Ongezeko la makundi ya vijana wasomi wasio na ajira za uhakika, kunaweza kuwa chanzo cha migogoro na vurugu zinazopelekea uvunjifu wa amani.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha Polisi Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Alice Mapunda, wakati akitoa mada ya namna ya kuthibiti migogoro katika mkutano wa Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi unaofanyika Chuo Cha Taaluma za Polisi (Moshi Police Academy) mjini Moshi.
Kamanda Mapunda ameainisha baadhi ya migogoro ambayo inaweza kuwa chanzo cha vurugu kuwa ni ugomvi kwa wakulima na wafugaji unaosababishwa na ufinyu wa ardhi yenye rutuba utokanao na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Aidha ameitaja sababu nyingine kubwa zinazoweza kuleta migogoro ni pamoja na kuongezeka la tofauti za watu wenyenacho ikilinganishwa na wale wasionacho.
Kamanda Mapunda amesema migogoro hiyo ikiachiwa iendelee bila ya kupatiwa ufumbuzi inaweza kuleta vurugu na madhara makubwa ikiwemo kutishia usalama wa taifa letu kwa ujumla.
Alisema ili kuepuka migogoro hiyo kuendelea, ipo haja kwa Serikali kuchukua hatua za makusudi za kutathimini na kuchambua viini halisi vya migogoro hiyo na kutafuta njia sahihi ambazo zitakuwa suluhisho la kudumu.
Alisema ni muhimu taifa likajifunza kutokana na migogoro na vurugu zilizokwishatokea siku za nyuma kama vile, mapigano ya koo kwa koo, mapigono ya wakulima na wafugaji, mapigano ya kati ya dini na dini pamoja na vurugu za kisiasa.
Naye Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa mpango wa Polisi Kata / Shehia uliobuniwa na Jeshi la Polisi hapa nchini, utaweza kusaidia kupunguza matukio ya kihalifu yakiwemo makosa ya usalama barabarani.
CP Mussa amesema Askari Kata na wale wa Shehia, wanaweza kuwa msaada mkubwa kwa askari wa vikosi vingine kutokana na kuchanganyika kwao na makundi ya jamii katika maeneo husika.
Kamishna Mussa amesema kuwa mpango huo umeleta mafanikio makubwa kwa upande wa Tanzania-Zanzibar katika visiwa vya Unguja na Pemba ambapo amesema kuwa hivi sasa makosa yanayotokea katika maeneo hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kipindi kabla ya kuanzishwa ambacho mpango huo wa Polisi Jamii.
Amesema kuwa askari hao wanaweza pia kutumika katika mkakati wa Usalama wetu Kwanza unaotoa fursa kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari kujifunza namna ya kuzuia uhalifu kwa kushirikiana na Polisi.
Alito mfano wa kazi za Askari hao wa Kata/Shehia ni pamoja na kuwavusha watoto na wazee wasiojiweza katika vivuko vya barabara ili kuwanusuru na majanga ya ajali za magari na vyombo vingine vinavyotumia barabara.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchni Inspeka Jenerali Saidi Mwema, amewaagiza Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi, kuhakikisha kuwa wanadumisha ushirikiano na kuwatumia wananchi katika kupata taarifa za wahalifu pamoja na nyendo zao.
Akichangia mada ya Ulinzi Shirikishi iliyotolewa na Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, kwenye Mkutano wa Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi unaoendelea katika Chuo cha Taaluma za Polisi mjini Moshi, IGP Mwema amesema kuwa pamoja na ufinyu wa bajeti unaozikumba idara mbalimbali za Serikali, lakini ipo haja kwa Makamanda kuwaona wananchi kama wadau muhimu kwao.
Naye Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaa Kamishna Msaidizi wa Polisi Ahamed Msangi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kamishna Robert Manumba, wamehimiza kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya Wapelelezi na Waendesha mashitaka wa Serikali na kongeza misako hadi maeneo ya vijijini ili kuutokomeza uhalifu nchini.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Timu ya Mfumo Shirikishi wa Ulinzi na Usalama ngazi ya Kata na Shehia, Bw. Abou Maddy, amesema mkakati wa Polisi Jamii utawezesha upatikanaji wa ajira kwa vijana waliopo kwenye mazingira magumu.
Amesema vijana hao wanaweza wakatumika katika masuala ua ulinzi katika maeneo wanayoishi na kupata posho itokanayo na michango ya wananchi wa eneo katika kushiriki Mpango wa Ulinzi Shirikishi.
Habari hii ni kwa mujibu wa Mohammed Mhina na Athumani Mtasha, wa Jeshi la Polisi – Moshi.