MASHIRIKIA ya kutetea uhai, PROLIFE- Tanzania na Human Life International (HLI) Tanzania, yanaendesha kampeni kupinga muswada ulioandaliwa na Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuhusu afya ya uzazi na masuala ya kijinsia uitwao "The East African Community Sexual and Reproductive Health Rights Bill, 2017" yakisema ni hatari.
Yanamwomba Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli na viongozi wa dini, kuuchunguza kwa makini na kuukataa hata kama utapitishwa na EALA.
Mkurugenzi wa HLI katika Nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza, Ukanda wa Mashariki na Kusini, Emil Hagamu, ameiambia FikraPevu, “Kuna uwezekano muswada umeandaliwa na kupenyezwa katika nchi husika bila viongozi wakubwa wakiwamo marais na mawaziri husika, kuujua vizuri…”
Wadau wameiambia FikraPevu kuwa muswada huo ukipitishwa EALA na Tanzania kuukubali, nchi itaanzisha mchakato wa kuingiza kwenye sheria zake, vipengele vinavyoruhusu haki ya afya ya uzazi wa mpango vilivyomo kwenye Mkataba wa Nyongeza wa Afrika (Maputo Protocol).
Kampeni hii imekuja baada ya FikraPevu kuripoti kuwa, wanaharakati kikiwamo Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) kupitia mkurugenzi wake, Tike Mwambipile, wanataka uibuke mjadala mpana kitaifa kuhusu kuingiza katika sheria za Tanzania, vipengele kadhaa vya Maputo Protocol, kuhusu haki za wanawake, ikiwamo kuruhusu utoaji mimba katika mazingira yatakayoainishwa kisheria.
Wanadai hali hiyo itapunguza madhara, mateso na vifo vya wanawake wanaofanya utoaji mimba usio salama vichochoroni ili kukwepa sheria za nchi zinazokataza abosheni.
Msimamo wa Tanzania
Mratibu wa mikoa na kanda wa huduma za afya ya uzazi na mtoto kitaifa katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Martha Shekinyau anasisitiza, “mwongozo wa serikali unataka mwanamke ambaye mimba imeharibika, ahudumiwe katika mazingira salama, penye mtaalamu, dawa na vifaa safi, sahihi na vya kutosha kwa kuangalia usalama wake.”
Vifaa mbalimbali vinavyotumika kutolea mimba.
Machi 24- 25, mwaka huu, HLI katika Ukanda wa Mashariki na Kusini ilikutana kwa dharura Dar es Salaam kujadili pendekezo la wanaharakati kuhusu kuhalalisha utoaji mimba pamoja na muswada huo na kutoa maazimio waliyosema yanahitaji kutekelezwa haraka.
Chini ya uenyekiti wa Hagamu, mkutano uliazimia kuwasiliana haraka na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu kuomba ushiriki wao, kuwashawishi wabunge wa Tanzania katika EALA kuupinga muswada, kukutana na viongozi wakuu wa EALA na kutumia vyombo vya habari kuelimisha umma madhara ya Muswada huo.
Ibara ya 14 (2c) ya Maputo Protocol kuhusu “afya ya jinsia na haki ya kizazi” inazitaka nchi zinazosaini ikiwamo Tanzania, kulinda haki ya kizazi kwa wanawake kwa kuruhusu utoaji mimba kitabibu, mimba inapotokana na kubakwa, kushiriki ngono na ndugu au mimba inapohatarisha afya na uhai wa mama.
Mkurugenzi wa HLI nchini Uganda, Padri Jonathan Opio akasema nje ya mkutano, “muswada huu utavuruga sheria za nchi wanachama. EALA haina uhalali wa kutunga sheria ili nchi zitekeleze wala kutunga sheria zinazovunja sheria za nchi.”
Mwanasheria anena
Mwanasheria Deodatus Balile, anaiambia FikraPevu kuwa hata kama EALA itapitisha muswada huo kuwa sheria, haiwezi kutumika hadi nchi iliridhie na kurekebisha sheria ili ziendane nayo.
“Nchi hailazimishwi kuridhia, inaweza kukataa au ikarekebisha vipengele kuendana na utamaduni wake,” anasema.
FikraPevu inaamini kuwa muswada huo wa Januari 20, 2017 ukiwa sheria, utapanua na kuchochea matumizi ya vidhibiti mimba kwa watu wakiwamo watoto wa shule na kuhalalisha utoaji mimba.
Kupitia Ibara ya 6, muswada utaondoa sheria zinazolinda maudhui ya picha na habari kwa watoto kwani utaruhusu maudhui kadhaa ya ngono.
Elimu ya ngono na ujinsia inayosisitizwa katika muswada ni kinyume cha Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (Sospa) ya Mwaka 1998 na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 zinazozuia ngono kwa watoto. Yaliyomo katika uswada yanawaingiza watoto katika mimba za utotoni nma utoaji mimba.
Mwalimu Ediltruda Muhozya, Mkufunzi wa Uimarishaji Familia Tanzania (Ufata) anaupinga muswada akisema, “wanandoa wengi wanaotumia njia hizo wanalalamika kuathirika maumbile kutokana na utendaji kazi wa homoni bandia zilizotengeneza vidhibiti mimba, maana zinaufanya mfumo halisi wa uzazi wa mwanamke kuwa bandia.
Wanawake wanaathirika kisaikolojia, kimwili na kijamii. Hivi, mwanafunzi hana ndoa, anapewa elimu hiyo ili iweje?”
Sehemu ya baruapepe ya HLI – Tanzania kwa wabunge wa EALA kutoka Tanzania ambayo FikraPevu imeiona inasema, muswada huo una mambo kadhaa yanayotia shaka.
“Mosi, ni hoja kwamba wananchi wa Afrika Mashariki wanahitaji kutungiwa sheria ya kuua watoto wao kabla hawajazaliwa (kutoa mimba);
Pili, muswada unataja kutungwa sheria ya kuruhusu watoto kujishughulisha na vitendo vya zinaa ili mradi wanakwepa mimba na magonjwa ya zinaa;
Tatu, muswada unasema sheria itungwe kutoa msukumo kwa matumizi ya vidhibiti mimba…Muswada unataka kututengenezea sheria za ushoga… unaridhia maovu mengine ya kuhasi watu kwa njia ya kufunga kizazi!”
Mbunge wa Afrika Mashariki, Nderakindo Kessy ameiambia FikraPevu kuwa, “Tanzania haijafikia hatua ya kujadili sheria kuruhusu utoaji mimba maana tamaduni na mazingira ya Kitanzania haziruhusu.”
Mwenyekiti wa Bodi ya HLI nchini Kenya, George Kegode akasema unatakiwa msimamo wa pamoja kupinga Muswada huu. “Muswada huu umeleta shida sana Kenya maana una vipengele vinavyohamasisha na kutaka kuhalalisha ushoga.”
Mkufunzi na Msaidizi wa Mkurugenzi wa Prolife Tanzania, Erasto Kimonge ameiambia FikraPevu kuwa, “mkataba unasema kutakuwa na huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu ya saratani. Kumbe wanajua kuna matatizo, lakini wanahamasishwa tu”