopungua watatu linapojadili na kuafikiana kuwa hilo ndilo suluhisho pekee kuokoa uhai wa mama.”

Mambo yanayosababisha uamuzi wa madaktari kuruhusu utoaji wa mimba kisheria na kimiongozo yanahusisha mimba kutungwa nje ya kizazi, matatizo yanayoongezeka mimba inapokua na kuhatarisha maisha ya mama kama vile kifafa cha mimba, shinikizo la damu na kisukari.

Kutokana na kubanwa na sheria za utoaji mimba kwa wale wasio na ruhusa ya daktari, wanawake wengi hulazimika kutumia njia zisizo halali kutoa mimba ikiwemo kununua vidonge vya uzazi wa mpango na kumeza kwa kiwango kikubwa.

Wanawake wengine hutumia majani ya aloevera, kunywa chai ya rangi yenye majani mengi, au maji ya majivu na kuingiza dawa za kienyeji sehemu za siri kama kijiti kibichi cha jani la muhogo.

Wanawake wengine hujaribu kutoa mimba kwa kujipiga ngumi tumboni ambapo mwanamke hupata maumivu makali na kiumbe kilichopo tumboni hutoka.  Vitendo hivi vinaweza kusababisha majeraha na damu nyingi kuvujia na kusababisha kifo.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayojishughulisha na kukuza, kuendeleza haki na maendeleo kwa watoto, vijana na wanawake (Kiwohede), Yusta Mwaituka, ambaye pia ni muuguzi na mkunga anasema utoaji mimba kienyeji umeshamiri sehemu nyingi.

Suluhisho

Kutoa elimu ya matumizi sahihi ya njia za uzazi wa mpango kwa wanawake wasioolewa ambao wanapata mimba zisizotarajiwa na kuishia kuzitoa licha ya wao kuongoza katika matumizi ya uzazi wa mpango.

Pia wananchi kuwa na taarifa kuhusu adhabu inayotolewa kwa kila anayeshiriki kutoa mimba ambayo ni; Anayetoa mimba anaweza kufungwa miaka 14 au hata maisha , anayeomba kutolewa mimba anaweza kufungwa miaka saba na anayetoa vifaa au dawa kugharamia utoaji huo anafungwa miaka mitatu.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *