Waziri Mkuu wa India Bw. Manmohan Singh anatarajiwa kuwasili nchini siku ya Alhamisi wiki hii kuanza ziara rasmi ya kiserikali kwa muda wa siku tatu akiwa mgeni wa Rais Jakaya Kikwete. Bw. Singh atakuwa anaingia nchini akitokea Ethiopia ambako atashirikia Mkutano wa pamoja wa Biashara kati ya India na Afrika. Ziara yake ya Ethiopia anaifanya kwa mara ya kwanza tangu ashike madaraka. Ziara yake katika Afrika itachukua siku sita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Dar-es-Salaam Bw. Singh anakuja nchini kuitikia mwaliko ambao ulitolewa na Rais Kikwete kwa Waziri Mkuu huyo wa taifa ambalo linapiga kasi zaidi ya maendeleo na ambalo lina nguvu ya Nyuklia. “Mheshimiwa Singh amekubali mwaliko huo katika barua yake aliyomwandikia Rais Kikwete na iliyokabidhiwa kwake na Balozi wa India katika Tanzania, Mheshimiwa K.V. Bhagirah wakati Balozi huyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete leo, Alhamisi, Mei 19, 2011, Ikulu, Dar es Salaam.” imeseta taarifa hiyo iliyosainiwa na Ikulu bila kusainiwa na mtu yeyote.
Akijibu mwaliko huo Bw. Sing amesema kuwa “Nakushukuru kwa barua ya kunilialika kuitembelea nchi yako nzuri. Itakuwa ni heshima kwangu kuitembelea Tanzania na naukubali mwaliko huo kwa furaha kubwa” na kuwa “Nina ari kubwa kukutana nawe na marafiki wengine wa Tanzania wakati wa ziara hiyo na kujadili njia ya kuuinua uhusiano kati ya nchi zetu kwenye ngazi mpya kwa manufaa ya wananchi wa nchi zetu mbili”
Ziara ya Bw. Singh nchini imekuja wakati ambapo taifa hilo la India likizidi kututumua nguvu zake za kiuchumi na ushawishi hasa katika eneo la Afrika na kuonekana ikiingia katika ushindani wa ushawishi kati ya na China pamoja na nchi za Magharibi ambazo zimekuwa na nafasi ya pekee katika bara la Afrika kwa muda mrefu.
Kabla hajaanza ziara yake hiyo ndefu leo Jumatatu Bw. Singh alielezea siku ya Jumapili mwelekeo wa ziara yake hiyo kuwa uhusiano kati ya India na Afrika utahusisha zaidi ni “kuipa uwezo Afrika na kubadilishana ujuzi, biashara na ujenzi wa miundombinu”. Bw. Singh amesema kuwa “uwepo wa watu wengi wenye asili ya India katika kila kona ya Afrika ni ushahidi wa wazi wa mahusiano yetu ya kihistoria.”
Bw. Singh anakuja Tanzania huku serikali yake nayo ikiwa imetoka kugubikwa na mlolongo wa kashfa ambazo zimechafua sifa yake ya muda mrefu kama kiongozi. Katika hili anajikuta anakaribishwa na mwenyeji wake Rais Kikwete ambaye naye serikali yake imekuwa ikiandamwa na kashfa nyingi na jina lake kuchafuliwa mbele ya wananchi kitu ambacho inadaiwa kuwa kilichangia kufanya vibaya katika uchaguzi mkuu uliopita.
Hata hivyo, Bw. Singh amekuwa mkali zaidi huku Waziri wake mmoja akiwa tayari kifungoni kutoka na kashfa za ufisadi. Kama ilivyokuwa kashfa ya EPA Tanzania Bw. Singh alijikuta serikali yake inagubikwa na kashfa kubwa zaidi ya ufisadi tangu uhuru pale mmoja wa mawaziri wake alipouuza njia za mawasialiano ya hewa kwa kampuni moja huku yeye mwenyewe akikatiwa kitu kidogo. Vyombo vya sheria vya India havikufanya ajizi kuwakusanya huyo Waziri wa Mawasiliano Andimuthu Raja pamoja na washirika wake ambao wote wanasotea katika jela maarufu ya Tihar.
Pamoja na kashfa hizo serikali yake ilijikuta inagubikwa na kujiuzulu kwa watendaji wake mbalimbali kufuatia kuhusishwa na kashfa za ufisadi. Hii ilikuwa ni pamoja na kujiuzulu kwa Mkuu wa Taasisi ya kuzuia rushwa ya India Bw. P. J. Thomas ambaye kuteuliwa kwake kulipingwa na wanaharakati wengine lakini aliteuliewa lakini baada ya kashfa kuzidi ilimlazimu kujiuzulu. Nafasi yake tukilinganisha na Tanzania ni sawa na ile ya Mkurugenzi wa TAKUKURU Dr. Edward Hosea.
Baada ya wananchi wa India kukerwa sana na ufisadi wanaharakati wa nchi hiyo walijikusanya pamoja wakiongozwa na mwanaharakati Gandhian Anna Hazare (73) kuanzisha mgomo wa njaa ambao uliungwa mkono na watu wengi na kusababisha serikali ya Singh kukubali kukaa chini na wanaharakati na wapinzani kuja na sheria kali ya kuisimamia serikali na hasa masuala ya utawala bora na kashfa. Sheria hiyo inafanana na ile tume iliyoundwa wakati wa Nyerere ya Chifu Erasto Mang’enya ambayo mfano wake hadi hivi sasa nchini haupo tena baada ya makali yake kukatwa katwa.
Pamoja na mlingano huo wa masuala ya kashfa katika serikali zao na kufanya vibaya katika chaguzi mbalimbali serikali ya India bado inaonesha kuwa na nguvu zaidi ya kiuchumi kuliko ile ya Tanzania na nafasi ya ziara hii yaweza kuwa nafasi ya pekee kwa Rais Kikwete kubadilisha mawazo na uzoefu na Bw. Singh ili kuweza kuifanya Tanzania ianze nayo kututumia misuli yake ya kiuchumi na nguvu ya kuogopwa katika eneo la Afrika.
Pamoja na matatizo yake nyumbani Bw. Singh anaanza ziara hii Afrika huku uchumi wa nchi yake ukizidi kupata nguvu na kama mwenyewe alivyosema siku ya Jumapili kuwa India siyo tu itakuwa ni nchi ambayo demokrasia inakua kwa kasi zaidi duniani bali pia anatarajia kuwa India itakuwa nchi ambayo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi.
Katika Tanzania Bw. Singh anatarajia kufanya mazungumzo na Rais Kikwete ambayo yatahusisha kuingia mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Sekta kubwa ambazo zinatarajiwa kunufaika katika baadhi ya makubaliano hayo hasa zitakuwa ni zile za Utalii na Usafiri hasa kwa sababu Tanzania inajaribu kuvutia watalii kutoka India mahali ambapo daraja la kati linazidi kuongezeka huku uwekezaji wa makampuni ya India nchini ukitarajiwa kuongezeka hasa katika maeneo ya ujenzi wa mahoteli ya kitalii na huduma za usafiri.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa India anayeshughulikia Afrika na Ulaya Bw. Singh atazungumza na Rais Kikwete kuhusu makubaliano mbalimbali hasa katika sekta za Utalii, Kilimo na tekinolojia ya mawasiliano. Hadi hivi sasa biashara kati ya India na Tanzania inafikia thamani ya karibu shilingi trilioni 1.5 kwa mwaka huku ikipendelea India zaidi. Tanzania inauza vitu vyenye thamani ya dola milioni 132.5 kwa mwaka wakati India inauza vitu vyenye thamani ya dola milioni 596.7 kwa mwaka. Hivyo bado kuna changamoto kubwa sana ya kuona makubaliano yoyote yanajenga mazingira kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania nao wanapata nafasi ya kuuza biashara zao huko India.
(Na M. M. Mwanakijiji)