KAMA lilivyo tatizo sugu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini, mauaji ya kinyama dhidi ya watuhumiwa wa uchawi yanazidi kushika kasi mkoani hapa ambapo watu kumi, wengi wao wakiwa wazee wa kuanzia umri wa miaka 60 wameuawa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita wilayani Misungwi mkoani hapa kutokana na imani za ushirikina pamoja na migogoro ya ardhi.
Chanzo chetu cha habari kilimwambia mwandishi wa habari hizi juzi kwamba watuhumiwa hao waliuawa kwa kucharangwa mapanga, kati ya Aprili 4 hadi Mei 2 mwaka huu.
Inadaiwa kuwa watuhumiwa hao hao waliuawa kwa nyakati na siku tofauti, huku baadhi yao wakinyofolewa sehemu zao za siri.
Kwa sharti la kutotajwa jina wala wadhifa wake, chanzo kiliwataja waliouawa kuwa ni pamoja na watu wawili, Habi Kwike(50) na Hollo Magoso(60) ambao waliaga dunia baada ya kukatwakatwa mapanga katika kijiji cha Inonelwa wilayani humo.
Wengine waliouawa walitajwa kwamba ni wanandoa wawili, Lusanika Makambi(70) pamoja na mkewe Welele Lupaga(65) waliokuwa wakiishi katika kitongoji cha Bukwaya kilichomo ndani ya eneo la kijiji cha Misungwi.
Chanzo hicho kiliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Mageni Makelemo(48) pamoja na mama yake Shinje Nguga(70), wote wakazi wa kijiji cha Ilalambogo.
Kiliwataja watuhumiwa wengine waliouawa kwamba ni Kahabi Wigungu (70) mkazi wa kijiji cha Iteja aliuawa Aprili 28 huku akiwa amenyofolewa sehemu zake za siri ambapo siku iliyofuata(Aprili 29) mwanamke mwingine ambaye alikuwa mkazi wa kijiji cha Bujingwa Ikwalala(78) naye alicharangwa mapanga na kisha akanyofolewa sehemu zake za siri”.
Kwa mujibu wa habari, siku hiyo hiyo, Leah Kuzenza(83) mkazi wa kijiji cha Mapilingo aliuawa kwa kuchinjwa kama mbuzi wakati akioga bafuni na kwamba mauaji mengine yalitokea Mei 2 mwaka huu mkazi wa kijiji cha Igenga, Nyasale Lunyilija(45) aliuawa kwa kukatwa mapanga na kisha mkono wake ukawekwa juu ya meza nyumbani kwake.
Inadaiwa kwamba idadi kubwa ya wanawake wameuawa kutokana na imani za ushirikina, tofauti na wanaume ambao wameuawa kutokana na migogoro iliyosababishwa na kugombania ardhi.
Wilaya ya Misungi ni miongoni mwa wilaya 3 mkoani Mwanza ambazo zimetajwa na Jeshi la Polisi kwamba zimekithiri kwa matukio ya mauaji ya kinyama kutokana na imani za kishirikana pamoja na migogoro ya ardhi.
Wilaya nyingine ni Kwimba pamoja na wilaya ya mkoa mpya wa Geita; hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyowahi kutolewa hivi karibuni na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Simon Sirro.
Alisema ofisi yake inatarajia kuunda kikosi maalumu cha askari polisi kwa ajli ya kufuatilia na kuwakamata wote, hasa wanalipwa ujira kwa ajili ya kufanikisha mauaji hayo.
Chonde chonde wananchi msiwaue ndugu zenu kwa imani ya uchawi huo sio utamaduni wetu Watanzania.Nnawaomba sn tuweke nguvu zetu ktk kufanya kazi ili tuijenge Tanzania hii inayohujumiwa na MAFISADI