“Wasiojulikana” washindwa kumfikia Lissu hospitalini

Jamii Africa

Wale wanaotajwa mara kwa mara kuwa ni “watu wasiojulikana” walikwama kumfikia na kumuua Tundu Lissu, akiwa amelazwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Taarifa za uhakika kutoka Nairobi zinaeleza kuwa vyombo vya usalama na walinzi waliokuwapo katika hospitali hiyo, walibaini mapema baadhi ya watu waliokuwa na kile kinachoitwa “nia mbaya kwa Lissu” na kuwadhibiti.

Habari hizi zimepatikana mwezi mmoja baada ya Lissu kuruhusiwa kutoka katika hospitali hiyo alimokuwa amelazwa kwa miezi minne akipatiwa matibabu, baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi mjini Dodoma, Tanzania alikokuwa akiendelea na vikao vya Bunge la Jamhuri.

Lissu alilazwa kuanzia Septemba 7, mwaka jana na aliruhusiwa kutoka Januari 6, mwaka huu. Hivi sasa mbunge huyo wa Singida Mashariki (CHADEMA) anaendelea na matibabu jijini Brussels, Ubelgiji.

Ally Hemed, mmoja wa viongozi wa CHADEMA waliokuwa wakimuuguza Lissu kwa miezi hiyo, ameithibitishia FikraPevu na kueleza kwamba majaribio hayo “yalizimwa” mapema.

“Napenda kukuhakikishia kuwa hapa kulikuwa na vita, hatukulala, maaskari hawakulala ili kuhakikisha usalama wa Lissu. Tulikuwa tunapata taarifa za kiintelijensia na kujipanga ili kuzuia lolote baya kutokea kwa Lissu akiwa hapa hospitali.

“Tulikuwa na uhakika kuwa waliopanga kumuua Lissu hawakufurahia uzima wake hapa hospitali, hivyo walikuwa tayari kummaliza ili kutimiza lengo lao kuu; kuua,” amesema Hemed.

Hemed ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Uenezi wa CHADEMA, alisema pamoja na kuhangaikia tiba na kupona kwake, nguvu nyingine ziliwekwa kuhakikisha usalama wake unakuwa imara.

“Hatukupata muda wa kupumzika, kila mara watu wa usalama walikuwa pamoja na sisi kuona hakuna upenyo wowote unapatikana kwa watesi wa Lissu kuja kummaliza,” amesisitiza Hemed.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alipokuwa katika hospitali ya Nairobi akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi mjini Dodoma, Tanzania

 

Lissu anena

Alipoulizwa kuhusu usalama wake alipokuwa hospitali ya Nairobi, Lissu alisema hakuwa na wasiwasi sana kwa kuwa aliamini vipo vyombo vya usalama na watu waliokuwa wamejitoa kuhakikisha anakuwa salama.

“Sikuwa na shaka na timu ya walinzi na wanausalama waliowekwa kunilinda, tishio lazima lingekuwepo, kwamba wabaya wangu waliotaka kuniua wasingependa kuona naishi, hivyo lazima wangejaribu kuja kunimaliza nikiwa Nairobi.

“Lakini niko huku natibiwa, naamini kazi kubwa ilifanyika kwa hawa wanausalama wangu, kwa kweli nawashukuru sana.

“Nilisikia na kuelezwa kwamba kulikuwepo na mambo kadhaa ya hovyo yaliyokuwa yakipangwa dhidi yangu, lakini Mungu ni mwema watesi wangu wameshindwa,” alisema Lissu.

Lissu alisema mauaji yaliyokuwa yakipangwa kwake yamejaa dhana ya kisiasa, jambo ambalo anaamini lisipopigiwa kelele sasa, litasambaa na kuwa jadi ili kuwatisha wale wenye mitazamo tofauti dhidi ya utendaji wa serikali na viongozi wake.

 

Mlinzi mkuu azungumza

Aliyetambulishwa kwa FikraPevu kuwa ni kiongozi wa kikosi cha ulinzi wa Lissu, (jina lake halitajwi kwasababu maalumu) alisema anashangaa kuona Tanzania aliyoiacha Mwalimu Julius Nyerere inatoweka kwa kasi.

Kiongozi huyo alisema hakuwahi kusikia Tanzania inakuwa na kile alichookiita “vita ya siasa” kama Kenya, lakini jaribio la kuuwawa kwa Lissu limemshtua na kuwashangaza Wakenya wengi.

“Sisi Kenya tuna vita kubwa ya kisiasa, lakini hatupigani marisasi (risasi), tunapingana tu na maisha ya wanasiasa na wafuasi wao yanasonga mbele, nyie mmeingiwa na mdudu gani watizedi (Watanzania),” alilalamika.

Alisema baadhi ya watu waliokuwa na nia mbaya na Lissu walidhibitiwa hata kabla ya kufika hospitali, wengine wakibainishwa kutoka mipaka waliyopitia.

“Hatukuwa na mchezo na uhai wa huyu mtu, tulijipanga vilivyo, kulikuwa na maelekezo kutoka juu hivyo tuliweka mzizi mkubwa kumlinda mheshimiwa wenu,” ameongeza.

         Tundu Lissu akifanya mazoezi katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya kabla ya kusafirishwa kwenda Ubelgiji kwa matibabu zaidi

Hemed alisema hakuna watu waliokamatwa kwa jaribio la kumdhuru Lissu alipokuwa amelazwa, ingawa wapo waliohisiwa na kuzuiwa nje ya malango ya hospitali hiyo iliyozidisha ulinzi baada ya kufika kwa Lissu Septemba 7, mwaka jana akitokea Dodoma, Tanzania.

Taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya askari waliokuwa wakimlinda Lissu walikuwa wametoka kwenye vitengo maalumu, ingawa haikuwekwa wazi ni kutoka Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa wa Kenya au Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo.

Lissu akiwa ndani ya gari lake, nyumba kwake Dodoma, ‘alimiminiwa’ risasi 38, huku 16 zikimuingia mwilini mwake; miguuni, mikononi na tumboni.

Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa risasi nane ziliingia kwenye mifupa na nyama za mwili wake, huku nane zingine zikifanikiwa kutokea upande wa pili kutoka eneo aliloshambuliwa, hasa miguuni na mikononi.

Risasi nane zingine zilibaki katika mwili wake na zilichanachana nyama za mwili na mifupa yake kuvunjwavunjwa; mguu wa kulia na mikononi ndiyo iliathirika zaidi.

Madaktari wa Hospitali ya Dodoma alikopokelewa na kufanyiwa matibabu ya awali, walifanikiwa kutoa risasi tatu, huku zingine nne zilitolewa Hospitali ya Nairobi.

Hata hivyo, risasi moja bado iko mwilini; kwenye nyama eneo karibu na mfupa wa uti wa mgongo. Madaktari wa Nairobi walieleza kuwa risasi hiyo haina madhara makubwa, “ikikaa kuliko kuitoa kwa sasa (wakati huo).”

Lissu katika hospitali zote; Dodoma na Nairobi alifanyiwa upasuaji mara 17, kati ya hizo nne akifanyiwa tumboni.

 

Ulinzi kumuona Lissu

Hospitali ya Nairobi iliyoko Mtaa wa Argwings Kodhek, jijini Nairobi, Kenya ina ulinzi kuanzia geti kuu na mageti mengine madogo.

Hata hivyo, kuwasili kwa Lissu kuliongezwa ulinzi na ukaguzi kwa kila mgeni na mgonjwa aliyepelekwa ndani ya hospitali hiyo.

Inaelezwa kuwa ulinzi uliowekwa wakati wa matibabu ya Lissu ulisimamiwa na idara kadhaa za usalama za Kenya. Kulikuwa na walinzi wasiopungua wanne katika geti dogo kabla ya kumuona Lissu, huku kamera za usalama zikiwekwa kila mahali.

Wageni wote wanaoingia ndani ya hospitali hiyo hukaguliwa kwa mashine na baadaye mikono. Kwa wale waliokuwa wakienda kumuona Lissu ilibidi kupitia hatua kadhaa za ulinzi na ukaguzi kabla ya kuruhusiwa kumuona.

Baada ya kupita geti kuu, wageni wa Lissu walitakiwa kufanyiwa ukaguzi mwingine “wa kawaida” – kwenye geti dogo na  kutakiwa kuacha simu zao hapo, kabla ya kutambuliwa na wasaidizi wengine wa Lissu waliotoka Tanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *