Waziri Mpango asisitiza uchumi umeimarika, aitaka sekta binafsi kushirikiana na serikali

Jamii Africa

Wakati mjadala ukiendelea juu ya hali ya uchumi nchini, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema uchumi wa nchi umeimarika na umekuwa kwa asilimia 6.8.

Kauli ya Waziri Dkt. Mipango inakuja siku chache baada ya kuwepo kwa kauli mbalimbali za wanasiasa na wadau wa sekta binafsi kulalamika kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa na ongezeko la kodi ya serikali ambalo halizingatii hali halisi ya uwekezaji.

Akizungumza leo jijini  Dar es salaam katika mkutano uliowakutanisha sekta binafsi na serikali kujadili hali ya biashara nchini, Dkt. Mpango amesema uchumi wa nchi umeimarika na amezitaka pande zote mbili kushirikiana ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya kufanya biashara.

“Sekta binafsi ikidorora, pia sekta ya umma hudorora, vyote vinategemeana” amesema Dkt. Mpango na kuongeza kuwa kuna fedha za kutosha katika mzunguko na serikali iko makini kuhakikisha inathibiti mfumuko wa bei.  Ameitaka sekta binafsi  kujenga mshikamano utakaosaidia  kuzinufaisha pande zote mbili.

Kwa Upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema yeye kama waziri kazi yake ni kuweka mazingira sawa ya ushindani ili wawekezaji wafanye biashara zao kwa uhuru bila upendeleo.

Amesema serikali inaendelea kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji ili sekta binafsi ijenge viwanda na kulipa kodi itakayowezesha wananchi kupata huduma za kijamii.

“Mimi kama waziri wa viwanda kazi yangu ni kuijenga sekta binafsi yenye ushindani ili kujenga viwanda, ajira, bidhaa zenye ubora na kulipa kodi”, amesema Waziri Mwijage na kuzitaka taasisi za serikali zifanye kazi vizuri na sekta hiyo na kuepukana na migongano isiyo na tija.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Roberto Jarin amesema licha TBL kuwa mlipa kodi mkubwa, katika kipindi cha miaka 6 iliyopita mapato ya kampuni hiyo hayajaongezeka kutokana na mabadiliko yanayojitokeza katika ya  sekta ya biashara nchini.  

Siku chache zilizopita Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alikaririwa na  kituo kimoja cha radio ambapo alisema licha ya uwekezaji kukua lakini sekta binafsi vikiwemo viwanda vya uzalishaji bidhaa zinapitia kwenye kipindi kigumu ambacho inakabiliwa na ukosefu wa mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara zao,

“Serikali kwa juhudi zake imeendelea kutengeneza mazingira mazuri ya biashara, kama kurekebisha njia za usafirishaji ikiwemo reli na viwanja vya ndege, lakini suala la kodi limekuwa ni tatizo, malalamiko mengi ya sekta binafsi yanatoka kwa namna ambavyo TRA wanakusanya kodi, ni kero kubwa, imekuwa kwa mwezi mmoja taasisi binafsi inaweza ikatembelewa na timu ya TRA tatu na zote zikaja na makadirio tofauti”.

Inaelezwa kuwa uzalishaji katika sekta binafsi umepungua kutokanaongezeko la kodi na benki nyingi kuacha kukopesha sekta binafsi ambayo inatumia mikopo hiyo kama dhamana ili kuendeleza uzalishaji.  

Mkurugenzi wa Benki ya Dunia (WB) nchini Tanzania, Bella Bird ameishauri serikali kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kufanya biashara na kukuza uchumi wa taifa.

Kwa mara nyingine tena, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameendelea kusisitiza kuwa hali ya uchumi sio nzuri na mapato ya serikali yameporomoka ambapo yameathiri utendaji na uzalishaji wa sekta binafsi na kuitaka serikali kumruhusu Mkaguzi wa Mapato ya Serikali (CAG) kuthibitisha hali hiyo.

“Kama Rais anaamini kuwa Mapato hayajaporomoka, aruhusu ukaguzi maalumu wa CAG kwenye Mapato ya Julai na Agosti 2017 na ukaguzi huo uwekwe wazi Kwa umma. Kodi inayokusanywa na TRA inaweza kulipa mishahara na kuhudumia Deni la Taifa tu”, ameandika Zitto katika ukurasa wake wa Twitter.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *