SHAURI la kudharau amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba lililokuwa limefunguliwa na ‘bibi kizee’ mmoja jijini hapa, Moshi Juma Mzungu(67) dhidi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza limetolewa uamuzi, ambapo wafanyakazi saba wametiwa hatiani na hivyo kuamriwa wakamatwe ili washtakiwe katika mahakama zenye uwezo wa kusikiliza kesi za jinai.
Shauri hilo ambalo lilikuwa kivutio kikubwa miongoni mwa wakazi wa Jiji tangu kufunguliwa kwake Desemba mwaka jana, liliamriwa jana na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Christian Mwashamwa.
Aliliambia Baraza kuwa baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na mlalamikaji, Baraza hilo limeridhika kwamba watuhumiwa kwa pamoja walidharau amri iliyokuwa imetolewa na Baraza hilo na kuamua kwenda kubomoa choo, bafu pamoja na banda la mama ntilie; mali ya mlalamikaji.
“ Baraza hili limeridhika na ushahidi uliowasilishwa na mlalamikaji ; na hivyo wale wote waliohusika na uvunjaji, wakiwemo watumishi wa halmashauri ya Jiji la Mwanza wanatakiwa wakamatwe ili washtakiwe katika mahakama zilizopewa mamlaka ya kuendesha kesi za jinai” Mwenyekiti aliliambia Baraza.
Alisema pia kuwa gari lenye namba za usajili SM 3359 Mitsubish Center, mali ya Halmashauri lililokuwa likitumiwa na maafisa hao siku ya tukio nalo linatakiwa likamatwe kama kielelezo.
Aliwataja wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji wanaotakiwa kukamatwa kuwa ni Abdon Baraka, Kitia Kagoroba, Mwita Wambura, Kasim, Kingi, Lazaro Matulanya pamoja na dereva wa gari hilo aliyetajwa kwa jina la Victor Mashamba.
Wengine waliokuwa wamefuatana na watumishi wa halmashauri ya Jiji wametajwa kuwa Shida Manyama, Sospeter Mjinja, Hamza Kalibuhe, Athumani Faraji na Hamis Faraji.
Mwenyekiti huyo alisema amri hiyo ilitolewa mwaka jana na kwamba ilikuwa inazuia kufanyika kwa shughuli zozote katika eneo na nyumba namba 244, Kitalu ‘L’ iliyoko katika mtaa wa Pasiansi Mashariki Jijini Mwanza.
“ Matokeo yake ni kwamba watu hao, wakiwemo watumishi wa Jiji ambao wanatakiwa kusimamia sheria za mipangomiji Desemba 23 mwaka jana, majira ya asubuhi waliamua kwenda kuvunja nyumba ya mlalamikaji ambaye ni Bibi Moshi Juma Mzungu, huku wakifahamu fika kwamba kesi ya msingi bado haijatolewa maamuzi” alisema.
Alisema kitendo hicho ambacho ni cha uonevu kilisababisha usumbufu kwa mlalamikaji ambaye ni bibi kizee na pia mjane.
Mwenyekiti huyo alisema kwa kufanya hivyo pia, watendaji wa Halmashauri ya Jiji waliingilia mwenendo wa kesi ya jinai ; kesi ambayo alisema bado inaendelea kulisikizwa katika mahakama ya mkoa.
Alisema Baraza limetoa adhabu hiyo ili liwe fundisho kwa watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na watendaji wengine katika ofisi za serikali jijini hapa ambao mara kwa mara wamekuwa na tabia ya kukiuka sheria za nchini na kusababisha kuwepo kwa mashauri mengi ya yanayotokana na migogoro ardhi jijini.
Katika shauri hilo, mlalamikaji alikuwa akitetewa na kampuni ya uwakili ya Muna Advocates ya Jijini hapa ambapo Halmashauri ya Jiji lilitetewa na wanasheria wake.
Habari hii imeandaliwa na Juma Ng’oko, Mwanza
wazee ni kundi lililosahaulika mwiongoni mwa wanajamii ya Tanzania. Wananyimwa huduma nyeti za afya,chakula na kumiliki ardhi kama hili la mwanza. zaidi ya yote ni mtizamo hasi ya wanajamii walionao kwa wazee, hebu angalia kichwa cha habari cha taarifa hii,WATUMISHI JIJI LA MWANZA HATIANI KWA KUBOMOA CHOO CHA KIZEE- NENO KIZEE LINA UKAKASI WA MTAZAMO HASI KWA WAZEE, hebu waandishi na wanajamii tubadilikeni kuhusu hili