Waraka wa Mchungaji kwa Watanzania

Jamii Africa

Ndugu Mtanzania,

Naomba kuwasilisha kwako waraka huu ukiwa ni mwamsho na na hamasa kwetu kama Wananchi na Taifa ili kulikwamua taifa letu kutoka katika hali mbaya ya kiuchumi tuliyonayo na kuzorota kwa Uongozi na Utawala.

Naomba upokee waraka huu kupima nafsi yako na wale watakao kuja kwako kuomba kura yako wakati wa uchaguzi, uwe ni wa Serikali ya Mitaa, Wabunge au Urais. Nakusihi utumie mwamko na hamasisho hili kujihoji nafsi kuwa wewe binafsi una nafasi gani na nguvu zako zina nafasi gani ili kuleta msukumo utakaoleta maendeleo ya kweli na kulikwamua Taifa kutoka kwenye shida zinazotuzingira na kutudumaza. Kutumia waraka huu, jiulize kwa makini ni nini maana ya Maendeleo na ni maendeleo ya namna gani unayataka na yatakusaidia vipi uzao wako na vitukuu vyako?

Matatizo ya Tanzania yamegawanyika katika makundi mawili ambayo  yanaoana na yanategemeana. Matatizo haya ni Uchumi (Umasikini, Ujinga na Maradhi) na Uongozi (Utawala holela, Uzembe, Rushwa, Uvivu, Kutowajibika, Uhujumu).

Jiulize; iweje kila siku mpya ina kiza kinono na si nuru yenye kukupa tumaini pamoja na vizazi vyako? Kwa  nini unaendelea kuwa Masikini, Unanyanyaswa na kuendelea kufanywa Mnyonge, Unadhalilishwa na kupuuzwa kama Mjinga? Waulize wote wanao kuomba kura, hasa wale ambao wanarudi kwa mara nyingine kila wakati wa uchaguzi wakiwa na chakula, pombe na nguo,   ni nini bora walichokifanya miaka yote tangu uwape dhamana ya kuongoza ? waulize iweje mpaka leo hali yako bado haijabadilika lakini hali zao zimeneemeka na kunona? Waulize ni ahadi gani wanaleta safari hii na ni mpaka lini uendelee kuwaamini?

Waulize mpaka lini Tanzania itaendelea  kulaumu Ukoloni, Ubeberu na Ubepari kuwa ndiyo vyanzo na virutubisho vya Umasikini, Unyonge na Ujinga wako? Kama Ubepari ni mbaya, mbona tunakimbilia kuukumbatia na kuuamini kuwa ni suluhisho? Ikiwa wanasema Ubepari ni mzuri mbona hatuneemeki kama Taifa na tunaendelea kuwa Masikini na kutegemea misaada?

Tunaambiwa  kuwa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, Azimio la Arusha na Vijiji vya Ujamaa vimeshindikana na kuwa vilikuwa vibaya kwa Taifa letu. Swali ambalo inabidi ujiulize kwa kuishi katika Ujamaa, Vijiji vya Ujamaa na Azimio la Arusha kwa miaka 40 ni  jee, nadharia ndizo zilikuwa mbaya au ni utekelezaji wa nadharia ya Ujamaa na Kujitegemea, Azimio la Arusha na Vijiji vya ujamaa ndiyo umeshindikana?

Jiulize, je kushindikana kwa sisi kama Taifa kuwa na maendeleo kutokana na misingi ya Ujamaa na Kujitegemea, Azimio la Arusha na Vijiji vya Ujamaa kulitokana na nini? Je ni ubatili na ubutu wa nadharia au ni kutokana na kukosekana kwa mfumo mzuri wa uongozi, ufuatiliaji na mtaji tosha kutokana na uzalishajji mali ili kutimilza njozi ya kujenga taifa linalojitegemea?

Jiulize kama ilikuwa ni utekelezaji na uongozi mbovu, ni kipi kilichofanyika kurekebisha matatizo ya awali ili kukwamua nchi yetu kiuchumi na kuwa na uongozi bora na si kufanya majaribio ya sera mpya?

Jiulize je mabadiliko haya ya sasa ya kuingia uchumi wa kibepari kupitia utandawazi, masoko huria na ubinafsishaji  wa rasilimali na njia kuu za uchumi yanayoshinikizwa matumboni  na akilini mwetu kutoka kwa wahisani, wafadhili, wawekezaji na hata viongozi wa Serikali na chama tawala ni kwa manufaa ya nani na yataleta mabadiliko gani ya kweli kwako kama Mtanzania ikiwa hujawekwa mstari wa mbele kunufaika na matunda ya mfumo huu mpya?

Jiulize nafasi yako kama Mtanzania ni ipi katika mchakato huu mpya wa kujenga uchumi na maendeleo?

Miaka 10 iliyopita niliandika haya yafuatayo hapa chini kama ningekuwa mgombea Uchaguzi Mkuu 2000. Nayarudia tena kwa kuwa naamini ni msingi mkuu  wa suluhisho la matatizo ya Uchumi na Uongozi yanaweza kutumika kama nyenzo na dira  na kuleta maendeleo  kama Wananchi binafsi, jamii na hata Taifa.

  • Kurudisha na kuimarisha Heshima, Utu na Hadhi ya Mwananchi na Taifa la Tanzania
  • Kurudisha na kuimarisha Heshima, Wajibu na Hadhi ya kazi na kufanya kazi kwa Watanzania wote, vijijini na mijini
  • Kuelimisha Wananchi haki zao kama raia, wajibu wao na sehemu yao katika Taifa na Serikali yao kupitia Katiba, Serikali Kuu, Bunge na Mahakama
  • Kuimarisha Ufanisi na Ustawi wa Jamii katika kupiga vita Ujinga, Umasikini, Njaa na Maradhi
  • Kuhakikisha kuwa Katiba, Sheria na Kanuni zilizowekwa zinatekelezeka kutokana na nyakati zilizopo, zinafuatwa ipaswavyo na vyombo vyote husika; Serikali, Bunge, Mahakama na Wananchi wenyewe. Aidha kuweka maamuzi na mipango ya Serikali wazi kwa Taifa zima ili kuhakikisha utendaji kazi, uadilifu na uwajibikaji wa Serikali unafanyika kwa dhati kufuatana na Sheria, Katiba na Kanuni na si kwa usiri
  • Kubuni mbinu za kiuchumi ili kumpunguzia mzigo mwananchi wa kawaida hasa wale wa kipato cha chini, wafanyakazi na wakulima ili kujenga nguvu kubwa ya taifa kuwa katika Tabaka la kati
  • Kuhakikisha kuwa njia kuu za Uchumi na uzalishaji mali zinaboreshwa na kutumika kwa manufaa ya kila Mtanzania na taifa la Tanzania linanufaika kwanza
  • Kuhamasisha na kuhakakisha kuwa Uzalishaji mali unafanyika kwa dhati, kisayansi, kiushindani, kiuwajibikaji, kiufanisi na kwa ubora wa hali ya juu kwa kutumia tija, kuongezeka kwa juhudi na maarifa ya uzalishaji mali huu
  • Kuhakikisha kuwa huduma za msingi zinaboreshwa na kupewa kipaumbele na kufikishwa kwa wananchi ili kujenga maendeleo ya kweli kwa jamii na Taifa;- Afya, Elimu, Maji safi, Chakula, Nyumba, Uchukuzi, Nishati na maendeleo ya Miji na Vijiji
  • Kuhakikisha kuwa vita dhidi ya Rushwa, Ubadhirifu, Udini, Ukabila, Uzembe, Ufisadi, Uhujumu, Uvivu, Uzururaji na Kutowajibika au kutokujituma kwa watendaji wa Serikali na taasisi zake (wakuteuliwa au kuchaguliwa), waajiriwa , wafanyakazi na wakulima ni vita vya Taifa zima na linahitaji ushiriki na kushirikisha Wananchi wote. Wananchi wote bila kujali kabila, rangi, jinsia, umri, elimu au mwelekeo wa kisiasa ni wajibu wao kushiriki katika vita hii

Vipengele hivi  si vigumu kutuumiza kichwa, ni rahisi sana kuvifuatilia na kuvifanyia kazi.

Ni mambo ya kawaida ambayo tuliyaweka mstari wa mbele tangu tupate Uhuru, lakini kwa miaka karibu 20, tumeondokana nayo na kuishia kuyazunguka kama punguani na kwa kudhamiria au bila kudhamiria tumeyapuuzia au kutoyapa umuhimu kwa dhati kama nguzo kuu za kulijenga Taifa. Tumeshindwa kuwa makini katika Uongozi na Utawala wetu, kitu ambacho kimezalisha uzorotaji na kudumaa kwa uchumi pamoja na takwimu zote zinazosema kuwa uchumi wetu unakua. Uchumi wa Tanzania utakuwa pale ambapo Mtanzania ataacha kutafuta makombo ili aweze kumaliza siku moja anayoamka akiwa hajui kesho ikoje.

Uzalendo; haki, nidhamu, kazi na sheria

Kutokana na udhoofu wa Uchumi na kuzorota kwa Uongozi, hadhi yetu na kujivunia kwetu kuwa Watanzania kama tulivyozoea kujivuna na kuimba “Tazama ramani utaona nchi nzuri… Nasema kwa kinywa na kufikiri nchi hiyo nzuri ni Tanzania” imeshuka na hatujiamini tena. tumekuwa wanyonge na kukubali kuburuzwa na viongozi wetu na hata wafadhili.

Tunahitaji kujirudishia Uzalendo na hadhi yetu kama Taifa. Tukubali makosa tuliyofanya kwa kukusudia au bila kudhamiria. Hiyo itakuwa hatua ya kwanza ya kutafuta suluhisho la matatizo yetu na kujirudishia hadhi yetu na ya Taifa letu.

Msahafu na maandiko yanasema, “asiyefanya kazi na asile” na nyongeza inasema “kwa jasho lako utaishi”.

Watanzania tumesahau nidhamu na wajibu wa kufanya kazi. Tumeendekeza malalamiko na manung’uniko, huku tukipunguza tija na juhudi kulilia motisha. Tumejenga tabia ya kuwa wavivu na kutafuta njia fupi kujipatia mapato au nyongeza ya mapato ili kukabili ukali wa maisha. Kama tutageuza nguvu zetu hasi kuhusu uchapaji kazi na kuzifanya chanya kuongeza uzalishaji mali na kuachana na kutegemea misaada, basi nafasi yetu ya kuwa na maendeleo ya kudumu yanayoendelea yatakuwa makubwa na hata viongozi wetu ambao wamekosa dira na mwamko wa kutuongoza wataona aibu tutakapoamka kudai haki zetu kutokana na jasho letu.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuangalia Kazi kwa mtazamo wa kimaendeleo na chanya. Bila kufanya kazi, kwa ufanisi, juhudi, maarifa na uhodari, hatutaweza achana na umasikini, ujinga, maradhi na unyonge. Iwe ni mijini kwenye maofisi, biashara, viwandani, mashambani au migodini. Iwe kazi za kuajiriwa au kujiajiri, ni lazima tuheshimu na tujitume na kujitututmua kufanya kazi na kazi ziwe ni zile halali za kutupa mapato halali.

Hadhi na utu wa Uzalendo na Utaifa na Taifa letu, vitakuwa havina maana kama Mtanzania hatajua wajibu na haki zake Kikatiba, hatajua na kutumia Sheria na kanuni za nchi kujilinda na kujiongoza. Viapo vyetu vya utii visiishie kuwa ni viapo hewa kwa ajili ya kuapa. Tunapoapa kulitumikia Taifa na kuimba wimbo wetu wa Taifa “Mungu Ibariki..” ni lazima tuwe wakweli na wenye Uzalendo wa kweli ndani ya moyo. Kuelewa haki yetu Kikatiba kutaongeza ufanisi wetu na hasa wajibu wetu kama Raia katika kuweka Sheria za kuilinda nchi yetu na kuwa makini kuchagua viongozi wa kutuongoza kama Taifa.

Wajibu wetu mwingine ni kuhakikisha kuwa kazi yetu haishii katika kulinda katiba na kujua haki zetu kama Watanzania, bali ni kufuata sheria hizo na kuzithamini. Tuwe mstari wa mbele kufuata sheria na kanuni tulizonazo na tuwakosoe na kuwafikisha kwenye sheria wale wote ambao kwa makusudi au bila kukusudia wamekiuka sheria au kanuni. Tusiwaonee haya wale wanaopindisha sheria au kuvunja sheria bila kujali sehemu yao katika jamii. Kama waziri anapinda Sheria ni wajibu wetu kama jamii kumwajibisha. Kama mbunge anavunja Sheria, ni wajibu kumfikisha mbele ya vyombo vya dola ili haki na hukumu kwa kuvunja Sheria ifanyike.

Sheria na kanuni hazikuwekwa zifuatwe na wananchi pekee. Watawala na Viongozi hawana kinga ya aina yeyote ya kuwaepusha kufuata kanuni,sheria au katiba. Sheria na katiba ziliundwa ili zifuatwe na kila raia na mkazi wa Tanzania.
Wakati wa Azimio la Arusha tulitamka kuwa ili tuendelee tunahitaji Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Tukatamka kuwa tunataka kujenga Taifa huru la Kijamaa na lenye Kujitegemea. Tukasisitiza kuwa vita dhidi ya Ujinga, Umasikini, Njaa na Maradhi vitashinda kama tutatumia Juhudi na Maarifa katika kazi zetu na maisha yetu.

Kazi tuliyonayo sasa si tofauti na ile ya mwaka 1967, ni ile ile na sana sana ni kulenga nyenzo kuu za maendeleo yetu kama Taifa na kibinafsi kwa kupitia milango miwili. Ili tujikwamue kutoka hali hii mbaya tuliyonayo kama Taifa, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwajibika na kuwa na nia ya kweli kuyafanya yafuatayo;

  1. Kuwa na Uongozi mkakamavu, mahiri, jasiri, fanisi na wenye kuona mbali. Utawala na uongozi wa nchi unahitaji na unategemea Uongozi mahiri kutekeleza sera na mipango, uongozi wenye ufanisi kuhamasisha uzalishaji mali na uwajibikaji na wenye kuwa wanyenyekevu na kuheshimu dhamana walizopewa
  2. Kujenga Uchumi imara na madhubuti. Hili litatusaidia katika vita dhidi ya Umasikini, Ujinga, Maradhi na Njaa

Uongozi; Serikali, Utawala, Dola

Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) zimebahatika kuwa na awamu si chini ya nne za uongozi wa Serikali kuu, ingawa kwenye Bunge na Mahakama, watumishi wake wameendela kuwa ni wale wale kwa muda mrefu.

Tatizo kubwa tulilonalo kama Taifa ni ufinyu wa viongozi bora na utashi binafsi wa wachache walio katika nyanja za uongozi kwa kukosa sifa muhimu kwa viongozi. Mzee Mwinyi amesema majuzi kuwa Tanzania ina viongozi wasomi wasioelimika. Kauli hii ni ya kweli na ni ya msingi kutambua kuwa uongozi si lelemama, ni kipaji na ni kazi ngumu.

Uongozi ni kujitolea na kuweka matwakwa na maslahi ya wengine kuwa mstari wa mbele na si matakwa binafsi na kujinufaisha. Marehemu John Kennedy rais wa Marekani alitoa kauli moja maarufu iliyosema kuwa “kiongozi ajiulize ni vipi atalitumikia Taifa na si Taifa kumtumikia yeye Kiongozi” Umashuhuri na uzuri wa Kiongozi unatokana na hekima, busara, uchapakazi, ufanisi, ufuatiliaji, uimara, uungwana, uwajibikaji na unyenyekevu wake. Ama fikra endelevu na upeo wa kuongoza ni muhimu na si kauli tamu au uzuri wa sura.

Uwezo wa Tanzania kuwa na maendeleo ya kweli utaanza na Uongozi bora.

Uongozi bora ni ule;

  • wenye mapenzi ya kweli na dhati na kujivunia Utaifa wake
  • wenye kujali na kulinda maslahi ya Taifa lake na watu wake
  • wenye uwezo wa kupanda mbegu imara ya Uzalendo kwa kila mwananchi bila kujali itikadi, rangi, kabila, dini, elimu, umri au jinsia
  • wenye uwezo wa kuhamasisha na kuchochea juhudi za maendeleo ya jamii, umma na Taifa
  • wenye nidhamu, watiifu, kuwajibika, tija, ufanisi, kujituma na ufuatiliaji wa hali ya juu
  • wenye usikivu, uungwana na unyenyekevu kukiri makosa, kukubali kukosolewa na kupokea na kufanyia kazi maoni ya wengine
  • wenye uwezo wa kufanya kazi, kufikiri, kuwa na upeo na wepesi wa kukabili na kufanya maamuzi magumu
  • usiolea uzembe, ubaguzi, unyanyasaji, uhujumu, ubadhirifu, rushwa, kudharau, kudhalilisha, kujuana au kulinda maslahi ya wachache au kikundi Fulani

Wajibu wetu kama Taifa na haki yetu kama wapiga kura kuchagua viongozi kutuongoza unabidi uachane na mfumo duni tulioujenga wa kuangalia sura na chama na tuangalie wagombea wetu wa uongozi kwa vigezo hivyohapo juu ili kuunda tabaka jipya la viongozi ambao ni wachapakazi na watakuwa manahodha wazuri kutuongoza katika safari yetu ya kulijenga Taifa.

Tukilegalega katika hili na kupuuzia wajibu juu mkubwa na kuendelea kuchagua viongozi na wawakilishi wabovu, tutakuwa hatuna sababu yeyote kulia na kulalamika kuwa tu masikini au wanyonge kwa kuwa ni Ujinga na Upumbavu wetu kutumia akili na busara zetu tulizopewa Mungu tumekimbilia kurudia makosa ya kuwapa dhamana ya uongozi watu ambao hawafai kutuongoza.

Tuchague viongozi si kwa kuangalia vyama au sura, bali tuangalie uwezo wao wa kuongoza, kuhamasisha na kufanya kazi. Tupime kauli zao na matokeo ya kazi zao kama wanavyojinadi.

Serikali ni watu, inaundwa na watu tuliowachagua na tunawapa watu hawa na Serikali mamlaka makubwa ya kutuongoza, kupanga na kulinda Taifa na Katiba yetu. Dhamana hii imefanywa kwa kuaminiana kuwa Serikali itafanya kazi kwa manufaa ya Wananchi wake na kwa matakwa na utashi wa Wananchi wake.

Inapotokea kuwa Serikali inafanya kazi tofauti na dhamana iliyopewa, ni wajibu na haki ya kila Mwananchi kudai na kuhoji mapungufu yanayoonekana au kuzungumzwa. Ni wajibu wa Serikali na Uongozi kujibu na kuwajibika kwa Wananchi waliowapa dhamana ya kuongoza Taifa.

Ikiwa Serikali na watendaji wake na Viongozi wanashindwa kufanya kazi zao kama wanavyotegemewa kuzifanya na kushindwa kutimiza matarajio ya Wananchi na Taifa, ni wazi kuna umuhimu wa kupima uwezo wa viongozi na kuhoji Uzalendo wao na kama bado wanastahili kulitumikia Taifa.

Kuanzia Rais, Mawaziri, Majaji, Mahakimu, Wabunge, Wakuu wa Taasisi na Mashirika, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Polisi, Magereza,Jeshi na watendaji wengine wa Serikali, tumaini la Watanzania na Taifa ni kuwa watu hawa wamepewa nafasi hizo kwa kuwa wanauwezo wa kitaaluma na kiutendaji kuwa viongozi na walinzi wa nguzo za Taifa letu kupitia Katiba na Sheria zake.

Hivyo basi pamoja na kuwa ni jukumu la sisi kama Raia na Taifa kudai uwajibikaji, lakini uzito wa kuhakikisha ufanisi wa Uongozi na uwajibikaji wake utaanzia na Mkuu wa Nchi ambaye ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu.

Wasifu wa Uongozi bora nilioutaja hapo juu, si wa Rais pekee, ni wa kila mtu aliye kiongozi na ni shurti kila Mtanzania aishi kwa kuviangalia na kuvitumikia vipengele hivyo bila kujali yeye ni Kiongozi au la.

Serikali yetu ni kubwa sana na ina watendaji wengi ambao sitaficha kusema kuwa asilimia 55% hawastahili kuwa viongozi kutokana na kushindwa kuwa na sifa nilizozitaja hapo juu.

Hii ni hatari sana kwa Maendeleo na Usalama wa Taifa letu. Hatuwezi kuendelea kujiongoza kiholela huku zaidi ya nusu ya viongozi wetu hawana Uzalendo au uchungu na nchi yao. Swali kwako Mtanzania ni kwa nini basi ukubali kuendelea kujichagulia viongozi wabovu wasiofaa na kuwapa dhamana kubwa sawa na kumpa Simba jukumu la kulinda Mbuzi wako?

Kinachikosekana kutoka Uongozi Mkuu hasa Urais na hata Mawaziri ni uwezo wa kudai kwa nguvu uwajibikaji na uadilifu. Hadithi na tuhuma za ufisadi zilizotawala Taifa letu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 ni kutokana na kuwa na Uongozi dhaifu, usiojali maslahi ya Taifa, uongozi uliojaa woga na kulindana na kushindwa kusimama kidete kulinda rasilimali za Taifa letu.

Viongozi wakuu wa jamii kuanzia wakuu wa vijiji, kata, tarafa, wilaya, mikoa hata Taifa, wameendelea kufanya kazi bila kupimwa na waajiri wao wawe Wananchi au Serikali kuu kuhusiana na ufanisi na uwezo wao katika safari ya kulijenga Taifa na kuleta maendeleo.

Mapendekezo yangu ambayo yataanzia na wewe Mtanzania ni kuwapima viongozi wako kwa kutumia vipimo vyepesi sana. Vipimo hivi ni kama ifuatavyo;

  • kupitia ripoti za kila mwezi, robo, nusu na mwaka mzima za maendeleo na kupima mafanikio na matatizo ya shughuli za maendeleo
  • kuhoji na kuhakiki viwango vya kuongezeka vita dhidi ya ujinga katika wilaya au mikoa kupitia shule za msingi, sekondari, vyuo na elimu ya watu wazima
  • kuhoji maendeleo ya afya kupiga vita maradhi, kuangalia takwimu za kupungua vifo vya Uzazi, vifo vya watoto, kupungua kwa uadimu wa lishe na magunjwa kama Kwashiakor, Utapiamlo, kupungua kwa magonjwa na vifo vya Malaria na Ukimwi
  • ongezeko la nyumba bora, maji safi, barabara nzuri, shule, hospitali na zahanati, vyanzo vya ajira, viwanda na shughuli za kilimo
  • hifadhi za chakula kukabiliana na njaa,  mauzo ya mazao ya biashara na chakula
  • matumizi bora ya fedha za bajeti ikiwa pamoja na kubana matumizi yasiyo ya muhimu, kudhibiti matumizi na mahesabu ya fedha za bajeti za matumizi na maendeleo
  • kukagua na kuhakiki shughuli za maendeleo kuwa ni endelevu na kuhakikisha hazizoroti

Kwa kifupi ni kuhoji na kutathmini, ni shule ngapi tulizonazo, ni ngapi zimeongezeka, ni wanafunzi wangapi wamehitimu shule, ni hospitali ngapi tulizonazo zina uwezo gani, msisitizo wa kinga ni mkubwa kiasi gani kulingana na tiba, kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji mali na hifadhi za mazao, kubana matumizi na matumizi mazuri ya fedha.

Nimeweka wajibu huu kwako wewe mwananchi kwanza na si ile kasumba ya kusubiri Kiongozi Mkuu-Rais au Waziri Mkuu ndio wawe wenye jukumu na uhalali wa kuhoji haya.

Vipimo hivi haviishii kwa Mbunge, Mkuu wa Wilaya au Mkoa ni mpaka kwenye Serikali kuu na hata vigezo hivi vinaweza tumika katika mashirika na taasisi za umma na zile binafsi.

Kama vigezo hivi vya uongozi bora na kupima uwajibikaji vingekuwa vikifuatwa kwa makini, tungeweza kuona uwiano wa maendeleo wa Taifa letu. Lakini ni mpaka pale tutakaboshinikiza na kudai kwa nguvu Utawala na uongozi bora, ndipo tutakapoona mafanikio na hivyo kuanza kupata tumaini la maendeleo ya Taifa zima.

Uongozi na Utawala bora huendana sambamba na dola. Katika Utawala bora, Serikali na Viongozi ni wabunifu wa mipango mizuri ya maendeleo, ni wapimaji wa kasi ya maendeleo na hufuata kanuni na sheria katika kufanya kazi zao.

Panapokuwa na Uongozi na Utawala mzuri, kero za wananchi hupungua na hata matumizi ya dola na vyombo vyake huheshimika na huwa ni kwa ajili ya manufaa ya Taifa.

Hali halisi ya Tanzania imejenga mfumo wa utawala unaolinda utashi na maslahi ya chama tawala au kikundi chenye nguvu za madaraka nja mali. Hali hii imefikia hatua ya kikundi hiki cha watawala kutumia nguvu za dola kutawala kwa mabavu, kukiuka sheria na kanuni alimradi wanatumia kinga ya uongozi.

Utawala wa namna hii si mzuri na hauna manufaa hata kidogo kwa nchi yetu au Taifa lolote. Tunapaswa kukemea na kuondokana na mfumo huu mbovu wa Utawala ambao unatumia dola na kuweka wajibu wa kwanza wa Uongozi ni kulinda matakwa ya Chama au kikundi maalum.

Aidha matumizi mabovu ya dola na vyombo vyake, Bunge, Mahakama, Polisi, Jeshi na Usalama wa Taifa yamesababisha kwa kiwango kikubwa kuzorota kwa Uongozi, kuweko kwa utawala mbovu ambao umeishia kuangamiza uchumi na juhudi za maendeleo ya Taifa.

Wajibu wa vyombo kama Bunge na Mahakama ni kuwa mihimili mingine ya Serikali. Bunge likitunga Sheria, Mahakama ikitoa tafsiri za sheria na Serikali kuu kufanyia kazi sheria. Badala ya vyombo hivi kuwa huru na hata kuhakiksha vyombo visaidizi kama Polisi, Jeshi, Mahakama, Magereza, Usalama wa Taifa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu vinabakia kuwa vyombu huru ndani ya mfumo wa kisiasa, vyombo hivi vimegeuzwa na kutumika kama silaha ya kulinda chama kinachotawala kwa kutoa vitisho kwa wananchi na vyama visivyo na madaraka.

Suluhisho la haya yote ni kuundwa kwa Katiba mpya na Sheria mpya ambazo zitalenga;

  • kutoa haki sawa kwa kila mwananchi bila upendeleo
  • kutofungamana na chama au kikundi cha siasa au watawala,
  • kuwajibisha Watanzania wote bila kujali nafasi zao katika jamii na Taifa,
  • kulinda maslahi, haki , uhuru na mali za Watanzania wote bila kujali itikadi, dini, elimu, jinsia, umri au kabila
  • kutoa tafsiri na maelezo ya kisheria na kanuni ambayo hayana utata au kukosa nguvu kufanyiwa kazi na kufuatiliwa
  • kumpa kila Mtanzania fursa na haki sawa katika kuchangia kwake ujenzi wa Taifa na hata kuongoza bila kuwa na vipingamizi vya kibaguzi ambavyo vimewekwa maksudi katika katiba ya sasa na Sheria kuzuia ushindani au kuwepo kwa uhuru kamili wa kujieleza na kufanya mambo ya siasa na uongozi
  • kujenga miiko mikali na maadili kwa viongozi, utawala na wanachi kwa ujumla
  • kuweka mfumo bora wa uteuzi au uchaguzi wa viongozi na wawakilishi

Penye nia pana njia, kama wote tutakaa mstari mmoja na kukubaliana kwa pamoja kuwa haya ndiyo tunayoyataka kutoka kwa viongozi wetu, mfumo wetu wa utawala na dola, nafasi ya kupata viongozi wazuri, kuwa na mipango mizuri itafanikiwa na hivyo kuruhusu wananchi na viongozi kuwajibika kwa dhati na kujituma ili kuhakikisha kuwa shughuli za Ujenzi wa Taifa kiuchumi unafanikiwa kukiwa na Amani, Mshikamano, Sheria na Uongozi Bora.

Uchumi

Tunapozungumzia Uchumi, tunazungumzia kazi, maliasili, mapato, matumizi, biashara, viwanda, kilimo, ajira na mengineyo.

Uchumi wetu hauwezi kujengeka kwa kutegemea misaada au wawekezaji kutoka nje kuja na kusukuma gurudumu la uzalishaji mali ili kutuongezea kipato. Aidha uchumi wetu hautajengeka kuwa madhubuti kwa kuanzisha mipango mipya au kufanya makosa yaleyale ya kale yaliyofanyika wakati wa Azimio la Arusha, Mipango ya kufufua uchumi 1985-2000 au mipango ya kuchochea uwekezaji na kuvutia wageni washike hatamu za Uchumi ya 1992-2010.

Uchumi utakaoleta matunda ya kweli na ya maana ni uchumi utakaotokana na juhudi za wananchi katika shughuli zote za uzalishaji mali. Tunahitaji tuwe na mipango inayoeleweka na rahisi kufanikisha safari hii ya kujenga uchumi kwa kutumia mazingira yetu, rasilimali zetu na kwa faida yetu.

Mipango mipya ya Uchumi iundwe kwa kutumia mazingira ya Taifa letu, uwezo wetu wa kifedha na uzalishaji mali, uchochee ushindani wa uzalishaji mali wa ndani na kuulinda dhidi ya utegemezi wa bidhaa za nje. Kipaumbele cha kutoa ruzuku, misamaha ya kodi na ushuru ilengwe kwa wazalishaji mali wa ndani kama kichocheo na motisha kwa kuongeza ufanisi na uzalishaji mali na si kwa wageni kama kivutio kuja wekeza.

Kiwango cha matumizi na kipato cha Mtanzania kwa vipimo vya kimataifa ni dola 1 ya kimarekani kwa siku. Hii ni sawa na shilingi 1500.00 kwa siku! Je hii ni sahihi kwa nchi yenye ardhi yenye rutuba nyingi, mali asili za kutosha na watu wenye nguvu za kuzalisha mali ambao wanachokosa ni Uongozi mahiri?

Kwa nini basi tusijisogeze kutoka umasikini wa kupindukia na kuwa katika daraja la kati? Njia ni nyingi za kuliongeze mapato Taifa letu, na kwa kuanzia nitaanzia na mapato na matumizi ya Serikali.

Mapato na Matumizi ya Serikali

Moja ya njia zitakazotumika kuimarisha uchumi ni kubadilisha mfumo wa mapato ya Serikali na kudhibiti matumizi.

Kwa kawaida, mapato ya Serikali hutokana na makusanyo ya kodi na ushuru. Viwango vya kodi na ushuru vya Tanzania vimewekwa kumkandamiza Mtanzania mtumiaji wa huduma na bidhaa anayetegemea mshahara mdogo au mapato madogo kutokana na shughuli zake za uzalishaji mali, huku makampuni na mashirika ya ndani na hasa ya nje yakilindwa kwa kutozwa kodi ndogo au kupewa kinga na kufutiwa kodi na ushuru kwa kisingizio cha vivutio kwa wawekezaji.

Nikilenga hoja yangu kwa wawekezaji, mfumo wetu wa kuingia katika mfumo wa soko huria una mianya mikubwa ambayo imeachia kukua kwa mizizi ya unyonyaji ambayo si kwamba imelipunguzia Taifa pato lake, bali pia limezidisha kukomaa kwa rushwa na kuongezeka kwa vitendo vya uhujumu na ufisadi.

Kwa kuanzia, Serikali itabidi kupitia mikataba yote na kuongeza viwango vya kodi na ushuru (taxes, duty and royalties) zinazopatikana kutokana na wazalishaji mali wawekezaji. Kiwango cha asilimia 3% tunachotoza kwa shughuli za uchimbaji madini, gesi, makaa na hata huko mbeleni madini ni kidogo sana. Serikali ifuatilie kwa makini mapato halisi ya makampuni yote yanayojishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na kuhakikisha kuwa Serikali inapata malipo ya kweli na yanayowiana na uzalishaji na mapato ya makampuni haya.

Serikali ipitie majedwali na ripoti za mapato ya kifedha (financial statements and bapance sheets) ya makampuni haya katika nchi zilikoandikishwa kila mwaka. Mfano pamoja na kuwa kampuni ya Barrick inatozwa asilimia 3% kama kodi kwa Serikali ya Tanzania, ni ukweli usiofichika kuwa Serikali na taifa la Tanzania linapunjwa. Mpango wangu utahamasisha kuchangua vitabu vya kampuni hii katika soko la mtaji la kimataifa kama NYSE, na kuangalia ni mapato kiasi gani ambayo wameyaorodhesha.

Mapendekezo ya kubadilisha viwango hivi vya mapato ya Serikali yanayotokana na uzalishaji mali wa makampuni mageni na hata enyeji, utahakikisha kuwa misamaha yote ya kodi na ushuru ambayo imetumika kama chambo cha kuvutia uwekezaji na kufanya biashara inafutwa au itapewa kipindi kifupi mno ili kupunguza hujuma na dhuluma.

Mapendekezo ya kuongeza mapato yatakuwa ni kuongeza viwango vya kodi za mapato kwa makampuni haya ya madini, nishati na utalii kutoka 3% hadi kufikia 30% katika kipindi cha miaka mitano tangu sheria ianze kutumika. Hili litasaidia kuongezeka kwa pato la kweli kwa Serikali kwa asilimia 27% kupitia kodi na ushuru.

Sheria za uwekezaji ni lazima ziwe kali ili kuondokana na wimbi la kufumuka kwa makampuni hewa au makampuni yasiyo na uwezo katika uzalishaji mali. Mifano ya Richmond, IPTL, Rites na mingine si midogo kupuuziwa. Wawekezaji wote kutoka nje ya nchi kwa shughuli zote za uzalishaji mali  watapaswa wawe na yafuatayo kabla ya kupewa leseni au kuingia mkataba wa kufanya kazi ndani ya nchi na kwa niaba ya nchi;

  • mtaji wa kutosha, japo asilimia 300% ya gharama nzima ya mkataba au shughuli za uzalishaji mali
  • dhamana ya kutosha kutoka Benki ya nchi mama na udhamini kutoka idara ya biashara ya nchi mama ambako kampuni au shirika hili limesajiliwa
  • historia chanya ya kikazi na kufanya miradi ya fani wanayokuja kuwekeza au kuingia mkataba si pungufu ya miaka 15 ya kazi zao kimataifa na nchini mwao
  • kuandikisha na kuuza hisa za shirika hili katika soko la mtaji la ndani DSE ili kuruhusu na kuhamasisha Watanzania na wafanyakazi wa shirika na makampuni haya kuwa washiriki katika umiliki wa mashirika haya
  • kuwasilisha vitabu vyao vya ukaguzi wa mahesabu kwa miaka 10 kabla ya kuja Tanzania na kuendelea kuwasilisha vitabu vyao ambavyo vinaripotiwa katika nchi zao, kwa mamlaka ya kodi Tanzania ili kuhakikisha kuwa hakuna mapungufu katika kuripoti mapato ya makampuni haya kwa shughuli zao za uzalishaji mali nchini Tanzania

Umiliki katika sekta binafsi na hasa kutoka kwa wawekezaji wa nje utungiwe mfumo na sheria ambazo zitahakikisha kuwa Umiliki wa Mashirika na Viwanda hivi kwa wazawa unakua na kufikia asilima 30% ya umiliki katika miaka 10 ya kwanza tangu shirika hili lianze shughuli zake za uzalishaji mali wake ziwe ni za madini, uvuvi, kilimo, utalii, huduma, bidhaa za matumizi au shughuli nyingine. Hili linawezekana kwa kuuza hisa katika soko la mitaji DSE au kugawa hisa kama motisha na bonasi kwa wafanyakazi wa Kitanzania katika mashirika haya.

Dhumuni la kuwa na sheria kama hizi ni kuhakikisha Tanzania inakaribisha wawekezaji ambao si matapeli au wahujumu ambao wanapita kutunyonya na kutuacha masikini huku wakiwanyanyasa Watanzania wanaofanya kazi katika mashirika na makampuni haya. Sheria hii itahakikisha kuwa kuwa Taifa haliendelei kunyonywa na hivyo maslahi na mali asili za Watanzania zinawanufaisha Watanzania na si wawekezaji pekee. Matarajio ya mpango huu ni kuwa Wawekezaji wenye utu watakubaliana na kufanya kazi na Serikali na Taifa kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mapato haya ya kutokana na ongezeko la kodi, ushuru na umiliki yataliongezea Taifa pesa za kuweza kuondokana na misaada na mikopo ambayo imetulemaza na kutufanya kuwa tegemezi na masikini. Kuongezeka kwa mapato kutokana na kodi na ushuru kutapunguza ule mzigo wa Serikali kutegemea mazao ya chakula na biashara katika kupata fedha za uendeshaji. Mapato haya yatakuwa moja ya nyenzo kuu za kujenga uchumi kwa kutumika katika kuboresha sekta za Elimu, Afya, Miundombinu na Nishati.

Kwa upande wa Serikali za Mikoa, Wilaya na Mitaa na halmashauri za miji na wilaya, mfumo wa kuruhusu kujipatia mapato kutokana na kodi za mauzo na mapato utatambulishwa ili Mamlaka hizi zianze kuwa na uwezo wa kujipatia mapato mbali na mgao kutoka Serikali kuu. Hii itakuwa moja ya mbinu itakayotumika ili kurudisha ule mpango wa madaraka mikoani na kupunguza ukubwa wa Serikali Kuu.

Sambambana kuongeza mapato, ni lazima Serikali ifanye kazi ya ziada kubana matumizi yake. Serikali itabidi iweke mkazo katika kubana matumizi na kuhakikisha hakuna ufujaji wa mapato au kuvuka viwango vya bajeti. Ripoti ya Mkaguzi mkuu wa mahesabu ya Serikali ya mwaka 2006-2007 inaonyesha matumizi na udhibiti mbaya wa pesa za Serikali zote za matumizi na maendeleo.

Kupunguza na kubana matumizi haya kutafanikiwa kwa kupunguza ukubwa wa Serikali, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kudhibiti matumizi holela ya mapato, malipo hewa au malipo yasiyo na vithibitisho. Masalio yote ya pesa ambazo hazikutumika katika mwaka wa fedha yarudishwe Hazina na yasitafutiwe matumizi ili fedha za bajeti zimalizike. Ziada irudishwe hazina na itumike kwa shughuli za maendeleo.

Tabia ya Serikali kuu kukopa na kuomba omba kwa wahisani na hata kwa kupita soko la mitaji Benki Kuu, inabidi idhibitiwe. Mazoea mabaya ya kukopa hujenga hisia za kutokuwajibika na kuthamini mali. Aidha hulemaza Taifa kuwa tegemezi na hivyo kukosa mwamko wa ubunifu katika uzalishaji mali na udhibti wa matumizi.

Tanzania ni nchi tajiri ambayo ikiweka mipango na mikakati ya nguvu kazi na kudhamiria kujitegemea, katika kipindi cha miaka 20 inaweza kuhama kutoka kundi la nchi masikini zisizona maendeleo au Dunia ya Tatu na kuwa katika kundo la nchi za dunia ya pili, nchi zenye maendeleo ya wastani kiuchumi. Serikali yetu ikitumia vizuri mapato yake, ikadhibiti matumizi na kuwa na mipango bora ya kiuchumi, Tanzania itapiga hatua kubwa kiuchumi na ile sifa tuliyojijengea miaka 20 ya kwanza tangu tupate uhuru itarudi.

Moja ya mambo ambayo yamegeuka kuwa utamaduni katika Serikali na ajira Tanzania ambayo huongeza marudufu matumizi ambayo yanachochea ubadhirifu ni kuwepo kwa ongezeko la masurufu na malipo ya ziada kwa ajili ya kushiriki kwenye makongamano, semina, kusafiri nje ya kituo cha kazi au kuwa mjumbe wa kamati maalum.

Hii inatokana na mfumo duni wa mishahara midogo inayolipwa kwa waajiriwa kutokana na kukomaa kwa dhana potofu iliyotokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kupitia Azimio la Arusha. Makosa yaliyotokea awali ambayo kwa kiasi kikubwa ni kiitikadi au uchache wa mapato kutokana na uchanga wa Taifa letu, uliishia kujenga chuki kwa kuwa na mishahara mikubwa ambayo inawiana na kazi na kukidhi makali ya maisha.

Badala ya Serikali kuongeza mishahara, motisha kwa wafanyakazi ulikuja kwa njia ya huduma kama magari na mafuta ya bure, huduma za afya za bure, nyumba, wafanyakazi wa ndani na nje kwa watendaji wa Serikali na mashirika. Njia hizi zilileta hasara kwa Serikali na Mashirika na hivyo kutoa mwanya kwa kuzuka kwa tabia ya kupenda na kutegemea huduma kama fidia ya ufinyu wa mishahara. Nitaliongelea kwa kirefu katika sehemu ya Ajira na Mishahara.

Serikali inaendelea kunapoteza pesa nyingi kwa kugharamia “mishahara” ya ziada ambayo inalipwa ili watu watimize wajibu wao. Mfano hakuna sababu kwa wajumbe wa kamati za bunge au tume za Rais kama ile ya EPA kulipwa masurufu ya kazi (allowance) huku wanapokea mishahara na kuwepo kwa katika Kamati au Tume ni moja wa wajibu na majukumu yao ya kazi.

Misafara ya ndani na nje ya nchi inapaswa kupunguzwa na Serikali itabidi ifute masurufu yanayolipwa wafanyakazi wake au wa mashirika ya umma kwa kushiriki katika vikao au safari nje ya vituo vyao vya kazi. Wajibu wa Serikali kwa mtumishi anayesafiri nje ya kituo cha kazi ni kulipia nauli, chakula na mahali pa kulala na si mshahara au marupurupu. Misafara na kusafiri daraja la kwanza ni gharama kubwa. Hakuna ulazima wa misafara na uwakilishi wetu hasa nje ya nchi uwe wa kila mtu na kila kitengo. Ukiondoa Raisi, Makamu wake, Waziri Mkuu, Spika na Jaji Mkuu, viongozi wengine wote wasafiri katika madaraja ya kawaida na si daraja la kwanza. Rais anaposafiri, hasa nje ya nchi hahitaji kuongozana na msururu wa wafanyakazi, viongozi au wapambe. Asafiri na wale ambao ni muhimu kwa mujibu wa madhumuni ya safari hiyo.

Serikali yetu imeshindwa kuwa makini na kuongeza matumizi yasiyo ya msingi ili kuhimili shinikizo na kutimiliza wajibu wa kisiasa. Mfano mzuri ukiwa ni ile Semina ya viongozi wakati awamu ya nne iliposhika madaraka kule Ngurdotu na zile safari za Mawaziri na watendaji wa Serikali mikoani kutuliza fukuto la vita vya Ufisadi, kwa kutumia kisingizio cha kutangaza na kuelimisha umma kuhusu bajeti.

Kwa kuwa tumeingia katika mfumo mpya wa Uchumi na ni ayetu ya kudhibiti atumizi holela, Serikali inabidi kuachana biashara ya kuwa “wenye nyumba” au huduma za magari na teksi bubu. Ukiondoa Raisi, Makamu wa Raisi, Waziri Mkuu, Spika, Jaji Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa majeshi ya Ulinzi na Polisi, viongozi wengine wote wa Serikali, majaji, mahakimu, makatibu wakuu, wakurugenzi, wakuu wa wilaya , wabunge na wengineo wote, watabidi waingie gharama kutokana na mishahara yao kulipia gharama za nyumba na usafiri wao kwenda na kutoka kazini.

Serikali inaingia gharama kubwa kutunza nyumba hizi na magari ambazo si za muhimu. Dhana ya kuufuma na kupata kila kitu kwa bure inabidi iishe. Serikali ipunguze madaraja ya Watendaji wake ambao wanastahili kupewa na kuishi katika nyumba za serikali na kutumia magari ya Serikali.

Kama Taifa tunaingia gharama kubwa sana kwa kuwapa viongozi “marupurupu” ya kuwa na magari mpaka matatu ya kazi, madereva, mafuta kwa hata safari binafsi, kuwa na nyumba za serikali huku watendaji hawa wakilipiwa umeme, maji, simu na hata chakula.

Taifa letu halijawa na mavuno mazuri ya utajiri wake ambao mkubwa kiasi hicho kuendekeza ufahari ambao ni ufujaji wa mali na mapato.  Hata nchi tajiri kama Marekani na Japani, ni viongozi wachache sana ambao hunufaika kwa kutegemea marupurupu kama nyumba na magari ya Serikali.  Tanzania ni nchi masikini kimapato, lakini tunajiendesha kwa majigambo na tunatumia fedha hovyo bila woga na kujiuliza tunapata wapi pesa kujiendesha. Pendekezo litakuwa ni kuwapa mikopo kununua magari, kuwalipisha kodi za pango la nyumba na kuhakikisha kuwa wanalipia bili zao za umeme, maji, simu, watumishi wa ndani na chakula chao.

Uchumi wetu utaanza kujengeka kwa uimara tukianza kujenga misingi bora ya maarifa na hii ni kupitia sekta ya Elimu.

Elimu

Mfumo wa elimu wa Tanzania unabidi kubadilika na kuhakikisha kuwa tunajenga mfumo wa elimu ambao unachochea ubunifu, unarahisisha uzalishaji mali na unawiana na maendeleo yetu. Tulirithi mfumo mbaya wa Elimu ya kikoloni ambayo lengo lake lilikuwa ni kuweka vizingiti ya kuelimika kwa Watanzania na kubana upeo wetu katika elimu kwa vitu vichache hasa ualimu na utabibu. Kuna haja ya kuachana na mfumo wa Elimu ya kufaulu na kuhakikisha kuwa kinachofundishwa kinaeleweka na kinaweza kutumika ipaswavyo na wanafunzi wote, kuanzia chekechea, shule ya msingi, sekondari, vyuo vya fani stadi , elimu ya watu wazima na hata elimu ya juu.

Tanzania ina wasomi wengi, lakini hawajaelimika na kuerevuka kutumia elimu zao kwa ufanisi. Aidha viwango vyetu na ubora wa elimu inayotolewa kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu ni vya hali ya chini  na duni kulinganisha na majirani wetu na kimataifa. Chimbuko la uduni huu ni pamoja na kurithi elimu duni ya kikoloni ni mfumo mbovu ambao nimeutaja hapo juu ambao unalenga kuzalisha wanafunzi wanaofaulu lakini wakiwa na uelewo mdogo wa masomo na fani walizosomea.

Lugha ya kufundishia pia imekuwa ni sababu ya kudhoofika kwa elimu yetu. Kasumba ya Kikoloni imetufanya tuthamini lugha ya Kiingereza ambayo ni lugha ya tatu kwa Mtanzania wa kawaida hata yule tunayemuita msomi. Tanzania pamoja na kuwa na makabila zaidi ya 120, tuna lugha moja kuu ambayo imetuwezesha kuwasiliana na kujenga Utaifa wetu Kiswahili.

Badala ya kuweka mkazo na mtaji kuboresha Kiswahili kikue na kutumika kufundishia ili wanafunzi wajifunze kwa urahisi nadharia ya masomo na kuelewa wanachofundishwa na kukitumia kwa urahisi katika kazi zao, tunaendelea kutumia lugha ngumu Kiingereza tukitegemea kuona maendeleo ya haraka.

Mpango wangu kuboresha Elimu ni kuhakikisha kuwa mitaala na silabasi za kufundishia zinalingana na mahitaji ya jamii. Kipaumbele kitakuwa si kuongeza shule pekee ili kuongeza maarifa na taifa la walioelimika, bali ni kuongeza ubora na viwango vya elimu, elimu ambayo itafundishika kwa urahisi na kuweza kutumika kwa vitendo kadri wanafunzi wanavyoendelea kujifunza. Mkazo utakuwa ni kutumia lugha ya Kiswahili ili Watanzania wawe wataalamu mahiri kwa lugha yao asili. Ikiwa China, Japani, Ufaransa, Sweden na Iran wana maendeleo hasa ya Sayansi na biashara kwa kutumia lugha mama kwa nini sisi Watanzania tuogope na kuona aibu kutumia Kiswahili?

Mkazo utakuwa ni kuwa na walimu wenye uwezo wa kufundisha na wenye mapenzi katika fani ya ualimu. Waalimu watapewa kila nyenzo zinazohitajika kuhakikisha kuwa kazi zao zinafanyika kwa ufanisi na mafanikio na matunda ya kazi zao yanaonwa na kupokewa na jamii nzima.

Katika mpango wangu, kila Wilaya itapaswa kuwa na Shule si chini ya mbili za Sekondari na chuo cha ufundi ambazo zitakuwa chini ya mamlaka za Tamisemi. Kila mkoa utapaswa kuwa na shule za sekondari ya elimu ya juu si chini ya 4, Vyuo vya ualimu, uuguzi na utabibu, kilimo, uvuvi na mifugo, , biashara na uhasibu, ufundi (mithili ya Dar Tec), sanaa utamaduni na michezo. Hili litawekewa malengo ya kukamilika kikamilifu na matunda kuonekana katika miaka 10 tangu utekelezaji uanze na mpango huu kutumika.

Katika elimu ya juu ya kiwango cha Chuo kikuu, msukumo utakuwa wa kuwa na chuo kikuu kwa kila mkoa ifikapo mwaka 2030. Katika hili, uchochezi wa kupanuka kwa sekta ya elimu utajumuisha watu binafsi, taasisi za kidini na jumuiya za maendeleo za mikoa.

Mpangu huu wa elimu pia utarudisha elimu ya watu wazima kwa kuundwa upya kwa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima. Hivi karibuni kumekuwa na ripoti na takwimu zinazoonyesha kuwa asilimia 31% ya Watanzania watu wazima, hawajui kusoma na kuandika. Hii ni aibu na jambo la kutisha na kufadhaisha. Ina maana kuwa hawa 31% hata uwezo wao wa kuzalisha mali ni wa mashaka kutokana na kukosekana msingi imara wa chemsha bongo.

Jukumu la Serikali kuu litakuwa ni kuratibu mfumo wa elimu na si kuendesha kila kitu kuhusiana na Elimu. Chini ya mpango huu, Serikali Kuu itasaidia kwa kipindi cha miaka minne kwa shule na vyuo kujijenga na uendeshaji wake na baada ya hapo, jukumu litakuwa katika Serikali ya mitaa na jamii kuhakikisha kuwa wajibu wa kuziendesha shule na vyuo hivi havitegemei Serikali kuu pekee.
Serikali kuu itakuwa tayari kutoa msaada na ushauri.

Serikali kuu itajenga mfuko na mfumo mpya wa mikopo ya Wanafunzi na kuachana na bodi ya mikopo ya Wanafunzi iliyoko sasa hivi ambayo ni kero kwa wananchi na wanafunzi.

Matarajio ya mpango huu wa elimu ni kuwa kwa kusogeza mchakato mzima wa elimu kwa mamlaka za mikoa, zitasaidia ile dhamira ya kusukuma madaraka mikoani, wananchi wa mikoa na wilaya watapata fursa sawa na wale walioko katika mikoa mingene ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikinufaika kwa kuwepo kwa kila aina ya shule na vyuo.

Msisitizo utakuwa katika elimu ambayo itazalisha watu ambao wako tayari kufanya kazi. Fani kama uhunzi, uashi, useremala, ufundi mchundo, bwana shamba, bwana maji, fundi umeme, magari, na ujenzi zitaongeza idadi ya watu wenye ujuzi si wa asili na kuvumbua binafsi, bali kwa kupata mafunzo na nyenzo za kuboresha vipaji asili katika fani hizo.

Tutakapoweza kuwa na msingi bora wa elimu ambayo utaongeza maarifa na kuchochea juhudi za kila mmoja wetu na kuhakikisha kuna ushiriki wa kila mmoja na kila mmoja ana nafasi ya kuwa bingwa katika fani yake, masuala kama ukosefu wa ajira au kukosekana kwa walio na utaalamu katika fani mbali mbali utapungua.

Lakini hatutaweza kufanikisha azma ya kuwa na mfumo na elimu bora ikiwa maslahi na vitendea kazi vya waalimu na shule zetu vitaendendelea kuwa duni na dhaifu, huku Serikali ikifumbia macho na kusukuma wajibu huo kwa Wananchi, Waalimu na uongozi wa shule na vyuo hivi. Suala la maslahi ya waalimu nitaliongelea kwa mapana na marefu katika kipengele cha Ujira, Mishaharana maslahi ya Wafanyakazi.

Afya

Hakuna jamii yoyote itakayoweza kuendelea bila kuwa na mipango madhubuti ya kiafya. Rev. Kishoka plan italenga katika kuhamasisha afya kwa kutumia kinga na si kusubiri matibabu. Kila wilaya itakuwa na hospitali ya wilaya, yenye waganga na wauguzi wa kutosha walio mahiri na wenye nyenzo tosha kufanya kazi zao kwa uhodari na ufanisi, na kila Mkoa utakuwa na hospitali kuu ya mkoa ambayo itakuwa ni ya rufaa na uwezo kama hospitali za Muhimbili, Mawenzi, Arusha , KCMC au Bugando.

Nia na mwongozo utakuwa si kutibu tu bali ni kutoa kinga na kuhamasisha kinga, kila wilaya itapaswa kuwa na mipango madhubuti ya afya ambayo itashabihiana na malengo ya Serikali kuu katika mipango ya kuimarisha afya. Serikali itatumia ushawishi kuhamasisha sekta na taasisi binafsi hasa za kidini kuanzisha na kusambaza Hospitali katika mikoa na wilaya. Serikali itawekeza nguvu na mkazo katika bajeti zake kuhakikisha kuwa katika kata na tarafa kunakuwa na zahanati ambazo zitaweza kutoa huduma ya kwanza na za kawaida kwa wananchi wa maeneo ya kata na tarafa hizo.

Elimu ya afya bora itahamasishwa katika ngazi zote za elimu, na jamii kwa ujumla. Mipango ya lishe na chakula bora, uzazi na malezi bora, mimba kwa watoto na wanafunzi, chanjo muhimu kwa watoto, vita dhidi ya kipindupindu, malaria, kifua kikuu, polio, ndui, degedege, kwashiakor, huduma kwa walemavu na wazee, utapiamlo na ukimwi vitakuwa ni vitu ambavyo vitakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha tunajenga kinga na tuna uwezo bora wa kutibu pale inapiobidi kutibu.

Maji safi ni sehemu ya Afya ingawa tunaweza kusema maji yanahitaji sehemu yake maalum. Kama kigezo cha afya, suala la maji safi na umuhimu wa maji safi utaendelea kufundishwa kila ngazi, mashuleni, vyuoni, kwenye kata, tarafa wilaya na mkoani.

Tishio la Ukimwi si la kuupuzwa hata kidogo. Tatizo la Ukimwi si la kiafya tu, bali ni hata usalama wa taifa. Ikiwa karibu nusu ya Watanzania ambao wana umri kati ya miaka 12 hadi 45 wako hatarini kupata ukimwi au karibu robo ya Watanzania wa umri wa kufanya kazi tayari wana virusi vya ukimwi, tujiulize je katika miaka 20 ijayo ni nani atakuwa hai na mwenye nguvu kuzalisha mali?

Mpango wa Serikali wa vita dhidi ya ukimwi utahamasishwa kwa kuomba taasisi za kidini na binafi pamoja na mashirika kuwa na elimu maalum katika maeneo yao kuhusu athari za ukimwi kwa jamii na Taifa.

Taifa lenye maarifa kutokana na elimu nzuri na afya njema, ni taifa ambalo litakuwa tayari kuwa na juhudi na mwamko kufanya kazi kwa juhudi ili kujikwamua kutoka umasikini na utegemezi.

Kilimo

Asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini na wanategemea Kilimo, Uvuvi na Ufugaji kama vyanzio vuya mapato ili kujipatia maendeleo. Kilimo chetu ni cha kujikimu, tunalima japo kidogo kututosha kwa leo na kesho, lakini msukumo wa kulima chakula cha kutosha hata mtondogoo na wiki mbili zijazo hatuna.

Hii inatokana na sera na nyenzo duni katika uzalishaji mali katika kilimo, uvuvi na ufugaji. Chini ya mpango huu, msukumo wa kuchochea mapinduzi ya kilimo utafanywa. Zile nguvu za sera ya Kilimo cha Kufa na Kupona zitatumika kuhamasisha Wakulima kutumia utaalamu wa kutumi pembejeo za mbolea, kuachana na majemb e ya mkono na kuanza kutumia maksai au matrekta, kutumia mbegu bora na kutunza mazao yao kwa kujenga maghala imara. Tanzania inahitaji kuondoka kutoka mfumo wa kilimo cha kujikimu na kuhamia katika mfumo wa kujitosholeza na kibiashara kwa kutumia maarifa ya sayansi na teknolojia.

Serikali itarudisha ruzuku katika zana za kilimo na shughuli za kilimo. Serikali itatoa msamaha wa ushuru na kodi kwa vitendea kazi vya kilimo kwa muda wa miaka mitano ikiwa ni uchochezi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, kujipatia nyenzo bora kwa unafuu ili kuimarisha shughuli za uzalishaji mali.

Kwa kupitia wizara ya Kilimo na taasisi za kilimo na vyuo vya kilimo, ubwana shamba, mifugo au uvuvi, Serikali itatoa changamoto kwa ushindani wa kilimo cha chakula na biashara na kuhakikisha kuwa kila kata na tarafa zina mabwana shamba wa kutosha ambao wanaelewa kazi zao na wanaweza kufundisha wakulima, wafugaji na wavuvi mbinu mpya na za kisasa za kilimo.

Pamoja na kuwa binafsi sikubaliani sana na matumizi ya mbegu maalum (Genetically Modified), Serikali itapaswa kutoa msukumo kwa maeneo maalumu ya kufanya majaribio ya kutumia mbegu hizi ili kuona na kupima uzalishaji mali, athari na masoko kutokana na mazao yanayotokana na mbegu maalum.
Kilimo cha matunda, maua, viungo vya kupikia (spices), ufugaji wa kuku, ng’ombe wa nyama na maziwa, mbuzi wa nyama na hata maziwa na hata ufugaji na kuzalisha farasi ni vitu ambavyo vinaweza kwa uwezo mkubwa kutuongezea kipato na si kudhania kuwa kilimo ni lazima kiwe cha mahindi, nyanya, kahawa na maharage pekee.

Mkazo utakuwa katika uzalishaji chakula cha kutosha kulisha Tanzania na hata kulisha Afrika Mashariki na Kati nzima. Mbinu bora za ukulima wa kisasa ikiwa ni pamoja na kuwezesha Wakulima kupumzisha ardhi hata kwa mwaka mmoja vitafanikiwa ikiwa wakulima watafundishwa na kusukumwa kuachana na kilimo cha kujikimu (subsistance).

Pamoja na kushamiri kwa msukumo wa Kilimo cha mazao ya nishati ambayo yana bei kubwa, mkazo na kipaumbele utakuwa kwenye kulima mazao ya chakula na biashara na kama hali itaruhusu, mazao ya nishati yataruhusiwa na kuchochewa kwa uangalifu ili tusife njaa huku wenzetu wakineemeka kwa bei rahisi ya mafuta.

Tanzania imejaliwa kuwa na vianzio vingi vya maji, mabwawa, mito na maziwa. Haya ni tosha sana kuhakikisha tunakuwa na mfumo bora wa umwagiliaji maji ikiwa kuna shida au kutotabirika kwa mvua.

Aidha katika shughuli za kilimo, hamasisho la kulima misitu ya mbao litawekwa kwa wananchi ambao wako kwenye mikoa ambayo ina rutuba ya kuzalisha misitu ya mbao. Mbinu za kitaalamu za sayansi kutoka kwa mabwana shamba wetu zitatumika kufanikisha lengo hili.

Taifa letu linabidi lirudi katika ramani ya kuzalisha Chai, Tumbaku, Kahawa, Pamba, Pareto, Katani, Korosho, Karafuu kwa ubora na kuwa katika ngazi za juu za uzalishaji wa mazao haya ya biashara. Msukumo hautakuwa kuzalisha kwa ajili ya kusafirisha nje tuu, bali utatumika kama kichochezi cha kuanzishwa viwanda vya kusindika (process) na kuzalisha zao la mwisho na mauzo yetu nje ya nchi yatakuwa ni bidhaa ambazo ni tayari kwa matumizi na si kwenda kwenye viwanda Ulaya, Marekani au Asia kuboreshwa na kuuzwa kwa mtumiaji.

Motisha kutoka Serikali kuu utahitajika ili kuanzisha wakulima wa mashamba makubwa (farmers) na kuwakusanya wakulima wadogo wadogo (peasants) kufanya kazi kwa ushirika ili kuimarisha jamii. Makosa yaliyotokea wakati wa Sera ya Vijiji vya Ujamaa, Vyama vya ushirika yanapaswa yaepukwe.

Vyama vya Ushirika vya wakulima, wavuvi na wafugaji, viundwe na wakulima wenyewe na viongozwe na wakulima na si wanasiasa au kufanywa ni vyombo vya siasa. Dhamana ya kuvijenga vyama vya ushirika wa Wakulima ni ya wakulima wenyewe. Shughuli za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji havitakuwa jukumu la wakulima pekee, bali viwe na uratibu wa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Mifugo, Chama cha Wakulima TFA, Vyuo vya Kilimo kama SUA, TAFICO, Ranchi za Taifa bodi za mazao za Ushirika kama KNCU na Mamlaka za mauzo kama Kahawa, Tumbaku na Pamba.

Ukulima wa kisasa si jambo la kutuchukua miaka 10 kuanza kufanyiwa kazi, ni jambo la kuanza kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo na Serikali isilipuuzie au kutokulipa umuhimu na kipaumbele.

Tanzania bado inategemea 50% ya mapato yake yatokane na Kilimo na 80% ya wananchi wake ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Neema tulizonazo ni nyingi kwa Taifa kuhangaika tunapokosa mvua kutokana na tishio la njaa. Hili lisitokee tena, nafasi ya kusahihisha yaliyopita tunayo, na sababu tunazo.

Lengo kuu litakuwa kwa Taifa kuweza kujitosheleza kwa Chakula na kuachana na mtindo wa kuagiza kila kitu mpaka pilipili. Ili kusisimua uzalishaji mali wa Chakula, Serikali itaweka udhibiti mkali katika uagizaji wa Chakula. Mbinu moja ya kuhamasisha uzalishaji mali wa kilimo utakuwa ni kutoa Ruzuku kwa Wakulima na zana za Kilimo, kuwa na kodi nafuu kwa bidhaa zinazozalishwa ndani na kuongeza marudufu viwango vya kodi na ushuru kwa vyakula vya kuagizwa ili kulinda uchumi wa ndani na mkulima.

Ikiwa Mataifa makubwa yaliyoendelea yanamlinda Mkulima wa nchi yao, iweje sisi “masikini” tushindwe kumlinda Mkulima wetu kwa kumpa unafuu wa kuzalisha Chakula na kumlinda kiushindani na vyakula vya kuagizwa?

Miundombinu na Nishati

Sasa hivi moja ya vikwazo vya kusambaa kwa maendeleo nchini ni kutokana na kuwa na miuondombinu mibovu na utegemezi wa mafuta na mvua katika kupata nishati.

Tangu mkoloni ajenge reli ya kati na Mchina kutusaidia na TAZARA, hatujawekeza msukumo wa kupanua au kuboresha mfumo wetu wa reli. Hali kadhalika hali ya barabara zetu na vyombo vya majini ni mbaya kwa kuhatarisha usalama na mwenendo mzima wa maendeleo.

Katika mpango huu wa Mchungaji, Serikali iweke mipango na malengo ya kuhakiksha kuwa ujenzi na upanuzi wa barabara kuu unafanyia katika kipindi cha miaka 30. Lengo litakuwa ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2050 kila mkoa na wilaya Tanzania itakuwa imeunganika katika mfumo mkuu wa barabara bora na imara ambazo ni za lami na upana wa kutosha ili kurahisisha usafirishaji na uchukuzi.

Aidha Reli zetu za Kati, Arusha na TAZARA zipanuliwe na kurekebishwa ili kuhakikisha kuna ufanisi wa usafiri wa watu na mizigo. Kwa kuwa kuna lengo la kuunganisha jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Kati na hata kupitia SADC kwa kuwa na mfumo mzuri wa uchukuzi kupitia Barabara na Reli, Serikali kwa kutumia wataalamu wa ndani na wa nje na wahisani itaweka mpango kabambe wa kufufua na kujenga barabara kuu na reli ambazo zitakuwa za viwango vya kimataifa na kurahisisha mtiririko wa maendeleo na huduma si kwa Tanzania pekee bali hata kwa majirani zake.

Katika nishati, nia ni kuachana na utegemezi wa mafuta na mvua kuzalisha umeme. Tanzania imejaliwa kuwa na mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme, lakini kutokana na kutotabirika kwa mvua na hali ya mazingira duniani ambayo yamepunguza mvua na vina vya maji, kuna haja ya kuwa na mpango wa kutumia na kuzalisha umeme kwa kutumia upepo na mionzi ya jua.

Lengo litakuwa ni kuhakikisha kuwa kwa kutumia sheria mpya za ushindani za EWURAS, vyanzo vipya vya nishati vinahamasishwa na kupewa kipaumbele. Maeneo tambarare kama Dodoma na Singida, yana uwezo mkubwa sana kuzalisha umeme wa upepo ambao unaweza kulisha zaidi ya 30% ya mahitaji ya umeme kwa Taifa. Hali kadhalika umeme wa jua, tuna maeneo mengi na hasa vijijini ambako kama tutaweka kipaumbele na jitihada, basi kila nyumba ya Mtanzania ifikapo mwaka 2050 itakuwa na umeme, uwe ni wa maji, upepo, jua au mafuta.

Kuwepo kwa nishati ya kutosha isiyochechemea itasaidia uzalishaji viwandani na kuboresha uhifadhi wa mazao na vyakula katika ghala kwa kuwa kutgakuwa na umeme wa kuaminika.

Ni katika sekta hii, Serikali itatoa vichocheo kwa wawekezaji wa ndani na wan je ambao watakuwa na uwezo katika kipindi cha miaka 5 kuthibitisha wana uwezo wa kuzalisha Umeme wa nguvu za jua na Upepo. Serikali itatoa msamaha na kurejesha 75% ya kodi iliyolipwa katika miaka mitano ya kwanza ikiwa miradi hii itakuwa tayari imeshafanya kazi bila wasiwasi katika miaka 7 ya kwanza tangu shughuli nzima za uzalishaji nishati zianze.

Kusambaa kwa nishati vijijini hakutasaidia hifadhi za chakula pekee, bali kutasaidia hata kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti ili kutengeneza makaa na kupata kuni za kupikia.

Serikali itapendelea ushindani wa uzalishaji umeme vijijini uendeshwe sin a watu binafsi pekee, bali mashirika ya maendeleo ya wilaya au mikoa kuchukua jukumu hili na ikiwezekana hata mashirika haya yawe ya ushirika wa wanavijiji.


Viwanda, Mashirika, Huduma na Biashara

Makosa ya Azimio la Arusha ni sawa na yale mapinduzi ya viwanda ambayo yalifanywa na Stalin kule Urusi na hata Mao wa China na ile sera ya Great Leap Forward. Aidha makosa ya wakati wa kubinafsisha viwanda miaka ya 1990-2008 ili kuachana na kuendesha viwanda kutokana na ufanisi mdogo na kuingia hasara hayatarudiwa.

Tumejifunza kuwa tunataka kuwa na viwanda, lakini kilichotushinda hapo awali ni kukosekana utaalamu, motisha, ubunifu na tija katika kuendesha viwanda hivi. Viwanda kama Machine Tools, Mgololo, Ufi, Mwatex na vinginevyo havikustahili kufa.

Makosa ya kuzubaa na kuendelea kuvikamua na kutumia mapato ya viwanda hivi kwa kazi nyingine ambazo hazihusiani na shughuli za uzalishaji mali wa viwanda hivi kama kujijenga kisiasa na vyama vya siasa, ulisababisha kwa kiwango kikubwa kuanguka kwa viwanda vyetu. Makosa ya kubebesha Mashirika na Viwanda mzigo wa Public Welfare, haukuwa mzuri. Ni mfumo huo ambao ulisababisha mapato ya wafanyakazi kudumaa na hivyo kuchochea vitendo vichafu ambavyo viliua moyo wa uchapa kazi, uwajibikaji na uadilifu.

Mpango wa Mchungaji ni kurejesha viwanda vya kusindika mazao ya chakula na biashara, viwanda vya mchecheto (processing) mazao kama katani, pamba, viwanda vya bidhaa za matumizi ya nyumbani na viwanda na yote haya ni katika jitihada za kupunguza uagizaji wa bidhaa za matumizi kutoka nje. Motisha utatolewa kwa viwanda vya zana za kilimo na ujenzi.

Msukumo wa kujijenga kiviwanda utalenga kujenga na kuimarisha viwanda kutokana na rasilimali tulizonazo zikiwa ni pamoja na kilimo na chakula, mifugo, uvuvi, misitu, madini, ngozi, nguo, madawa, mbolea, na kama tutakuwa na uwezo, viwanda vya teknolojia kama vifaa vya umeme.

Kwa kuwa tutakuwa tumeweka nguvu katika nishati, kuwepo kwa umeme wa kutosha kutakuwa ni motisha kukaribisha viwanda vya wawekezaji wa kimataifa ambao hukimbia nchi zao kutokana na gharama kubwa za uzalishaji na kutafuta gharama rahisi za kuzalisha mali. Kukaribisha wawekezaji hawa, hakuna maana kuwa Tanzania itakubali wafanyakazi wake wanyonywe au kudhalilishwa kwa kuwa ni vibarua wa bei poa. Serikali itahakikisha kuwa sheria za kazi za nchi na kimataifa zinafuatwa ikiwa ni pamoja na kanuni za usalama viwandani.

Mashirika kama SIDO na NDC, yatapewa msukumo wa kuchochea ukuaji wa viwanda na taaluma za ndani. Wahitimu kutoka vyuo vya VETA , watapewa miongozo na usimamizi na kusaidiwa shughuli zao kupitia SIDO. NDC itarudishwa kuwa nguvu iliyoleta maendeleo ya viwanda kabla ya zoezi ka kuuza mashirika.

Kama Taifa, tumejijenga kwa kuwa na biashara ndogo ndogo na si biashara kubwa. Tumejenga utamaduni wa kukimbila biashara za bidhaa dhaifu na zisizo na ubora na kutokana na mtazamo duni, tunashindwa kukabili ushindani wa kibiashara kutoka kwa wageni.

Elimu ya biashara, utunzaji mahesabu, bajeti, masoko na matangazo ya biashara, yatasaidia sana kuhakisha sekta hii ya biashara na viwanda inakuwa kwa ushindani na umahiri. Tukiangalia wenzetu Wakenyana hata Rwanda, mipango yao ya maendeleo ni shirikishi katika kuelimisha wafanyabiashara wao mbinu bora za kufanya biashara.

Bodi kama BET na BIT zinabidi ziungane na TCCIA kuwa na mikakati bora ya kuimarisha viwanda na biashara.  Pendekezo moja ambalo litasaidia jamii na wafanyakazi katika nyanja hii na hasa katika Viwanda na Mashirika ya Biashara na Huduma ya umma ni kuanza kuwashirikisha wafanyakazi katika umiliki wa vyombo hivi kwa kutoa hisa za mashirika haya kwa wafanyakazi wake, ili nao wanufaike na mgawanyo wa riba za mapato. Hii itakuwa ni motisha na kichocheo kikubwa cha kujenga Uwajibikaji, Uaminifu, Tija na Utii (loyalty).

Katika kila nyanja ya uzalishaji mali, huduma na kuwa na malengo bora ni kiini cha mafanikio. Waliosema kuwa mteja ni mfalme hawakukosea. Viwanda, Mashirika na Wafanyabiashara wetu wanabidi kujizatiti na kukabili ushindani kwa kuwa na huduma na bidhaa bora, kuwa watangazaji wa bidhaa za ndani ili kuongeza mapato ya ndani.

Wajibu mkuu wa Serikali utakuwa kuchochea na kuhamasisha wafanyabiasha na wenye viwanda vidogo na kuwa (SME) na mipango ya kutoa mikopo na dhamana ya mikopo kama SACCOS kwa wale ambao mipango yao ya kiuzalishaji mali itaridhika kuwa inatekelezeka na inafaida kwa jamii na kuongeza ajira na pato la Taifa.

Maji na Mazingira

Maji ni kitu muhimu katika Uhai wa Taifa. Maji yanahitajika kwa mwili wa binadamu, kurahisisha ukuaji wa mazao, kuendesha viwanda na matumizi mengine ya kawaida na hasa usafi. Kama nilivyosema awali, Tanzania tuna bahati kubwa sana ya kuzungukwa na Maziwa makubwa matatu, maziwa ya wastani wa kati karibu manne, mito mikubwa karibu sita pamoja na mabwawa na bahari.

Mjerumani alipokuja Tanganyika 1885, aliweka mpango wa kilimo “masterplan” ya kulisha Afrika Mashariki na Kati kwa kutumia bonde la Wembere ambalo liko Singida jirani na Tabora. Ikiwa MKoloni aliona rutuba hiyo na kuona vianzio bora vya maji ili kuhakikisha umwagiliaji unatokea, inakuwa je sisi tunashindwa kujitosheleza chakula huku tuna maji na vianzio vya maji tele?

Kwa nini mji kama Dar Es Salaam unaendelea kupanuka na kukua lakini mfumo wa maji ni ule wa Mjerumani na Muingereza? Je viwanda vyetu vinaposhindwa kufanya kazi kutokana na kukosekana maji, hasara ni ya nani? Je wananchi wanapougua magonjwa kama Kipindupindu, linaloumia si Taifa?

Kwa wastani, Mtanzania wa kijijini hutembea si chini ya kilometa mbili kwenda kwenye mto au kisima kuteka maji. Umbali huu kwenda na kurudi utamchukua Mtanzania huyu si chini ya nusu saa kubeba ndoo moja. Sasa kama Mtanzania huyu inambidi aende safari tatu au nne kwa siku mtoni au kisimani kuteka maji, hatuoni kuwa tunaingia gharama za MUDA kwa mwananchi huyu kutumia masaa matatu ambayo angekuwa anafanya kazi nyingine au kujisomea na si kuhangaika kwenda kuteka maji au kukata kuni?

Wizara ya maji na Idara za maji zinapaswa kushirikiana na idara na taasisi nyingine kuhakikisha kuwa ile sera ya kumfikishia Mtanzania maji nyumbani kwake ifikapo mwaka 2025 inatimia.
Mapendekezo yangu ni Serikali kuweka fungu maalum kwa ajili ya mradi wa kusambaza maji, kuondoa au kupunguza kodi na ushuru kwa vifaa na pampu za maji na mashine za kumwagilia, kuhakikisha kuwa kila wilaya inalipa kipaumbele suala la maji kwa matumizi ya watu, maji kwa umwagiliaji na kuendesha viwanda na biashara.

Maji yanaendana na Mazingira. Vitu hivi vinashibana na vina tegemea. Suala la mazingira si kuhusiana na uchafuzi wa mazingira pekee (pollution) bali ni uratibu mzima wa kuhakikisha kuwa Uoto wa asili haupotei na kudumaa kutokana na matumizi mabaya ya ardhi na mazingira.

Dunia yetu sasa hivi inakabiliwa na kubadilika kwa hali ya hewa ambayo imesababisha ukosefu wa mvua, kuongezeka ukame na jangwa, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari, uchafuzi wa mazingira kutokana na mabaki ya kemikali za viwandani na matumizi ya mafuta, kupotea kwa misitu kutokana na biashara ya mbao na kuni, kupotea kwa viumbe hai na wanyama kutokana na kushindwa kuhimili mabadiliko ya mazingira.

Tanzania kwa kuwa bado tupo katika hatua ya kujijenga upya kama Taifa, tuna nafasi kubwa sana kuwa mabingwa wa hifadhi za mazingira kwa kuchochea msukumo kwa Watanzania kulinda mazingira na kudumisha usafi wake.

Mapinduzi ya Kijani yanawezekana sana Tanzania. Tunauwezo kwa kuotesha misitu mikubwa, kupunguza mmomonyoko wa ardhi na udongo, kupunguza takataka ambazo haziozi, kulinda vianzo vya maji, kutumia nishati za upepo na jua ili kupunguza matumizi ya mafuta na kusafisha maeneo ya mito na maziwa ambayo yanapoteza samaki na viumbe wengine kutokana na uchafu.

Tanzania ina bahati sana kuwa uzorotaji wa viwanda vyetu pamoja na kuwa kumelidumaza Taifa, lakini kunalipa Taifa fursa kubwa ya kuwa nchi yenye mazingira safi na mazuri kwa Wananchi wake hivyo kusaidia uimara wa afya, kuongezeka kwa uzalishaji mali na kuendelea kuwa kivuti cha utalii.
Kampeni za kulinda mazingira, kata mti panda mti, zitaendelezwa na kuongezewa fedha za maendeleo. Serikali itoe nafasi maalumu na ufadhili kwa taasisi na watu ambao wanabobea katika mambo ya mazingira na hata ubunifu wa uzalishaji mali kupitia mapinduzi ya kijani.

Wajibu huu wa kulinda na kusafisha mazingira utasukumwa kwa mamlaka za miji na vijiji chini ya uongozi wa Wizara na idara husika za mazingira na TAMISEMI.

Lengo ni kurutubisha nchi, iweze kuendelea kuwa na ardhi nzuri, maji mengi, afya njema na hivyo kukua kiuchumi.

Madini, Misitu na Utalii

Sekta hii, imekimbiwa na Serikali na inasokomezwa kwa wageni huku wazawa wakinyimwa kwa makusudi nafasi ya kuzalisha mali au kuwa wabia wenye hisa katika nyanja hizi tatu.

Tanzania ina vivutio vya utalii vikubwa katika kila mkoa na utalii wetu hauishii Serengeti, Kilimanjaro  na Ngorongoro. Mpango wa maendeleo ya Utalii unaopendekezwa ni wa kuhakikisha kuwa kila mkoa unajitangaza kwa kutumia vitu asilia ambavyo ni vivutio vya utalii.

Mfano hai ni yale majabali yaliopo Singida mjini. Kama Serikali ya mkoa ingekuwa makini, basi ingetengeneza mazingira mazuri kuhakikisha kuwa Uzuri wa majabali hayo unatangazwa kitaifa na kimataifa na kusogeza Watalii kutembelea Singida. Nenga Kitonga, Sekenke, Gombe, Bujora, Ujiji, Tunduma na kwingineko, tuna vivutio vingi vya kuwapa watalii nafasi ya kuona mambo mengine ambayo ni ya kuvutia na hivyo kuongeza pato la Taifa na maeneo yenye vivutio.

Tunajinyima mapato kutokana na uvivu wa kufikiri na uzembe wa kufanya kazi. Sekta ya Utalii ikitumika vizuri na Serikali kuratibu ipaswavyo, inaweza kutupatia si chini ya 25% ya mapato ya Taifa. Kuanzia vinbali  ya kuingia nchini, nauli ndani ya nchi, huduma ndani ya nchi na hata vivutio vya kitalii.

Lakini kabla hatujakimbilia kwa Watalii wa Ulaya na kwingineko, tunapaswa kuhimiza na kuelimisha Utalii kwa Watanzania wenyewe. Watanzania wahamasishwe kutembea na kujua uzuri wa nchi yao. Wengi wetu tunatangaza Serengeti lakini  hata kufika hatujawahi, je tutawezaje kujitangaza na kuuza bidhaa ambayo wenyewe hatuitumii?

Utalii utakuwa marudufu ikiwa tutaweza kuwa na miundombinu bora ya usafiri na huduma muhimu kama umeme, maji na hospitali. Mtalii hatafurahi kuja kutembea halafu akwame kwenye giza pasipo na maji nyikani.

Utajiri wetu wa Madini, tuulinde. Mipango ya Serikali ya awamu za pili mpaka ya nne ambazo zimeruhusu kuingia kiholela kwa mashirika ya kitapeli yakimataifa kujishughulisha na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi si mzuri na utatufilisi kama Taifa.

Wanajiolojia duniani wametamka kuwa Tanzania ina hazina kubwa sana ya dhahabu. Bei ya dhahabu kwenye soko la dunia ni karibu dola elfu moja kwa aunsi.  Mkataba wa Serikali na kampuni ya Barrick unaipa Serikali pato la 3% kwa kila aunsi, hi ni sawa na dola $30! Huku ni kupunjwa na kujidhulumu.

Ukweli ni kuwa tunaruhusu dhahabu yetu itajirishe wengine huku sisi tunaendelea kuchechemea. Hakieleweki kuwa wekezaji huyu wa dhahabu auze aunsi moja kwa $1000.00, Tanzania ipate $30.00 na asamehewe kodi na ushuru kwa miaka 10 kama kivutio cha kuwekeza.

Pendekezo ni kusitisha mikataba yote na kama nilivyotamka awali, mgawo wetu wa madini uongezeke mpaka kufikia asilimia 30% na misamaha yote ya kodi na ushuru ifutwe.

Shirika la STAMICO kushirikiana na mamlaka ya kodi TRA vinabidi viratibu na kusimamia shughuli zote za uchimbaji madini na kuhakikisha kuwa madini hayachimbwi kiholela, kila kinachochimbwa kinahakikiwa, kupimwa na kutozwa ushuru ipaswavyo.

Msukumo utakuwa ni kwa Serikali kupitia NDC kuanzisha viwanda vya kusafisha na kufua udongo wa madini na kuyasafisha, hivyo kuongeza ajira nchini, kuongeza pato la nchi na kutuwezesha kuachana na utegemezi wa   kupeleka udongo nje kutengeneza vinoo vya dhahabu.

Misitu yetu nayo inabidi kuimarishwa. Kwanza wajibu wa kulinda misitu uwe si kuvuna mbao tuu, bali ni kulinda mazingira na kuwezesha mvua.  Biashra ya mbao imeshamiri duniani na tusipokuwa makini na kudhibiti uholela wa biashara hii, tutapoteza fedha nyingi na kuishia kuwa jangwa.

Mpango kabambe wa kupanda  na kukuza misitu mithili ya misitu ya mvua ya Kongo upewe kipaumbele. Kuanzia maeneo ya Kigoma, kusambaa nyanda za Kusini na hata kuelekea tambarare kama Singida na Dodoma, kuna haja ya kuwa na kampeni ya Kitaifa ya kuotesha miti na misitu.

Ajira, Mishahara, Marupurupu na Mapato ya Mtanzania

Kila kazi inahitaji ujira ambao utafidia jasho, nguvu na maarifa yaliyotumika katika kufanya kazi na kuzalisha mali.

Udhaifu wa mfumo wetu wa mishahara na mapato ambao umetokana na dhana potofu za kisiasa na hali halisi ya uchumi wetu, umeliingiza Taifa letu hasara ya kukimbiwa na wataalamu na kundi kubwa la Watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi. Kuanzia Madaktari, Wahandisi, Wanasheria, Wachumi, Wahasibu hata kazi kama za kwenye migodi, ukuli na udereva, Watanzania wanaendelea kuikimba nchi yao kutokana na ugumu wa maisha unaotokana na uhaba wa kazi, mishahara midogona masumbufu mengine mengi.

Hata vijijini ambako ndiko asilimia 80% ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo, ukimbizi na kuhamia mijini kunaongezeka kila siku kutokana na bei ndogo za mazao na kuendelea kukomaa kwa umasikini bila dalili za tumaini la neema.

Wimbi hili la wahamiaji wakimbizi linaweza kusitishwa kwa kuwa na mipango bora ya kuhamasisha ajira na malipo mazuri kwa kazi za viwandani,maofisini, mogodini na hata mashambani.

Uongozi na utawala mbovu unachangia sana katika hali hii ambayo Watanzania wanaogopa kufanya kazi kwa nguvu zao katika nchi zao kwa kuona kuwa wataendelea kunyonywa na mtetezi wao Serikali imekaa mguu pande na kuruhusu unyonyaji na dhuluma ziendele kumpunja Mtanzania ajira na kipato.

Badala ya kutafuta mbinu mpya za kuchochea uzalishaji mali kuongeza mapato na kuhakikisha kuwa kima cha chini cha mapato na umasikini wa kutupa kinaongezwa kuwiana na thamani ya sarafu yetu, Serikali imeruhusu mianya mibovu ya kuongeza vipato kwa wafanyakazi wa mashirika na Serikali na hivyo kuchochea rushwa, ubadhirifu, uhujumu na ufisadi.

Hali yetu ya kutumia mapato ya mashirika na Serikali kutoa huduma za bure kwa wafanyakazi wake kama chakula, nyumba, afya na usafiri, ilisababisha mashirika mengi kufa kwa kuwa na matumizi ya kawaida na si kutumia mapato kuongeza ufanisi au ubora wa bidhaa na huduma ili kuhimili ushindani na hivyo kuongeza mishahara ya wafanyakazi.

Hali hii ya uvumilivu wa mishahara midogo huku tukifurahia masurufu na marupurupu, ndiko kulikozaa matumizi mabaya ya mapato, matumizi yasiyo na stakabadhi na wafanyakazi wengi kukosa tija na motisha wa kufanya kazi na kuishia kutafuta njia fupi na miradi ili kujipatia kipato cha ziada.

Lililo baya zaidi ni ule uamuzi wa Chama tawala CCM kuvunja Azimio la Arusha na miiko ya maadili ambayo ilidhibiti viongozi kutumia madaraka yao na kudhulumu ili kujipatia mapato ya ziada.

Kila Mtanzania anajaribu kuwa mjanja ili apate fedha za ziada kukimu ukali wa maisha. Umasikini na Unyonge wa wafanyakazi mijini umefikia hatua ya wafanyakazi hawa wawe wa mashirika ya umma, binafsi au Serikali kupoteza muda mwingi wa kufanya kazi kwa kuweka nguvu zao katika miradi binafsi na hivyo kupunguza ufanisi katika kazi zao za kuajiriwa.

Suluhisho ni kuleta mfumo mpya wa sheria na malipo ya kazi ambayo yatahakikisha kuna uwiano wa mapato ya mwajiri na waajiriwa.

Serikali itabidi ipandishe kima chake cha chini cha mishahara na kuweka utaratibu wa kuongezamishahara ya wafanyakazi kila mwaka kutokana na ufanisi na kwa kutumia vigezo vya kitaalamu vya asilimia.

Mfano Marekani, waajiri wengi pamoja na Serikali wana madaraja matano ya ufanisi. Daraja la 5 ikiwa ni ufanisi wa hali ya juu, na daraja la kwanza ikiwa ni ufanisi wa hali ya chini usioridhisha. Waajiri wengi huongoza mashirika na taasisi ikiwa ni pamoja na Serikali kwa kulenga kuwa na daraja la tatu (au kwa lugha ya kishule Tanzania “pata japo karai-C”) na hilo hutumika kuwa kigezo cha chini cha ufanisi. Kupitia madaraja haya, kuongezeka kwa mshahara wa mfanyakazi wa Marekani kila mwaka unatokana na ufanisi wake, mpaka pale mfanyakazi huyu atakapoamua kutafuta kazi yenye mshahara mkubwa wa kuanzia na kuendelea kuongezewa mshahara kutokana na ufanisi.

Serikali ya Marekani imeweka kima cha chini cha ujira na mapato ya umasikini (poverty line) hivyo kila mwajiri huweka ngazi za mishahara kwa kuangalia viwango vya mishahara kutokana na kazi katika soko (kufananisha na waajiri wengine), kupima uzoefu na ujuzi ambao mwajiriwa anauleta kama kigezo kingine cha kudai mshahara wa kuanzia kazi.

Sisi tunaweza kuwa na mfumo kama huo na kwa kiasi kikubwa utasaidia kuongeza ufanisi na kuchochea tija.

Kwa Serikali kuu, ni vyema kuwa na zile ngazi za kiserikali bila kujali cheo. Mfano ukuu wa wilaya unaweza kuwa na daraja GS 1 hadi 5, yule wa 5 akiwa ni mkuu wa wilaya mwenye ujuzi wa kutosha, hivyo mishahara yao pamoja na kuwa ni ya daraja, pia itaongezeka kutokana na ufanisi, kiwango cha elimu na ujuzi wa kazi.

Tumetangazia dunia tumeingia mfumo wa soko huria, basi vitendo vyetu viendane na soko huria na si kuacha kundi kubwa la Wafanyakazi na Wakulima wakihangaika kimapato kwa mfumo wa zamani wa kijamaa ambao ulihakikisha kuwa mapato yanadhibitiwa ili kutimiza ile kauli ya binadamu wote ni sawa.

Kuhusu ajira, niliongelea umuhimu wa kuthamini kila kazi halali ambayo huingiza kipato halali ina umuhimu katika jamii yetu.

Tumejenga kasumba ya kuona kuwa kazi za “maana” ni zile za kuajiriwa, za kisomi, mashirikani na viwandani na kazi za kujiajiri nazo ni lazima ziwe za hadhi ya kisomisomi. Hiyo ni dhana zubafu na inadumaza kukua kwa Taifa letu.

Kwenye kipengele cha elimu nilizungumzia vyuo vya michezo, muziki na sanaa kama vyuo vya ziada kuongeza wigo wa ajira. Nchi za wenzetu zilizoendelea, michezo, sanaa za maigizo, utamaduni na hata muziki ni vitengo vikubwa vinavyotoa ajira zenye kulipa ujira mkubwa kuliko hata wa waajiriwa wa ofisini. Haya yamefanikiwa kutokana na fanii hizi kuendeshwa kibiashara na si viburudisho pekee.

Wastani wa malipo na mapato wa wacheza mpira wa miguu kwa timu za daraja la kwanza kwa nchi za Uingereza, Ufaransa, Ureno, Italia, Ujerumani, Hispania, Uholanzi na nchi nyingine za bara la Ulaya si chini ya dola milioni 500 kwa mwaka. Kwa nchi kama Marekani, mapato na thamani ya timu zote za mpira wa kulipwa wa magongo, mpira wa vikapu, American Football na Baseball  ni kubwa kuliko mapato na bajeti ya nchi yetu ya mwaka huu 2008.

Tunauwezo wa kutoa ajira kupitia utamaduni, sanaa na michezo ikiwa tutabadilisha mtazamo wetu wa kazi hizo na kuziendesha kibiashara.

Mtanzania akilipwa ujira bora na hata kuhakikishwa ajira, atafanya kazi kwa ufanisi wa hali yajuu.

Maendeleo ya Mijini na Vijijini

Pamoja na kuwa na mikakati mikubwa nilihyoitaja hapo juu, bado kuna umuhimu wa kuweka nguvu za maendeleo ya miji na vijiji katika moja ya mipango madhunuti ya kuimarisha Uchumi na Uongozi. Bila kuwa na uwiano na msukumo wa kutosha wa maendeleo ya miji  na vijiji, Tanzania itaendelea kuwa na viraka vya maendeleo na hata ile nia ya kupeleka maendeleo kila kona itaonekana kama kazi bure.

Jukumu hili la maendeleo ya miji na vijiji litawekwa chini ya Wizara ya TAMISEMI, likishirikisha sekta zote za umma za afya, elimu, kazi, nishati, uchukuzi na miundo mbinu, kukaribisha watu binafsi na taasisi ili Tanzania nzima ipate nafasi sawa ya kuwa na maendeleo na kuchangia katika gurudumu la maendeleo.

Maji safi vijijini ,barabara za lami kuunganisha wilaya, reli kuzunguka kila mkoa si kazi ya Serikali kuu, inahitaji ushiriki wa wananchi wote na mamlaka zao za mikoa na hata wilaya.

Vijiji vya ujamaa vilijengwa kwa nia ya kufikisha maendeleo kwa Watanzania wengi kwa kukaa katika sehemu moja. Sera hii ilikuwa na walakini wa kukosa mipango madhubuti, fedha za kutosha na huduma muhimu kama ilivyodhamiriwa. Lakini hakuna kilichoharibika sana zaidi ya kuendeleza mipango hiyo kwa kupima tulikotoka, uwezo wetu na tunakokwenda.

Nimezungumzia awali ulazima wa kuwepo kwa shule na hospitali kila wilaya, haya yatafanikiwa kwa kupata msukumo kutoka Serikali kuu, TAMISEMI, sekta binafsi na wananchi wenyewe ikiwa ni sehemu ya maendeleo ya miji na vijiji.

Katika mchakato huu wa  mipango miji, masuala ya ardhi, barabara na mitaa, maji, umeme, simu, ukusanyaji taka, kupendezesha miji, mgawanyo wa maeneo viwanda, ofisi, makazi, shule, hospitali, sehemu za ibada, bustani za kupumzikana sehemu za starehe yatakuwa ni sehemu ya maendeleo ya miji na vijiji.

Serikali kuu itahakikisha kuwa kila sheria na taratibu zinafuatwa na itaratibu shughuli zote ikiwa mamlaka za miji, vijiji na TAMISEMI zitashindwa kuwa makini kuleta maendeleo haya.

Hitimisho

Lengo kuu la ujumbe huu ni kutoa hamasa na mwamsho kwa mwananchi ajue wajibu wake na kutambua kuwa maendeleo ya kweli kwake binafsi, jamii na Taifa lake yanawezekana na uwezo wa kufanisha maendeleo hayo upo na utaanzia na yeye Mwananchi kuamua kasi ya maendeleo yake kwa kuwapima viongozi na kuchagua viongozi ambao watarahisisha upatikanaji wa maendeleo haya. Lengo la pili ni kuhakikisha katika kurekebisha mfumo wetu wa uchumi, Serikali inajenga msingi na kuruhusu na kuachia sekta binafsi na ushirika kuendeleza shughuli za kila siku.

Hatuwezi kusema Serikali isiwe na dhamana ya kwanza ya kujenga misingi bora ambayo itatoa mwanya na kuruhusu sekta binafsi na jamii kuchukua kijiti (baton on relay) baada ya msingi na uratibu kujengwa.

Kwa kuwa mpango huu ni wa kufufua uchumi na kulijenga upya Taifa, nafasi ya kwanza katika mpango huu inakwenda kwa Serikali na si kusukumizwa kwa watu binafsi au wananchi. Hii si adhabu kwa Serikali bali ni wajibu wa Serikali yeyote kuhakikisha kuwa inajenga msingi madhubuti kwa shughuli zote za uchumi na maendeleo ya wananchi na kisha kuratibu shughuli hizo huku watu na sekta binafsi, taasisi zisizo za kibiashara-NGO, wawekezaji na vyama vya ushirika vikiendeleza na kupokea wajibu wa kufanya shughuli hizo kwa kila siku.

Hakuna ambalo haliwezekani kama tutaweka akili, mawazo na mioyo yetu na kuiongeza nguvu tutafanikiwa. Lakini kama tutaendela kuwa na aina ya Uongozi tulioshuhudia katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, ni dhati kuwa hatutaweza kupiga hatua hata moja na kuwa Taifa lenye maendeleo na kuondoka katika dhihaka na unyonge wa kuitwa nchi masikini.

Tija, ufanisi, umahiri ni wetu kama watu binafsi, lakini panapokuwa na uongozi mbovu, hali hii huwa ni kizingiti cha kuchochea maendeleo.

Narudia tena, ni wajibu wetu, kila mmoja kuleta maendeleo na tutaanza kwa kujihoji nafsi, kupima na kutathmini viongozi wetu na kuwa wakweli kwa kukataa kuburuzwa kwa ahadi hewa au kudhalilishwa Umasikini na Unyonge wetu kwa Chakula, Pombe na Nguo kila wakati wa uchaguzi unapofika.

Jiamini wewe ni bora na unastahili vilivyobora.

Mungu ibariki Tanzania na Watu wake,

Wako,

Rev. Kishoka

12 Comments
  • nimekusoma mada yako ni ya kisayansi sana. na ninkubaliana nawe kwamba ccm inahitaji upasuaji mkubwa na si kuvua magamba badala yake wavue mioyo yao ya ubinafsi na kuvaa mipya ya kuwajua watu na shidas zao

  • Mbuga umechangia vizuri. Namsikitikia sana Kijana mdogo kam Nape, ambye aliwahi kuonekana ni mhimu sana. lakini mara baada ya kupewa ukuu wa wilaya, alifyata mkia. sasa amepewa sehemu ya kupika jungu na kulipua. Kwa maoni yangu anatumiwa vibaya na mfumo dhalimu, bora ajiengue aanze harakati za kuwatetea watanzania. aache kabisa majungu yake na kuwatumikia mabwanyenye wa nchi hii.

    • SAMAHANI KWA MAWAZO YANGU TOFAUTI LAKINI EBU NISAIDE TOFAUTI YA CCM NA CDM WOTE HAWA HAWANA NIA NJEMA NA TAIFA

  • sikubaliani na mchungaji kwamba mbowe ajihudhuru uenyekiti. Kwani sasa Mbowe anaouwezo wa kushawishi wanachama.

  • WEWE MCHUNGAJI KWA NINI USIANZISHE CHAMA CHAKO UKAJA NA HIZO SERA KULIKO KUPENDEKEZA WENZAKO WAFANYE A, B, Cs?

    UKIPITIA KWA UMAKINI HUO WARARA UNA CHEMBECHEMBE ZINAZOONESHA MWISHO NI KUCHOCHEA VURUGU KWA KUTAKA WATU NDANI YA CHAMA WAANZE KUFARAKANA KUPIGANIA NAFASI MPYA.

    NIONAVYO CHADEMA WAKIJARIBU KUFUATA HUO WARAKA, YATAWAPATA YALIYOWAPATA NCCR -1996-2000 ILI KUVUNJA MSHIKAMANO HATIMAE KUSAMBARATISHA CHAMA.

    ACHA CHADEMA KIFUATE MIPANGO YAKE. HAYO NI MAMBO YA NDANI YA CHAMA NA KINA WATAALAM.

    kAMA UNAFIKIRI HAKIKO SAWA, ANZISHA CHA KWAKO USHINDANE NACHO. LAKINI PIA JIKITE KATIKA MAMBO YA KIROHO ZAIDI ACHANA NA SIASA

  • Ni kweli kabisa Victor anachotakiwa kufanya huyu mchungaji mwenzentu ni kuitafuta amani zaidi na kwa watu wote na mambo ya kaisari amwachie kaisari yeye afanye mambo ya mungu zaidi. NEEMA YA BWANA WETU YESU KRISTO ITAWALE KWA WATANZANIA WOTE, AMEN.

  • hayo ni mawazo ya mchungajiiiiiiiiiiii anataka kuchochea vurugu badala ya amani

  • Walaka wako Mchungaji ni mzuri sana, lakini mimi kwa maoni yangu naona ingekuwa vema sana ukiwa kama mtumishi wa Mungu kuuzungumzia muskabari wa nchi yetu kwa ujumla pasipo na kulkilenga chama chochote cha kisiasa.

  • Bishop Pius Erasto Ikongo

    Mtu yeyote mwenye mapenzi mema na Nchi yetu hawezi kumpongeza Lusekelo anaejiita mzee wa upako. Kwani tarehe 20/2/2013 saa tatu alitoa matamko ambayo Mkristo wa kweli hawezi kutamka mambo kama hayo. Katika kipindi hicho cha Tarehe 20/2/2013 Saa tatu usiku na Chanel Ten alitukashifu sana sisi Viongozi wa Dini za Kikristo Tanzania pamoja na Waziri Mkuu.
    Matamshi yaliyotolewa na Anton Lusekelo anayejiita mzee wa upako siyo matamshi mazuri kama kweli tunataka kupunguza vurungu za Kidini hapa kwetu TZ kama sio kumaliza kabisa. Kupitia kipindi hicho Lusekelo alisema kwa msisitizo ya kwamba, Wachungaji waliokutana na Waziri Mkuu katika kikao cha Mchungaji aliyeuwawa huko Geita walienda kujipendekeza tu, ili kupiga picha na Waziri Mkuu.

    Matamko hayo ni kashfa kubwa sana kwetu sisi Viongozi wa Dini za Kikristo pamoja na Waziri wetu Mkuu. Sisi tulifahamu Waziri Mkuu ameacha majukumu yake mazito na ya Kiserekali kwenda kuwafariji Waumini pamoja na Viongozi wa Dini Waliokutanika pale, kwa uchungu wa kuuwawa Mtumishi wa Mungu, ambaye pia kwa Waziri Mkuu ni Mwananchi wake. Aidha Waziri Mkuu alikuwa katika jitihada za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo. Tunamshangaa sana Lusekelo hakuongea chochote kuhusu uovu wa mauaji hayo kwani inaonekana kwake yeye mauaji hayo si kitu.

    Jambo la pili: Lusekelo alisema, Maaskofu, Wachungaji, pamoja na Wakristo wote wanaozungumzia suala la Uchinjaji wa Wanyama Tanzania ni Wapumbavu,Wajinga na Wapuuzi.

    Hayo kwetu sisi tukiwa Watumishi wa Mungu, ni kashfa kubwa sana, na inatupa picha ya kwamba huyo Lusekelo AMETUMWA KUTUTUKANA SISI.

    Hivyo tunamshangaa sana mtu wa Mungu kuwatukana watumishi wenzake. hata hivyo bado tunatafakari ni kwa jinsigani chombo cha habari kama Chanel Ten, wanaojua maadili ya vyombo vya habari kiruhusu mtu kama Lusekelo kutoa kashfa mbaya hivyo. Pia kwa kawaida mtu mwenye maadili mazuri jambo ambalo tayari Waziri mkuu amekwisha kulitolea tamko hawezi kulizungumzia katika vyombo vya habari. Naomba Uongozi wa Chanel Ten mfungeni gavana huyo mtu asiye na maadili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *